Watu wengi tunatamani kupata
mafanikio kwa lengo la kupata fursa ya kuishi maisha mazuri, maisha yenye
furaha, maisha ambayo unaweza kusaidia wasiojiweza n.k. Lakini, waliowengi
ndoto hizo, zinaonekana kuendelea kufifia kadili umri unavyozidi kuwa mkubwa!.
Kwa kuangalia mifano ya watu wengi waliofanikiwa, unagundua kuwa mafanikio si
kitu chochote zaidi ya kuwa na nidhamu ya kufanya vitu vya kawaida kila siku.
Mafanikio hayatokani na miujiza
bali ni kitu kinachojitokeza kutokana na mambo ya msingi ambayo ni madogo
madogo yanayohitajika kupangwa na kufanyika kila siku. Kwahiyo, tunaweza kusema
kwamba, mafanikio ni ujuzi au kusoma vitu vya kawaida— lakini wakati mwingine
tunahitaji mtu fulani wa kutukumbusha na kutuonyesha njia ambayo ni rahisi
kufuata na kuweza kufikia mafanikio tunayo yataka. Na hapa nitaeleza umuhimu wa
kuwa na mpango mzuri kama hatua mojawapo ya kufuata ili kuweza kufika kwenye
mafanikio makubwa kuliko unavyoweza kufikiri.
Kujenga maisha, kujenga kitu
chochote kile, ni kama kujenga nyumba; unahitaji kuwa na mpango. Chukulia
mfano, kama ungeanza kubeba na kuanza kuweka matofari kwenye msingi alafu
akatokea mtu akakuuliza “Unajenga kitu
gani?” Je? Utaweka chini matofari uliyobeba na kumwambia kuwa hujui unacho
jenga?” au utamwambia unachotaka kujenga kuwa ni nyumba hata kama bado
haijajengwa. Mfano huu unatufungua akili na kutufundisha kuwa, mara zote“nyumba inaanza kujengwa mara tu inapokuwa
imekamilika”.
Tukirudi kwenye maisha tunaona
kuwa imekuwa vigumu sana kwa watu walio wengi kuweza kuweka mipango madhubuti
ya maisha ya ndoto yao. Kwasababu ni ukweli usiopingika kuwa wengi wetu
hatujabainisha kwa dhati kuwa uko mbeleni tunataka maisha ya namna gani na
kwakuwa hilo halipo katika maandishi tumejikuta hatuna cha kupanga kufanya kwa
siku, wiki, mwezi, mwaka au zaidi. Tunaamka asubuhi na kufanya chochote
kinachojitokeza kwenye akili na fikra zetu. Kwa maana nyingine tumekuwa watu wa
kushughulikia mambo mapya na matukio tu! Hii ni hatari na ni changamoto kubwa
sana iliyoko mbele yetu.
Kila mmoja wetu ambaye haliziki
na maisha aliyonayo kwa sasa, inabidi kujenga utamaduni wa kuwa na nidhamu ya
kufikiri kwanza juu ya jambo ambalo unatarajia kulifanya. Baada ya kufikiri, unahitaji
kuandika mawazo yako juu ya aina ya maisha unayotamani kuyaishi miaka mitano,
kumi na zaidi ijayo, kwa kufanya hivyo utakuwa tayari umekamilisha nyumba kabla
ya kuanza kujenga.
Ukijaribu kutafakali mafundisho
mbalimbali kutoka kwa watu waliofanikiwa, utagundua kitu kimoja ambacho
kinasisitizwa sana ni “usianze siku yako
mpaka itakapokuwa imemalizika vizuri”—angalau orodha ya mambo ya kufanya.
Jitahidi kuwa na orodha ya mambo ya kufanya kabla ujaanza kutenda kazi za siku,
na mengi yawe ni yale yenye mchango katika kukufikisha kwenye malengo yako ya
muda mrefu (k.m: miaka 5, 10, 25 au zaidi). Katika kupanga orodha ya mambo ya
kufanya, jaribu kuacha nafasi ya kufanya marekebisho kadili utakavyoendelea,
acha nafasi kwaajili ya mikakati ya ziada, lakini kikubwa hapa cha kusisitiza
ni kumaliza kwanza jambo unalotaka kulifanya kabla ya kulianza. Usiaze wiki mpaka iwe imekamilika. Chora
ramani ya jinsi itakavyokuwa, iwekee sura na umbo au weka jengo lake, na baada
ya hapo anza kuifanyia kazi.
Utaratibu huu ufanyike kwa mwezi
ujao—Usianze mwezi, mpaka uwe na mpango tayari mezani. Na kubwa zaidi, usianze
mwaka mpaka umalizike kwenye karatasi. Siyo wazo baya, ikifikia mwisho wa
mwaka, ukakaa chini na familia kwaajili ya kuweka mpango binafsi kwa mwaka
ujao, kaa chini na weka mpango kazi, kaa chini na mshauri wako wa mambo ya
fedha kuweka ramani ya jinsi pesa itakavyopatikana. Panga kalenda yako na kwa
vitu vyote vinavyowezesha maisha yako kwenda mbele hasa kule unakokutaka.
Mpendwa msomaji, endelea kuitumia vizuri MAARIFASHOP ili kujifunza mambo mbalimbali yatakayokuwezesha kupata mafanikio. Ili kupata makala mpya kila zinapochapishwa, bonyeza neno TUMA MAKALA MAARIFASHOP kisha sajiri barua pepe yako. Na kama unapenda kupata mafunzo ya kila siku kwa njia ya whatsap bonyeza neno MAFUNZO.
No comments:
Post a Comment