Wednesday, May 11, 2016

Ukweli Kuhusu Mwekezaji ni Huu


“Usitegemee kipato kutoka kwenye chanzo kimoja peke yake BALI wekeza ili kutengeneza chanzo cha pili” ~ Warren Buffet
 
Bilashaka wewe unayesoma makala hii, umesikia mara nyingi maneno kama “uwekezaji, mwekezaji n.k. Pengine niseme kuwa, kwa nchi kama Tanzania ambayo iliwahi kuongoza na kuendesha siasa zake pamoja na uchumi wake kwa kufuata falsafa na kanuni za mifumo ya ujamaa na hata ukomunisti, neno “uwekezaji na wawekezaji” ni vitu ambavyo ni vigeni na vinachukuliwa kuwa ni kazi ambazo ni maalum kwa wazungu!. Watanzania wengi bado hawaamini kama mtanzania tena ambaye ni
mweusi anaweza kuwa mwekezaji”.

Unaposikia kuwa mtu fulani ni mwekezaji, mara moja akiri yako inakutuma kuwa huyo lazima atakuwa ni mtu mkubwa sana mwenye majumba, viwanja, viwanda, magari, pesa nyingi n.k. Pengine inawezekana picha uliyonayo kichwani mwako kuhusu mwekezaji ndiyo imekufanya uogope kuwa mwekezaji.

Sasa swali linakuja huyu mtu anayeitwa mwekezaji ni nani? Unaweza ukashangaa jinsi jibu lake lilivyo rahisi. Watu wengi huwa wanajiweka mbali na uwekezaji kutokana na sababu kwamba uwekezaji ni kitu ambacho ni kigumu sana na kinahitaji mchakato mrefu sana au wanafikiria kuwa, ili kuwa mwekezaji ni lazima uwe na pesa nyingi.

Njia rahisi ya kuelezea dhana nzima ya uwekezaji ni kama vile; kununua kitu kwa matumaini kwamba ukikiuza utapata pesa zaidi ya ile uliyonunulia. Mfano halisi mwingine ni kumfikiria mkulima anavyofanya shughuli zake za uzalishaji.

Tuseme kwamba mkulima amenunua mbegu ya mahindi na kuzipanda kwa matumaini ya kwamba muda mfupi mbegu moja tu itampatia punje nyingi za mahindi. Kwa maana nyingine ni kwamba; tayari mkulima huyu atakuwa na zaidi ya kile alichokipanda ardhini.

Kwahiyo, inatosha kusema kwamba mkulima ni “MWEKEZAJI”.

Mfano wa kilimo cha mahindi hapo juu unaweza kulinganishwa na ununuaji wa hisa, ambao nao unaweza kuelezeka vile vile kama kitendo cha mkulima anayepanda mbegu moja kwa matumaini ya kupata mbegu nyingi zaidi ya kile alichopanda. Kama wewe ni mwekezaji, unatenga pesa kununua hisa kwenye kampuni fulani kwa matarajio ya kupata faida au pesa zaidi ya hizo ulizotumia.

Kiukweli ni kwamba, “uwekezaji siyo mchezo wa kamali au kubahatisha”. Kwasababu, kamali ni kile kitendo cha kuweka pesa katika hatari ya kubahatisha matokeo yasiyojulikana na ambayo hayatabiriki kwa matumaini kuwa utaweza kapata pesa zaidi. Sehemu ya mkanganyiko huu kati ya uwekezaji na kamali (bahati na sibu), unaweza kutokana na jinsi ambavyo watu wengi wanavyotumia pesa zao kuwekeza. Wengi tumekuwa na tabia ya kuwekeza kwenye miradi ambayo tumesikia na kuona juu juu eti! Inalipa sana!

Kwa mfano: unaweza kusema kwamba mtu anayefanya maamuzi ya kununua hisa kwa kutumia tu maneno aliyosikia mitaani, kimsingi ni sawa na kutumia pesa yako kucheza kamali au bahati na sibu kwenye kumbi za starehe. Mwekezaji wa kweli na ambaye ni makini, huwa hatupi tu pesa yake kwenye mradi wowote unaopita mbele yake.

Kujifunza na kubobea kwa maana ya kuzijua na kuzielewa vizuri kanuni za uwekezaji inachukua muda au inahitaji uwekezaji wa muda mrefu kwenye elimu juu ya mambo ya fedha na uwekezaji.

Kufahamu na kuelewa vizuri mambo yote ya msingi juu ya uwekezaji, itakuwezesha wewe kuanza uwekezaji bila woga. Unaelekea wapi baada ya hapo ni juu yako. Hii ina maana ya kwamba; aina ya mwekezaji na kiwango gani cha uwekezaji utakachokuwa nacho ni juu yako.

Jinsi ya kuwa mwekezaji aliyefanikiwa itategemea zaidi elimu yako. Kutokana na utofauti huu wa elimu juu ya biashara na uwekezaji, ndiyo maana kuna wawekezaji wadogo na wakubwa.

Sasa wakati umefika wa wewe kuacha woga wa kuwa mwekezaji. Anza kuchukua hatua moja baada ya nyingine kwa kuanza taratibu kujifunza kanuni na mbinu madhubuti za uwekezaji. Kumbuka kuwa maisha mazuri na uhuru wa kipato vyote vitawezekana endapo utaamua kwa dhati kuanza mara moja safari yako ya uwekezaji.

Endapo unataka kuwa mwekezaji mkubwa, jitahidi sana kujifunza kupitia mtandao wa MAARIFA SHOP. Acha kufanya maamuzi ya uwekezaji kwa kutumia taarifa za mitaani badala yake soma vitabu na makala hasa zinazohusu masuala mazima ya uwekezaji na ujasiriamali kwa ujumla. Bonyeza neno “NIUNGANISHE” ili kujipatia makala nzuri moja kwa moja kupitia barua pepe yako, kila mara zinapochapishwa.

Kwa Ushauri na Mafunzo: Bonyeza neno MAFUNZO hapa utapata mafunzo kila mara


No comments: