Wednesday, April 29, 2015

Ni Vigumu Sana Kufanikiwa Kama Mara Nyingi Unaituma Pesa Yako Kununua Vitu na Kubakia huko Bila Kurudi




Mara zote ukishakupata pesa (kuingia mfukoni), kinachofuata huwa ni kuzitumia hata kama ukizitunza kwanza, mwisho wake huwa ni kutumika kwaajili ya kukidhi mahitaji ya vitu na huduma mbalimbali. Watu wengine upenda kusema kwamba “pesa ni mzunguko”. Mzunguko wa pesa una vipengele viwili ambavyo ni “Kuingia na Kutoka”. Kwa lugha rahisi tunaweza kusema kuwa pesa ina milango miwili, kuna mlango wa pesa kuingia na kutoka kwako.

Kwa yeyote anayetafuta mafanikio makubwa ni lazima kuangalia milango hii miwili (kuingia na kutoka) na hapa ndipo kuna tokea makundi mawili ya watu ambao ni masikini na tajiri. Kwa upande wa maskini tayari wamejenga hofu kubwa sana na muda wote wana wasiwasi ya pesa kutoka na kupotea. Kutokana na hofu hii, maskini wengi sana wemejijengea tabia ya kuibana pesa ikisha ingia mifukoni mwao, huku wakidhani kuwa hilo ni suluhisho la wao kutoishiwa na pesa. Matokeo yake linapokuja suala la kuwekeza au kuchangamkia fursa kubwa wanakuwa waoga sana wa kuthubutu kutokana na hofu ambayo imejengeka kwa muda mrefu ndani ya fikra zao.

Wenzao ambao ni matajiri wao, mara tu pesa inapoingia, kitu cha kwanza ujiuliza ni kitu gani wanaweza kukitoa ili kuondoa kero kwenye jamii ikiwemo le iliyowazunguka. Kwahiyo, wao uweza kuiachia pesa yao kutoka lakini kwa malengo ya kuituma malighafi ambayo pengine ikiunganishwa na mambo mengine uweza kurudi na bidhaa au Huduma ambayo ni hitaji muhimu kwenye jamii. Kwa kufanya hivyo, hata wale maskini walioogopa kuiachia pesa yao mwanzoni, wakati huu uweza kuituma kwa matajiri hao na mzunguko uendelea hivyo hivyo na mwisho ni umaskini uliokithiri.

Kama tulivyoona kuwa kuna milango miwili ya pesa kuingia na kutoka. Mlango wa kwanza ni wa kuingilia (pesa inaingia mfukoni) na wa pili ni wa kutokea (pesa inatoka nje ya mfuko wako). Pesa ikishatoka nje ya mfuko wako, kuna mambo mawili ambayo yanatokea; kwanza pesa inaweza kutumwa mali ambayo iwapo itaongezewa thamani na kutoa bidhaa au huduma ambayo ikiuzwa tena inarudisha ile pesa iliyotoka mwanzoni na nyongeza juu (faida) na hii yongeza ni kwasababu ya thamani iliyoongezeka.  Pili pesa inaweza kutoka nje ili kufuata vitu ambavyo kwako wewe unakuwa ni mtumiaji wa mwisho; kiasi kwamba pesa iliyotumwa vitu vya aina hii, kamwe haiwezi kurudi hata ungefanyaje.

Watu wengi hasa waajiriwa pamoja na wakulima, huwa pesa zao zikishatoka kwa mwenyewe, mara nyingi huwa hazirudi kwasababu ya kutumwa vitu ambavyo wewe ndiye mtumiaji wa mwisho. Sababu kubwa ya waajiriwa ufanya hivyo ni kwasababu ya kutegemea mshahara mwisho wa mwezi. Hali hii humfanya mtumishi pamoja na mkulima kuishi maisha ya kawaida sana ambayo huwa hayabadiliki miaka nenda rudi. Baadhi ya vitu ambavyo pesa ikitumwa kuvifuata yenyewe hairudi ni vingi sana; mfano: Runinga Redio, Karo za wanafunzi, gari la kutembelea, n.k.

Bila kuingilia mipangilio mbalimbali ya watu walionayo, unaweza kuona kuwa pindi tu tunapoanza kazi ya kuajiriwa tunaanza vizuri lakini muda mfupi tu! tunawahi kutekwa na utamaduni wa kupeleka pesa kule ambako huwa hairudi. Na kwenye jamii tulizomo watu wanahamasishana kufanya hivyo. Na mpaka sasa watu wengi wamekuwa wakiishi kwa mazoea, kwamba unapopata ajira eti unashauriwa na wenzako kununua kiwanja na kujenga nyumba ya kuishi na vitu vingine vyenye kupeleka pesa bila kurudi.  

Watanzania, tunahitaji kubadili tabia pamoja na mtazamo wetu juu ya mapato na matumizi ya pesa; tunahitaji kujifunza ni jinsi ya kutuma pesa ikarudi pamoja na vitu. Pia, tunahitaji kuwa na mikakati na mbinu za namna ya kuifanya iwe nyingi badala ya utaratibu uliozoeleka wa kubana matumizi. Tukiweza kuyafanyia kazi yote haya hakika tutakuwa tumepiga hatua moja muhimu sana ya kutufikisha kwenye mafanikio tuyatakayo.

Mpendwa msomaji, endelea kuitumia vizuri MAARIFASHOP ili kujifunza mambo mbalimbali yatakayokuwezesha kupata mafanikio. Ili kupata makala mpya kila zinapochapishwa, bonyeza neno TUMA MAKALA MAARIFASHOP kisha sajiri barua pepe yako. Na kama unapenda kupata mafunzo ya kila siku kwa njia ya whatsap bonyeza neno MAFUNZO

Monday, April 20, 2015

Kumaliza Siku Kabla ya Kuianza Ndiyo Siri ya Mafanikio Makubwa Maishani



Watu wengi tunatamani kupata mafanikio kwa lengo la kupata fursa ya kuishi maisha mazuri, maisha yenye furaha, maisha ambayo unaweza kusaidia wasiojiweza n.k. Lakini, waliowengi ndoto hizo, zinaonekana kuendelea kufifia kadili umri unavyozidi kuwa mkubwa!. Kwa kuangalia mifano ya watu wengi waliofanikiwa, unagundua kuwa mafanikio si kitu chochote zaidi ya kuwa na nidhamu ya kufanya vitu vya kawaida kila siku.
Mafanikio hayatokani na miujiza bali ni kitu kinachojitokeza kutokana na mambo ya msingi ambayo ni madogo madogo yanayohitajika kupangwa na kufanyika kila siku. Kwahiyo, tunaweza kusema kwamba, mafanikio ni ujuzi au kusoma vitu vya kawaida— lakini wakati mwingine tunahitaji mtu fulani wa kutukumbusha na kutuonyesha njia ambayo ni rahisi kufuata na kuweza kufikia mafanikio tunayo yataka. Na hapa nitaeleza umuhimu wa kuwa na mpango mzuri kama hatua mojawapo ya kufuata ili kuweza kufika kwenye mafanikio makubwa kuliko unavyoweza kufikiri.
Kujenga maisha, kujenga kitu chochote kile, ni kama kujenga nyumba; unahitaji kuwa na mpango. Chukulia mfano, kama ungeanza kubeba na kuanza kuweka matofari kwenye msingi alafu akatokea mtu akakuuliza “Unajenga kitu gani?” Je? Utaweka chini matofari uliyobeba na kumwambia kuwa hujui unacho jenga?” au utamwambia unachotaka kujenga kuwa ni nyumba hata kama bado haijajengwa. Mfano huu unatufungua akili na kutufundisha kuwa, mara zote“nyumba inaanza kujengwa mara tu inapokuwa imekamilika”.
Tukirudi kwenye maisha tunaona kuwa imekuwa vigumu sana kwa watu walio wengi kuweza kuweka mipango madhubuti ya maisha ya ndoto yao. Kwasababu ni ukweli usiopingika kuwa wengi wetu hatujabainisha kwa dhati kuwa uko mbeleni tunataka maisha ya namna gani na kwakuwa hilo halipo katika maandishi tumejikuta hatuna cha kupanga kufanya kwa siku, wiki, mwezi, mwaka au zaidi. Tunaamka asubuhi na kufanya chochote kinachojitokeza kwenye akili na fikra zetu. Kwa maana nyingine tumekuwa watu wa kushughulikia mambo mapya na matukio tu! Hii ni hatari na ni changamoto kubwa sana iliyoko mbele yetu.
Kila mmoja wetu ambaye haliziki na maisha aliyonayo kwa sasa, inabidi kujenga utamaduni wa kuwa na nidhamu ya kufikiri kwanza juu ya jambo ambalo unatarajia kulifanya. Baada ya kufikiri, unahitaji kuandika mawazo yako juu ya aina ya maisha unayotamani kuyaishi miaka mitano, kumi na zaidi ijayo, kwa kufanya hivyo utakuwa tayari umekamilisha nyumba kabla ya kuanza kujenga.
Ukijaribu kutafakali mafundisho mbalimbali kutoka kwa watu waliofanikiwa, utagundua kitu kimoja ambacho kinasisitizwa sana ni “usianze siku yako mpaka itakapokuwa imemalizika vizuri”—angalau orodha ya mambo ya kufanya. Jitahidi kuwa na orodha ya mambo ya kufanya kabla ujaanza kutenda kazi za siku, na mengi yawe ni yale yenye mchango katika kukufikisha kwenye malengo yako ya muda mrefu (k.m: miaka 5, 10, 25 au zaidi). Katika kupanga orodha ya mambo ya kufanya, jaribu kuacha nafasi ya kufanya marekebisho kadili utakavyoendelea, acha nafasi kwaajili ya mikakati ya ziada, lakini kikubwa hapa cha kusisitiza ni kumaliza kwanza jambo unalotaka kulifanya kabla ya kulianza. Usiaze wiki mpaka iwe imekamilika. Chora ramani ya jinsi itakavyokuwa, iwekee sura na umbo au weka jengo lake, na baada ya hapo anza kuifanyia kazi.
Utaratibu huu ufanyike kwa mwezi ujao—Usianze mwezi, mpaka uwe na mpango tayari mezani. Na kubwa zaidi, usianze mwaka mpaka umalizike kwenye karatasi. Siyo wazo baya, ikifikia mwisho wa mwaka, ukakaa chini na familia kwaajili ya kuweka mpango binafsi kwa mwaka ujao, kaa chini na weka mpango kazi, kaa chini na mshauri wako wa mambo ya fedha kuweka ramani ya jinsi pesa itakavyopatikana. Panga kalenda yako na kwa vitu vyote vinavyowezesha maisha yako kwenda mbele hasa kule unakokutaka.

Mpendwa msomaji, endelea kuitumia vizuri MAARIFASHOP ili kujifunza mambo mbalimbali yatakayokuwezesha kupata mafanikio. Ili kupata makala mpya kila zinapochapishwa, bonyeza neno TUMA MAKALA MAARIFASHOP kisha sajiri barua pepe yako. Na kama unapenda kupata mafunzo ya kila siku kwa njia ya whatsap bonyeza neno MAFUNZO

Friday, April 10, 2015

Siri ya Kinua Uchumi wa Kaya ni Kubadili Mtazamo Wako Juu ya Pesa

PESA NI MATOKEO YA BIDHAA NA HUDUMA; NA VYOTE HIVI UTOKANA NA KAZI
 Uchumi wa kaya hautakua iwapo kila mwaka unawazia kupata pesa bila kufikiria utazalisha bidhaa au huduma gani kwenye jamii yako, hasa jamii iliyokuzunguka, uchumi wako hauwezi kukua iwapo wewe kila mwaka unakuwepo kwenye orodha ya kaya za kupata msaada wa chakula kutoka serikalini au kwa wahisani mbalimbali. Unaposikia watu wakisema kuwa uchumi wa nchi fulani ni mkubwa, mfano: Japani, Marekani, China n.k. maana yake ni kwamba watu wa nchi hizo wamechapa kazi sana na kwa kufanya hivyo, wameweza kuzalisha bidhaa nyingi mbalimbali na hivyo kuweza kuvuna (kuchuma) kwa wingi.

Bidhaa yoyote lazima itokane na kazi na bidhaa kama bidhaa ndiyo pesa yenyewe. Mantiki hii inatukumbusha kauli aliyowahi kuitoa Rais wa zamani wa Tanzania Mwalimu Julius K. Nyerere, aliposema “Pesa Siyo Msingi wa Maendeleo” kauli hii ilikuwa ya kifalsafa zaidi, na  watu wengi wakati huo, hawakuielewa kwa mtazamo wa kwamba pesa  yoyote ambayo ni halali ni matokeo ya kazi halali. Badala yake, walio wengi waliipokea kauli hii  kwa uelewa tofauti na sana sana kwa mtazamo “hasi”. Kutokana na watu wengi kuwa na mtazamo hasi juu ya kauli hii ya pesa siyo msingi wa maendeleo, basi Mwalimu Nyerere alichukuliwa na kudhaniwa kuwa miongoni mwa watu ambao hawakupenda watanzania wapate pesa.

Falsafa ya “pesa siyo msingi wa maendeleo” bado inaendelea kupingwa hadi leo hii na kupingwa kwa falsafa hii, kunazidi kudhihilisha uelewa mdogo juu ya pesa. Na hapa ndipo tulipo jikwaa na kuanguka hasa kiuchumi, kwasababu watu wengi tunawaza kupata pesa ndipo tufanye kazi. Kaya nyingi kwa sasa zimetoa kipaumbele kwa shughuli ambazo zinaleta pesa hapo hapo (fasta) na hivyo kujikuta mwaka hadi mwaka wakiwa hawana muda tena wa kufanya vitu vyenye kuleta pesa nyingi baadae na kwa muda mrefu. Mara nyingi miradi yenye kuondoa umaskini kwenye kaya, inahitaji kuvumilia na kuwa tayari kufanya kazi bila kulipwa kwa muda huo huo (malipo baadae).

Hapo zamani wakati watu walipokuwa na mfumo wa biashara wa kubadilishana vitu moja kwa moja (bartering system), uchumi wa kaya ulikuwa imara sana, kwasababu kila mmoja ilibidi afanye kazi ili kupata bidhaa. Wakati huo, kulikuwa hakuna ujanja ujanja na ilikuwa vigumu kwa mtu kumzurumu au kuishi kwa rushwa kwani utaratibu ulikuwa ni kwamba ili upate bidhaa fulani, ulitakiwa uwe na bidhaa ya kwako. Jambo hili lililazimu kila mmoja mwenye uwezo wa kufanya kazi kuwajibika ipasavyo ndio aweze kuishi. Ni bahati mbaya sana baada ya kuingia mfumo wa pesa ambayo ukaa katikati ya muuzaji na mnunuzi wa bidhaa, watu wengi tukasahau, tukaanza kuweka nguvu na fikra nyingi kwenye kutafuta hicho kitu cha katikati “pesa” bila kukumbuka kuwa kitu ambacho huwaleta pamoja watu hawa wawili yaani muuzaji na mnunuzi, huwa siyo “pesa” bali ni BIDHAA.

Mara nyingi mtu anapouza bidhaa anapewa pesa kama uthibitisho wa kukiri kupokea bidhaa hiyo. Matatizo yanaanzia pale huyo mtu anaposahau ndani ya akili yake kuwa bado ile bidhaa anayo mikononi mwake, na cha ajabu, mtu huyo anaanza kuabudu na kuthamini sana ile “pesa” kuliko hata ile bidhaa aliyokuwanayo. Mfano: kama ni mkulima hatafikiria tena kununua mbegu bora au mbolea ili kujipanga kuzalisha mazao mengi zaidi msimu unaofuata. Kitakachotokea ni kwamba mkulima huyo atachukua pesa hizo na kufanyia vitu vingine tofauti na uzalishaji wa mazao, lakini ikumbukwe kuwa hiyo pesa anayotamba nayo ilitokana na kuuza mazao na si vinginevyo. Matokeo yake mkulima huyo, msimu unaofuata  anajikuta hana pesa tena ya kuendesha kilimo chake kwa tija zaidi na hivyo kujikuta akipata mavuno kidogo sana kuliko msimu uliopita!.

Ipo mifano mingi tu ya watu kutokuwa na tabia ya kukumbuka pesa waliyonayo ilitoka wapi na hivyo kujikuta wakitenga kiasi kidogo sana kwaajiri ya kuendeleza miradi hiyo ambayo ndio hasa uwaingizia pesa nyingi. Tunahitaji kutambua kuwa pesa tuliyonayo kuna kitu kinaileta na kwa maana hiyo tuweke nguvu zetu kwenye hicho kitu badala ya pesa yenyewe. Iwapo tutaanza kuiona pesa kwa mtazamo huu, tutakuwa tumepiga hatua kubwa kimaendeleo na kwakufanya hivyo tutakuwa tumejitenga na kundi kubwa la watu wenye mawazo ya wastani  wanaodhani pesa inapatikana kwa bahati! 

Pia, mtazamo wetu juu ya pesa ukibadilika, tutagudua kuwa huwezi kupata pesa kwa ujanja ujanja. Mambo yote haya yakifanyika, yatafanya uchumi wa kaya na taifa kwa ujumla kuweza kukua kwa kiwango cha kuridhisha. Ewe mtanzania, badili fikra zako juu ya pesa leo, tufanye kazi kwa bidii ili tuzalishe bidhaa na huduma mbalimbali, na kwa njia hii tutawezesha kaya zetu na taifa letu kuinuka kwa maana tutavuna (tutachuma) kwa wingi zaidi. Tukumbuke kuwa dhana nzima ya UCHUMI ni  kuchuma/kuvuna tulichokifanyia kazi” na hili ndilo dhumuni letu katika kupata maisha bora.

Mpendwa msomaji, endelea kuitumia vizuri MAARIFASHOP ili kujifunza mambo mbalimbali yatakayokuwezesha kupata mafanikio. Ili kupata makala mpya kila zinapochapishwa, bonyeza neno TUMA MAKALA MAARIFASHOP kisha sajiri barua pepe yako. Na kama unapenda kupata mafunzo ya kila siku kwa njia ya whatsap bonyeza neno MAFUNZO

Thursday, April 2, 2015

Mwanzo wa Kuipata Pesa ni Kuijua Kwanza




Je? Na wewe ni mmojawapo wa wanaotafuta pesa? Kama jibu ni ndiyo, hiyo pesa unajua ni nini? mbali na kufahamu sura tu ya sarafu na noti? Ukiacha hilo, kuna cha zaidi unachojua kuhusu pesa? Ikiwa jibu ni “hapana” sasa wewe pesa utazipataje wakati huzijui? Mara nyingi watu husema kuwa, “huwezi kuona kitu usichokijua”! Mpaka sasa, ufahamu na uelewa uliopo juu ya pesa ni mdogo sana labda tu! ufahamu uliopo ni wa kujua jinsi pesa zinavyogawanyika na walio wengi tunafahamu zaidi kutoa na kujumlisha pesa, hasa wakati wa kurudisha chenji kwa mteja. Ukiacha hilo, taswira kubwa na ndefu iliyopo nyuma ya pesa (noti na sarafu) haionekani kirahisi kwa watu walio wengi. Ufahamu na uelewa mdogo juu ya maana pana ya pesa upo kwa watu wengi, na hali hii ni kwa wote waliokwenda shule na wale ambao hawakwenda kabisa.  

Ukweli ni kwamba “Pesa ni kitu chochote kinachowezesha watu kubadilishana vitu na huduma. Hapa ndo kuna mkanganyiko kwasababu watu wengi mpaka sasa wanaamini pesa ni kitu halisi na hivyo kusababisha wao kuweza kuiabudu na kuamini pesa kama inavyoonekana katika hali yake ya noti na sarafu. Mtazamo wa kuichukulia pesa kama kitu halisi, unawafanya walio wengi kuwekeza nguvu kubwa Katika kusaka/kutafuta pesa yenyewe kama ilivyo. Lakini wakisha ipata wanagundua kuwa, hitaji lao siyo makaratasi ya noti bali ni vitu na huduma mbalimbali hapo ndipo huzipeleka kwa wenye vitu na huduma, huku wakibakia tupu kabisa.

Katika kutafuta pesa kunakuwa na dhamira tofauti kati ya maskini na tajiri; “Watu maskini wanawekeza muda na nguvu yao kwa dhamira ya kutafuta pesa lakini watu matajiri wanawekeza muda, akili na nguvu yao kwa dhamira ya kutafuta “vitu na huduma”. Kwasababu maskini wengi waliamini kuwa mwisho wa utafutaji wao ni pesa, basi ndipo ugundua kuwa sio mwisho, kumbe mwisho wao ni kupata vitu na Huduma (chakula, dawa, mavazi; usafiri, elimu, utaalam, nguvukazi n.k.). Kwahiyo, pamoja na kutafuta pesa hiyo kwa kutumia nguvu kubwa na muda mrefu, mtu huyo ujikuta akilazimika kuzipeleka mwenyewe kwa tajiri ambaye wakati huo ana vitu na huduma fulani fulani. Kwa maana nyingine tunaweza kusema kuwa watu hawa wanaishi kwa kutafuta pesa na kisha kulipa bill! au madeni basi.

Mahitaji ya mwanadamu ni mengi sana na hayana kikomo, lakini pamoja na hayo, mahitaji haya yamegawanyika katika makundi makuu mawili: yaani “Vitu na Huduma”. Tunaposema “Vitu” inamaanisha vitu halisi na vinavyoshikika kama vile nguo, meza, komputa simenti, gari, simu, vyombo, spare, vitabu n.k); na tunaposema “Huduma” ni vitu ambavyo havishikiki navyo ni kama; usafiri, habari, utaalam, ulinzi na usalama, maombi, ufundi n.k. Kwahiyo, kutokana na ukweli huo hapo juu, ndiyo maana siku zote pesa itakwenda kule kulipo na vitu au huduma hakuna sehemu nyingine.

Kutokana na ukweli huu, ni wazi kwamba unapoona pesa imeingia mfukoni mwako, basi ujue kuna mtu ametuma pesa hiyo kufuata kitu fulani kwako, na iwapo huna kitu chochote ulichonacho basi hutapata pesa yoyote kwasababu hakuna kitu cha kufuata kwako. Sasa unachotakiwa kufanya leo ni kuanza kubadili swali ambalo watu wengi ujiuliza pindi wanapohitaji kupata pesa; swali lenyewe huwa ni hili hapa: “Nitapata pesa wapi?” na kwa kuwa wengi ujiuliza  swali hilo, ndiyo maana huishia tu! kutafuta pesa bila mafanikio.

 Iwapo utaendelea kujiuliza swali la nitapata pesa wapi ndivyo itakavyozidi kuwa vigumu kupata jibu ambalo litakuongoza kupata pesa. Kwahiyo, mtanzania mwenzangu ni wakati sasa wa kubadili swali lako kutoka “nitapata pesa wapi?” kwenda “Pesa itakuja kwangu kufuata nini?”. Na kila mara utakapojiuliza swali la pesa itafuata nini kwako, basi jibu jibu lake tu! litakuwa ndiyo pesa yenyewe kwa maana nyingine utaona watu wakibisha hodi mlangoni kwako, kwaajili ya  kukuletea pesa ambayo miaka yote umekuwa ukikimbia huku na huko kuitafuta bila mafanikio!. Sasa unachotakiwa kufanya ni utafiti katika mazingira yanayo kuzunguka na maeneo mengine unayoweza kuyafikia ili kutambua mahitaji, kero na changamoto zilizopo. Matokeo ya Utafiti yatakusaidia kubuni na kuzalisha vitu au huduma ili kukidhi mahitaji ya jamii husika, na ukifikia hapo ndipo utaona ndani muda mfupi watu wakituma pesa ili ikafuate vitu na huduma kutoka kwako.

Kwahiyo, uwanja ni wako wewe mtanzania unayetafuta mafanikio, kwani tuna imani kubwa sana kuwa unaweza kupata pesa nyingi, iwapo utakubatia na kuifanyia kazi falsafa hii ya “Pesa itakuja kwangu kufuata nini?”.

Mpendwa msomaji, endelea kuitumia vizuri MAARIFASHOP ili kujifunza mambo mbalimbali yatakayokuwezesha kupata mafanikio. Ili kupata makala mpya kila zinapochapishwa, bonyeza neno TUMA MAKALA MAARIFASHOP kisha sajiri barua pepe yako. Na kama unapenda kupata mafunzo ya kila siku kwa njia ya whatsap bonyeza neno MAFUNZO