PESA NI MATOKEO YA BIDHAA NA HUDUMA; NA VYOTE HIVI UTOKANA NA KAZI |
Bidhaa
yoyote lazima itokane na kazi na bidhaa kama bidhaa ndiyo pesa yenyewe. Mantiki
hii inatukumbusha kauli aliyowahi kuitoa Rais wa zamani wa Tanzania Mwalimu
Julius K. Nyerere, aliposema “Pesa Siyo
Msingi wa Maendeleo” kauli hii ilikuwa ya kifalsafa zaidi, na watu wengi wakati huo, hawakuielewa kwa
mtazamo wa kwamba pesa yoyote ambayo ni
halali ni matokeo ya kazi halali. Badala yake, walio wengi waliipokea kauli hii
kwa uelewa tofauti na sana sana kwa mtazamo
“hasi”. Kutokana na watu wengi kuwa
na mtazamo hasi juu ya kauli hii ya pesa siyo msingi wa maendeleo, basi Mwalimu
Nyerere alichukuliwa na kudhaniwa kuwa miongoni mwa watu ambao hawakupenda
watanzania wapate pesa.
Falsafa
ya “pesa siyo msingi wa maendeleo” bado
inaendelea kupingwa hadi leo hii na kupingwa kwa falsafa hii, kunazidi
kudhihilisha uelewa mdogo juu ya pesa. Na hapa ndipo tulipo jikwaa na kuanguka
hasa kiuchumi, kwasababu watu wengi tunawaza kupata pesa ndipo tufanye kazi.
Kaya nyingi kwa sasa zimetoa kipaumbele kwa shughuli ambazo zinaleta pesa hapo
hapo (fasta) na hivyo kujikuta mwaka hadi mwaka wakiwa hawana muda tena wa kufanya
vitu vyenye kuleta pesa nyingi baadae na kwa muda mrefu. Mara nyingi miradi
yenye kuondoa umaskini kwenye kaya, inahitaji kuvumilia na kuwa tayari kufanya
kazi bila kulipwa kwa muda huo huo (malipo baadae).
Hapo
zamani wakati watu walipokuwa na mfumo wa biashara wa kubadilishana vitu moja
kwa moja (bartering system), uchumi wa kaya ulikuwa imara sana, kwasababu kila
mmoja ilibidi afanye kazi ili kupata bidhaa. Wakati huo, kulikuwa hakuna ujanja
ujanja na ilikuwa vigumu kwa mtu kumzurumu au kuishi kwa rushwa kwani utaratibu
ulikuwa ni kwamba ili upate bidhaa fulani, ulitakiwa uwe na bidhaa ya kwako.
Jambo hili lililazimu kila mmoja mwenye uwezo wa kufanya kazi kuwajibika
ipasavyo ndio aweze kuishi. Ni bahati mbaya sana baada ya kuingia mfumo wa pesa
ambayo ukaa katikati ya muuzaji na mnunuzi wa bidhaa, watu wengi tukasahau, tukaanza
kuweka nguvu na fikra nyingi kwenye kutafuta hicho kitu cha katikati “pesa” bila kukumbuka kuwa kitu ambacho
huwaleta pamoja watu hawa wawili yaani muuzaji na mnunuzi, huwa siyo “pesa”
bali ni BIDHAA.
Mara
nyingi mtu anapouza bidhaa anapewa pesa kama uthibitisho wa kukiri kupokea bidhaa
hiyo. Matatizo yanaanzia pale huyo mtu anaposahau ndani ya akili yake kuwa bado
ile bidhaa anayo mikononi mwake, na cha ajabu, mtu huyo anaanza kuabudu na
kuthamini sana ile “pesa” kuliko hata
ile bidhaa aliyokuwanayo. Mfano: kama ni mkulima hatafikiria tena kununua mbegu
bora au mbolea ili kujipanga kuzalisha mazao mengi zaidi msimu unaofuata. Kitakachotokea
ni kwamba mkulima huyo atachukua pesa hizo na kufanyia vitu vingine tofauti na uzalishaji
wa mazao, lakini ikumbukwe kuwa hiyo pesa anayotamba nayo ilitokana na kuuza
mazao na si vinginevyo. Matokeo yake mkulima huyo, msimu unaofuata anajikuta hana pesa tena ya kuendesha kilimo
chake kwa tija zaidi na hivyo kujikuta akipata mavuno kidogo sana kuliko msimu
uliopita!.
Ipo
mifano mingi tu ya watu kutokuwa na tabia ya kukumbuka pesa waliyonayo ilitoka
wapi na hivyo kujikuta wakitenga kiasi kidogo sana kwaajiri ya kuendeleza
miradi hiyo ambayo ndio hasa uwaingizia pesa nyingi. Tunahitaji kutambua kuwa
pesa tuliyonayo kuna kitu kinaileta na kwa maana hiyo tuweke nguvu zetu kwenye
hicho kitu badala ya pesa yenyewe. Iwapo tutaanza kuiona pesa kwa mtazamo huu,
tutakuwa tumepiga hatua kubwa kimaendeleo na kwakufanya hivyo tutakuwa tumejitenga
na kundi kubwa la watu wenye mawazo ya wastani
wanaodhani pesa inapatikana kwa bahati!
Pia, mtazamo wetu juu ya pesa
ukibadilika, tutagudua kuwa huwezi kupata pesa kwa ujanja ujanja. Mambo yote
haya yakifanyika, yatafanya uchumi wa kaya na taifa kwa ujumla kuweza kukua kwa
kiwango cha kuridhisha. Ewe mtanzania, badili fikra zako juu ya pesa leo,
tufanye kazi kwa bidii ili tuzalishe bidhaa na huduma mbalimbali, na kwa njia
hii tutawezesha kaya zetu na taifa letu kuinuka kwa maana tutavuna (tutachuma)
kwa wingi zaidi. Tukumbuke kuwa dhana nzima ya UCHUMI ni “kuchuma/kuvuna
tulichokifanyia kazi” na hili ndilo dhumuni letu katika kupata maisha bora.
Mpendwa msomaji, endelea kuitumia vizuri MAARIFASHOP ili kujifunza mambo mbalimbali yatakayokuwezesha kupata mafanikio. Ili kupata makala mpya kila zinapochapishwa, bonyeza neno TUMA MAKALA MAARIFASHOP kisha sajiri barua pepe yako. Na kama unapenda kupata mafunzo ya kila siku kwa njia ya whatsap bonyeza neno MAFUNZO.
No comments:
Post a Comment