Ukifuatilia
na kutafakari suala zima la mapato na matumizi ya pesa kwa watu walio wengi, utagundua
kuwa kuna tatizo kubwa la msingi. Fikiria mkulima wa Tanzania ambaye
amebahatika kuishi maeneo yenye misimu miwili ya mvua wanapata Mazao mara mbili
kwa mwaka, hii ikiwa na maana kwamba, anapata fedha mara mbili kwa mwaka, maana
yake mtu huyu akipata pesa leo, pesa nyingine itapatikana baada ya miezi sita. Lakini
kwa mkulima anayeishi maeneo yenye msimu mmoja wa mvua, wanapata mavuno mara
moja kwa mwaka mzima, hii ikimaanisha kuwa huyu mtu anapata pesa mara moja kwa
mwaka. Wafanyakazi na hasa wa serikali na makampuni binafsi wana pata fedha
kila mwezi. Wafanyabiashara wadogo na wa kati wanapata pesa kwa wiki na wengine
kila siku. Wafanyabiashara wakubwa na matajiri wengine wanapata pesa kwa saa,
dakika na wengine kama makampuni ya simu wanapata hadi kwa sekunde.
Uzoefu
umeonyesha kuwa unapochukua muda mrefu kuingiza pesa nyingine ndivyo unakuwa
maskini wa kutupwa na maisha yanakuwa magumu kweli kweli. Sababu kubwa ya
umaskini huo ni kutokana na ukweli kwamba mahitaji au matumizi ya mtu yeyote
huwa ni kila siku na wakati huo huo mapato ni kwa mwaka au kila baada ya miezi
sita kwa Wakulima walio wengi. Kutokana na hali hii tunaona kuwa hakuna
ulinganifu ulio sawa kati ya kupata na kutumia pesa. Kupishana kwa mapato na
matumizi ndiko kunakofanya watu wengi na hasa Wakulima kuishi Katika madeni
makubwa ambapo inapofika msimu wa mavuno Wakulima hawa tayari wanakuwa
wanadaiwa, kiasi kwamba inapotokea msimu haukwenda vizuri wengine ulazimika
kuuza hata vipande vya ardhi waliyokuwa nayo ili kulipa madeni, wengine huwa
hawasubili kuvuna ndipo wauze badala yake wanauza Mazao yao ya yakiwa bado
kukomaa shambani.
Katika
wilaya za Karagwe, Bukoba na Muleba ambako zao la kahawa linalimwa kwa wingi Wakulima
wengi uchukua fedha kama mkopo kutoka kwa wafanyabiashara kabla ya kahawa
kukomaa wenyeji wanaita “Butura”. Biashara ya “Butura” ni maarufu sana mkoani
Kagera. Watu upewa pesa kabla ya Mazao kukomaa huku wakikubaliana kulipana Mazao
pindi yakikomaa. Katika Wilaya ya Ngara wao huuza mahindi yakiwa hata bado
kubeba, maeneo ya usukumani suala hili liko sana kwenye zao la mpunga japo
wengi uwa wanakopa pesa kutoka kwa wafanyabiashara ili kupata pesa ya palizi na
kuhemea ndege“kumoja” n.k.
Kwasababu
wanachukua muda mrefu kupata pesa, ndiyo maana wakishapata pesa wanachangamka
sana kuzidi kipimo na hii ni kutokana na sababu kuwa mara nyingi wakati wa
msimu, pesa uja kwa mkupuo, hali ambayo huwafanya kuzitumia ovyoovyo na wengine
ujaribu na kuongeza mke wa pili, kunywa pombe kupindukia, harusi na sherehe nyingi.
Kutokana na matumizi ambayo uambatana na mihemuko ya kila aina, watu uweza
kuishiwa pesa walizokuwa nazo mara tu baada ya takribani mwezi mmoja hadi
miwili.
Baada
ya watu kuishiwa pesa zilizotokana na mavuno, watu wengi hurudia hali yao ya
kutokuwa na pesa na hapa ndipo, utaanza kusikia lugha za “hakuna mzunguko wa
pesa” Eti kila mmoja anaanza kusema pesa hakuna siku siku hizi; Kumbe
kiuhalisia siyo kwamba hakuna pesa, isipokuwa ni kwamba hakuna cha kuuza wakati
huo. Pesa huwa inafuata vitu vilipo pamoja na huduma zilipo. Hali hii ujenga
hofu sana miongoni mwa wanajamii hasa kutoka Katika kaya masikni na pia kukata
tamaa.
Kutokana
na hofu na imani kwamba kijjini hakuna pesa, wengi wao na hasa vijana uchukua
uamzi wa kukimbilia mijini wanakoamini kuna mzunguko wa pesa wasijue kuwa hata
huko wanakoamini kuwa na mzunguko mzuri wa pesa bado utalazimika kuwa na vitu
au huduma ndipo uzipate, bila kuwa na vitu/huduma – wewe hata kama uko mjini
unakoamini kuwa kuna mzunguko wa pesa, bado pesa utaziona tu kwa wengine na si
kwako!!!!.
Kwahiyo
kama wewe ni mmoja wa wadau wa maendeleo, njia pekee ya kuwakomboa Wakulima ni
pamoja na kutafuta njia ya kufupisha muda wa kupata fedha nyingine angalau
ukiweza kushuka kutoka miezi sita mpaka mwezi mmoja. Hikiwa hivi ndivyo, basi
itakuwa ni hatua moja muhimu sana Katika kupambana na umaskini hasa Wakulima.
Mpendwa msomaji endelea kuitumia vizuri MAARIFASHOP, ili kujifunza mambo mbalimbali yatakayokuwezesha kufanikiwa. Kupata makala mpya kila zinapochapishwa, bonyeza sasahivi neno- hivi; TUMA MAKALA MAARIFASHOP kisha sajiri barua pepe yako na kama unapenda kupata mafunzo ya kila siku na makala mpya kwa njia ya whatsap bonyeza neno MAFUNZO.
KARIBU TUCHUKUE
HATUA PAMOJA!!
No comments:
Post a Comment