Tuesday, February 27, 2018

Andika Mawazo Yako na Ukae Kimya

Watu wengi wana mawazo mazuri, wana ndoto kubwa, lakini mojawapo ya sababu ya kwanini hakuna kinachofanyika ni kwamba wengi tunaongea sana. Utakuta mtu ndo kwanza amepata wazo la kufanya kitu fulani, lakini saa hiyo hiyo anaanza kuwashirikisha anaowaita marafiki zake. Na kuanzia hapo inakuwa kila siku ni...
kuongea ongea juu ya wazo hilo jipya. 

Baada ya siku si nyingi, anapata wazo jingine na hapo lile la mwanzo linasahaulika na anaanza kuongelea wazo jipya. Mwisho wake ni kwamba unaendelea kujenga mazoea ya kufikiri wazo na kulitoa kwa marafiki na ndugu basi! Matokeo yake miaka inavyozidi kwenda unajikuta huna mradi wowote wa biashara ambao umeweza kuufanikisha.

Tabia hii ya kupenda kuwashirikisha wazo lako changa watu wengine, inakuingiza kwenye hatari kubwa sana. Kwasababu hao unaojaribu kuwashirikisha wazo lako, yawezekana ni watu ambao hawajawahi kuwazia wazo lako kwa kiwango ambacho wewe unafikiri juu ya wazo hilo. Lakini pia, hao wanaoitwa marafiki, unaweza ukakuta kuwa ni wale watu ambao hawana hamasa yoyote ya kufanikiwa, ni wavivu, wabinafsi na inawezekana hapo walipo wamefika mwisho, wamebakia kusubili muujiza utokee ndipo watajirike—jaribu kuwa mwangalifu!

Katika hali ya kawaida haiwezekani wewe upate kuwa na wazo zuri mwezi mzima halafu umshirikishe rafiki yako na yeye siku na saa hiyo hiyo akwambie “haiwezekani”. Ukiamua kumsikiliza kama wengi tunavyofanya nakuhakikishia kuwa itaendelea kuwa vigumu sana kwako kuweza kufanikisha mradi wowote wa maana. Ebu! Fikiria rafiki yako, anakwambia, hicho kitu unachotaka kufanya hakijawahi kufanywa na mtu yeyote na kwamba wewe utawezaje? Eti! unaambiwa husifanye jambo fulani kwasababu hakuna aliyewahi kufanya hivyo—ushauri wa namna hii utaendelea kuupata sana, kama utaendelea kuwa mtu wa kuongeaongea tu!

Unapoamua kumwaga mawazo yako kwa wengine, ujue kuwa kwa namna moja au nyingine yatapokelewa kwa hisia na mtazamo tofauti kulingana na uelewa wa watu unaowambia. Mara nyingi watu wakiambiwa jambo ambalo liko nje ya fikra zao au uelewa wao, moja kwa moja upata hofu na baadae woga, kutegemea na ukubwa na upya wa wazo lako. Wakishapata hofu juu ya wazo lako, kinachofuata ni kutaka kujaribu kuhamishia hofu yao kwako. Hapo wataanza kukupa mifano ya watu waliowahi kujaribu na wakashindwa, watakueleza hatari zote zinazoweza kujitokeza endapo utendelea na mpango wa kutekeleza wazo lako hilo. Kwahiyo, wewe bila kujua, unashitukia umeambukizwa woga na hofu ambayo kimsingi hukuwanayo hapo awali.

Baadhi ya maneno yanayodhihirisha hofu ya marafiki zako juu ya wazo lako ni kama maneno ya “huwezi”, “haiwezekani”, “ni ngumu sana kufanikiwa” n.k. Ndiyo maana ukiendelea kuhubiliwa maneno hayo mara kwa mara, utajikuta taratibu taratibu unaanza kuyaamini. Hali hii ndiyo mwisho wake ukusababishia kukosa ujasiri wa kuthubutu pindi zinapotokea fursa mbalimbali.

Kwa taarifa yako ni kwamba pale rafiki au ndugu yako akikwambia “huwezi” maana yake ni kwamba yeye ndiye “hawezi”. Mara zote usilichukulie jibu la “huwezi” kama ndiyo jibu lako. Pia, usijaribu kulitumia jibu la “huwezi” kama kisingizio au kikwazo cha kukuzuia wewe kutekeleza wazo lako kama ulivyolifikiria hapo awali.

Achana na kuongea ongea sana! Maneno ya nita……anza biashara, shule, kutafuta pesa, kufanya mazoezi mwaka huu hayasadii sana. Nataka nikwambie kwamba maneno yote ya “nita….nita…!” ni kuongea tu! Na ni sawa na “mvuke”—hakuna vitendo hapo.

Nitawezaje kuendeleza wazo langu bila kuongea?
Sasa, ili kuepuka mawazo yako kuwa kama “mvuke”, inabidi kuanzia sasa kila ukipata wazo zuri, cha kwanza kufanya ni kuliandika na kisha kulifanyia kazi huku ukiwa kimya.
 

 SOMA; SHULE YA “MAISHA YAKO” INATAKA MALENGO NA MIPANGILIO YAKO IWE NI KWA MAANDISHI
 

 Unapoandika wazo lako, unapata fursa ya kutathimini kile ulichotakiwa kufanya kwa kulinganisha na kile ulichokifanya. Mfano; kama umeanza siku yako usiongee kwamba mimi leo nitafanya hili na lile; wewe unachotakiwa ni kuandika orodha ya mambo ambayo unatakiwa kuyafanya kwa siku hiyo basi! Kama yale uliyoyaandika kwenye orodha umekamilisha asilimia 40% basi ujue kuwa bado wewe ni walewale waongeaji tu! Lakini kama utakamilisha kuanzia asilimia 70-100%, basi ujue kuwa sasa umeanza kuwa mtu wa vitendo zaidi na siyo maneno.

Hapa nizidi kukusihi kuwa, kila wakati ujitahidi kuruhusu vitendo vikuongoze na siyo kuongozwa na maneno. Tumia muda wako mwingi kutenda na kila wakati “yape nafasi matendo yako yaongee kwa sauti” kuliko maneno.

Kila ukipata wazo zuri kumbuka kauli mbiu hii “andika mawazo yako na ukae kimya”.
Endelea kujifunza kupitia hapa MAARIFA SHOP; ili upate kujiongoza kuelekea maisha ya neema.

Kupata mafunzo kila siku kwa njia ya whasap bonyeza neno MAFUNZO

No comments: