Tuesday, August 11, 2020

Ulimwengu Mpya wa Ajira Unamuhitaji Nani?


Ukosefu wa ajira ni miongoni mwa changamoto kubwa kwa jamii yetu na hasa vijana. Lakini pia, pamoja na kuwepo kwa changamoto hii, bado na wale wanaofanikiwa kupata ajira wanaipoteza muda mfupi. 

Pengine hali hii inatokana na ukweli kwamba tuko kwenye ulimwengu mpya wa ajira,lakini waliopo wana tabia za mfumo wa ajira wa zamani. 

Katika mfumo wa zamani wewe unaambiwa tu cha kufanya, na hauhitajiki kufanya maamuzi wala kufikiri zaidi. Kila kitu juu ya namna utakavyotenda kazi zako kiko tayari kimeandaliwa, kwahiyo wewe ni kufuata maelekezo yaliyokwishatolewa basi!. 

Maisha ya ajira kwa mfumo wa zamani, kipaji chako hakihitajiki, ubunifu wako hauhitajiki, ilimradi unajua kufuata maelekezo, unajua kuwahi kazini na wewe ni mtiifu kwa wakubwa. Kwasababu kila kitu. 

Wanaotafuta na walioko kwenye ajira wanatakiwa kutambua ukweli kwamba, sasa tuko kwenye ulimwengu mpya wa ajira. 

Ndani ya ulimwengu huu mpya, mfumo wa ajira tayari umekwishasukwa ili kumruhusu mwajili kukubadilisha kirahisi na kuleta mtu mwingine – “kama kipuri cha kwenye gari

Uthibitisho wa kusukwa kwa mfumo wa ajira ni uwepo wa idara na vitengo mbalimbali katika taasisi na mashirika. 

Idara na vitengo katika taasisi na mashirika mbalimbali vimewekwa siyo kwa bahati mbaya bali ni kwa makusudi, ili kuwawezesha waajili kufanya mabadiliko ya watu kirahisi na wakati huo kazi zikaendelea bila kukwama popote. 

Ndani ya ulimwengu mpya wa ajira wewe umegeuzwa mashine, ili iwe rahisi kukupima. Na ikiwa unaweza kupimwa, basi ni rahisi kuweka mtu mwingine. 

Kama ni rahisi kuweka mtu mwingine basi ni rahisi kumpata mtu mwingine kwa bei nafuu. 

Kwa maana nyingine, sekta ya ajira kwasasa ipo karne ya kubadilishabadilisha wafanyakazi. 

Kwahiyo, wewe kama mtumishi unatakiwa kujibadilisha ili iwe vigumu sana kukubadilisha kwa kuleta watu wengine kwenye nafasi yako. 

Katika ulimwengu mpya wa ajira unachotakiwa kukifanya ni kujibadilisha na kuwa mmojawapo wa wale watu ambao ni muhimu sana. 

Unahitajika kuwa mwenye tafakari ya asili, mtetezi, na mtu unayejali watu wengine. 

Ili kutengeneza umuhimu sehemu ya kazi unatakiwa kufahamu kwamba wewe umezaliwa kama mtu ambaye ni umuhimu sana. 

Kama mfumo umekuwa unakuchukulia kama mtu asiye muhimu, usivunjike moyo, tambua kwamba bado kuna njia mbadala kwako wewe. 

Kuweza kuwa mtu muhimu kwenye shirika au taasisi ni mchakato. Ni njia ambayo wewe unajenga tabia ambazo zitakufanya kuwa mtu muhimu ambaye haepukiki.

Unaweza kujifunza kuwa wa mtu muhimu kwa watu wengine. 

Maisha mazuri ya mbeleni yatakuwa ni kwa wale tu ambao wako tayari kutoa mchango wao halisi kwa kufanya kazi nzuri. 

Kuweza kuwa mtu muhimu sana kutategemea zaidi kiwango cha thamani utakachoweza kuzalisha. 

Kudiri utakavyotoa thamani kubwa kwenye jamii ndivyo soko litavyokurudishia zaidi. 

Anza leo maisha ya kujifunza kuwa mtu muhimu na hakuna atakeyethubutu kukuondoa kwenye nafasi yako ya ajira. 

Endelea kutumia maarifa kwa kujiunga na kundi letu la WHATSAP kwa kubonyeza neno MAFUNZO, kupata mafunzo ya kila siku na namna ya kujibadilisha kuwa mtu muhimu sana kwenye shirika au taasisi ulikoajiriwa. 

Kupata makala kila zinapochapishwa bonyeza kiungo hiki;NITUMIE MAKALA kisha sajiri barua pepe yako.

No comments: