Kaya na Uchumi

Hii Ndiyo Hasara ya Kulipa Kwanza Watu Wengine


“Unapopata pesa ukatenga akiba kwanza, tunasema umejilipa kwasababu pesa hiyo imebaki kwako na ndiyo mbegu ya kuzalisha pesa nyingi zaidi” ~ Cypridion Mushongi
Watu wengi tunajua kuwa ukishafanya kazi ya mwajiri kinachobakia ni kulipwa mshahara au ujira, nje ya hapo hatuna habari. Ukilipwa na mwingine unafurahi sana. Furaha unayoipata ukiwa umelipwa mshahara, pengine ndiyo inakusukuma kutumia mara moja kipato chako kila unapolipwa. Hali hii ya kufurahia kulipwa pesa na wengine ndiyo imezidi kutuweka utumwani maisha yetu yote.

Kila tunapolipwa pesa, kazi yetu ya kwanza huwa ni
kujipatia mahitaji na kulipa madeni (kutumia) basi! Tunatumia pesa inaisha ndipo tunatafuta pesa nyingine. Yaani inakuwa ni kama mchezo wa “paka na panya”.

Ukweli ni kwamba, paka anapomuwinda panya na kufanikiwa kumkamata, mara moja biashara ya kutafuta panya mwingine huwa inaishia hapo hapo. Na panya aliyekamatwa akishaliwa, ndipo paka anapata wazo la kutafuta panya mwingine.

Ebu jiulize wewe binafsi ni kitu gani ambacho huwa unafanya kwanza pindi unapoingiza pesa mfukoni? Twambie unapokuwa umepokea mshahara; umefanya biashara umepata faida; umepata zawadi kutoka kwa wazazi, watoto au marafiki huwa kwanza unafanya nini?. Birashaka utaniambia matumiziya kifamilia au yako binafsi. Ukiniambia matumizi ninakuelewa, kwani hata mimi nilizoea kufanya hivyo __ kutumia!.

Imekuwa kawaida yetu wengi tunapopata pesa huwa tunaanza na kutumia (kujipatia mahitaji na kulipa madeni), kabla ya kufanya kitu kingine. Mara nyingi tunawahi kununua vitu ambavyo tunadhani ni muhimu wakati siyo muhimu. Kwasababu, hatuwezi kudhurika wala kuathirika tukivikosa __ na hakuna ulazima wa kuvipata leo leo.

Tukishapata pesa tunajikuta tuna mahitaji mengi ambayo tunataka pesa yoyote tuliyopata itumike mara moja kuyatimiza. Jiulize kabla ya kupata hiyo pesa, mbona ulikuwa huna shauku ya kupata hayo mahitaji unayoyaita ya muhimu? Ina maana wewe kwako matumizi yanaonekana kadiri unavyopata pesa? Niambie, hayo matumizi yalikuwa wapi kabla ya hapo?. Jaribu kulifanyia kazi hili, lisije likawa ndicho kizingiti cha wewe kukosa mtaji wa kufanya vitu vyenye kukuletea pesa nyingi hapo mbeleni.

Wajasiriamali pamoja na wawekezaji waliobobea wanatwambia kwamba “haijalishi unapata pesa kiasi gani, BALI ni kiasi gani unakaa nacho”. Watu wengi tunajitahidi kutafuta pesa na Mungu mara zote ameweza kutujalia tumepata, lakini shida yetu kubwa ni kushindwa kukaa na pesa.

Tunahitaji kuweza kuitunza pesa kwa muda, kabla ya kufanya maamuzi yoyote juu yake. Hii itakuwa ni hatua muhafaka sana kwa yeyote ambaye ana dhamira ya dhati ya kufikia uhuru wa kipato ambao ni endelevu au kipato bila kikomo.

Jenga utamaduni wa kuhakikisha kila unapopata pesa yoyote, itunze kwanza japo kwa muda fulani kabla hujakimbilia kufanya matumizi ya aina yoyote ile. Waweza kuiweka sehemu utakayoona ni salama kama vile benki.

Katika kipindi hicho ambacho utakuwa umeamua kutunza pesa zako, endelea na maisha yako uliyokuwa nayo kabla ya kupata hizo pesa. Jitahidi, kuendelea na maisha yako kana kwamba huna pesa uliyotunza. Yawezekana wakati ukiendelea kutunza pesa, kuna kitu cha thamani ambacho unatamani kukinunua na ukiangalia pesa uliyotunza unaona kabisa bei yake iko ndani ya uwezo wako; lakini husifanye hivyo, kwasababu pesa yako itakuwa kwenye kipindi cha kutunzwa au kuhatamiwa.

Suala la kutunza au kuhatamia pesa kwanza kila unapoipata, yawezekana lisieleweke kirahisi. Lakini nia na madhumuni ya utaratibu huu ni kutaka wewe ujenge nidhamu ya pesa, ili hatimaye uwe mtu mwenye uwezo mkubwa wa kuimiliki au kuiendesha pesa __ na sio wewe kumilikiwa au kuendeshwa na pesa.

Kuna watu ambao wakiwa na pesa utawajua tu! wanakuwa na furaha sana, wanachangamka zaidi, na pia utawaona wakitembelea sokoni na madukani, huku wakinunua hiki na kile. Watu wa namna hii, unakuta hawana muda wa kutulia mpaka pesa hizo ziishe. Kwao ni mpaka pesa ziwaishie ndipo wanapata upya akiri nzuri ya kufikiria maendeleo.

Ukweli ni kwamba, kila tunapopata pesa tunashawishika kuitumia, matatizo ndio yanajitokeza, mara tunaona vitu vizuri n.k. Hali hii ndiyo uletaa tabia ya kupendelea matumizi kwanza kabla ya kutenga Akiba.

Ni muhimu kujiwekea akiba kila upatapo pesa. Ili kujenga tabia ya kuweka akiba ni lazima ujizoeshe kwanza kukaa na pesa kwa muda, bila kufanya chochote au matumizi yoyote. Ukishakuwa umeweza hilo, hatua ya pili ni kuanza utaratibu wa kutenga asilimia fulani kama akiba. Suala hili la akiba ndilo linatakiwa kupewa kipaumbele namba moja pindi tupatapo pesa yoyote ile.

Kwa maana nyingine ni kwamba, tunatakiwa kupanga matumizi kwa pesa le tu inayobaki baada ya kutoa akiba. Utaratibu huu wa kutenga akiba kwanza ndio tunaita kujilipa kwanza kabla ya kulipa watu wengine. Hapa unatakiwa utofautishe “kujilipa mshahara” na “kujilipa kwanza”.

Unapopata pesa na ukatenga akiba kwanza, tunasema umejilipa kwasababu pesa hiyo imebaki kwako na ndiyo mbegu ya kuzalisha pesa nyingi zaidi.

Lakini, ukipata pesa ukaenda kununua mahitaji yako au kulipa madeni uliyokuwa nayo kwanza, basi ujue kuwa moja kwa moja umefanya kazi ya kulipa watu wengine kwanzakabla ya kujilipa wewe. Tabia hii ya kulipa watu wengine kwanza kila mara tunapopata pesa, ndio imetufanya tuwe maskini hadi leo. Pia, tabia hii ni mbaya na inasemekana ndiyo imechangia kwa kiasi kikubwa kuzalisha maskini wengi duniani.

Kama wewe ndio kwanza unaanza safari yako ya kuelekea kwenye utajiri, niseme hakuna namna, ni lazima ujifunze kuwa na tabia hii nzuri ya kujilipa kwanza wewe kabla ya kutumia pesa kwa mambo mengine.

Anza leo kutumia kanuni hii ya kutenga akiba kwanza na matumizi mengine ndiyo yafuate. Kwa ufupi ni hivi: pata pesa, itunze kwanza kwa muda, halafu kabla ya kuitumia tenga akiba kwanza, baada ya hapo fanya matumizi yako ya muhimu na kisha zinazobaki fanya mambo yako ya anasa. Jaribu kuishi kwa utaratibu huu mpaka pale utakapoona umewekeza vya kutosha katika miradi inayokuletea mapato makubwa yasiyokuwa na kikomo.

Kwakuwa pesa siyo hesabu ni tabia, unahimizwa kujifunza kwa hali na mali tabia hii ya “kujilipa kwanza”, halafu mambo mengine mazuri yatafuata, endapo utaanza leo.

Ili kujfunza tabia ya kutafuta, kumiliki na kendesha pesa, usiishie tu kusoma makala hii, bali ujenge utamaduni wa kujisomea masuala ya pesa na biashara hasa kupitia mtandao wako wa http://maarifashop.blogspot.com.

Hapa utakutana na makala nzuri zitakazozidi kukufungua akiri na hatimaye kuharakisha safari yako ya kwenda kwenye mafanikio makubwa.

Pia, kwaajili ya kupata makala hizi pamoja na mafunzo mbalimbali kupitia e-mail yako unaweza kujiunga na mtandao wa MAARIFA SHOP kwa kubonyeza neno NITUMIE MAKALA...


  Kisa cha Wewe Kuitwa Bahili ni Hiki

“Watu wengine wameitwa wabahili kwasababu wameamua kudhibiti pesa zao zisichukuliwe kiholela na watu wengine”.

Imekuwa ni kawaida kusikia watu wakilalamikia wenzao kuwa ni wabahili. Wengine wanasema eti hawa wanaoitwa wabahili ni wagumu sana kupata pesa yao!; pia inasemekana kwamba watu hawa hawapendi pesa yao itoke kwenda kwa watu wengine ~hawataki kutoa riziki

Pengine ni vizuri tujiulize ni kwa namna gani mtu anaitwa bahili? Ukifuatilia utagundua kuwa, mtu anayeitwa bahili, mara nyingi ni mtu yule ambaye hapendi kutumia pesa yake kwa vitu ambavyo havimuhusu yeye moja kwa moja.

Kwa mfano ukimfuata akuchangie mchango wa harusi, jubilei, mahafari n.k. hachangi au anachanga kidogo sana; hanunui vitu kwa fasheni mpaka asukumwe na dhamira yake ya ndani, hanunui vitu kwa kushitukizwa na wauzaji, lazima awe amepanga hivyo tokea alipotoka nyumbani kwake.

Sababu ya watu hawa kuitwa wabahili ni kwamba, ili wakupe pesa yao lazima na wewe huwe na thamani ambayo inalingana au kubwa kuliko pesa waliyonayo. Endapo wakiona hakuna thamani watakayoipata, basi wabahili hufanya maamuzi ya kutokutoa pesa yao.
Ikumbukwe kuwa mahusiano katika maisha ya binadamu yanaongozwa na ubadilishanaji wa thamani” .

Kinachofanya kuwe na umoja na mshikamano kati ya mtu na mtu au kikundi ni thamani aipatayo mhusika. Kwahiyo, inatosha kusema kuwa “thamani” ni manufaa au uhitaji na kwa mantiki hii watu utoa pesa zao mfukoni ili kununua thamani kwaajili ya kutatua kero mbalimbali.


Thamani ndiyo huwafanya watu wengine kupeleka pesa kwa watu wengine. Kwa maana nyingine, maisha yetu yote yanatawaliwa na jambo moja tu nalo ni “kubadilishana thamani”. Tunaposema kubadilishana thamani maana yake ni kwamba, kila mtu anamiliki thamani tofauti na mwingine na ni vigumu mtu mmoja kumiliki thamani za aina zote, ndiyo maana ni lazima na ni kwaida watu kununua thamani ambazo hawana kutoka kwa watu wengine. 

Kimsingi suala la kubadilishana thamani huwa linakuwa hivi: mimi ninazalisha thamani nyingi ambazo nazitumia kukidhi matakwa yangu na wengine. Ili watu wengine waweze kupata thamani kutoka kwangu lazima wanipatie pesa (tubadilishane), na mimi utuia pesa hiyo hiyo kununulia thamani kutoka kwa watu wengine.

Maisha ya kubadilishana thamani yanatufundisha na kutuonyesha kwamba, ukiwa na thamani kwaajili ya watu wengine, huwezi kupata ugumu wa kupata pesa kutoka kwa mtu yeyote yule, ilimradi una thamani haitakayo. Kwa ujumla wewe uliye na thamani kubwa, hutamuona mtu anayeitwa “bahili”.

Sasa kama maisha yetu yanastawi kwa watu kubadilishana thamani, iweje leo watu wengine wawalalamikie wenzao juu ya ubahili? Na kama mtu ameamua kwa hiari yake kubania rasirimali zake, iweje alaumiwe? Kwasababu rasilimali alizonazo mtu siyo za kwako, wewe unawajibika kwenye rasilimali zako tu. 

Ubahili unatokea mara nyingi katika mazingira ambayo kunakuwa hakuna kitu cha kubadilishana. Upande mmoja unajaribu kutumia nguvu ili kujipatia pesa au bidhaa kutoka upande mwingine bila kulipa au kuchangia chochote ~ hali hii ikiachwa na kuendelea mara nyingi ndiyo uzaa unyonyaji na hili limeingia kwenye jamii yetu bila kujua.

Watu wengine wameitwa wabahili kwasababu wameamua kudhibiti pesa zao zisichukuliwe kiholela na watu wengine. Kutokana na tamaa ya kutaka kupata pesa za watu wengine bure, ndiyo maana jamii yetu ya sasa haina tena upendo wowote kwa mtu ambaye ni bahili wa rasilimali zake binafsi na wala siyo za mtu. 

Watu wengi leo wana chuki sana na matajiri eti! ni wabahili, hawataki kutoa misaada n.k. LAKINI kama wewe hutajikita katika kuzalisha thamani itakayogusa maisha ya huyo tajiri basi sahau kabisa kupata pesa ya huyo tajiri. 

Ukiona unasifiwa kuwa wewe siyo bahili basi ujue kuwa, watu waliokuzunguka wanaweza kuipata pesa yako bila kulazimika kuwa na kitu cha kubadilishana na wewe. Wakiona hawajapata chochote cha bure kutoka kwako, hawachelewi wanaanza kukulalamikia kwamba wewe hutoi pesa na inapobidi wanakuita “bahili” mkubwa sana.

Waliofanikiwa katika maisha ni wale wanaobana pesa yao dhidi ya watu wengine ambao wako tayari kula pesa yako bila kukupatia chochote chenye thamani. Kwahiyo, ndugu wananchi, ni wakati muhafaka sasa wa kuamua kusimamia na kudhibiti kikamilifu matumizi ya pesa yetu hatakama ni kidogo. Kuanzia sasa tujitahidi na tuhakikishe asilimia kubwa ya pesa tunayoipata tuiwekeze vizuri katika miradi yenye kutuhakikishia kipato kisichokuwa na kikomo. 

Tusitishwe wala kuogopeshwa na wale waliojpanga kutuita wabahili. Tunatambua kwamba wale wanaotuita majina ya ubahili, wana malengo ya kutaka kujipatia pesa na utajiri wetu bure bila ya kufanya kazi. Tuhakikishe tunajipanga kutowasikiliza, ili mipango yao ya utunyonya ikwame, ili hatimaye tuibuke washindi na kuishi maisha ya ndoto zetu.

Pengine uwezo wa kusimamia na kudhibiti mapato yako utaupata kwa kuendelea kujifunza kila siku juu ya masuala ya fedha na ujasiriamali. 

Kwahiyo, ukiamua kuwa unajipatia makala mpya kila zikitoka kwenye Blog ya www.maarifashop.blogspot.com, bonyeza KUPATA MAKALA” kisha unaweka E-MAIL yako na hapo utaanza kujipatia makala nzuri za mafunzo moja kwa moja kila zikitoka.


SIRI YA KUINUA UCHUMI WA KAYA NI KUBADILI MTAZAMO WAKO JUU YA PESA

Uchumi wa kaya hautakua iwapo kila mwaka unawazia kupata pesa bila kufikiria utazalisha bidhaa au huduma gani kwenye jamii yako, hasa jamii iliyokuzunguka, uchumi wako hauwezi kukua iwapo wewe kila mwaka unakuwepo kwenye orodha ya kaya za kupata msaada wa chakula kutoka serikalini au kwa wahisani mbalimbali. Unaposikia watu wakisema kuwa uchumi wa nchi fulani ni mkubwa, mfano: Japani, Marekani, China n.k. maana yake ni kwamba watu wa nchi hizo wamechapa kazi sana na kwa kufanya hivyo, wameweza kuzalisha bidhaa nyingi mbalimbali na hivyo kuweza kuvuna (kuchuma) kwa wingi.

Bidhaa yoyote lazima itokane na kazi na bidhaa kama bidhaa ndiyo pesa yenyewe. Mantiki hii inatukumbusha kauli aliyowahi kuitoa Rais wa zamani wa Tanzania Mwalimu Julius K. Nyerere, aliposema “Pesa Siyo Msingi wa Maendeleo” kauli hii ilikuwa ya kifalsafa zaidi, na  watu wengi wakati huo, hawakuielewa kwa mtazamo wa kwamba pesa  yoyote ambayo ni halali ni matokeo ya kazi halali. Badala yake, walio wengi waliipokea kauli hii  kwa uelewa tofauti na sana sana kwa mtazamo “hasi”. Kutokana na watu wengi kuwa na mtazamo hasi juu ya kauli hii ya pesa siyo msingi wa maendeleo, basi Mwalimu Nyerere alichukuliwa na kudhaniwa kuwa miongoni mwa watu ambao hawakupenda watanzania wapate pesa.

Falsafa ya “pesa siyo msingi wa maendeleo” bado inaendelea kupingwa hadi leo hii na kupingwa kwa falsafa hii, kunazidi kudhihilisha uelewa mdogo juu ya pesa. Na hapa ndipo tulipo jikwaa na kuanguka hasa kiuchumi, kwasababu watu wengi tunawaza kupata pesa ndipo tufanye kazi. Kaya nyingi kwa sasa zimetoa kipaumbele kwa shughuli ambazo zinaleta pesa hapo hapo (fasta) na hivyo kujikuta mwaka hadi mwaka wakiwa hawana muda tena wa kufanya vitu vyenye kuleta pesa nyingi baadae na kwa muda mrefu. Mara nyingi miradi yenye kuondoa umaskini kwenye kaya, inahitaji kuvumilia na kuwa tayari kufanya kazi bila kulipwa kwa muda huo huo (malipo baadae).

Hapo zamani wakati watu walipokuwa na mfumo wa biashara wa kubadilishana vitu moja kwa moja (bartering system), uchumi wa kaya ulikuwa imara sana, kwasababu kila mmoja ilibidi afanye kazi ili kupata bidhaa. Wakati huo, kulikuwa hakuna ujanja ujanja na ilikuwa vigumu kwa mtu kumzurumu au kuishi kwa rushwa kwani utaratibu ulikuwa ni kwamba ili upate bidhaa fulani, ulitakiwa uwe na bidhaa ya kwako. Jambo hili lililazimu kila mmoja mwenye uwezo wa kufanya kazi kuwajibika ipasavyo ndio aweze kuishi. Ni bahati mbaya sana baada ya kuingia mfumo wa pesa ambayo ukaa katikati ya muuzaji na mnunuzi wa bidhaa, watu wengi tukasahau, tukaanza kuweka nguvu na fikra nyingi kwenye kutafuta hicho kitu cha katikati “pesa” bila kukumbuka kuwa kitu ambacho huwaleta pamoja watu hawa wawili yaani muuzaji na mnunuzi, huwa siyo “pesa” bali ni BIDHAA.

Mara nyingi mtu anapouza bidhaa anapewa pesa kama uthibitisho wa kukiri kupokea bidhaa hiyo. Matatizo yanaanzia pale huyo mtu anaposahau ndani ya akili yake kuwa bado ile bidhaa anayo mikononi mwake, na cha ajabu, mtu huyo anaanza kuabudu na kuthamini sana ile “pesa” kuliko hata ile bidhaa aliyokuwanayo. Mfano: kama ni mkulima hatafikiria tena kununua mbegu bora au mbolea ili kujipanga kuzalisha mazao mengi zaidi msimu unaofuata. Kitakachotokea ni kwamba mkulima huyo atachukua pesa hizo na kufanyia vitu vingine tofauti na uzalishaji wa mazao, lakini ikumbukwe kuwa hiyo pesa anayotamba nayo ilitokana na kuuza mazao na si vinginevyo. Matokeo yake mkulima huyo, msimu unaofuata  anajikuta hana pesa tena ya kuendesha kilimo chake kwa tija zaidi na hivyo kujikuta akipata mavuno kidogo sana kuliko msimu uliopita!.

Ipo mifano mingi tu ya watu kutokuwa na tabia ya kukumbuka pesa waliyonayo ilitoka wapi na hivyo kujikuta wakitenga kiasi kidogo sana kwaajiri ya kuendeleza miradi hiyo ambayo ndio hasa uwaingizia pesa nyingi. Tunahitaji kutambua kuwa pesa tuliyonayo kuna kitu kinaileta na kwa maana hiyo tuweke nguvu zetu kwenye hicho kitu badala ya pesa yenyewe. Iwapo tutaanza kuiona pesa kwa mtazamo huu, tutakuwa tumepiga hatua kubwa kimaendeleo na kwakufanya hivyo tutakuwa tumejitenga na kundi kubwa la watu wenye mawazo ya wastani  wanaodhani pesa inapatikana kwa bahati! Pia, mtazamo wetu juu ya pesa ukibadilika, tutagudua kuwa huwezi kupata pesa kwa ujanja ujanja. Mambo yote haya yakifanyika, yatafanya uchumi wa kaya na taifa kwa ujumla kuweza kukua kwa kiwango cha kuridhisha. Ewe mtanzania, badili fikra zako juu ya pesa leo, tufanye kazi kwa bidii ili tuzalishe bidhaa na huduma mbalimbali, na kwa njia hii tutawezesha kaya zetu na taifa letu kuinuka kwa maana tutavuna (tutachuma) kwa wingi zaidi. Tukumbuke kuwa dhana nzima ya UCHUMI ni  kuchuma/kuvuna tulichokifanyia kazi” na hili ndilo dhumuni letu katika kupata maisha bora.

 

UNAKUWA MASKINI KADILI UNAVYOCHELEWA KUPATA FEDHA INAYOFUATA BAADA YA KUPATA LEO

Ukifuatilia na kutafakari suala zima la mapato na matumizi ya pesa kwa watu walio wengi, utagundua kuwa kuna tatizo kubwa la msingi. Fikiria mkulima wa Tanzania ambaye amebahatika kuishi maeneo yenye misimu miwili ya mvua wanapata Mazao mara mbili kwa mwaka, hii ikiwa na maana kwamba, anapata fedha mara mbili kwa mwaka, maana yake mtu huyu akipata pesa leo, pesa nyingine itapatikana baada ya miezi sita. Lakini kwa mkulima anayeishi maeneo yenye msimu mmoja wa mvua, wanapata mavuno mara moja kwa mwaka mzima, hii ikimaanisha kuwa huyu mtu anapata pesa mara moja kwa mwaka. Wafanyakazi na hasa wa serikali na makampuni binafsi wana pata fedha kila mwezi. Wafanyabiashara wadogo na wa kati wanapata pesa kwa wiki na wengine kila siku. Wafanyabiashara wakubwa na matajiri wengine wanapata pesa kwa saa, dakika na wengine kama makampuni ya simu wanapata hadi kwa sekunde.

Uzoefu umeonyesha kuwa unapochukua muda mrefu kuingiza pesa nyingine ndivyo unakuwa maskini wa kutupwa na maisha yanakuwa magumu kweli kweli. Sababu kubwa ya umaskini huo ni kutokana na ukweli kwamba mahitaji au matumizi ya mtu yeyote huwa ni kila siku na wakati huo huo mapato ni kwa mwaka au kila baada ya miezi sita kwa Wakulima walio wengi. Kutokana na hali hii tunaona kuwa hakuna ulinganifu ulio sawa kati ya kupata na kutumia pesa. Kupishana kwa mapato na matumizi ndiko kunakofanya watu wengi na hasa Wakulima kuishi Katika madeni makubwa ambapo inapofika msimu wa mavuno Wakulima hawa tayari wanakuwa wanadaiwa, kiasi kwamba inapotokea msimu haukwenda vizuri wengine ulazimika kuuza hata vipande vya ardhi waliyokuwa nayo ili kulipa madeni, wengine huwa hawasubili kuvuna ndipo wauze badala yake wanauza Mazao yao ya yakiwa bado kukomaa shambani.

Katika wilaya za Karagwe, Bukoba na Muleba ambako zao la kahawa linalimwa kwa wingi Wakulima wengi uchukua fedha kama mkopo kutoka kwa wafanyabiashara kabla ya kahawa kukomaa wenyeji wanaita “Butura”. Biashara ya “Butura” ni maarufu sana mkoani Kagera. Watu upewa pesa kabla ya Mazao kukomaa huku wakikubaliana kulipana Mazao pindi yakikomaa. Katika Wilaya ya Ngara wao huuza mahindi yakiwa hata bado kubeba, maeneo ya usukumani suala hili liko sana kwenye zao la mpunga japo wengi uwa wanakopa pesa kutoka kwa wafanyabiashara ili kupata pesa ya palizi na kuhemea ndege“kumoja” n.k.

Kwasababu wanachukua muda mrefu kupata pesa, ndiyo maana wakishapata pesa wanachangamka sana kuzidi kipimo na hii ni kutokana na sababu kuwa mara nyingi wakati wa msimu, pesa uja kwa mkupuo, hali ambayo huwafanya kuzitumia ovyoovyo na wengine ujaribu na kuongeza mke wa pili, kunywa pombe kupindukia, harusi na sherehe nyingi. Kutokana na matumizi ambayo uambatana na mihemuko ya kila aina, watu uweza kuishiwa pesa walizokuwa nazo mara tu baada ya takribani mwezi mmoja hadi miwili.

Baada ya watu kuishiwa pesa zilizotokana na mavuno, watu wengi hurudia hali yao ya kutokuwa na pesa na hapa ndipo, utaanza kusikia lugha za “hakuna mzunguko wa pesa” Eti kila mmoja anaanza kusema pesa hakuna siku siku hizi; Kumbe kiuhalisia siyo kwamba hakuna pesa, isipokuwa ni kwamba hakuna cha kuuza wakati huo. Pesa huwa inafuata vitu vilipo pamoja na huduma zilipo. Hali hii ujenga hofu sana miongoni mwa wanajamii hasa kutoka Katika kaya masikni na pia kukata tamaa. 

Kutokana na hofu na imani kwamba kijjini hakuna pesa, wengi wao na hasa vijana uchukua uamzi wa kukimbilia mijini wanakoamini kuna mzunguko wa pesa wasijue kuwa hata huko wanakoamini kuwa na mzunguko mzuri wa pesa bado utalazimika kuwa na vitu au huduma ndipo uzipate, bila kuwa na vitu/huduma – wewe hata kama uko mjini unakoamini kuwa kuna mzunguko wa pesa, bado pesa utaziona tu kwa wengine na si kwako!!!!.

Kwahiyo kama wewe ni mmoja wa wadau wa maendeleo, njia pekee ya kuwakomboa Wakulima ni pamoja na kutafuta njia ya kufupisha muda wa kupata fedha nyingine angalau ukiweza kushuka kutoka miezi sita mpaka mwezi mmoja. Hikiwa hivi ndivyo, basi itakuwa ni hatua moja muhimu sana Katika kupambana na umaskini hasa Wakulima.
TWENDE KAZI PAMOJA!!

No comments: