Sunday, June 28, 2015

Wewe ni Mjasiriamali Lakini Punguza Hili

“Watu wengi tunatumia kitu cha bure “usingizi” kujikosesha fursa hadimu”
“Masaa (muda) tunayotumia kufanya kazi ndiyo pesa yenyewe”
Kitu kinachoitwa “usingizi” ni kitu ambacho kipo siku zote na muda wote, na wakati huo huo ni kitu ambacho unatakiwa kuwa makini nacho hasa kama unataka mafanikio makubwa. Usingizi ni kitu ambacho huwezi ukakitumia kikaisha, kwahiyo, hata ukiukosa kwa muda fulani, bado utaukuta muda wowote ukiutaka. Usingizi” ni zawadi ambayo kila mwanadamu amepewa kiasi cha kutosha na ni kitu ambacho hakina ukomo. 

Habari njema ni kwamba, usingizi wa mtu hauwezi kuibiwa na wala mtu akilala usingizi wake, si rahisi kutumia usingizi wako. Kwa maana nyingine, tunasema kwamba usingizi ni hazina ya kwako peke yako. Usingizi haununuliwi kutoka kwa mtu mwingine, kwasababu kila mmoja ana wa kwake. Usingizi wote tulionao ni kitu ambacho tunakipata bure na itoshe kusema “Mungu aksante kwa zawadi hii ambayo tunapata bure kwa kipindi chote cha maisha yetu”.

Ajabu ni kwamba, “watu wengi tunatumia kitu cha bure “usingizi” kujikosesha fursa” hadimu ya kutafuta maisha ya ndoto yao. Tabia ya kuendekeza usingizi, imesababisha kupoteza muda mwingi, ambao tungeutumia katika uzalishaji na hatimaye kupata kipato. Mara nyingi watu ambao wanaendekeza usingizi na uvivu, ndio hao hao ambao kila kukicha wanalalamika maisha magumu na kibaya zaidi wanawatwisha mzigo wa lawama watu wengine, eti hawakuwajibika ipasavyo!.

Ikumbukwe kuwa, mwili wako usipotumia nguvu katika kazi zenye kuzalisha mali, bado nguvu uliyonayo itatumika kupiga soga, kuangalia runinga, kupiga umbea, kuangalia mpira, n.k. ukishakuwa umefanya vyote hivi, pale nguvu ikikuishia moja kwa moja mwili wako utajisikia kupumzika na hivyo kupata usingizi utakao kulazimu kulala. Hali hii inapojirudia rudia, inakujengea mazoea ya uvivu, jambo ambalo litakukosesha nguvu na uwezo wa kupambana na umaskini.

Mjasiriamali ukishaanza kushindwa kuutawala usingizi wako, basi ujue kuwa mambo mengi mazuri yataanza kukupita. Mfano: unakuta kuna watu wengi wanaofahamu kuwa, ili kulinda afya zao ni muhimu kuamka mapema na kufanya mazoezi, lakini mpaka sasa ni watu wachache wanaoweza kufanya mazoezi masaa yale ya alfajiri. Utakuta mtu anakwambia mimi ninapenda kufanya mazoezi asubuhi lakini, usingizi wa saa kumi na moja huwa ni mtamu, siwezi kuuacha. Mtu huyohuyo, ambaye anashindwa kuacha usingizi wa alfajiri anajikuta akiambulia magonjwa. Ukishakupatwa na magojwa ni wazi kwamba kuna mengine yatakusababishia maumivu makali ambayo, yatakukosesha usingizi ule uliokuzuia mwanzoni kuamka mapema na sasa kuukosa tena kwa gharama kubwa.

Usingizi pamoja kwamba ni kitu kizuri, lakini kinachukua “masaa” yetu mengi ambayo tuna uwezo wa kuyatumia vizuri katika shughuli nyeti za uzalishaji mali. Ikumbukwe pia kuwa, pesa uliyonayo inatokana na muda uliowekeza kwenye shughuli za uzalishaji mali. “Masaa (muda) tunayotumia kufanya kazi ndiyo pesa yenyewe” kwasababu uzoefu unaonyesha kuwa mtu ambaye anaamka na kuanza kazi mapema (alfajiri) kila siku amepiga hatua kubwa sana kimaendeleo kuliko anayechelewa kuamka.

Kwahiyo kama kuna kazi ya muhimu katika maisha yako, acha usingizi ukafanye hiyo kazi, kwani unapomaliza kazi hiyo, utalala usingizi wako kwasababu usingizi ni kitu ambacho kipo na hakipotei kamwe. Tukiendelea kufanya kazi kwa bidii ni wazi kwamba tutapata mafanikio makubwa ndani ya muda mfupi na hapo tutakuwa na fursa na muda wa kutosha sana kulala usingizi. Wewe ndiye mwenye maamuzi juu ya matumizi ya muda na nguvu yako. Chagua kuwekeza muda na nguvu nyingi kwenye shughuli za uzalishaji mali na ufanye maamuzi kwa kuanza leo, maana ujachelewa.  

Mpendwa msomaji, endelea kuitumia vizuri MAARIFASHOP ili kujifunza mambo mbalimbali yatakayokuwezesha kupata mafanikio. Ili kupata makala mpya kila zinapochapishwa, bonyeza neno TUMA MAKALA MAARIFASHOP kisha sajiri barua pepe yako. Na kama unapenda kupata mafunzo ya kila siku kwa njia ya whatsap bonyeza neno MAFUNZO

Wednesday, June 24, 2015

Chimbuko la Pesa ni Hili Hapa

  • Afya Bora Ndiyo Machimbo ya Kudumu  ya “Pesa” tuliyonayo!
  • Watu Wengi  Bado Wanaamini Kuwa Kitu Kinachoitwa “Afya” Kitajileta Chenyewe!
Katika maisha ya siku hizi inashangaza sana kuona kuwa pesa tunazotafuta zimekuwa zimekuwa adui yetu mkubwa wa miili na afya yetu kwa ujumla. Ndiyo maana leo hii, watu wengi “wanakula dawa kama chakula badala ya kula chakula kama dawa”. Maana yake ni kwamba, watu wengi wanayo pesa lakini, Asilimia kubwa inatumika kununua dawa ili waweze kusogeza maisha yao mbele. Mwanaharakati mmoja kutoka bara la Asia aliyejulikana kwa jina la “Dalai Lama”, alipoulizwa kitu ambacho kiliwahi kumshangaza zaidi kuhusu ubinadamu, alijibu kuwa ni Binadamu:

“Kwasababu, binadamu anatoa afya yake sadaka, ili kutafuta pesa. Alafu anatoa pesa yake sadaka, ili kurudisha afya yake. Na sasa anaanza kuhofia juu ya mstakabari wa maisha yake ya baadae (future), kiasi kwamba anashindwa kufurahia maisha yaliyopo wakati huu; Matokeo yake ni kwamba mtu huyu hawezi kuishi wakati huu (uliopo) au ujao; anaishi kama vile hatakaa aje kufa na alafu anakufa kama vile hakuwahi kuishi”

Maono ya mwanaharakati huyu yanatuonyesha kwamba, muda mwingi wa maisha yetu hatufanyi kitu chochote kinachohusu afya zetu isipokuwa tunaelekeza nguvu, ujuzi, maarifa na rasilimali nyingine kwenye mambo tu ya kutafuta pesa peke yake. Fikra za waliowengi ni kwamba bado wanaamini kuwa kitu kinachoitwa “afya” kitajileta chenyewe, ilimradi uwe na pesa, na wengine wasiojua wanaamini katika “Pesa Kwanza na Afya Baadae”.

Kwa sasa hali ya afya kwa waliowengi siyo nzuri, na hii ni kutokana na kutokuwa na malengo na mipango inayohusu afya. Mipango mingi inalenga zaidi kujiendeleza kiuchumi, kielimu, kujenga nyumba nzuri, kuongeza uzalishaji, kununua magari n.k. Ni watu wachache wenye kuwa na malengo na mikakati ya kujenga na kuimalisha afya zao. Mara nyingi, watu wanakumbuka kujali afya zao pale wanapougua au kuanza kusikia maumivu. Wataalam na wadau wengine wa masuala ya afya, wanatwambia kwamba, pale unapoanza kujisikia maumivu ndani ya mwili au kuumwa kabisa, basi ujue kuwa umechelewa kula chakula kama dawa. 

Mara nyingi, imekuwa ni kawaida kuletewa chakula bora pale tunapokuwa tayali tunaumwa na kulazwa hospitalini, ndiyo maana ukitembelea wagonjwa, unapishana na watu wakipeleka machupa makubwa ya jwisi na matunda ya kila aina. Vyakula hivi ambavyo tunaletewa tukiwa wagonjwa, hakuna mtu anayeweza kukuletea tena nyumbani kwako ukiwa mzima, kwasababu, ni matarajio yetu kuwa, ukisharudia hali yako nzuri kiafya, utachukua jukumu la kuendelea kujali afya yako wenyewe. Lakini, cha ajabu, hatufanyi hivyo mpaka tunapoletewa vyakula kwa mara nyingine, pindi tunapougua tena!. Ukweli ni kwamba, jambo la kuimalisha na kulinda afya zetu tumelichukulia la mzaa sana. Kwahiyo, ni muhimu sana tukatambua kuwa mafanikio makubwa tunayotafuta kwasasa yataweza kufikiwa kwa haraka iwapo tutazipa afya zetu kipaumbele namba moja, nje ya hapo maisha bora yatabaki kuwa ndoto ya milele.

Ukitafakari kwa kina sana, utagundua kuwa afya bora ndiyo machimbo ya kudumu ya “Pesa” tuliyonayo. Afya bora ndio utupatia rasilimali “nguvukazi”na pindi nguvu kazi yetu tunapoiwekeza kwa ufanisi hasa katika shughuli za uzalishaji ndipo tunapata bidhaa au huduma ambazo watu wengine utoa na kuleta pesa kwetu, ili kujipatia bidhaa/huduma husika. Pesa ndiyo utuwezesha kupata mahitaji yaliyo mengi kwa muda tunaoutaka na hatimaye kufikia maisha bora ambayo ndiyo ndoto yetu ya muda mrefu.

Kwakuwa, pesa tuipatayo, chimbuko lake ni afya bora, ni muhimu kwa kila shilingi ya pesa tunayoipata, mgao wa kwanza uelekezwe kwenye kuimalisha na kulinda afya. Tunasema suala la matumizi ya pesa kwenye afya, liwe ndio kipaumbele namba moja kwasababu afya ndiyo kisima chetu cha pesa. Unapoamua kutenga pesa kwaajili ya afya yako, maana yake ni kwamba unazifanya pesa zako kuwa rafiki mkubwa wa mwili wako. Pesa zinakuwa rafiki yako pale unapozitumia kujenga, kuimalisha na kulinda afya yako kwa ujumla. Pesa haziwezi kuwa rafiki wa mwili wako, kama hazijatumika kulisha chembe hai za mwili kupitia ulaji wa vyakula na virutubisho muhimu. Nje ya hapo, chembe hai za mwili wako hazina uhusiano na na pesa yako iliyoko mfukoni, benki au kwenye miradi yako ya biashara.

Wito kama unataka mafanikio makubwa anza sasa kuweka malengo ya kupata afya njema na kipato. Ni muhimu vitu hivi viwili viende pamoja kwasababu katika maisha ya Ujasiriamali, vinategemeana sana na vinapoungana ndiyo tunapata furaha ya kweli. Kwahiyo, jitahidi sana kujali afya wakati wote wa safari yako ya kusaka mafanikio ili ukifika maisha ya ndoto yako uwe una afya njema na hapo utafurahia zaidi kuliko anayeumwa kwasababu aliunyima sana mwili wake wakati wa safari ya kusaka mafanikio.

Mpendwa msomaji, endelea kuitumia vizuri MAARIFASHOP ili kujifunza mambo mbalimbali yatakayokuwezesha kupata mafanikio. Ili kupata makala mpya kila zinapochapishwa, bonyeza neno TUMA MAKALA MAARIFASHOP kisha sajiri barua pepe yako. Na kama unapenda kupata mafunzo ya kila siku kwa njia ya whatsap bonyeza neno MAFUNZO

Monday, June 15, 2015

Pesa Nyingi Inapatikana Hapa



  • Unapoamua kuwekeza nguvu kazi yako kwenye shughuli za uzalishaji ndipo unapata bidhaa.

  •  Unapokuwa na bidhaa/huduma ndipo watu wengine sasa huamua kutoa na kutuma pesa zao kwako, ili kujipatia bidhaa/huduma husika.

 Leo hii watu wengi tunahangaika, tunanungunika na tunalalamikiana juu ya kukosekana kwa pesa. Kila mtu anamtuhumu mwenzie juu ya hali duni ya maisha. Maisha duni yametokana na kukosekana kwa mahitaji. Ili binadamu apate mahitaji, kwa sehemu kubwa anahitaji pesa na hii mara nyingi inatokana na bidhaa au huduma ambazo umezalisha mwenyewe. Uzalishaji wa bidhaa au huduma zilizonyingi unategemea zaidi matumizi ya nguvukazi, ambayo chimbuko lake ni afya bora. Mtu mwenye afya bora, kwa vyovyote vile ni mtu mwenye kuwa na nguvu yakutosha kufanya shughuli mbalimbali na hasa za kiuchumi. Nguvukazi hatupewi na mtu yeyote, bali unakuwanayo kwa kuzaliwa ilimradi, uwe na utaratibu wa kujali afya yako basi!.

Kwakuwa kila mmoja wetu anamiliki na kuitawala nguvukazi yake mwenyewe, maamuzi ya kutumia nguvukazi yako kwa mtu mwenyewe. Kuna kundi la watu wanaotumia nguvukazi yao zaidi kwenye “Uzalishaji Pesa” na kuna wengine wanaitumia zaidi kwenye shughuli ambazo siyo za uzalishaji wa pesa (Non Income Generating Activities ~ NIGA). Hapa Tanzania, bado watu wengi wanawekeza nguvukazi kubwa zaidi kwenye shughuli zisizo za uzalishaji pesa. Shughuli nyingi ambazo siyo za uzalishaji pesa, zinatumia sana pesa, hali inayopelekea watu wengi kutumia kuliko wanavyozalisha pesa. Kama nguvu-kazi yetu nyingi inawekezwa zaidi kwenye shughuli ambazo siyo za uzalishaji, basi tujue kabisa kuwa tutapata bidhaa/huduma kidogo, na hatimaye tunaishia kupata pesa kidogo.

Watu wengi tunataka na tunatamani sana “maisha bora”; maisha ambayo tutakuwa na uwezo endelevu katika kupata chochote tunachohitaji kama lilivyo kusudio la Mungu kutuweka hapa duniani. Kwakuwa, maisha bora ndiyo kusudio la watu wengi, basi inatupasa tubuni mchakato wa maisha bora badala ya hali ya sasa ambayo tumejikita kwenye shughuli za kutafuta pesa ambazo hazina mpangilio. Kwa sasa ukichunguza harakati nyingi za kutafuta pesa, unagundua kuwa kila shuguli inajitegemea kiasi kwamba kukamilika kwa shughuli moja hakuna uhusiano wowote na shughuli nyingine. Jambo hili la kufanya shughuli ambazo hazina mpangilio maalumu unaolenga kupata maisha bora, ndiyo linatufanya tukose mwelekeo na hatimaye kushindwa kuyafikia maisha ya ndoto yetu. Kwahiyo, zoezi la kutafuta pesa na hatimaye maisha bora ni lazima kulifanya kuwa la ki-mchakato zaidi kuliko ki-shughuli zaidi. Kupitia fikra, utafiti, vitabu na hitoria za watu waliofanikiwa; nimejifunza kuwa, ili uweze kuyafikia maisha ya ndoto yako (maisha bora) ni muhimu upitie mchakato maalum. Mfano ni kama huu hapa chini:

AFYA BORA     NGUVUKAZI     BIDHAA     PESA     MAHITAJI     MAISHA BORA

Ukichunguza mchakato wa kupata pesa hapo juu unaona moja kwa moja kuwa pesa siyo matokeo ya mwisho ambayo binadamu anayatafuta bali pesa ni sehemu tu ya mchakato wa maisha bora. Katika mchakato wa kupata maisha bora, pesa ipo katika nafasi ya nne kati ya vitu sita muhimu ambavyo vinahitajika kupewa kipaumbele kama unataka kufanikiwa. Mafanikio makubwa yameshindikana kufikiwa na watu wengi, kwasababu ya kutilia mkazo zaidi kitu kimoja tu! ambacho ni PESA. Michakato yetu mingi ya kutafuta pesa, haitilii mkazo vitu vingine kama “afya, nguvukazi na bidhaa”. Kwa maana nyingine tunaweza kusema kuwa hatupati pesa kwasababu mara nyingi mchakato wa kutafuta pesa na hatimaye maisha bora “tunauanzia katikati”.

Unapopanga mkakati au mchakato wa kutafuta pesa na wakati huo huo ukaacha kuzingatia na kujali afya yako, basi ujue kuwa uwezekano wa wewe kupata maisha bora ni mdogo sana. Kumbuka afya bora ndio chimbuko la nguvu ulizonazo ambazo ndio hukupatia rasilimali “nguvukazi”. Unapoamua kuwekeza nguvu kazi yako kwenye shughuli za uzalishaji ndipo unapata bidhaa au huduma ambazo hugeuka kuwa pesa. Unapokuwa na bidhaa/huduma ndipo watu wengine sasa huamua kutoa na kutuma pesa zao kwako, ili kujipatia bidhaa/huduma husika. Kwahiyo, iwapo utakuwa umezalisha bidhaa nyingi utapata pesa nyingi na ni pesa hiyohiyo ambayo na wewe utaitoa na kuituma kwa watu wengine ili kupata bidhaa/huduma na hatimaye kukidhi mahitaji yako mbalimbali. Unapofikia hatua ya endelevu wa kupata kile unachohitaji kwa muda muhafaka, ni wazi kwamba unakuwa tayari umefikia maisha bora ambayo ni ya ndoto yako na hapa ndipo unaanza kupata vitu vile ulivyokuwa ukivipenda lakini ulilazimika kuviacha kwa muda ili kuruhusu mchakato wako wa maisha bora ukamilike.

Kwahiyo, tunapojiandaa kuanza safari ya kutafuta mafanikio ni lazima tujitahidi kuanza mchakato wa kutafuta maisha bora, kwa kuanza na ujenzi wa afya bora, ili itupatie nguvukazi itakayo tuwezesha kuzalisha bidhaa za kuleta pesa nyingi kukidhi mahitaji kwa kiwango endelevu na  hatimaye kufikia maisha bora ambayo ndiyo ndoto yetu.

Mpendwa msomaji, endelea kuitumia vizuri MAARIFASHOP ili kujifunza mambo mbalimbali yatakayokuwezesha kupata mafanikio. Ili kupata makala mpya kila zinapochapishwa, bonyeza neno TUMA MAKALA MAARIFASHOP kisha sajiri barua pepe yako. Na kama unapenda kupata mafunzo ya kila siku kwa njia ya whatsap bonyeza neno MAFUNZO

Saturday, June 6, 2015

Elimu ya Ajira Haiwezi Kukupa Kazi

http://maarifashop.blogspot.com
  • Zaidi ya Asilimia 90% ya Watu Wenye Utajiri Mkubwa Walitafuta Pesa Nje ya Mfumo wa Ajira....Maana Walitengeneza Kazi!.


Katika makala ya “Ajira Siyo Kazi ni Ajira na Kazi Siyo Ajira ni Kazi.... niliandika kuhusu tofauti iliyopo kati ya kazi na ajira, ambapo tuliona kuwa kazi” ni majumuisho ya majukumu mbalimbali uliyojipa wewe mwenyewe kazi, unajisimamia na kujiwajibisha mwenyewe kutimiza majukumu uliyojipa mwenyewe bila kutegemea kulipwa chochote mpaka matunda ya kazi hiyo yapatikane, hata kama ni muda mrefu (mwaka na zaidi). Na tuliona kuwa “Ajira” ni kufanya kazi ambayo siyo ya kwako, waweza kuwa unaipenda au huipendi. Kwa maana nyingine katika ajira unapangiwa majukumu maalum ya kufanya na mwenye kazi, ukiyakamilisha basi umemaliza kazi, zaidi ya hapo yanayobaki hayakuhusu.

Ukifuatilia kwa undani zaidi juu ya mfumo wa elimu duniani, utagundua kuwa mfumo huu umetujenga katika mtazamo wa kutafuta na kupata “AJIRA” badala ya “KAZI”. Kama hivi ndivyo, basi tujue kuwa tumepata elimu ya yale tu! ambayo wenye kazi wanayataka na lengo lake likiwa ni moja tu “kupata watu watakaomudu majukumu ambayo watapangiwa na wenye kazi. Haijalishi  kama elimu hii inazingatia maslahi na matakwa yako, ukishindwa unatupwa nje na kubatizwa jina la “huna akiri na wewe uliyepatwa na mkasa huu ukilikubali tu jina hili, umekwisha!.

Ukifahuru usijisifu sana na wala ukishindwa usijilaumu wala kuumia sana, kwani unapofahuru ni sawa na kusema “umekuwa mahili katika kujua yale tu kwa kiasi kikubwa wanayoyataka wengine”. Lakini tukumbuke kuwa yale wanayoyataka ni mambo machache sana ukilinganisha na yale yote unayoyahitaji ili kupata maisha ya ndoto yako. Unapokuwa umeshindwa tunasema husiumie sana kwasababu yawezekana yale uliyoyajua na kuyapenda kuyasoma hayakuwa mengi na hayakufundishwa kwasababu tu hayakuwa katika orodha ya yale wanayotaka wenye kazi. Kwahiyo, unaposhindwa mtihani usivunjike moyo bali huendelee kujiona kuwa wewe ni mwenye akiri nyingi na unaweza vitu vingi, isipokuwa vitu hivyo abavyo unaviweza, bado vingi haviko kwenye mitahala ya elimu rasimi ambayo umeshidwa. Habari njema ni kwamba, vitu hivyo unavyovijua vizuri, ukivitumia unaweza kutengeneza kazi kubwa yenye kukuletea matunda mengi sana, ambayo watu watakuletea pesa nyingi ili ujipatia matunda hayo.

Ukiwa wewe ni msomi, utakubaliana na mimi kuwa iwapo ukiamua kwenda nje ya mfumo wa ajira utagundua kuwa mambo mengi yaliyoko nje ya ajira ni tofauti kabisa na yale tuliyonayo vichwani mwetu na hasa sisi wenye shahada kutoka vyuo vikuu. Kumbe yale mambo ya nje ya ajira nayo yanahitaji kujifunza upya bila kujali kuwa wewe una cheti au shahada. Lakini, masomo ya nje ya ajira yenyewe hatuingii darasani bali tunajifunza kwa kuanza kufanya kile unachotaka kujifunza. Masomo ya mfumo wa nje ya ajira unanikumbusha maneno aliyowahi kuyasema mtaalamu wa zamani katika fani za hisabati na fizikia bwana Albert Einstein kuwa “ELIMU ni kile kinachobaki baada ya kuwa umesahau yale uliyofundishwa shuleni”. Hapa kwetu Tanzania, hali ni mbaya kwa maana yale tuliyofundishwa shuleni na vyuoni mengi hayatumiki nje ya mfumo wa ajira. Matokeo yake tunajikuta tunasahau mambo mengi, huku tukibakiza elimu kidogo sana, kitu ambacho kinafanya wasomi wengi kuishi maisha duni ambayo siyo maisha ya ndoto zetu.

Ukizingatia maneno ya Bwana Albert Einstein ni dhahiri kwamba, elimu iliyobaki vichwani mwetu ni kidogo, kiasi kwamba haiwezi kututoshereza kukabiliana na changamoto nyingi ambazo ziko nje ya mfumo wa ajira. Kwahiyo, wakati ni sasa ambapo tunatakiwa kuwekeza nguvu nyingi kwenye kujifunza haraka mambo mapya ambayo mengi hatukuweza kuyapata shuleni na kwenye ajira. Aina ya mambo ya kujifunza yatategemea mtu mweneywe pamoja na kazi anayopanga kuitengeneza. Jitahidi kujifunza kwa wale wote ambao wamefanikiwa katika kile unachopanga kukifanya kama wapo. Ili uweze ujifunza kutoka kwa wazoefu unahitaji kujifunza mbinu mbalimbali za kujenga mahusiano na urafiki kwa watu wanaokuzidi au wanaishi maisha yale unayoyataka. Tunahitaji kujifunza kwa kuanza na usomaji wa vitabu na makala mbalimbali, vyote hivi vitakuhamasisha na kukujenga kifikra. Fikra sahihi ndizo zitafungua uwezo wa akiri yako kuona na kuchangamkia fursa mbalimbali za kiuchumi, ambazo zitakuwezesha kupata utajiri au maisha yale unayoyatamani siku zote.

Mwisho! Kumbuka kuwa, karibia asilimia 90% ya watu walio na utajiri mkubwa ni wale waliotafuta pesa nje ya mfumo wa ajira ...... maana walitengeneza kazi!.

Mpendwa msomaji, endelea kuitumia vizuri MAARIFASHOP ili kujifunza mambo mbalimbali yatakayokuwezesha kupata mafanikio. Ili kupata makala mpya kila zinapochapishwa, bonyeza neno TUMA MAKALA MAARIFASHOP kisha sajiri barua pepe yako. Na kama unapenda kupata mafunzo ya kila siku kwa njia ya whatsap bonyeza neno MAFUNZO