“Kama nina funguo za mlango wa asilimia 90 ya mafanikio yangu, sitajali sana endapo funguo za mlango wa asilimia 10 zitapotea” ~ Cypridion Mushongi.
Kuwepo kwa uongozi wa pamoja kumetupumbaza wengi kiasi kwamba watu wengi tumejenga tabia ya utegemezi wa fikra na mtazamo. Muda mwingi tumekuwa na matarjio makubwa kutoka kwenye uongozi wa pamoja. Lakini ikumbukwe kuwa uongozi wa pamoja au wa jumla unatokana na uongozi wa mtu mmoja mmoja. Bila kuimarika kwa uongozi wa mtu mmoja mmoja, maisha..
yetu yatakuwa duni sana.
Lengo kuu la kuwa na uongozi wa pamoja ni kuhakikisha uongozi wa mtu binafsi unaendeshwa katika mazingira ambayo mamlaka ya mtu mmoja mmoja haziingiliani, na kuhakikisha kuna usalama kwaajiri ya kufanya shughuli zetu.
Malengo mengine ya pamoja ni kuhakikisha tunavuna rasilimali kwa kufuata utaratibu tuliojiwekea wenyewe ili kuhakikisha vizazi vijavyo vinafaidika na rasilimali hasa zile za asili n.k. Pia ni kuweka utaratibu wa elimu na maarifa, kutengeneza njia ambazo zinarahisisha usafiri wa watu na mali zao.
Kwa ujumla kazi ya uongozi wa pamoja ni kutengeneza na kuweka mazingira rafiki, ili kila mmoja wetu aweze kufanya kazi kadiri awezavyo na kwa kiwango cha juu zaidi.
Tatizo kubwa tulilonalo kwasasa ni uongozi na usimamizi wa mambo binafsi. Watu wengi hatufanyi kazi zetu sawa sawa na badala yake, macho na masikio yetu tumeelekeza zaidi kwa uongozi wa jumla au wa kijamii, kiasi kwamba muda mwingi tunabaki kushangaa na kujiuliza ni kwanini uongozi wa kijamii hauboreshi maisha yetu?; hauleti maendeleo yoyote?; hauleti chakula n.k. Maswali haya na mengine mengi, ni vitu ambavyo vimeteka mawazo ya watu wengi hapa nchini. Kwa mfano; mpaka sasa watu wengi tuna kilio cha kuletewa maemndeleo, lakini hatuna muhafaka wa maendeleo gani tunataka.
Pia, unaona kwamba wengi tunaamini sana kuwa maendeleo yetu yataletwa na watu wengine hasa viongozi wa kijamii. Kimsingi imani za namna hii juu ya maendeleo, hazitatukomboa kwa namna yoyote ile.
Ukweli ni kwamba wakati uongozi wa kijamii ukiendelea kutimiza majukumu yake, suala la kutafuta maendeleo na mafanikio linabakia kuwa la binafsi zaidi. Lazima kila mmoja wetu awe na ndoto ya maisha gani mazuri anataka awe nayo.
Kutokana na tabia yetu ya kupenda kuongozwa na jamii kila wakati, tumejikuta hatuna hata dira binafsi. Ndiyo maana kila inapofika wakati wa bajeti ya kitaifa, unakuta wengi tuko kwenye runinga (TV), kuona bajeti inatusaidiaje. Lakini kumbuka kuwa wao wanapanga bajeti kwaajiri ya mambo ya jumla jumla au ya kijamii, ambayo yanachangia si zaidi ya asilimia 10 ya mafanikio ya mtu mmoja mmoja. Kwa maana nyingine ni kwamba mtu binafsi anawajibika kujiletea maendeleo kwa asilimia 90.
Kama ninawajibika kujiletea maendeleo binafsi kwa asilimia 90, maana yake ni kwamba kiongozi wangu mkuu ni kichwa changu. Kumbe inabidi kuwe na uboreshaji wa kichwa (akiri) nikimaanisha kuboresha fikra, mtazamo, taarifa ulizonazo n.k. lakini haya ninayosema huwezi kuona umuhimu wake mpaka pale utakapotambua mipaka ya uongozi wa kijamii. Kama unadhani na kuamini kuwa uongozi uliopo nje ya kichwa chako utakutendea miujiza au utakuletea maendeleo pole sana, maana haitakaa itokee hivyo unavyotaka.
Kwanini tunasema kiongozi wako mkuu ni kichwa chako?
Mafanikio yoyote yanaendana na uwezo ulionao katika kuchagua, kuamua na kutenda. Wale walio na uwezo wa kuchagua, kuamua na kutenda, ndio wenye uwezo pia wa kuwa matajiri wakubwa na kupata mafanikio makubwa.
Kichwa chako ndicho kinakuongoza juu ya nini ufanye, uache na utende. Yote haya yanatendeka pasipo kuonekana lakini matokeo yake baada ya muda huweza kuonekana kwa macho ya wengi. Na hapa ndipo unaona watu wanashituka wakidhani umepata jana tu kumbe ni mrudikano wa matokeo yaliyokuwa yakipatikana kidogo kidogo kutokana na maamuzi na matendo yetu ya kila siku.
Kumbuka kuwa hivi ulivyo ndivyo akiri yako ilivyo. Lakini kama hali uliyonayo hauipendi, bado unayo nafasi ya kuweza kubadirisha na kuwa katika mwelekeo unaoutaka wewe. Bado nafasi unayo ya kufanya mabadiriko makubwa katika maisha uyatakayo.
Kwakuwa kiongozi mkuu wa maisha yako ni kichwa chako, jitahidi kukitumia vizuri sana katika kufanya yale yote ambayo ungependa yatokee maishani mwako. Usipende kulalamika kutokana na kudhani kwamba watu wengine wapo tu kwaajiri ya kufikiri na kutenda kwaniaba yako.
Ndiyo, maana hata tukipata uongozi wa kijamii unaotimiza majukumu yake kwa asilimia 100, bado mchango wake kwenye maendeleo yetu binafsi hauzidi asilimia 10! Kama hivyo ndiyo, kwanini ninapoteza muda mwingi wa maisha yangu kuangaikia kupata asilimia 10 ya maendeleo/mafanikio? Isitoshe, hiyo asilimia 10 sina uwezo binafsi wa kufanya ipatikane, isipokuwa nina uwezo wa kusababisha asilimia 90 ya maendeleo yangu binafsi ipatikane ikiwa ni pamoja kuamua ni muda gani nipate maendeleo ya aina fulani.
"Kama nina funguo za kufungua mlango wa asilimia 90 ya mafanikio yangu binafsi, sitajali sana endapo funguo za kufungua mlango wa asilimia 10 ya mafanikio zitapotea".
Kila unapoianza siku yako jiangalie kwenye kioo na ujiulize swali hili: Mimi ni nani? Jibu: “Mimi ni kiongozi mkuu wa maisha yangu na ndiye niliye na funguo za asilimia 90 ya mafanikio yangu na leo ninakwenda kufungua tena”.
Endelea kujifunza kupitia hapa MAARIFA SHOP , ili upate kujiongoza na siyo kulalamika kila kukicha.
No comments:
Post a Comment