Sunday, November 13, 2016

Je? Unatafuta Utajiri Au Unaangaika Kuwa Maskini


“Mtu aliye na tabia ya kuangaika vile vile ana tabia ya kutaka kila kitu apate leo leo, mwisho wake anaambulia kupata vitu vidogo vidogo” ~ Cypridion Mushongi
 
Leo wakati natafakari juu ya utajiri, nimekumbuka sana mwanzoni mwa miaka ya 2000. Miaka hiyo nilikuwa na rafiki yangu ambaye alizoea kusema “Mwaga mtama kumkamata kuku kirahisi na usiangaike kumkimbiza kuku unaweza kuvunjika mguu kabla ujamkamata”. Ni kawaida kukuta watu wakikimbiza kuku pindi wanapohitaji kitoweo. Hali hii huwafanya wengine kuumia kwasababu ya kutumia nguvu nyingi kupita kiasi.

Tabia ya kumkimbiza kuku kila mara tunapohitaji kitoweo, inafanana sana na tabia tuliyonayo katika kutafuta utajiri. Ukifuatilia kwa undani utagudua kuwa michakato yetu ya kutafuta utajiri ni
ya kukimbizakimbiza, kuhangaika sana, kubahatisha na wakati mwingine ni ya kukurupuka. Mbinu ya kutumia “mtama” ili kumkamata kuku kirahisi inatufundisha umuhimu wa kujiandaa na kujipanga katika maisha hasa pale tunapoamua kutafuta kile tunachokipenda—“Utajiri”.

Tabia ya kuhangaika sana, imesababisha watu wengi kujawa fikra ya kwamba maisha ni magumu. Ndiyo maana unapokutana na baadhi ya watu ukawauliza hali ya maisha inavyowenda, utasikia wakisema “tupo tunaangaika” au “maisha ni kuangaika”. Wengine wanadiriki kusema bila kuangaika maisha hayaendi. Kimsingi dhana ya kuhangaika na maisha katika fikra zetu inaleta picha ya ugumu, woga, kukosa uvumilivu na hali ya kupenda njia za mkato.

Ukichunguza kwa undani neno kuangaika linaleta tafsiri isiyo rasmi ambayo ni ile hali ya mtu kubahatisha kile ambacho anajaribu kukifanya. Ni ile hali ya mtu kufanya mambo ambayo hayana mpangilio maalum. Unafanya mambo ambayo kimsingi hayana mtiririko wa kuleta matokeo makubwa yaani kila shughuli inajitegemea. Kila unapoamka, unafanya kile tu kilichojitokeza akirini mwako muda huo na inawezekana kabisa kitu unachofanya leo kisiwe na uhusiano kabisa na kile ulichofanya jana yake. Hii ndiyo staili ya maisha ya watu waliowengi.

Watu waliofanikiwa, wanahakikisha shughuli wanazofanya kila siku zinakuwa na mwendelezo maalum na zinakuwa na uhusiano wa moja kwa moja na kile kinachotarajiwa kupatikana ndani ya muda fulani; iwe ni baada ya mwaka mmoja, mitano, kumi na kuendelea. Watu waliofanikiwa wanatufundisha kuwa, utajiri hauji kwa kuhangaika bali ni kwa kujipanga na kufanya kile unachokifanya kwa hamasa na kwa kukipenda kile unachofanya.

Mtu yeyote aliye na tabia ya kuangaika vile vile anakuwa ni mtu wa kutaka kila wakati apate leo, matokeo yake anaishia kupata vitu vidogo vidogo, kama ni pesa zinakuwa ni kidogo. 

Mtu anayeangaika, hataki kusikia kitu kinachoitwa kusubili bali badala yake anataka leo leo. Ukishakuwa mtu wa leo leo, lazima utaangaika tu maana hakuna namna. Binafsi sijui wewe, siamini kama maisha ni kuangaika! Unapoona unaangaika sana ujue kuwa kuna kila dalili ya wewe kubahatisha kile unachokitafuta.

Suala zima la kuhangaika linaanzia kwenye fikra. Sisi ndio wenye kujiona tunahangaika. Endapo unafikiri na unaona kuwa unaangaika, basi hunabudi kufahamu kuwa kinachokusababishia kuhangaika ni tabia yako ya kupenda kupata leo.

Mtu anayehangaika huwa hafanyi vitu kumaliza au kuvifikisha mwisho, akifanya leo jambo lisiishe na likawa halikuzaa matunda ndani ya muda mfupi basi yeye mara moja anaacha kufanya tena anahamia kwenye jambo lingine jipya ambalo hana uzoefu nalo.

Mtu anayeangaika hana uzoefu wa kila kitu, kwa maana anashika hili na lile kila siku ilimradi mambo yaende. Wengine wana msemo wa kwamba “Bora mkono uende kinywani”. Endapo uko karibu na watu wenye kupenda kusema bora mkono uende kinywani, huu ni muda wa kuanza kukaa mbali nao, maana usipofanya hivyo watakupoteza.

Unapohangaika maana yake hautulii sehemu moja au kwenye kitu kimoja kiasi kwamba unakuwa ni mtu mwenye wasiwasi. Utajiri unahitaji kutulia kifikra, kimawazo na pia lazima ufanye vitu vyenye mwendelezo kila siku. Unapokamilisha kazi za siku moja thamani yake inayopatikana kila siku ndiyo uleta mafanikio makubwa au ushindi mkubwa “utajiri” kwa siku za mbeleni.

Wanaoangaika wana tabia ya kupenda kufanya vitu vingi kwa mara moja. Matokeo yake inakuwa ni kila kitu kugusagusa kidogo kidogo. Nguvu ambayo ingetumiwa kufanya vitu vichache na kuvikamilisha, inagawanywa au inatawanywa kidogo kidogo kwa shughuli nyingi. Mfumo wa maisha ya namna hii, ndiyo udhoofisha utendaji kazi, na kumfanya mtu kuwa mchovu wa kupindukia kila siku. Mtu anakuwa na msongo wa mawazo kwasababu tu ya kuzoea kila kitu kuhangaika. Mwisho na mwisho watu wanakuwa maskini.

Inaumiza sana kuona kila siku unafanya kazi nyingi, unachoka sana lakini kila unapotathimini mafanikio na maendeleo uliyoyapata miaka mitano au 10 iliyopita, huoni chochote cha maana. Yote haya ni kwasababu umeamua mwenyewe kuangaika kuwe sehemu kubwa ya maisha yako.

Acha kuhangaika, tulia na ujipange sawa sawa. Jitahidi kujua na kufahamu mwisho wa safari yako kabla ya kuanza safari. Lazima kuanzia mwanzo ujue unatafuta maisha ya namna gani. Anza kwa kujiuliza ndoto yako ya maisha mazuri unayoyataka miaka 5 au 10 ijayo ni ipi? kisha fikiria utafaya nini katika kipindi hicho chote, ni tabia gani utaibadili ili kuendana na maisha unayoyataka n.k. Ninakuhakikishia ukienda kwa mpangilio huo, utaanza kufanya vitu kwa kujiamini, utafanya kazi kwa bidii na hamasa kubwa. Mambo yote haya yatakupelekea kupata mafanikio makubwa ambayo ni endelevu bila kuangaika kama watu wengine – “Funguo za kila kitu kizuri unazo wewe, fungua sasa hivi”

Kwa maoni na ushauri bonyeza neno “MAARIFA SHOP” kuweka e-mail yako

No comments: