Sunday, October 11, 2020

BIBLIA TAKATIFU-WEWE UNAPENDELEA KUSOMA VIFUNGU GANI JUU YA PESA?

 “Chanzo cha maovu duniani siyo pesa bali kukosa pesa mfukoni” ~ Cypridion Mushongi


Upatikanaji wa pesa kwa mtu yeyote unategemea sana imani na mtazamo wa mtu juu ya pesa.

Linapofika suala la pesa, watu tunagawanyika katika makundi makuu matatu; ambayo ni..
Kundi la kwanza: ni wale wanaochukia pesa kwenye nafsi zao bila kujua. Kundi hili, wanaona pesa kama chanzo cha maovu mengi yaliyoko duniani. Watu wengi wa kundi hili, ni watu maskini; na ndani ya nafsi zao, wanaamini matajiri wamelaaniwa na kamwe hawatakwenda mbinguni.

Kundi la pili: ni wale watu wanaotaka kuwa na pesa kidogo au kiasi, ilimradi zisiwe nyingi. Mara nyingi, hili ni kundi la watu wa tabaka la kati na ndilo lenye waajiriwa wengi. Pia, kundi hili, linaamini katika kuridhika na kile kidogo walichonacho. Watu wengi kwenye kundi hili wanapendelea kuhamasisha watu wengine waone umuhimu wa kumshukuru Mungu kwa hicho walichonacho. Yamkini kundi hili linatumia muda wake mwingi kuomba, ili Mungu awajalie wazidi kuendelea kuwa jinsi walivyo —“hili ni kundi ambalo kwalo, kuendelea kubaki kwenye ukanda wa faraja (comfort zone) ndiyo lengo kuu”.

Kundi la tatu: ni kundi ambalo watu wanapenda kuwa na pesa nyingi bila kujali maisha waliyokulia. Katika kundi hili, tunaamini kuwa Mungu anakupa kiasi chochote cha pesa unazotaka. Lakini pia tunaamini kuwa, "chanzo cha maovu na maradhi mengi duniani ni kutokuwa na pesa mfukoni". Malengo makuu kwa watu wa kundi hili, ni kutumia kila aina ya uwezo tuliopewa na Mungu kuzalisha bidhaa na huduma nyingi, ambazo hatimaye zinaondoa kero na matatizo ya watu wengine.

Kwa kifupi katika kundi la tatu, kuna imani kwamba kadiri mtu anavyotatua matatizo ya watu wengi zaidi, ndivyo atakavyoweza kutajirika zaidi—katika hili limeamua kujitoa, kuwa wavumilivu, kutokata tamaa hadi malengo haya yatimie. Ni bora kufa tukiwa tunajaribu kuliko kufa maskini tukiwa tumekaa.

Mimi ninafikiri Mungu anaangalia yale yote tunayofanya kwa kutumia vipaji na zawadi tulizopewa na yeye. 

Ninadhani ni wajibu wa kila binadamu kutumia zawadi (kipaji, muda na utajiri) tuliyopewa na Mungu kuboresha maisha ya binadamu na kuifanya dunia kuwa ni salama na mahali pazuri pakuishi.

Kwa wale ambao mnasoma na kufuatilia masuala mbalimbali ya biblia, mtakubaliana na mimi kuwa, BIBLIA inasema mengi juu ya utajiri na pesa. 

Inasemekana kuwa biblia ina vifungu vingi vinavyozungumzia pesa kuliko mada nyinginezo. 

Kila vinaposomwa vifungu vya biblia vinavyohusu pesa, mara nyingi uleta maana na hisia tofauti kwa makundi matatu ya watu yaliyotajwa hapo juu.

Maana yake ni kwamba, kila kundi linapendelea kusoma na kuamini vifungu tofauti juu ya somo la pesa.

Utofauti huu unatokana na mtazamo, jinsi watu wanavyojiona, jinsi wanavyojichukulia na jinsi wanavyoiona dunia

Kwa mfano; watu wa kundi la kwanza (maskini), wanapendelea zaidi kusikia na kufuatilia vifungu katika biblia, ambavyo vinazungumzia zaidi maovu ya pesa.

Mojawapo ya vifungu vya biblia, ambavyo watu maskini (kundi la kwanza) wanapenda kusikia na kufuatilia ni mfano ukisoma; 
Mathayo 19:21-26 anasema: “Yesu akamwambia ukitaka kuwa mkamilifu, enenda ukauze ulivyonavyo uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni, kisha njoo unifuate. 
“Yule kijana aliposikia neno lile, akaenda zake kwa uzuni; kwasababu alikuwa na mali nyingi. 
“Yesu akawambia wanafunzi wake amini nawambieni, yakwamba itakuwa shida tajiri kuingia katika ufalme wa mbinguni”. 
“Nawambia tena ni rahisi zaidi ngamia kupenya tundu la sindano, kuliko tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu”

Pia, ukisoma kitabu cha Yakobo 5:1-6; anasema:

“Haya basi enyi matajiri! Lieni mkapige yowe kwasababu ya mashaka yenu yanayowajia. Mali zenu zimeoza na mavazi yenu yameliwa na nondo. Dhahabu yenu na fedha yenu zimeingia kutu, na kutu yake itawashuhudia, nayo itakula miili yenu kama moto.

“Angalieni ajira ya wakulima waliovuna mashamba yenu, ninyi mliouzuia kwa hila, unapiga kelele, na vilio vyao waliovuna vimeingia masikioni mwa Bwana wa majeshi”.

“Mmefanya anasa katika dunia na kujifurahisha kwa tamaa; mmejilisha mioyo yenu kama siku ya machinjo. Mmehukumu mwenye haki mkamua; wala hashindani nanyi”.

Kundi la pili; ambalo linajumuisha watu kutoka tabaka la kati wakiwemo waajiriwa, wao upendelea kufuatilia vifungu ambavyo vinazungumzia umuhimu wa watu kuridhika na kushukuru kwa kile walichonacho.

Miongoni mwa vifungu vya biblia, ambavyo watu wa tabaka hili upendelea kusikia na kufuatilia ni ukisoma kitabu cha Ayubu 36:11; anasema:

”Kama wakisikia na kumtumikia watapisha siku zao katika kufanikiwa na miaka yao katika furaha”.

Pia, ukisoma; Mithali 19:23 “Kumcha Bwana huelekea uhai; Atakaa ameshiba; hatajiliwa na ubaya”

Katika kundi la tatu ambalo zaidi linajumuisha matajiri linapendelea kufuata vifungu vya biblia ambavyo vinazungumzia namna ambavyo Mungu uwalipa fadhira matajiri na kuwapa adhabu maskini.

Kwa mfano; ukisoma Mithali 17: 16:

“Nini maana yake, mpumbavu kuwa na fedha mkononi mwake ya kununulia hekima, Ikiwa hana moyo wa ufahamu?”.

Pia, ukisoma kitabu cha Mathayo 25:14-30—juu ya taranta walizopewa watu watatu, anasema:

“Maana ni mfano wa mtu atakaye kusafiri, aliwaita watumwa wake akaweka kwao mali zake. “Akampa mmoja taranta 5, na mmoja talanta 2, na mmoja talanta moja; kila mtu kwa kadiri ya uwezo wake; akasafiri.

“Mara yule aliyepokea talanta tano akaenda akafanya biashara nazo, akachuma faida talanta nyingine tano. “Vile vile na yule mwenye mbili, yeye naye akachuma nyingine mbili faida. “Lakini yule aliye aliyepokea moja alikwenda akafukua chini, akaficha fedha ya bwana wake. Baada ya siku nyingi akaja bwana wa watumwa wale, akafanya hesabu nao. 
“ Akaja yule aliyepokea talanta tano, akaleta talanta nyingine tano, akisema, Bwana uliweka kwangu talanta tano; tazama talanta nyingine tano nilizopata faida. “Bwana wake akamwambia, vema, mtumwa mwema na mwaminifu; ulikuwa mwaminifu kwa machache, nitakuweka juu ya mengi; ingia katika furaha ya Bwana wako. 
“Akaja na yule aliyepokea talanta mbili; tazama, talanta nyingine mbili nilizopata faida.” Bwana wake akamwambia vema mtumwa mwema na mwaminifu; ulikuwa mwaminifu kwa machache nitakuweka juu ya mengi; ingia katika furaha ya bwana wako. 
“Akaja na yule aliyepokea talanta moja, akasema, Bwana, nalitambua ya kuwa wewe u mtu mgumu, wavuna usipopanda, wakusanya usipotawanya; “basi nikaogopa, nikaenda nikaificha talanta yako, katika ardhi; tazama, unayo iliyo yako.

“Bwana wake akajibu, akamwambia, wewe mtumwa mbaya na mlegevu, ulijua yakuwa navuna nisipopanda, nakusanya nisipotawanya. “Basi ilikupasa kuiweka fedha yangu kwa watoao riba; nami nikija ningalipata iliyo yangu na faida yake.

“Basi nyang’anyeni talanta hiyo, mpeni yule aliyenazo talanta kumi. “Kwa maana, kila mwenye kitu, na kuongezewa tele, lakini asiye na kitu, hata kile alichonacho atanyang’anywa. “Na mtumwa yule asiyefaa, mtupeni mbali katika giza la nje; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno”.

Swali kwako; wewe unadhani ni vifungu gani katika biblia ambavyo unaona vinaendana na mtazamo wako, malengo, maono yako, hisia zako, maombi yako juu ya pesa?; Je? Ni vifungu vya watu wa tabaka la kati au la chini (maskini) au la matajiri?. Bilashaka jibu sahihi unalo wewe mwenyewe.

Kwa upande wangu mimi, nipende kusema kuwa ninaheshimu sana uhuru wa mawazo na imani kwa ujumla, ikiwa ni pamoja na wale wote wasiomwamini Mungu.

Mara nyingi, sipendi watu wanaolazimisha nikubali imani zao, na mimi pia sina mpango wowote wa kulazimisha wakubali imani yangu.

Nadhani Mungu hajali mtu tajiri wala maskini—BALI anampenda kila mtu kwa jinsi alivyo. Lakini, kama unataka kutajirika, basi hakikisha unachagua dini na wahubiri wako kwa makini sana.

Natumaini Makala hii imekuongezea kitu fulani, ikiwa ni pamoja na kukuongezea ufahamu na ujuzi juu ya masuala mazima ya ulazima wa kila binadamu kupata pesa kiasi chochote anachohitaji.

Kwahiyo endelea kuitumia vizuri MAARIFASHOP ili kujifunza mambo mbalimbali yatakayokuwezesha kuitoa nje pesa iliyoko ndani yako.

Kupata makala mpya kila zinapochapishwa, bonyeza kiungo hiki; INGIA MAARIFASHOP kisha sajiri barua pepe yako na kama unapenda kupata mafunzo ya kila siku na makala mpya kwa njia ya whatsap bonyeza neno MAFUNZO.

No comments: