Katika mchakato wa kutafuta utajiri kuna dhamira kuu mbili zinazotuchochea kufanya kila tunachokifanya, ili kutimiza ndoto ya kutajirika. Dhamira ya kwanza ni ile mtu anapolenga kuonekana tajiri machoni mwa watu wengine na dhamira ya pili ni“Dawa ya kutibu ugonjwa wa kujiona tajiri ni kuweka ndoto ya maisha mazuri unayoyataka kwa maandishi” ~ Cypridion Mushongi
ile mtu anapolenga kuwa tajiri bila kujali wale wanaomtazama au wanaomzunguka.
Uzoefu wangu umeonyesha kuwa, watu wengi ni maskini kwasababu ya kupenda sana kufanya vitu ambavyo vinawafanya waonekane matajiri. Matokeo yake wanawekeza muda wao mwingi kwenye vitu vyenye kuleta mafanikio ya muda mfupi au ambayo siyo endelevu, ilimradi watu wengine wanafurahi na kuwapa sifa zote za tajiri.
Waajiriwa wengi tumejengwa na kuishi katika mazingira ambayo mara nyingi yanawafanya watu wanaotuzunguka kutuona kuwa sisi ni matajiri. Wakati mwingine, mazingira haya haya ya ajira yanatufanya hata sisi wenyewe kujiona ni matajiri. Hali hii ya kuonwa au kujiona tajiri, ndiyo imetufanya tubweteke na hivyo kujikuta tukipunguza kasi ya kukuza na kuendeleza utajiri ambao ni haki yetu ya msingi.
Ukweli ni kwamba, binadamu tunaishi katika ulimwengu wa vitu viwili viwili: Mfano: katika fani ya umeme kuna hasi na chanya; katika jinsia kuna mwanamke na mwanaume; shuleni kuna kufauru na kushindwa mtihani; katika vita kuna kusonga mbele na kurudi nyuma; katika hesabu kuna kujumlisha na kutoa n.k.
Katika maisha napo kuna watu wawili yaani “tajiri na maskini”. Lakini kwasababu tu ya watu kupenda kuzifurahisha na kuziridhisha nafsi zao, wameamua kwenda kinyume na sheria na kanuni ya asili kwa kuweka mtu wa tatu yaani “tajiri, tabaka la kati na maskini”.
Waajiriwa wengi tupo zaidi kwenye kundi linaloitwa tabaka la kati. Tabaka hili kwa asilimia kubwa linaundwa na wasomi, ambao mara nyingi ujitahidi kufanya vitu vinavyowafanya kuendelea kubaki katika tabaka la kati. Ndiyo maana, muda mwingi upenda kufanya vitu vinavyofanana na vya wenzao hata kama siyo malengo yao. Kwa maana nyingine, hawafanyi vitu kutokana na dhamira zao za ndani bali wanasukumwa zaidi na matukio ya nje ambayo kimsingi ni ndoto za watu wengine.
Imekuwa ni kawaida kusikia mwajiriwa akilalamika na kujisemea moyoni kuwa “watu wote wamejenga nyumba nimebaki mimi tu!” au “watu wengi niliosoma nao wana pesa nimebaki mimi”.
Sasa ukijiuliza mtu anafikia hatua ya kusema hivyo maana yake ni kwamba hajui kwamba hao anao waona wamefanikiwa wamesukumwa na ndoto na dhamira zao, wakafanya jitihada mpaka wakafikia hapo walipo. Akiri inamtuma kwamba walikuwa wapo wamekaa kama yeye halafu imetokea ghafla wamemzidi!
Waajiriwa tunahitaji kutambua kuwa hili linaloitwa tabaka la kati ni nafasi na fursa nzuri ya kuweza kuvuka mstari kwenda kwenye utajiri. Lakini kwasababu tukishaingia ndani ya tabaka hili, nguvu yetu kubwa tunaiwekeza katika namna ambayo inatufanya tuzidi kubaki katika kundi hili. Matokeo yake, ukistaafu ajira inakuchukua karibu miaka mitatu hivi kuendelea kubaki katika tabaka hili la kati, ambapo baada ya hapo unarudi kule ulikotoka mwanzoni kabla ya kupata ajira —“unarudi tena kwenye kundi la watu maskini”
Tulio kwenye ajira tufahamu kuwa tayari tumeingia tabaka la kati kuelekea kwenye utajiri. Ni muhimu tukaendelea kukaza kamba, ili tuvuke mstari wa kutoka kwenye umaskini kwenda kwenye utajiri. Kosa kubwa tunaloendelea kulifanya ni kufikiri tumetajirika eti! kwasababu watu wengi hasa maskini wanatuona na kutwambia kuwa sisi ni matajiri. Nasema mwajiriwa popote ulipo, hujawa tajiri japo unayo nafasi kubwa ya kuwa tajiri kama ukiamua.
Kwanini waajiriwa wengi tunajiona matajiri japo siyo matajiri?
Ukichunguza kwa makini utagudua kuwa kuna vitu waajiriwa tunafanya ambavyo vinatufanya tuonekane matajiri. Vitu hivi vimekuwa ni mojawapo ya sababu kubwa ya sisi kushindwa kuwa matajiri. Kwa mfano; mwajiriwa anapojenga nyumba yake ya kuishi, akanunua gari la kutembelea, akasomesha watoto shule za “english medium” akawa na shamba n.k. basi!
Baada ya hapo kila pesa inayopatikana inakuwa ni kwaajiri ya kuendeleza vitu hivyo pamoja na kwamba haviingizi pesa yoyote mfukoni. Ikitokea pesa ikabaki baada ya kuendeleza vitu hivyo, inachukuliwa kama pesa ya ziada na mara nyingi utumika zaidi kwenye kufanikisha matukio ya kifamilia na kijamii. Tukio likiisha na pesa inaisha na inafikia wakati unakuwa mtu wa kutafuta pesa kwasababu tu ya tukio fulani basi _ hii ni hatari!
SOMA; Umuhimu wa Kutafuta Pesa Bila Sababu ni Huu
Ukweli ni kwamba mambo ya kujenga, kupeleka watoto shule nzuri, kununua gari n.k. ni vitu ambavyo pia ufanywa na matajiri. Kwa maana hiyo, mtu ukishaona umekamilisha baadhi ya vitu hivyo vinavyofanywa na matajiri, basi wewe unaona umefika na unatulia huku ukizidi kujiona tajiri tayari. Hii ndiyo kusema kwamba unaonekana tajiri mbele ya macho ya watu wengine japo katika uhalisia wewe siyo tajiri.
Je? Nitajuaje kama mimi ni tajiri?
Nirahisi sana kujipima wewe mwenyewe binafsi na ukagundua hali halisi ya kiwango cha utajiri ulionao. Njia rahisi ni kujiuliza maswali na kuyapatia majibu wewe mwenyewe. Majibu hayo usimwambie mtu yeyote kwasababu, hilo ni suala lako binafsi.
Ninaamini baada ya kupata majibu ya maswali haya hapa chini, utachukua hatua za makusudi, kwasababu uwenda majibu yakatoa hali halisi juu ya mwenendo wa maisha yako.
- Leo hii likitokea tetemeko la ardhi nyumba yako ya kuishi ikaanguka unaweza kuijenga upya kwa muda gani bila kuhitaji msaada?
- Nikifukuzwa ajira, watoto wangu wanaweza kuendelea kusoma shule nzuri?
- Je? Ninaweza kuishi kwa miezi mitatu bila kupokea mshahara?
- Je? Familia yangu inaweza kuendelea kuishi maisha inayoishi sasa endapo nikifa kesho?
- Endapo nikiacha kufanya kazi pesa niliyonayo inaweza kuisha baada ya muda gani?
Lazima suala la kutafuta utajiri litokane na dhamira na msukumo wa ndani ya mtu mwenyewe, kuliko maneno ya sifa ambayo usemwa mara nyingi na watu wanaokuzunguka.
Kumbuka kuwa watu wengine wanapotuona kuwa sisi ni matajiri inawezekana wanajilinganisha na hali duni waliyonayo. Kwahiyo, si busara hata kidogo kuwasikiriza wanachokwambia. Inakubidi wewe uwajibike kwa ndoto yako basi! Masuala ya kusifiwa, kupongezwa uyachukulie kama vikolezo katika safari yako ya maisha uyatakayo.
Katika mazingira ambayo huna ndoto ya maisha mazuri, mara nyingi ni rahisi sana kusikiliza na kuamini mengi yanayosemwa mtaani juu yako, hata kama ni tofauti na uhalisia wa mambo.
Unahitaji kuona utajiri kupitia ndoto yako ya maisha mazuri unayoyataka badala ya kujiona tajiri kupitia macho ya watu wengine. Kama unaendelea kujiona tajiri kupitia watu wengine basi jua kwamba utajiri wako siyo halisi na yawezekana ni utajiri wa bandia –kuwa mwangalifu sana!
Dawa ya kututibu “ugonjwa wa kujiona tajiri” ni kuandika kwa maandishi ndoto ya maisha mazuri tunayotaka. Ndoto ya maisha mazuri, itakufanya kuwa na dira au ramani ya mambo yote unayotakiwa kuyafanya, ili kuwa na maisha mazuri ambayo ni pamoja na uhuru wa kipato au fedha.
Ndoto ya maisha mazuri, itakufanya kuachana na tabia ya kufanya vitu vya kuiga au kutazamia. Ndoto yako iliyo katika maandishi, inakusaidia usipumbazwe na sifa na maoni juu yako kutoka kwa watu wengine, kwasababu ndani ya fikra zako unakuwa na kiongozi ambaye ni ndoto yako ya maisha mazuri.
Ukiwa na ndoto kiongozi kwenye safari yako ya kuwa tajiri, hautajali yanayosemwa juu yako bali utaendelea kuvumilia hata kama ndoto yako ya utajiri itatimia baada ya miaka 10 ijayo.
Kwa maoni na ushauri jiunge na mtandao huu kwa kubonyeza neno “MAARIFA SHOP”
No comments:
Post a Comment