Tuesday, March 31, 2015

Anza Safari ya Mafanikio kwa Kuanza Kujitoa Kwenye Kundi la Watu Wenye Mawazo ya Wastani!



Moja ya sababu kubwa inayofanya watu wengi kushindwa kufikia ndoto za maisha wayatakayo ni kuishi kwenye jamii ambayo  imejaa watu wengi wenye mawazo ya Wastani (watu wa kawaida), na watu hawa, kila mara  wanakulazimisha uwe kama wao. Na kosa kubwa unalolifanya au ambalo unatarajia kulifanya ni kuwa kama wao. Madhara ya kuwa kama wao ni kwamba kila mara unapotaka kufanya kitu chochote kikubwa inabidi upate ruhusa au ushauri kutoka kwao, ukifikia hatua hii basi ujue anayepanga uishije ni wao na siyo wewe tena.

Kila unapofikiria kufanya kitu na mara tu ukagundua kiko tofauti na wenzako, ghafla utapata washauri huria, ambao hawakuwahi kuwazia au kufanya hicho kitu unachopanga kufanya. Watu hawa watakwambia, hicho kitu hakijawahi kutokea na wewe utawezaje? Eti mtu anakwambia husifanye jambo fulani kwasababu hakuna aliyewahi kufanya hivyo. Mtu wa namna hii msikilize mpaka mwisho akimaliza muage na uondoke na kuanzia hapo punguza mazoea naye. Kadili utakavyopunguza mahusiano/mazoe na watu hasa wenye mawazo ya Wastani na hasi, ndivyo maisha yako yatakavyoanza kuboreka.

Jiulize ni mara ngapi umetamani kufanya biashara lakini umeshindwa kwasababu watu wengi unaowajua walifanya biashara wakashindwa? Kwahiyo, na wewe unaogopa hasara! Mara nyingi woga unaoupata unatokana na kuzungukwa na watu wengi wenye mawazo ya Wastani (mawazo yanayofanana) na wengi wao hufanya vitu vinavyofanana. Endapo huko katika hali hii ni wazi kwamba, kila utakapo kuwa na ndoto ya kuwa na maisha ya tofauti na hao rafiki zako waliokuzunguka, utapata majibu ya wewe huwezi!, wakishakwambia hivyo, basi na wewe unapata hofu ya kushindwa ambayo huzaa woga na mwisho unashindwa kuthubutu. Unapaswa kufahamu kuwa unapokutana na mtu na ukamshirikisha ndoto yako akakwambia uwezi basi ujue yeye kwa nafsi yake ndiye hawezi, hivyo jibu lake usilichukulie kama ndiyo jibu lako na usitumie majibu yake kufanya maamuzi ya wewe kutokuanza kufanya mambo yanayokupeleka kwenye ndoto ya maisha uyatakayo.

Watu wengi wanakwama kutimiza ndoto zao kwasababu, walio wengi wanapenda kutazamia majibu kutoka kwa wengine, huku wakisahau kuwa kila mmoja katika safari ya maisha anakuwa na mtihani wenye maswali tofauti na ya mwingine. Kwahiyo, unapojaribu kutumia majibu ya maswali ya mwingine kujibia maswali yako, basi ujue kuwa utashindwa tu! Cha muhimu hapa ni kwamba tujitambue kuanzia leo kuwa kila mmoja ana maswali yake binafsi na mwenye uwezo na ujuzi kuyapa majibu ya kweli ni wewe mwenyewe.

Kumbuka kuwa, ili mafanikio yoyote yapatikane, yanaanza na fikra ambapo unahitaji kuanza kujifikilia na kujiona wewe mwenyewe kama mafanikio. Kinachotakiwa ni wewe kufikiri na kutenda kimyakimya bila kujali wengine wanakuonaje na mafanikio yakipatikana yatapiga kelele ambazo kila mmoja atazisikia. Ukishafanikiwa, watu wataanza kushangaa na wengi watadhani umefanikiwa siku hiyo, kumbe safari ulianza siku nyingi lakini kwasababu ulikuwa unatekeleza ndoto yako Ndiyo maana walikuwa hawakuoni.

Kazi yako kubwa leo, ni wewe kuacha kuwa mfungwa wa kundi hili la watu wenye mawazo ya wastani, na utambue kuwa kulifanikisha hili, unahitaji kufanya maamuzi magumu na kuwa jasiri. Fanya vitu ambavyo ni muhimu kwako siyo kwasababu kila mmoja anavifanya, na huu ndiyo utakuwa mwanzo wa safari yako kuelekea kwenye mafanikio makubwa. Ili uweze kufanya mambo ambayo ni muhimu kwako ni vizuri ukaongozwa na imani ya vitu viwili ambavyo ni: maisha yatakuwa mazuri wakati ujao kuliko sasa na mimi nina uwezo na nguvu wa kuweza kufikia maisha mazuri!

Mpendwa msomaji, endelea kuitumia vizuri MAARIFASHOP ili kujifunza mambo mbalimbali yatakayokuwezesha kupata mafanikio. Ili kupata makala mpya kila zinapochapishwa, bonyeza neno TUMA MAKALA MAARIFASHOP kisha sajiri barua pepe yako. Na kama unapenda kupata mafunzo ya kila siku kwa njia ya whatsap bonyeza neno MAFUNZO

Friday, March 27, 2015

Je? Unajua Kuwa Ukiwa Capitalist (Bepari) ni Sifa na Heshima Kubwa?



Katika makala hii, nimetumia maneno mawili yaani CAPITALIST na CAPITAL kama yalivyo katika lugha ya kinngereza, lengo likiwa ni kutaka kueleweka vizuri na kurahisisha uchambuzi wangu juu ya chuki iliyojengeka kwa mtu anayeitwa “Bepari” hapa Tanzania. 

Katika nchi ya Tanzania ambayo iliwahi kuendesha siasa na uchumi wake kwa kufuata sera za mlengo wa kijamaa (socialism), ukiambiwa wewe ni “capitalist au bepari  mkubwa”  kama huna roho ya uvumilivu unaweza kuhisi umetukanwa, umedhalilishwa na wakati mwingine kuona kama umekashifiwa (kashifa), eti tu kuitwa bepari!. Hii yote ni kwasababu mapokeo yetu kuhusu mtu ambaye ni capitalist , yamekuwa ni hasi kiasi cha kuambiwa kuwa mtu wa namna hiyo ni mnyonyaji, mwizi, mwenye roho ya kinyama na majina mengine mabaya unayoyajua hapa duniani. Ukijaribu kuongea na baadhi ya watu hapa kwetu Tanzania, utakuta wapo watu wanaopenda kujisifu! Eti wao ni watu safi kwa kigezo tu! cha kutokuwa ma-capitalist, jambo hili linashangaza sana.

Ukichukulia tafsiri ya kawaida,  ni kwamba capitalist ni mtu ambaye ni "Bepari". Ili kuelewa vizuri maana pana ya mtu ambaye ni capitalist ni vizuri kuelewa kuwa neno hili chimbuko lake ni neno “capital” lenye maana ya” mtaji”. Kwahiyo, capital ni kitu chochote kinachotumika kuzalisha vitu au Huduma na hivyo tunaweza kusema kuwa mifano ya capital ni kama vile  trekta, mashine za kusaga, cherehani, ardhi, pesa taslim, nguvu kazi n.k.

Hatahivyo, wakati mwingine ni vigumu kuzalisha vitu au Huduma Fulani Fulani kwa kutumia aina moja ya capital. Kwa mfano: Iwapo mjasiriamali akiamua kuzalisha mahindi na baadae unga, yawezekana mtu huyu akahitaji kuchanganya aina ya mtaji zaidi mmoja (ardhi, mashine ya kusaga na kukoboa, nguvu-kazi, pesa taslimu n.k). Katika kuchanganya aina tofauti za mitaji pamoja na vitu vingine vinavyohitajika kufikia kupata unga wa mahindi, ndipo vitu vyote hivyo uwekwa katika mpangilio maalumu kuanzia jinsi mahindi yatakavyolimwa,yatakavyosindikwa na jinsi unga utakavyo uzwa kwa wateja. Mpangilio huu maalumu Ndio baadae huleta kitu kinachoitwa “mfumo wa kuingiza na kutoa pesa taslim (system of cash flow). Kwahiyo, mtu yeyote anayemiliki na kuhakikisha “mfumo” unafanya kazi kwa kiwango cha juu mpaka kufikia kuzalisha bidhaa iliyokusudiwa (k.m. Unga) na hatimaye kuuzwa na kupata pesa si mwingine bali ni "CAPITALIST (BEPARI)".

Hivyo basi, itoshe kusema kuwa, iwapo watanzania wakianza kuwekeza na hatimaye  kumiliki mfumo wa uzalishaji bidhaa na huduma (pesa), ni wazi kwamba watakaofanya hivyo, watakuwa watu wenye kuheshimika sana. Mtu ambaye ni capitalist hapa Tanzania ataheshimika sana kwasababu, ni capitalist huyohuyo, ndiye serikali inamtegemea kupata kodi mbalimbali kwaajili ya kuendesha na kughalimikia Huduma mbalimbali za kijamii kama vile matibabu, elimu, barabara, maji, pembejeo za kilimo n.k. 

Kwa sasa ni vyema ukafurahi pindi unapoitwa “capitalist” kwasababu kwakuwa mtu wa namna hiyo, tayari unakuwa umesaidia familia nyingi kupata ajira na Mahitaji mengine mengi. Tofauti na zamani ambapo tulifundishwa shuleni kuwa ubepari ni WIZI na kwa kufanya hivyo walimu wetu hawakujua kuwa walikuwa wanaua kabisa  fikra za kijasiriamali na vipaji tulivyopewa na mwenyezi Mungu. Ili kurudisha vipaji na fikra za kijasiriamali, ni vyema watanzania tukaanza kuchukua hatua na jitihada za dhati kabisa, ikiwa ni pamoja na kusoma sana vitabu, kujifunza kila siku kutoka kwa waliofanikiwa na kuthubutu bila kuogopa changamoto zinazoweza kujtokeza mbele ya safari ya mafanikio.

Mpendwa msomaji, endelea kuitumia vizuri MAARIFASHOP ili kujifunza mambo mbalimbali yatakayokuwezesha kupata mafanikio makubwa. Ili kupata makala mpya kila zinapochapishwa, bonyeza neno TUMA MAKALA MAARIFASHOP kisha sajiri barua pepe yako. Na kama unapenda kupata mafunzo ya kila siku kwa njia ya whatsap bonyeza neno MAFUNZO

Monday, March 23, 2015

Suruhisho Pekee la Kuweza Kupata Mafanikio Makubwa kwa Kila Jambo Unalofanya ni Kufanya Vitu Vichache Ambavyo ni Muhimu



Kwa sasa, watu wengi duniani wanakabiliwa na tatizo la msongo wa mawazo katika maisha, sababu mojawapo ikiwa ni pamoja na tabia ya kuendekeza kufanya kila kitu kila wakati. Tabia hii inatokana na hulka ya walio wengi kutaka kila mara kufanya kazi ili kumfurahisha na kumridhisha kila mtu, jambo ambalo limekuwa likichangia kwa kiasi kikubwa katika kupunguza sana ufanisi na ubora wa kazi tunazofanya kila siku na hivyo kutumbukia katika umaskini. Endapo una tabia ya kufanya kazi kwa kumridhisha mtu ni rahisi sana kuwa “mbabaishaji”; kwasababu kila kazi yenye kuhitaji uharaka, utarundikiwa wewe na ukiweza utapewa motisha au posho nyingi. Mwisho wake ile nguvu yako unaitawanya kidogo kidogo katika kukamilisha kazi zote zinazokujia. Ukiwekeza kidogo kidogo kwa kazi nyingi zitakazokujia, mwisho utapata matokeo ya kiwango cha chini sana! Na huu utakuwa mwanzo wa wewe kuitwa “mbabaishaji. 

Tabia ya kutaka kufanya kila kitu, inatokana mafundisho tokea utotoni, ambapo uhamasishwa kusema “NDIYO” kwa kila jambo. Kumbe ni muhimu tangu mwanzo watoto wetu tuwafundishe kusema "HAPANA" na siyo kuwapongeza kila mara kwa kusema "NDIYO" peke yake. Mara nyingi hata watu wazima, unapofanya kazi ukapongezwa anavutiwa na kuhamasika sana na hivyo kuingia kwenye mtego wa kutaka ufanye na kumaliza kila kazi iliyopo mbele yako. Kutokana na tabia hiyo ya kuvutiwa na pongezi unajikuta kila kazi unaikubali hata kama ulikuwa unafanya kazi nyingine za muhimu. Kwahiyo, ni vizuri ujifunze tabia ya wachapakazi hodari ambapo wao uhamini sana falsafa ya “kidogo lakini kizuri” (Less but Better).

Watalamu wanatwambia kuwa ili mtu aweze kufanya kazi kwa kiwango cha juu, ni lazima ajifunze au tujifunze na tuache tabia ya kufanya shughuli nyingi tena ndogo ndogo. Kwani, hii Ndiyo sababu watu wengi anaposhirikishwa fursa Fulani Fulani za Biashara mara nyingi hutoa visingizio vya kuwa hawana muda (busy) au utasikia mtu anakwambia nina mambo mengi sana. Kwa watu walio wengi, hili la kuwa na kazi au mambo mengi sana wanalichukulia kama ni sifa ya uchapakazi na uwajibikaji hodari. Kwahiyo, wanatumia U-Busy kama kipimo cha utendaji bora wa kazi hata kama vitu wanavyofanya havina tija.

Watu waliopata mafanikio makubwa kwa njia halali, mara nyingi wanashauri kwamba, mafanikio makubwa yanahitaji sisi kuwekeza katika vitu vichache ambavyo inakuwa rahisi kuweza kuvipa muda wa kutosha na kuvifanya kwa ufanisi mkubwa. Na katika kulitekeleza hilo, wanatuhasa pia, tuanze mara moja kujijengea utamaduni wa kuweka vipaumbele katika maisha, kwani tusipo fanya hivyo, mtu mwingine atatuwekea vipaumbele ambavyo tutapoteza muda wetu kutekeleza vipaumbele hivyo ambavyo hatuvipendi.

Mara nyingi unapokabiliwa na suala zima la kutekeleza vipaumbele vya watu wengine ni wazi kwamba utafanya kazi hiyo huku ukiwa huipendi na kama huna mapenzi ya dhati kwa hicho unachokifanya basi itakupelekea kufanya kazi hiyo chini ya kiwango. Na iwapo utaendelea kufanya kazi zako chini ya kiwango ni lazima uwe maskini, kwasababu kwa muda mrefu ambao utafanya kazi chini ya kiwango ndani mwako itajengeka tabia ya uvivu hasa ule wa kufikiri. Ukiwa na uvivu wa kufikiri, huwezi kuwa mbunifu na matokeo yake mbinu zako za kupambana na changamoto za maisha zinakuwa zimepitwa na wakati. Kwahiyo, safari yako ya kuelekea umaskini wa kutupa inakuwa imeanza hapo. Ewe mtanzania jitahidi kuwa mjasiri, ili uweze kufanya maamuzi magumu juu ya vitu vichache ambavyo ukiwekeza nguvu zako zote utaweza kufikia haraka maisha ya ndoto yako.

Mpendwa msomaji, endelea kuitumia vizuri MAARIFASHOP ili kujifunza mambo mbalimbali yatakayokuwezesha kupata mafanikio. Ili kupata makala mpya kila zinapochapishwa, bonyeza neno TUMA MAKALA MAARIFASHOP kisha sajiri barua pepe yako. Na kama unapenda kupata mafunzo ya kila siku kwa njia ya whatsap bonyeza neno MAFUNZO

KARIBU TWENDE KAZI PAMOJA

Tuesday, March 17, 2015

Siri ya Waliofanikiwa ni Kuwekeza Kwao Zaidi Kwenye Aina ya Mapato Yasiyokuwa na Kikomo (Tuli)




Unapoanza safari yako kuelekea kwenye mafanikio makubwa ni vizuri ukafahamu ni aina gani ya kipato unachopata kwa sasa? Kwahiyo, ili kuweza kufahamu sifa na aina za vipato, ni muhimu kujua kuwa zipo aina kuu tatu za vipato ambazo ni: Mapato ya Ajira (mshahara); Mapato Hai (kujiajiri); Mapato yasiyo na kikomo au Tuli, (Passive Income).
1.      Mapato ya Ajira (Earned Income)
Haya ni mapato yanayotokana na kufanya kazi ya kuajiriwa (mshahara), ambayo mtu huyapata kutokana na ajira yake. Katika aina hii ya kipato, vigezo vya kukuwezesha ulipwe ni pamoja na aina ya kazi na wadhifa au cheo chako. Pia, mapato haya yanajumuisha mapato yoyote yatokanayo na ajira binafsi (kujiajiri), biashara ndogondogo na shughuli nyinginezo ambazo unapata kipato kutokana na juhudi na muda uliotumika. Kwa maana nyingine, ni kwamba kama husiposhugulika au ukasimama kufanya kazi na kipato kinakoma pale pale.
Ø  Uzuri wa Mapato ya Ajira
·         Mapato yanaongezeka zaidi kulingana na muda na ukubwa wa shughuli inayofanya
·         Hauitaji mtaji kuweza kupata mapato haya
·         Mtaji ni nguvu au ujuzi wako mwenyewe
Ø  Ubaya wa Mapato ya Ajira
·         Uwezi kupata utajiri wa kudumu kwa aina hii ya mapato yanayotokana na mshahara. Kwasababu mshahara unapata, unakula na unanaisha.......Unapata unakula zinaisha.....
·         Siyo mapato endelevu, ukiacha kufanya kazi mapato yanakoma.
·         Mapato haya ya ajira yanatozwa kodi kubwa kuliko aina nyingine zote za mapato na Waajiriwa wanalijua vizuri hili.
Mfano; kwa mtu anayelipwa mshahara wa kiasi cha 1,350,000/- anakatwa kodi hivi:
Aina ya Makato
Kiasi (TSh)/Mwezi
Kodi (Income Tax)
260,400.00
Bima ya Afya
40,500.00
Chama cha Wafanyakazi
27,000.00
Mfuko wa Pensheni
67,500.00
Jumla
394,900.00
Sasa, ebu fikiria mtu anakatwa karibu Shilingi 400,000/- kila mwezi, kiasi ambacho kwa mwaka kinafikia karibu shilling 4,800,000/-. Unaweza kukuta mtu ana biashara yenye mtaji upatao shilingi million 15, siajabu kukuta analipa kodi kiasi kisichozidi shilingi 500,000/- kwa mwaka.
2.      Mapato Hai (Active Income)
Aina hii ya mapato, kwa kiasi fulani inafanana na mapato ya ajira yanayo jumuisha mishahara, kwani mapato haya yanatokana na kuuza na kununua bidhaa kubwa kubwa kama magari, nyumba, kiwanja n.k. Mchakato huu ni kwamba, unanunua kitu halafu unakiuza kwa faida, halafu basi. Ili uweze kupata mapato mengine inakubidi, utafute kitu kingine au ununue kitu kingine haraka ndipo upate tena pesa. Maana yake ni kwamba lazima uwe kazini (active) muda wote huku ukiendelea kuchakarika ndipo upate mapato. Kama ilivyo kwa mapato ya mshahara, pindi unapoacha kununua na kuuza vitu, mapato nayo yanakoma mara moja.
Ø  Uzuri wa Mapato Hai
·         Mapato haya hayahitaji watendaji kazi wengi ili kufanikisha shughuli ni wewe tu mwenyewe. 
·         Kodi yake ni ndogo kulinganisha na ile ya mapato ya ajira
·         Unapata zaidi kutokana na jitihada zako za kutafuta na uchangamkia fursa.
·         Unaweza kufanya na kupata pesa hata pasipokuwa na mtaji. Mfano, unachukua mali (sema gari), Unamwambia jamaa utamletea pesa yake baada ya siku mbili hivi, kumbe wakati huo umeisha tafuta mteja tayari unampelekea, unauza unamlipa jamaa wewe unabaki na faida. Tayari umeisha tengeneza pesa bila hata kuwa na mtaji ~ yaani ni ujanja ujanja tu!
Ø  Ubaya Wake
·         Inahitaji utaalam na ujanja wa hali ya juu na kufahamika pia, unaweza kupewa vitu feki, kuzurumiwa, kuibiwa, kupata hasara n.k.
·         Unaendelea kushughulika wewe mwenyewe ndipo unapata faida
·         Unaweza kupata hasara kutokana na kubadilika kwa hali ya mambo juu ya bidhaa husika. Mfano: mitindo/fasheni, msimu, bei n.k.
3.      Mapato Yasiyo na Kikomo (residual or passive income).
Ni mapato mtu anayoyapata pasipokuwa na ulazima wa kushughulika/kufanya kazi kwa wakati huo au kwa maana nyingine ni mapato “Tuli”. Mapato haya mara nyingi yanatokana na kazi au shughuli uliyokwisha kufanya kitambo na kuendelea kupata mapato haya “Kimya Kimya”. Unayapata kutokana na vitega uchumi ulivyoweka. Mfano: kama umenunua nyumba na kupangisha na kila mwisho wa mwezi unapewa kodi ya pango, basi mapato hayo ndiyo yanaitwa yasiyo na kikomo au TULI.
Unashughulika mara moja tu na kisha unaendelea kupata pesa kwa muda mrefu bila hata wewe mwenyewe kushughulika tena/ zaidi. Pia mapato yatokanayo na Mtandao,  nakala za albamu ya muziki, filamu au vitabu n.k. ni hayana kikomo. Unaendelea kutoa nakala na kuuza miaka na miaka.
Ø  Uzuri MapatoYasiyo na Kikomo (Tuli).
·         Unaendelea kupata pesa kwa muda mrefu baada ya kazi/shughuli ya awali
·          Unakuwa na MUDA  wa ziada kufanya mambo mengine. Unabaki  kucheza gofu na kutalii huku pesa zinaingia
·         Hayatozwi kodi kubwa kama mapato ya aina nyingine.
Ø  Ubaya wa MapatoYasiyo na Kikomo (Tuli)
·         Wakati mwingine hugharimu sana kuwekeza katika hatua ya awali.
·         Huitaji uvumilivu (patience) kwani yaweza kuchukua muda mrefu kabla ya kuanza kupata mapato haya. “Lakini Yakianza Kuingia Unatumia Hadi Unasahau”.
Hizi ndizo aina kuu tatu za mapato yatokanayo na shughuli mbalimbali katika maeneo makuu manne ya mafanikio ya kifedha - Biashara, sanaa, michezo, uvumbuzi wa kisayansi au teknolojia, utunzi wa vitabu pamoja na kujenga mtandao (Network Marketing Business). Kwahiyo, kama una ndoto ya kupata mafanikio makubwa kimaisha, unashauriwa kufanya shughuli zinazopelekea kupata mapato “Tuli”.
Hii ni kutokana na ukweli kwamba mapato Tuli, ndiyo mapato pekee ambayo ni imara, endelevu na yanarithika. Sababu nyingine inayotufanya tukushauri kupata mapato haya ni kwamba, watu wengi waliofanikiwa (matajiri) duniani, wamejipanga na kujikita katika kupata mapato haya. Ili kuendelea kujielimisha zaidi juu ya undani wa mapato haya - "tuli", kupitia mtandao wako wa maarifashop, tutaendelea kukuletea mafunzo juu ya aina hii ya mapato, ili hatimaye kila mmoja wetu aweze kuchukua hatua za maksudi tayari kuelekea kwenye maisha ya ndoto zetu.

Mpendwa msomaji, endelea kuitumia vizuri MAARIFASHOP ili kujifunza mambo mbalimbali yatakayokuwezesha kupata mafanikio. Ili kupata makala mpya kila zinapochapishwa, bonyeza neno TUMA MAKALA MAARIFASHOP kisha sajiri barua pepe yako. Na kama unapenda kupata mafunzo ya kila siku kwa njia ya whatsap bonyeza neno MAFUNZO

~TWENDE KAZI PAMOJA~!