Unafahamu Makosa ni Mfuko Ulioficha Vitu Vizuri?
Kwenye mchakato wa biashara, ujasiriamali na maisha kwa ujumla, kuna makosa mengi yanayoendelea kufanyika. Wakati mwingine utulazimu kulipa gharama kubwa, ili kurekebisha makosa yaliyofanyika. Kwahiyo, tuseme kwamba makosa ni gharama, ndiyo maana wengi ujitahidi sana kukwepa kufanya makosa—Japo bado wanafanya makosa!! Lakini,
uzoefu
umeonyesha kuwa, pamoja na kulipa gharama zitokanazo na makosa fulani
fulani bado makosa hayo hayo ni fursa nzuri sana ya kujifunza na kuweza
kuwa bora zaidi. Hapa chini kuna mfano halisi wa jinsi nilivyoweza
kujifunza kitu kikubwa baada ya kufanya makosa:
Siku
ya Jumapili ya tarehe 12/11/2017, nilisafiri kutoka Nyakanazi
(Biharamulo) kwenda Kasulu (Kigoma). Mara likatokea basi kutoka Kahama,
nikaamua kwenda kuuliza kama inawezekana kusafiri na basi hilo. Kondakta
aliponiona kama mtu mwenye nia ya kusafiri, akaniwahi kwa kuniuliza
ninakokwenda. Kusikia hivyo bila hata ya kutafakari nikamwambia nakwenda
Kasulu, naye akasema nauli hadi Kasulu ni shilingi 15,000/-.
Baada
ya kulipa nauli niliingia kwenye gari na safari ikaanza mara moja. Kwa
mshangao mkubwa, tulipofika stendi kuu ya mabasi mjini Kibondo,
tukaambiwa mwisho wa gari ni hapo stendi na wakasema abiria wote
tuliolipia nauli ya moja kwa moja hadi Kasulu, tuingie kwenye gari
(TOYOTA ICE), ambalo lilikuwa limepaki pembeni tayari kwenda Kasulu.
Hapa ndo kusema kuwa “tulifaulishwa”. Baada
ya kupanda ICE hiyo, ndipo nikagundua kuwa wale tuliofaurishwa,
tulikuwa ni wachache (watu wanne tu). Changamoto ikawa ni kwamba, lazima
tusubili abiria wengine waje kujaza gari ndipo liweze kuanza safari ya
kuelekea Kasulu. Kwa jinsi ilivyokuwa siku ya jumapili, niliona kwa
haraka haraka niliona hiyo ICE itachelewa sana kuondoka (labda saa kumi
jioni badala ya kuondoka saa sita na nusu mchana). Baada ya kukaa stendi
kwa muda wa saa nzima bila kuona abiria anayekuja kupanda ICE hiyo,
ndipo nilianza kulaumu na kulaani, nikajiuliza maswali mengi yasiyokuwa
na majibu; “kwanini hawa vijana wamenifanyia yote haya”? Hawajanitendea
haki”, “wamenidanganya” …... nikawa na kila aina ya malalamiko yote
unayoyajua.
Baada
ya muda akiri yangu ilifunguka nikagundua nimefanya MAKOSA makubwa
wakati wa kulipa nauli. Nilitakiwa kulipa nauli hadi Kibondo, nauli
inayobaki ningepanda gari ambalo ningeona linafaa kupanda. Kimsingi,
mimi ndiye nilikuwa mjinga, kwasababu sikujua taratibu na kanuni zisizo
rasimi kwenye sekta ya usafirishaji wa abiria. Nilitakiwa kuuliza mwisho
wa basi ni wapi—sikufanya hivyo, badala yake, niliishia kujibu kile
nilichoulizwa na kondakta. (kondakta: unasafiri kwenda wapi? Mimi:
Kasulu; kondakta: nauli ni 15,000/-; lipa nauli tiketi hii hapa; Mimi:
Nikalipa….).
Baada
ya kukiri makosa yangu kwenye usafiri niliamua kuwajibika kwa kulipa
tena nauli ya shilingi 8,000/- na nikapanda BASI JINGINE lililokuwa
likitokea Mwanza ambalo lilisimama stendi (Kibondo) kushusha abiria.
Safari hii sikufanya kosa nilikuwa wa kwanza kumuuliza kondakta kama
basi lake linafika Kasulu.
Ukifuatilia
kisa hiki kizima utaona ni kama vile nililipa shilingi 8,000/- zaidi.
Lakini, ukweli ni kwamba pesa hiyo haikulipwa kama nauli bali kama
gharama au hada (karo) ya mwanafunzi ambaye alitakiwa kulipia
masomo na kupata majibu ya kile ambacho nilikuwa sijui kwenye masuala
yote yanayohusu usafiri hasa wa magari ya kuungaunga (kupokezana
vijiti).
Baada ya akiri yangu kuichukulia shilingi 8,000/- kama “hada/karo”
ya kufuta ujinga, hali ile ya kulalamikia upotevu wa pesa haikuwepo
tena. Niliona ilikuwa ni haki hizo pesa zaidi nizilipe, kwasababu,
kuanzia siku hiyo nilikuwa tayari nimejifunza jinsi ya kuwa makini
wakati wa safari hasa unapotumia magari ya kuungaunga.
Jifunze Kubadili Makosa Kuwa Masomo
Ukiyachukulia
makosa kama masomo, uwezo wako wa kutatua au kurekebisha makosa yako
unaongezeka. Mfano mzuri ni kama nilivyoeleza hapo juu, endapo siku hiyo
nisingeamua kulichukulia KOSA langu kama somo, pengine ningechelewa
sana kwenda nilikokuwa naenda. Kwasababu ningeona ni kupoteza pesa kwa
kulipa nauli mara mbili.
Sisi
kama viongozi wa maisha yetu, ni muhimu sana kuyachukulia makosa kama
fursa ya kujifunza kitu kipya juu ya hicho unachofanya, iwe ni kwenye
maisha au biashara. Katika kitabu cha “Before You Quit Your Job” (bofya KITABU kupata nakala)—Bwana Robert Kiyosaki anasema; makosa ni kama alama za barabarani zinazoamrisha kusimama. Kwamba makosa ni kama yanakwambia “wewe, sasa ni muda wa kusimama…. tulia kidogo…. kuna kitu hujui …. Ni wakati wa kuacha na kufikiri kwanza. Bwana “Kiyosaki” pia anaendelea kusema kwamba “makosa ni ishara inayokuonyesha kwamba sasa ni muda wa kujifunza kitu kipya ambacho ulikuwa hukijui hapo mwanzo”
Kwahiyo,
kila wakati unapofanya makosa, simama, chukua hatua ya kujifunza kitu
kipya. Kama kuna kitu hakiendi vizuri kwa jinsi ulivyotegemea au
kimekwenda kinyume na matarajio yako, jipe muda wa kufikiri kwa kina.
Ukishagundua somo lililokuwa limejificha ndani ya mfuko wa makosa,
lazima utakuwa mwenye shukrani kwa makosa hayo.
Waajiriwa na Wajasiriamali Wana Falsafa Gani Juu ya Makosa?
Waajiriwa na wajasiriamali ni watu wanaoishi dunia mbili tofauti na falsafa yao juu ya neno “makosa”
ni tofauti sana. Kwa waajiriwa kufanya makosa ina maana kwamba kuna
kitu hujui kabisa na wewe ni mjinga. Ndiyo maana mwajiriwa yeyote
akifanya makosa, mara nyingi anajifanya hajafanya makosa yoyote;
anakataa na anasema makosa yamefanywa na watu wengine siyo yeye.
Mwajiriwa atafanya kulaumu wengine juu ya makosa yake—Jambo hili lipo
sana kwenye maofisi mengi ya umma na ya watu binafsi.
Ni
waajiriwa wachache sana wanaochukulia makosa kama fursa ya kujifunza
na kuongeza uwezo wao wa kufikiri. Kila mara waajiriwa tunakuwa makini
hadi kupitiliza, huku tukijitahidi kukwepa kufanya makosa, kwasababu
tunaamini makosa nikitu kibaya sana.
Kwa
maneno mengine ni kwamba watu wengi wanaoishi kwa kukwepa kufanya
makosa mara nyingi ni watu wa kulaumu na kulalamikia wengine. Watu wa
namna hii ni wagumu sana kukubali kwamba wamefanya makosa, matokeo yake
huwa ni vigumu sana kwao kupata muhafaka wa makosa yaliyotendeka jambo
ambalo husababisha makosa yale yale kujirudia mara kwa mara.
Wajasiriamali wao wanaamini makosa ni kitu kinatokea nje ya ufahamu wako ulionao kwa wakati huo. Pia, wanaamini makosa ni kitu ambacho kinaweza kumtokea mtu yeyote bila kujali kisomo, umri na uzoefu wa mtu. Kutokana na Imani hii ya wajasiriamali juu ya kitu “makosa”, wemejifunza kitu kimoja cha muhimu katika biashara au maisha, nacho ni “kuyakiri makosa”.
Kitendo
cha kukiri makosa ndicho uwapa uwezo wa kusimama na kuanza tena pale
inapotokea wakaanguka. Unapokubali kuwa makosa yametendeka na wewe
pengine umehusika, ndipo akiri yako inafanyakazi katika viwango vya juu
zaidi na hivyo kupata suruhisho la kudumu juu ya matatizo na changamoto
zinazokukabili.
Sasa
ni wakati wa kufikiri juu ya maisha mazuri unayoyataka. Ni wakati wa
chukua hatua (anza kufanya kwa vitendo), huku ukitambua kuwa makosa
yatakuwa ni sehemu ya mchakato wa kufanya hicho unachofanya. Kila
yatakapojitokeza makosa badala ya kutafuta mchawi, wewe yafungue makosa
hayo, ili hatimaye uweze kunufaika na (masomo, ukweli na fursa)—yawezekana
vyote hivi viko ndani ya mfuko wa makosa. Unatakiwa kuacha kulalamika,
fungua mfuko wa makosa sasa na endelea kusonga mbele.
Jinsi ya Kuwa Mkubwa Kuliko Matatizo
“Utasonga mbele tu pale utakapoacha kujibinafsisha matatizo yanayoendelea kutokea katika mchakato wa maisha yako” ~ Cypridion Mushongi
Njia
mojawapo ambayo ni kisababishi kikubwa cha hisia hasi na hasira ni hali
ya kupenda kujibinafsisha au kujimilikisha matatizo yanayoendelea
kutokea. Tabia au hali hii ya kupenda kujibinafsisha ni...
hatari kama ilivyobainishwa na bwana Ouspensky kwenye kitabu chake cha “In Search of the Miraculous: Fragments of an Unknown Teaching”(“nitumie kitabu”).
Hali
hii ya kujibinafsisha matatizo, mara nyingi utokea pale unapochukulia
jambo lililotokea kama la kwako binafsi au unalihusisha moja kwa moja na
mtu au kitu fulani. Kila mara unaona matokeo ya matukio ya kuudhi au
hali mbaya kama ya kwako binafsi. Wakati mwingine unaona matokeo ya
matukio ya kuudhi kama mashambulizi dhidi ya kile unachokiamini wewe.
Unajikuta unajihusisha kwa hisia zako zote na kujitambulisha na hali
hiyo, kiasi kwamba inakuathiri kihisia, kifikra na kimtazamo katika hali
ambayo ni hasi.
Walimu
wakubwa katika masuala ya kidini, kama vile Buddha na Yesu, wamesistiza
umuhimu wa kujitenganisha wewe na matukio yanayoendelea kutokea, ili
kupata utulivu na kudhibiti hisia ulizonazo.
Kwa upande mwingine mtaalam wa masuala ya saikolojia na falsafa bw. William James kutoka chuo kikuu cha Harvard (Marekani), aliwahi kuandika kuwa “hatua ya kwanza kwa tatizo au ugumu wowote ule ni kuwa tayari kulipokea kama lilivyo”.
Pia mtaalam huyu aliwahamasisha watu kuwa kitu chochote ambacho
hakiwezi kutibiwa lazima kivumiliwe. Kwa maneno mengine ni kwamba
tunahitajika kujenga tabia ya kujitenganisha na mtu au hali ambayo
inatufanya sisi kuwa na hasira au kuudhika. Inabidi tuondoe nguvu ya
hisia zetu kwa mambo yanayotupa hasira, ili kupata utulivu na amani.
Njia
hii haina maana kwamba ukubali kila kitu kibaya kinachokujia BADALA
yake, inakuhamasisha kutumia nguvu yako ya akiri katika kudhibiti hisia
hasi. Unajiwajibisha wewe binafsi kurudi nyuma kidogo na kukabiliana na
matatizo au changamoto kwa akiri na busara zaidi. Unatumia akiri kuona
hali halisi ilivyo na kufanya maamuzi mazuri ya kutatua tatizo lililopo.
Hakuna watu wanaoweza kukudhibiti wewe labda kama kuna kitu fulani
ambacho unahitaji kutoka kwao.
Lazima
watu wengine wawe na kitu fulani ambacho bado wanaweza kukupatia au
kuzuia usikipate. Mara moja utakapojitenga kihisia na mtu au kitu na
ukawa hauhitaji chochote kutoka kwao, basi wewe huko huru. Hali hii ya
kufanya mazoezi ya kujitenganisha na matukio au watu wanaokukwaza ni
nguvu ambayo unaweza kuipata kwa kuijenga kupitia mazoezi ya kiakiri.
Mazoezi haya yanaweza kukufanya ukawa mtaalam na bingwa wa kutatua
matatizo yanayosababisha hasira.
Jambo
moja unaloweza kulifanya ili kusaidia watu wengine, ni kuwatia moyo wao
kuweza kujitenga na matukio ya matatizo na kutokushawishiwa na hisia
katika kuliona na kulitatua tatizo. Wahamasishe, kuona ugumu na
matatizo, kama vile yanatokea kwa wengine. Waulize ni ushauri gani
wangeweza kutoa kwa mtu mwingine anayekabiliwa na tatizo kama hilo la
kwao. Kwa kujitenga na hali inayotokana na hisia zilizoamshwa na tukio,
wewe pamoja na wengine mtazidi kuwa na uwezo zaidi wa kutatua tatizo kwa
ufanisi.
Kikubwa
tunachojifunza hapa ni kwamba, wewe mtu binafsi ndiye mwenye uwezo wa
kuamua ukubwa wa tatizo. Suala la tatizo kuwa kubwa au dogo ni la
kihisia zaidi kuliko uhalisia. Na inaonekana kwamba matatizo tunayoyaita
makubwa mengi ni yale tuliyosimuliwa na wakubwa zetu kuwa ni makubwa
nasi tumeendelea kushikiria hisia hizo. Kwahiyo, inatupasa kila tukio
tunalodhani ni tatizo kwetu tujenge utamaduni wakuwa tunalitafakari upya
sisi kama sisi na tuliangalie na kulipima katika mazingira halisi ya
wakati huo uliopo, ili kusudi tuweze kupata suruhisho lenye kuondoa
tatizo lote kwa ujumla.
Ni
muhimu sasa tutambue kuwa matatizo yataendelea kutokea kwa yeyote yule
anayetaka na asiye taka, maskini na tajiri, aliyesoma na ambaye
hakusoma, aliyejiajiri na aliyeajiriwa. Kitu cha msingi sana unachopaswa
kukumbuka kila mara ni kwamba “wewe ni mkubwa sana kuliko matatizo uliyonayo”.
Jambo la kushangaza ni kwamba watu wengi wameamua kuwa wadogo kuliko
matatizo wanayokabiliana nayo na ndiyo maana wanajiona wana matatizo
makubwa kuliko wenzao. Hali hii imesababisha watu wengi kukata tamaa ya
maisha.
Mpendwa
msomaji, yawezekana baada ya kusoma makala hii, umepata maswali mengi
na pengine ungependelea kupata majibu na kuendelea kujifunza zaidi.
Hivyo, napenda kukutaarifu kuwa bado unayo fursa ya kuwa mmojawapo wa kundi la wasomaji wa mtandao wa maarifashop: ni rahisi kwani unahitaji tu kuweka e-mail yako kwa kubonyeza neno “INGIA” .
Ukimaliza
kufanya hivyo, tayari wewe utakuwa na fursa ya kuwasiliana na mimi muda
wowote na utaweza kupata makala, vitabu moja kwa moja kupitia e-mail
yako kila mara vinapowekwa vitu vipya.
Fikra zetu kutoka ndani ya akiri zetu
ndiyo kila kitu. Fikra ndilo dirisha unalotumia kuangalia dunia na mambo yake
yote. Ukishakuwa umelitabua hili utakubaliana
na mimi kuwa unahitaji kuanza mara moja kujitathimini juu ya mwenendo wako.
Unahitaji, kujenga na kuinua heshima yako juu na hii ikiwa ni pamoja na kupanua
dirisha lako la fikra ili kuona zaidi fursa za mafanikio.
Ili kupanua dirisha la fikra, inabidi kutunza kujiamini na kujikinga dhidi ya athari
zitokanazo na changamoto mabalimabali za kimaisha.
Na hapa unahitaji kufahamu mambo
5 yatakayo kuwezesha kufanya uchunguzi wa undani ya fikra zako na hatimaye
kupata msingi imara wa kuweza kuzijenga upya, ili ziwe katika mwelekeo ambao ni
chanya.
Ninatumaini kuwa, ukishakuwa umefahamu nini cha kufanya, basi utaweza
kufahamu ni kitu gani unatakiwa kufanya na ni kwanini ni muhimu kwako.
Katika kuchunguza undani wa akiri yako na hatimaye kupanua
dirisha lako la fikra zako, unahitaji kufikiria mambo 5 ya msingi:
1. Jua Kuwa Maisha Yako, Yanatengenezwa na Fikra Unazozipa Kipaumbele
Kila Siku.
Ukisoma
kitabu cha Bwana James Allen kiitwacho “As a Man Thinketh” anatoa mafundisho ya kwamba, wewe
binadamu ndiye unayetengeneza au kuharibu maisha yako mwenyewe kutokana na fikra
juu ya fikra ulizonazo akirini mwako. Na pale unaporuhusu mawazo yatokee
unakuwa ni muhanga wa maelfu ya mawazo hasi na imani finyu zinakuzunguka
kupitia duara lenye taarifa hizo kila muda unaopita.
Unapokuwa
mfikiriaji mahili wa mawazo (mtu mwenye kufikiri na kuchagua kile unachofikiria),
basi jua kuwa hapo una uwezo wa kujenga maisha ambayo ni chanya na kutembea
kila siku kuelekea kwenye ndoto yako ya maisha mazuri.
2. Jua Kuwa Kubadili Kitu Chochote Nje ya Wewe, Lazima Ubadili Fikra
Zako Kwanza.
Kama
unataka watu wengine wabadili mtazamo wao wa jinsi wanavyochukulia au kukuona, lazima
uanze kujibadili wewe kwanza. Kama unataka kubadili uchumi, jibadili wewe. Kama
unataka kubadili hali ya maisha, jibadili wewe mwenyewe. Kama unataka kubadili
dunia, jibadili wewe mwenyewe. Hiyo ndiyo kazi ya ndani yako ambayo utengeneza upenyo
halisi na kuelekea kwenye mafanikio.
3. Jua Kuwa Fikra Chanya Hazijengwi kwa Siku Moja.
Mwelekeo
wa fikra ulizonazo ziwe chanya au hasi, zinajengwa ndani ya mzunguko wa siku
30. Baada ya siku 30 za kufanya kitu fulani, jua kwamba imekuwa tabia yako. Na maoni
yako juu ya mwenendo wa maisha uliyonayo, pia ni matokeo ya tabia ya fikra zako
za kila siku.
Kwahiyo, usifanye kitu hiki siku ya Jumatatu peke yake na
kutarajia kuwa millionia siku ya jumanne. Tambua kwamba ukiweka siku 30 za
kufikiri mambo chanya fikra zako zitabadilika kwa kiasi kikubwa sana. Na baadae
unapanda viwango kwenda hatua nyingine ya juu zaidi na kuendelea…
4. Jua Kuwa Unatengeneza Maisha Mazuri kwa Kujenga Taswira Nzuri
Mwenyewe.
Taswira
yako inatengenezwa na picha ya iliyoko kwenye ubongo na ambayo inachezesha
fikra zako kwa siku nzima. Ni jinsi gani unavyojiona wewe mwenyewe kufanikiwa
au kutofanikiwa. Ndiyo sababu, jambo namba moja hapo juu ni muhimu sana.
5.
Jua Kuwa
Kile Unachokiamini Ndicho Kinawezekana
Kama kweli unaamini unaweza kufanya chochote na
ukafanyia kazi imani hiyo, basi kwa hakika utaweza kufanikisha ndoto yako. Ni lazima uamini kuwa unaweza kufanya kitu chochote. Unaweza
kuimba kwamba “unaaamini unaweza kupaa,”
lakini hauamini kwamba unaweza kufanya hivyo na kwahiyo, sheria ya uvutano bado
inafanya kazi.
Na
inaweza kuwa kukuhamasisha ukajikuta unapendekeza kuwa unaweza kusogeza mlima
kwa kutumia mbegu ya ndogo sana ya zao la ulezi, lakini wote tunajua kuwa hicho
ni kitu ambacho hakiwezi kutokea. Lakini unapokuwa umeweka malengo, unaweza kwa
dhati ukayatimiza kwa kwenda kuyafanyia kazi, na ikawezekana kuwa hivyo.
Hakikisha kuwa unafanya kazi na kutimiza majukumu yako ya kila siku yanayohusu
maendeleo yako binafsi.
Jitahidi
kuweka fikra chanya na kujua kwamba sehemu yako ya ubongo inayoitwa subconscious itakuongoza wewe kuchukua
hatua moja baada ya nyingine hadi kufanikisha hicho ulichokipanga kukifanya
kuwa dhahiri. Endapo utakuwa umenielewa nazungumzia nini juu kuchukua hatua
dhidi ya ya mambo 5 hapo juu, basi hapana shaka unaweza kuishi ndoto zako. Na
hiki ndicho ninachokutakia ukifanye.
AMUA KUWA
RAIS WA MAISHA YAKO LEO
Maisha
unayoishi sasa ni maisha yako, kama kuna sehemu yoyote ya maisha yako ambayo
huipendi wewe ndio una jukumu la kuibadilisha. Hakuna mtu mwingine yeyote
ambaye anaweza kuwa na uchungu na maisha yako ila wewe mwenyewe. Na wala hakuna
mtu yeyote anayeweza kuyabadili maisha yako bila yaw ewe mwenyewe kuwa tayari
kwa mabadiliko.
Kuanzia sasa jichukulie wewe kama raisi wa maisha yako, na jichukulie wewe ndio mtu wa mwisho wa kufanya maamuzi juu ya maisha yako. Na sio tu unajichukulia hivi, bali ndio ukweli wenyewe. Wewe kama raisi maamuzi yako yanaweza kusababisha mafanikio au yakasababisha kushindwa. Kama tulivyoona kwenye siku ya kwanza upo hapo ulipo kutokana na maamuzi uliyofanya na machaguo uliyofanya. Ili kwenda mbele zaidi unahitaji kufanya maamuzi bora zaidi na kuboresha machaguo yako.
Miasha ni kuchagua, ukichagua kufanikiwa ndiyo utakachokipata, ukichagua kuwa wa matatizo na kushindwa ndicho kitakachotokea. Usipochagua kabisa utapata kile kilicho kibovu kabisa ambacho ni kushindwa. Kipato unachopata leo ndio kipato ulichoamua kupokea, kama kipato unachopata sasa hakikuridhishi amua kupata zaidi ya hapo. Fanya hilo kama lengo lako, weka mipango na anza kufanyia kazi mpango wako wa kujiongezea kipato. Ukikaa tu na kulalamika kwamba kipato hakikutoshi huku hufanyi chochote cha kukiongeza unapoteza muda wako.
Wewe ndio raisi wa maisha yako, wewe ndio mfanya maamuzi mkuu na wewe ndio unayetengeneza maisha yako. Kama utakuwa na mtizamo hasi utajenga maisha ya matatizo na kushindwa na kama ukiwa na mtizamo chanya wa kuona unaweza kubadili maisha yako utatengeneza maisha ya mafanikio na furaha. Yote haya yapo mikononi mwako ni wewe tu ufanye maamuzi sahihi na kuyasimamia.
~ TWENDE KAZI PAMOJA ~
2 comments:
Nakubaliana nawe kuwa lazima uwe raisi wa maisha yako ili utawala uendelee na hatimaye ufanikiwe kweli
Tatizo letu wengi tunachelewa kuchukua hatua kwasababu ya kasumba ya kufikiri kuwa viongozi ni wale wa kisiasa tu ndio maana ata mkuu wa kaya anasubili mkuu wa wilaya amwambie kuwa ni muhimu kuweka akiba ya chakula; Dereva wa basi anaendesha gari kwa mwendo kasi naye anasubili abiria wa mwambie ni hatari. Ndugu hapo ndo tulipo Tanzania uijuavyo.
Post a Comment