“Maskini anatumia muda wake mwingi kufanya kazi za watu wengine na akilipwa pesa anaitumia yote kununua suruhisho kutoka kwa watu wengine ili kutatua matatizo yake” ~ Cypridion Mushongi.
Kila wakati inapotajwa biashara, wengi wetu tunawahi kufikiri kuwa ni kununua vitu kwa bei ya chini na kuuza kwa bei ya juu. Hii siyo maana halisi ya neno “biashara”. Biashara ni..
ile kazi unayofanya, unayoipenda na ambayo hujapangiwa na mtu. Kwa maneno mengine ni kwamba unajipangia mwenyewe, unaguswa kufanya kile unachofanya baada ya kuona kuna tatizo fulani na wewe moyo na akiri yako vikakusukuma kutafuta suruhisho.
Ukweli ni kwamba kazi nyingi ambazo zimewahi kuwaletea heshima na utajiri baadhi ya watu hapa duniani, ni zile zilizotatua matatizo na kero za watu wengi. Ndiyo maana ninasema “matatizo ya watu wengine ni biashara kwako”.
Kwa maana nyingine ni kwamba “kila tatizo duniani ni biashara”. Kulitambua hili tu peke yake ni mtaji na ni biashara tosha kwako unayesoma makala hii. Nasema hivyo kwasababu, uzoefu umeonyesha kuwa watu wengi hawajaweza kuwa na mawazo ya biashara yanayotokana na matatizo au kero zilizopo kwenye jamii—wachache sana wanafanya hivyo.
Mimi kama mtaalam wa mambo ya uchumi na kocha wa masuala ya ujasiriamali, biashara na uwekezaji mara nyingi nimefuatwa na watu wakiomba ushauri juu ya biashara gani wafanye, ambayo itaweza kuwalipa haraka iwezekanavyo! Unakuta mtu anakwambia mimi nina mtaji wa shilingi milioni 10 lakini sijui nifanye biashara gani itakayonitoa kimaisha.
Kama mtaalam na kocha nimegundua kuwa rafiki zangu hawa wanahitaji mwongozo wa jinsi ya kugeuza matatizo yaliyoko tayari kwenye jamii kuwa biashara kubwa. Maana bila mawazo kama haya ya kugeuza matatizo kuwa biashara, hata kama una mtaji mkubwa kiasi gani hautaweza kufanya lolote la maana.
Inawezekana tu kugeuza matatizo kuwa biashara, endapo utaweza kuleta suruhisho la matatizo yaliyopo. Kwahiyo, ni sahihi kabisa tukisema kuwa “biashara yako ni sawa na suruhisho unazotoa kutatua matatizo ya watu wengine”. Unapotambua tatizo ndani ya jamii ya watu fulani, kazi yako wewe ni kutumia akiri zako zote kutatua lile tatizo. Ukishakuwa umetatua, maana yake umepata suruhisho la tatizo husika. Kinachotokea ni kwamba watu ambao tayari walikuwa wakiguswa na tatizo hilo watamiminika kwako kupata suruhisho hilo.
Kwahiyo, kupitia mfumo wa kubadirishana ina maana watakuachia pesa na wewe utawapa suruhisho lako nawe utabaki na pesa zao—na hiki ndicho wengi tunatafuta. Kwahiyo, jinsi dunia ilivyo ni kwamba kama wewe unataka pesa nyingi lazima utatue matatizo mengi. Kwa maneno mengine ni kwamba “pesa uliyonayo ni sawa sawa na kiwango cha matatizo unayotatua kwa watu wengine”. Kama muda wako mwingi unautumia kutatua matatizo ya kwako binafsi basi ujue hakuna atakaye kuja kununua suruhisho, kwasababu wewe una suruhisho kwaajiri ya kutatua matatizo yako tu!
Sasa kama matatizo yaliyopo duniani ni biashara inakuwaje sina biashara?
Huna biashara na ni maskini kutokana na ukweli kwamba, ile pesa kidogo unayoipata unaitumia kununua suruhisho kutoka kwa watu wengine na kwakufanya hivyo wewe unakuwa ni mtu wa kutumia pesa na sikuzalisha pesa. Kwahiyo, wewe siyo rahisi kutajirika kwani kila pesa unayoipata huiwekezi katika kutafuta suruhisho la matatizo ya watu wengine.
Wakati mwingine inaweza kuwa vigumu kutatua matatizo yako binafsi uliyonayo na hivyo kulazimika kununua suruhisho kutoka kwa watu wengine, lakini wakati huo huo ukazidi kutumia sehemu ya muda wako kutatua matatizo ya watu wengine kwa kuja na suruhisho au ufumbuzi.
Watu waliowengi wanatumia muda wao mwingi kufanya biashara za watu wengine, na wanalipwa pesa kwa kufanya hivyo. Jambo la kusikitisha ni kwamba, pesa yote unayolipwa kama mshahara kutokana na kufanya kazi za watu wengine, inatumika yote kununua suruhisho kutoka kwa watu wengine—hii ni ajabu kabisa!
Wakati mwingine si vibaya kufanya kazi za watu wengine (ajira). Kibaya ni kutumia pesa yote itokanayo na ajira kununua suruhisho la matatizo yangu kutoka kwa watu wengine—yaani wewe hautatui tatizo la mwingine isipokuwa wewe tu! Kama hivi ndivyo kila siku, basi tambua kuwa umaskini na ufukara lazima iwe halali yako. Tulioajiriwa tunahitaji kujiwekea utaratibu wa kutenga kiasi cha pesa kila mara tunapolipwa pesa yoyote kutokana na ajira tuliyonayo.
Zoezi hili la kutenga pesa lifanyike kwa malengo ya kuanzia angalau muda wa mwaka mmoja na kuendelea; mf. Miaka 5, 10, 20…...n.k. Ukitaka kufanya miaka zaidi ya 10 ni sawa, maana suala ni wewe kuamua. Pesa uliyotunza kwa kipindi cha kuanzia mwaka mmoja hata kama ni shilingi laki mbili (200,000/-), inatosha kabisa kwa wewe kuwekeza katika kuanza kutatua matatizo ya watu wengine—leta suruhisho la matatizo na kero za watu wengine. Kumbuka kuwa ukiwa na suruhisho la matatizo ya wengine lazima watakuletea pesa ili wao wapate kutumia suruhisho lako kutatua matatizo yao, na hapa ndipo utajipatia pesa nyingi na hatimaye kupata uhuru wa kipato.
Najua utaniuliza sasa watu wote wakifanya hivyo nani ataajiriwa? Natambua kuwa watu wote hawawezi kuwa sawa na hawawezi kufanana, lazima kuna watakao kuwa wanaanza kuajiriwa ili kujifunza kazi na wengine kutafuta mtaji. Kinachotakiwa ni watu kujenga utamaduni wa kung’atuka baada ya kuwa tumetumikia ajira zetu angalau kwa kipindi kisichozidi miaka 5 au 10.
Baada ya kung’atuka kwenye ajira kazi iwe ni moja tu! kuanza kutatua matatizo ya watu wengine na kwakufanya hivyo, tutakuwa tumepunguza tatizo la ajira duniani. Kwasasa, tatizo la ajira lipo sana hasa kwenye nchi zinazoendelea—Tanzania! kutokana na ukweli kwamba, watu tukishakuwa tumeajiriwa tunakaa kama waajiriwa kwa muda mrefu sana, kiasi kwamba pale inapowezekana tunaomba tuongezewe miaka baada ya kufikisha umri wa kustaafu—miaka 60.
Ndugu msomaji wangu wa MAARIFA SHOP huu ni wakati wako wa kuacha kutumia muda wako mwingi kutatua matatizo yako binafsi, kwani kwa kuendelea kufanya hivyo, itakuwa ni ndoto kupata pesa ya kutosha kuishi Maisha yale unayoyapenda. Kuanzia sasa jikite zaidi katika kutafuta suruhisho la matatizo ambayo yamekuwa sugu kwenye jamii yako.
Watu wanazo pesa nyingi na wako tayari kutupatia kwa hiari sisi ambao tunafanya kazi usiku na mchana kujaribu kutatua matatizo, kero na changamoto za watu wengine na ndiyo maana tunasema kwa hali hii “Utajiri ni lazima”. Ninapomalizia kusoma makala hii nitaendelea kukumbuka maneno haya “Pesa zitakuja kwangu endapo nitajikita katika kutoa suruhisho la matatizo ya watu wengine”
No comments:
Post a Comment