Sasa hivi kuna tatizo kubwa sana la
ukosefu wa ajira hasa kwa vijana. Ukosefu wa ajira ni jambo ambalo linazidi
kuwawangisha vichwa wadau wengi wa
maendeleo na hasa serikali. Ni kweli serikali ina jukumu la kuhakikisha
wananchi wake wanakuwa na shughuli ya kufanya ili kujiongezea kipato. Lakini,
wakati jitihada za serikali zikiendelea, sisi wenyewe tunaodai kukosa kazi
tunayo majukumu makubwa zaidi ya kufanya kuliko kutegemea watu wakutupatia
ajira. Kwahiyo, ni vyema tushughulikie kwanza yale yote yaliyondani ya uwezo
wetu ambayo nina imani yanaweza kuchagia kwa asilimia 80% katika kutupatia
suruhisho la kudumu juu ya kero hii ya kukosa kazi. Hivyo basi, hatua ya kwanza
kabisa ni kutafakari na kufikiri kwa kina juu ya tofauti iliyopo kati ya kazi
na ajira. Maana unaweza kujikuta muda wako mwingi unautumia kutafuta ajira
ukifikiri ni “Kazi”.
Kazi na ajira ni vitu viwili tofauti
kabisa, na haviwezi kulinganishwa kwa kiwango chochote kile. Kazi inalipa sana na
malipo yake mengine hayana kikomo, tofauti na ajira ambayo malipo yake ni
kidogo na yanaweza kukoma muda wowote. Kitu cha ajabu kabisa ni kwamba watu
wengi wanapendelea “ajira” kuliko “kazi” kwasababu, ulipohitimu elimu yako
ulikaririshwa kuwa kazi inayotambulika rasimi ni ajira. Hii inatokana na mazoea
ambayo tumeyajenga tokea tukiwa wadogo kuwa kazi yenye heshima ni ambayo
umeajiriwa, ndiyo maana wale wote wanaofanya shughuli za kuajiriwa eti! ndio
wanaitwa “Wafanyakazi”. Kwahiyo, wale
wote ambao hawana ajira na hasa ajira rasimi, wanajiona na kujisikia kuwa
hawana kazi na kutafuta njia usiku na mchana ili angalau siku moja waweze
kuajiriwa. Hali hii, ya kushindwa kupata majibu sahii juu ya kazi ni ipi na
ajira ni ipi. Matokeo yake kumeibuka makundi mawili ambayo ni kundi la wenye
jukumu la kutoa ajira na kundi jingine ni la wenye kupata ajira. Kundi la
wapata ajira ni wengi sana; Eti! Kazi yao ni kutafuta wapi ajira ilipo, na pale
mtu anapotafuta ajira akakosa kwa muda huo, moja kwa moja anasema sina kazi!
Hii inashangaza sana.
“Ajira” ni kufanya kazi ambayo siyo ya kwako,
waweza kuwa unaipenda au huipendi. Watu wengine hawapendi kazi walizoajiriwa
kuzifanya, lakini yawezekana wanaendelea
kufanya kazi hizo kwasababu wanalipwa pesa. Kutokana na hali hii, watu wengi
hulazimika kutafuta kazi nyingine pale tu malipo yanapokuwa hayatoshelezi
mahitaji ya muhusika. Mwenye kazi “mwajiri”
anapokuwa amekuajiri kwenye kazi yake ambayo “siyo ya kwako”; wewe moja kwa moja unahesabika kuwa ni sehemu ya
gharama za uendeshaji wa kazi au kampuni! Hii ni sawa na kusema kuwa waajiri
wengi wanawaona wafanyakazi (waajiriwa) kama gharama za uzalishaji!. Hii haina
maana kwamba waajiri hawawathamini waajiriwa wao, bali wakati wa kufanya
tathimini ya maendeleo ya kazi inawabidi kufanya hivyo, ili kupanga mipango
mikakati ya kuwezesha matunda ya kazi husika yapatikane kwa gharama nafuu.
“Kazi” ni
majumuisho ya majukumu mbalimbali ambayo kwa mwenye kazi unajiwajibisha
mwenyewe katika kuyatimiza hayo uliyojipa mwenyewe, bila kutegemea kulipwa
chochote mpaka matunda ya kazi hiyo yapatikane. Unapofanya kazi siyo lazima
alipwe, kwasababu mara nyingi kazi inakuwa ni mchakato wako wa maisha na
haupangiwi na mtu yeyote, wewe mwenyewe unajipangia ni nini ufanye, kwa malengo
yapi na ni nani unamlenga kunufaika na matokeo (matunda) ya kazi yako. Iwapo
matokeo ya kazi yako yanatoa suluhisho la matatizo au kero zilizopo kwenye
jamii husika, basi ujiandae kulipwa malipo ambayo hayana kikomo, kwasababu watu
watanunua matunda ya kazi yako, ili kukidhi mahitaji yao, hivyo ni rahisi wewe
kuweza kutajirika kutajirika kupitia utatuzi wa kero na matatizo mbalimbali.
Kutokana
na maana pana ya “kazi” tunaona
kwamba kazi inaweza kupatikana popote lakini ajira haipatikani kila sehemu.
Kazi ni nyingi sana ajira ni chache sana, hii inamanisha kwamba watu wanapenda
vitu ambavyo vimeishapikwa tayari, kazi yao ni kupakua na isitoshe hata kwa
kupakua tu! unalipwa na mwenye kazi. Kazi ni ya kudumu wakati ajira ina ukomo;
kwenye kazi hakuna bosi, isipokuwa bosi wako ni malengo na ndoto zako lakini
kwenye ajira kuna bosi ambaye anayo madaraka ya kuamua juu ya nini kifanyike na
wakati mwingine kifanyike vipi na huyu ndiye anamiliki na kuongoza hatima ya
mafanikio yako
na hasa ya kiuchumi. Kwenye kazi unachukua muda mrefu kuanza
kulipwa tofauti na ajira ambayo, ukianza tu ajira yako unaanza kulipwa maramoja
au mwisho wa mwezi huo huo. Pengine tofauti hii ya muda wa kulipwa kati ya
mwenye kazi na mwenye ajira ndiyo inayowafanya watu wengi na hasa wasomi wa
fani mbalimbali kupendela “ajira”
kuliko “kazi”.
Kutengeneza
na kufanya kazi kunahitaji kujitoa, ubunifu, kufikiri sana, kuvumilia na zaidi
ya yote, kazi inahitai ujasiri na ninadhani ujasiri huu wa kufanya kazi bila
kulipwa kwa wakati huo ndiyo mzizi mkuu wa neno “Ujasiriamali”. Kwenye ajira kila kitu ambacho unakifanya unadai
ulipwe, kwahiyo, kama hakuna malipo hicho kitu au shughuli haiwezi kufanyika.
Kwa uhalisia ni haki ya mwajiliwa kudai malipo ya kila nguvu anayowekeza kwenye
ajira yake kwasababu, mwajiriwa kama mwajiriwa yeye hana umiliki wowote wala
hisa juu ya matokeo au mapato yote ya
kile kilichozalishwa bali mwenye kumiliki hicho ni mwenye kazi.
Waajiriwa hupewa sehemu ndogo sana ya kile chote kilichozalishwa. Makampuni
mengi, kila mwisho wa mwaka huwa wanafunga mahesabu na kupima wamepata faida
kiasi gani lakini siyo rahisi kwa mwenye kampuni kutoa gawio (dividend) kwa
wafanyakazi wake kwasababu, wafanyakazi (waajiriwa) wote, wanahesabika kama
sehemu ya gharama na siyo sehemu ya faida, na faida hii ndiyo motisha na
kichocheo kikubwa cha yeye kuendelea kuwekeza na kutengeneza kazi nyingi ambazo
zinaweza kutoa ajira kwa watu wengi zaidi.
Kwakuwa
kazi unajipatia mwenyewe, ni wakati muhafaka sasa wa kujipa kazi badala ya
kusubili kupewa kazi (ajira). Tusisubili wale wakutuletea kazi, kwa maana
hatujui wataleta lini na kwa malengo yapi. Tuzidi kukumbuka kuwa ajira haziwezi
kuwa nyingi kama kazi zinazotengenezwa ni chache. Tuzidi kujipa kazi kwani
chochote tutakachozalisha, watu wako tayari kununua, ilimradi kina manufaa
kwao. Anza leo, kuanza kujitenga na watafuta ajira, pia jiepushe na tabia ya
kulalamikia watu wengine kwa mambo ambayo ni majukumu yako. Kwahiyo, bila
kujali umesomea nini, anza leo kufikiria ni kitu gani unaweza kukizalisha
ambacho kina uwezo wa kutatua kero na changamoto mbalimbali katika jamii.
Kwakufanya hivyo, utakuwa umepata suluhisho la kudumu juu ya kero ya muda mrefu
ambayo ni ukosefu wa “kazi”.
Mpendwa msomaji, endelea kuitumia vizuri MAARIFASHOP ili kujifunza mambo mbalimbali yatakayokuwezesha kupata mafanikio. Ili kupata makala mpya kila zinapochapishwa, bonyeza neno TUMA MAKALA MAARIFASHOP kisha sajiri barua pepe yako. Na kama unapenda kupata mafunzo ya kila siku kwa njia ya whatsap bonyeza neno MAFUNZO.
No comments:
Post a Comment