Tuesday, March 27, 2018

Umuhimu wa Kutambua Kabila Lako Jipya ni Huu



Kabila ni kundi la kipekee ambalo linajitegemea katika kuendesha maisha yake. Kwa kiasi kikubwa kabila, ni kundi ambalo linajitosheleza, na watu wake wanachangamana kwa kiasi kidogo sana na jamii pana ya kitaifa. Pia, kabila ni mgawanyiko wa..
mahusiano ya kijamii katika jamii ya jadi, ambayo inahusisha familia au jamii ambazo zinaunganishwa na ujamaa, uchumi, dini au undugu wa damu, ikiwa na utamaduni sawa, lugha na matamshi yanayofanana, na mara nyingi zinakuwa na kiongozi anayetambulika kwao.

Ni ukweli usiopingika kuwa, linaloitwa kabila limebaki jina tu siku hizi! Kwasababu, watu wa asili moja kwasasa wana mtazamo tofauti wa maisha, imani tofauti, uelewa na elimu tofauti, wanaongea lugha tofauti, shida na changamoto tofauti, matumaini na matarajio tofauti. Mabadiliko haya yamesababishwa na vitu vingi, ikiwa ni pamoja na; uwepo wa ongezeko la matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano, ongezeko la watu walioelimika zaidi, urahisi wa watu kusafiri kutoka sehemu moja kwenda nyingine, n.k.

Kutokana na mabadiliko hayo, watu wengi kutoka kabila moja la asili hawana tena mshikamano kama zamani, ambao kimsingi ulitokana na kuishi maisha yanayofanana karibu kwa kila kitu. Kukosekana kwa kundi (kabila) ambalo mnafanana, kunakufanya wewe binafsi ukose nguvu na hamasa ya wewe kupambana na hali yako. Kwa namna yoyote ile binadamu tunahitaji sana kushirikiana na watu wengine, ili kupata mafanikio makubwa. Wataalam wanasema kwamba pale mnapokutana watu mnaofanana na kujumuika pamoja, kuna furaha ya ajabu uweza kutokea na hivyo kumfanya kila mtu kufunguka.

Tumezoea kuwa watu hawachagui kuwa katika makabila yao ya asili – yaani, unapata tu kabila lako la asili pindi tu unapozaliwa. Kutokana na mazoea haya, wengi wetu hatujishugulishi na mchakato wa kutafuta/kutambua kabila letu halisi (jipya) nje ya lile la asili. Nadhani hata wewe unayesoma makala hii, utakuwa unajiuliza maswali mengi juu ya kwanini mtu anatakiwa kutafuta kabila lake halisi? Kwasababu, umehubiliwa sana juu ya athari za ukabila! Lakini, kwa wale wote tulio na ndoto ya kufanikiwa, huu ndio wakati muhafaka wa kutafuta kabila letu halisi – “waweza kuliita kabila jipya”.

Tunahitaji kufahamu kwamba, kabila jipya haliwezi kupatikana hivi hivi, lazima kuwe na jitihada fulani fulani, ambazo unatakiwa kuzifanya wewe binafsi. Bila jitihada, itakuwa vigumu sana kupata kabila lako halisi na huo ndio utakuwa mwanzo wa kuporomoka kwa uchumi wako na kukosekana kwa furaha ya kweli maisha yako yote. Kwahiyo, ni muhimu sasa kutafuta watu popote duniani ambao mna mfumo wa imani unaofanana, shauku na hamu ya maisha bora inayofanana, lakini pia, lazima kuwa karibu na watu ambao maadili yao yanafanana na yako.

Nitawezaje kutafuta kabila langu halisi (jipya)?

Anza na Elimu binafsi: Kutafuta kabila lako halisi au jipya ni rahisi sana, kama unayo nia ya dhati ya kubadili shauku yako kuwa taaluma. Katika kubadili shauku yako kuwa taaluma, kitu cha kwanza unachotakiwa kufanya ni kuanza kukazania sana suala zima la “elimu binafsi” – hii itakuwa ndio mlango wa kila kitu utakacho. 

Elimu binafsi ni elimu ambayo muhusika hafuati mfumo rasimi. Mtu binafsi, ndiye unayeamua usome na ujifunze kitu gani, muda gani ujifunze, na kipi ukifanyie kazi. Kwa maneno mengine ni kwamba, chini ya utaratibu wa “elimu-binafsi”, ni wewe unajiendeleza kielimu kulingana na kile kitu ambacho una shauku na msukumo wa ndani kukifanya kwa malengo ya kuboresha maisha yako au kupata mafanikio unayoyataka. Kwasasa elimu binafsi inawezekana sana, kwasababu, unaweza kujifunza taaluma yoyote kuanzia tiba hadi kupiga picha. Siku hizi kuna kozi nyingi sana, kinachohitajika tu! ni wewe kumiliki simu au komputa basi!

Ni kwanini “elimu-binafsi” sasa? Kwasababu, ile elimu uliyopata shuleni na baadae chuoni, kwasasa, yenyewe peke yake, haina uwezo tena wa kukuwezesha kukabiliana na changamoto zilizopo. Mafanikio ya kweli kwasasa, hayawezi tena kuletwa na elimu ya cheti, diploma au shahada peke yake. Naweza kusema kwamba, uwezo wa kupata mafanikio makubwa kupitia elimu rasimi peke yake unazidi kupungua siku hadi siku.

Kupitia elimu binafsi, tunapata fursa kubwa na uwezo mkubwa wa kujitambua, kujifahamu, kutambua nguvu na udhaifu uliopo. Pia, unapata fursa ya kujua ukweli juu ya wewe mwenyewe binafsi – unapata kujua wewe ni nani katika watu wa jamii ya kitanzania na dunia kwa ujumla.

Tunaposema wewe ni nani maana yake ni kwamba, tunataka ndani ya nafsi yako utoe msimamo juu ya haya; (mahusiano na watu, kazi, ajira, pesa, afya, mafanikio, kusaidiana, dini, upendo, kutoa zawadi, familia na ndugu, kuinua wengine, unapenda kufanya nini n.k.). Vyote vilivyotajwa hapo juu na vingine vingi, vinahitaji wewe kuvitafakari kwa kina hasa kutokea ndani yako. Baada ya kutafakari, lazima utengeneze au utoe msimamo wako wa jumla, juu ya namna gani unavyoweza kuyaishi mambo yote yaliyotajwa hapo juu kwa muda wote wa maisha yako hapa duniani. Msimamo wa jumla juu ya mambo mbalimbali ya kijamii, kiuchumi, kiimani na maisha kwa ujumla ndio utakaokutofautisha wewe na watu wengine.

Ukishatambua vizuri kuwa huyo mtu "anayeitwa wewe" ni nani hasa, ni rahisi sana kuanza kujitofautisha au kujifananisha na watu wengine. Ukishajitofautisha na wengine, husiishie hapo, badala yake endelea na hatua ya pili ambayo ni “kutambua kabila lako jipya”.

Pili, tambua kabila lako: Katika kulitambua kabila lako unapaswa "kujiambia ukweli" juu ya wewe hasa; kuanzia na unataka nini, una changamoto gani, una fursa zipi, nani ni maadui zako, njia ipi ukiifuata itakufikisha haraka unakotaka kwenda n.k. Wakati mwingine unaweza ukaangalia vitu vinavyokusumbua maana kuna watu wengine nao wanasumbuliwa na hivyohivyo! Pengine unataka kupunguza unene, kuna wengi wana malengo hayo hayo, unataka pesa nyingi wako watu kama wewe pia; unapenda kuwa mtu mwenye kuwa na uhuru wa kuchagua chochote kile unachokipenda – wako wengi wanaotaka hivyo. Uzuri ni kwamba, ukijitambua wewe ni nani, ni rahisi sana kujitenga na watu ambao siyo wewe.

Ukishajitenga na wale wote ambao siyo wewe, unatakiwa kutoka nje na kuionyesha dunia kuwa wewe ni mtu wa namna gani kulingana na vile vyote unavyofanya, vile unavyoamini, vile unavyopenda na vile vitu vya thamani unavyotoa au kuzalisha. Kwakuweza kuionyesha dunia vile ulivyo pamoja na thamani unayotoa kwa wengine. Watu wengi watakaojiona wanafanana na wewe (watu sahihi), wataanza kuonyesha nia na shauku ya kushirikiana na wewe katika nyanja mbalimbali za kimaisha. Kimsingi ni kwamba, hapa unatafuta na kutafutwa na watu wote wenye kuwa na hamu inayofanana, maumivu na machungu yanayofanana na ya kwako-(watu sahihi).

Kadili watu wengi watakavyozidi kupata uelewa juu yako, ndivyo idadi ya watu wenye nia na madhumuni kama yako itakavyoendelea kuongezeka kwa kasi. Idadi ikishakuwa kubwa mtashitukia mmetengeneza jumuia ya watu wenye malengo na mitazamo inayofanana, na kuanzia hapo tayari utakuwa umepata kabila lako halisi au jipya! – hili unalijenga kwa kuzingatia maslahi ya mafanikio na maendeleo. Kabila jipya, linakuwa la msaada zaidi kimaendeleo kuliko hilo kabila lako la asili (kuzaliwa), japokuwa, kabila lako la asili nalo lina nafasi yake, lakini siyo kubwa kama hili jipya. Ukishakuwa kwenye kabila lako jipya, unatakiwa kuendelea na jitihada za kujenga mahusiano na mshikamano na watu wa kabila lako kwa lengo la kusaidiana, kufundishana na kuhamasishana juu ya kutimiza ndoto za maisha ya mafanikio.

Tatu, zama ndani ya kile unachofanya: Kama ambavyo mtu atakaye kujifunza lugha mpya haraka hujitahidi kuzama ndani ya mazingira na mila au tamaduni za lugha unayotaka kujifunza; vivyohivyo, njia ya haraka ya kutimiza ndoto na malengo yako ni kuzama ndani ya malengo yenyewe. Kwa mfano; kama ndoto yako ni kutafuta ajira, lazima uzame ndani zaidi kwenye hilo, ikiwa ni pamoja na kusoma vitabu vinavyohusiana na aina ya ajira unayoitaka, kutengeneza wasifu wako ukawa tayari muda wote, utajifunza mbinu za kufahuru usahili, na tabia nyinginezo utakazoona zinafaa. Kama malengo yako ni kuwa mwana masumbwi bora (ngumi za kulipwa), itabidi kuzama ndani kwa kurukaruka kamba kila siku asubuhi, mazoezi ya kupiga ngumi viroba vya mchanga, kuwa na programu ya kuangalia video za mashindano ya ngumi n.k.

Kwa maana nyingine ni kwamba, mkakati wowote wa “kuzama kwa undani” ni kipindi ambacho unapaswa kujitolea sana juu ya jambo unalolifanya au unalotaka kulifanya. Suala hili la kujitolea wewe binafsi linahitaji nguvu kubwa ya akiri, fikra na msukumo wa ndani. Nguvu hii, inaweza kupatikana kwa kujumuika pamoja na watu ambao wana maadili yanayofanana au kushabiiana na yako. Kwahiyo, ni muhimu kukutana na kabila lako, ili kutafakari, kujifunza, kusherekea na kufurahi pamoja. Unapokutana na kabila lako au wenzako mkajadili kwa undani mada fulani, mkafurahi pamoja, kuna kitu fulani cha kusisimua huwa kinatokea ndani yenu. Msisimko na furaha ipatikanayo kutokana na kuzama ndani ya jambo fulani, umwezesha kila mmoja wenu kujifunza vizuri zaidi kutoka kwa wengine, lakini pia na wewe unapata fursa ya kufundisha watu wengine.

Siku zote, mkusanyiko wa watu mnaopendana na mnaoaminiana, unasaidia sana katika kujifunza mambo mengi mazuri kutoka kwa marafiki na jamaa wa kabila lako jipya. Baada ya kujifunza, kutafakari na kufurahi pamoja kupitia matukio yanayowakutanisha pamoja watu ambao mna mtazamo na maadili yanayofanana, kila mmoja huweza kurudi nyumbani akiwa tayari na mawazo mapya ya kimafanikio na maendeleo. Pia, matukio ya pamoja kama hayo, husaidia sana katika kumjenga mtu upya – kifikra, kimawazo na kimsimamo. 

Kutokana na fikra na mawazo mapya, watu huweza kuongeza ubunifu wa hali ya juu, ambao huwawezesha kuzalisha vitu vyenye thamani kubwa. Ili yote haya yatokee, lazima kuendeleza na kukuza elimu yako binafsi, tambua kabila lako jipya na kupitia kabila hilo, muungane katika kuandaa na kufanikisha matukio ya kukutana pamoja kwa lengo la kujifunza/kufundisha wengine na mwisho mfurahi pamoja na ikiwezekana angalau mkutane mara moja au mbili kwa mwaka.

Kuweza kubadili mtazamo na fikra ni jambo linalohitaji sana kujitoa kwa kuzama ndani ya falsafa unayopenda kuiishi. Ndiyo, maana ni muhimu sana kuzungukwa na watu wanaokutia hamasa na kukuweka vizuri. Pili ni muhimu, kulisha ubongo wako maarifa na elimu inayofanana na jinsi unavyotaka kuwa.

Suala la maarifa na elimu ndiyo umekuwa msingi wa kuanzishwa kwa blog hii ya https://maarifashop.blogspot.com: Lengo likiwa ni kukuzamisha zaidi kwenye mtazamo na fikra mpya za pesa, biashara, uongozi na uchumi ambazo zote hizo zinaweza kubadili maisha yako kuwa mazuri hadi kufikia kiwango unachokitaka.

Ni matumaini yangu kuwa, kuna kitu cha msaada umekipata baada ya kusoma makala hii na kwakuwa kazi ya kujifunza ni endelevu, basi endelea kuufanya mtandao wako wa
MAARIFASHOP kuwa miongoni mwa kimbilio lako hasa pale utakapokuwa umeamua kuzama ndani ya jambo lolote linalohusu uongozi, pesa, uwekezaji, biashara, uchumi na afya ya jamii. Kujifunza zaidi bonyeza neno niunganishe" kwa lengo la kuwa karibu zaidi na mtandao huu muhimu.

Kupata mafunzo kila siku kwa njia ya whasap bonyeza neno MAFUNZO

1 comment:

palmyrayapp said...

The 12 Best Casino Websites to Visit In 2021 - Mapyro
Discover 강릉 출장샵 the best casino sites to visit. 계룡 출장마사지 Find all the best casinos to play slots, table games, poker 광주광역 출장샵 and casino games in 광명 출장샵 one 사천 출장샵 place!