Wednesday, February 3, 2016

Kuishi Maisha ya Chapati ni Hatari Tupu!



“Umaskini Unakuja Kwako Bila Gharama Yoyote LAKINI Unaondolewa kwa Gharama Kubwa Sana”


Chapati ni bidhaa ambayo ni chakula tunachokipenda sana na pia ni bidhaa inayokubalika na kuhitajika kwa kiasi kikubwa katika maeneo mengi ya hapa nchini Tanzania. Lakini......
kama ilivyokawaida ya bidhaa nyingi za chakula, bidhaa hii inadumu kwa muda mfupi na zaidi ya hapo inaharibika au kuoza kabisa.

Kwahiyo thamani yake hushuka au kuisha mara baada ya muda wake kuisha. Thamani ya chapatti inatokana na yule mtengenezaji, kwani yeye ndiye anaamua kiwango gani cha thamani kiwemo ndani ya chapatti.

Thamani ni kile kiwango cha umuhimu uliomo ndani ya bidhaa au huduma. Pia thamani ni ubora ambao huifanya bidhaa au huduma fulani kupendeka au kuhitajika. Kwa mantiki hii inatosha kusema kuwa thamani ni ule uhitaji, umuhimu, faida, urahisi ambao mara nyingi huwekwa kwenye bidhaa au huduma fulani fulani. Kwa ufupi, thamani ni matokeo ya kile akipatacho mtu baada ya kuwa ametumia bidhaa au huduma yako kukidhi mahitaji yake.

Thamani ikishawekwa ndani ya bidhaa/huduma husika, mara nyingi huwa haiongezeki, sana sana huendelea kushuka na mwisho wake huisha kabisa. Thamani ya bidhaa ikishawekwa na mtengenezaji huwa habadiriki tena, isipokuwa huendelea kutunzwa na kuhakikisha inatumika kabla ya muda wake kuisha (expire date).

Bidhaa hasa ya chakula ikishafikia muda wake wa kutumika, moja kwa moja huwa ni kitu cha kutupwa kutokana na ukweli kwamba, huwa ni kitu kisichokuwa na manufaa yoyote kwa matumizi ya binadamu na wanyama wengine.

Uongezaji wa thamani za bidhaa ni tofauti kwa binadamu?
Binadamu ni kiumbe mwenye akiri na mwenye kujitambua, hivyo suala la kuongeza thamani yake ni tofauti kabisa na utaratibu wa kuongeza thamani ya bidhaa au huduma. 

Tofauti na bidhaa, binadamu yoyote mwenye akiri timamu tumepewa uwezo na mwenyezi Mungu wa kuibadili kwa maana ya kuongeza na kupunguza thamani tuliyonayo mbele ya jamii au dunia.

Hapa tunaposema thamani yako, tunamaanisha uhitaji au umuhimu wako katika kuleta suruhisho mbalimbali za changamoto na kero nyingi zinazowakabili watu wengine, bila kujali idadi ya hao wengine.

Kwa maana nyingine, sisi binadamu tumepewa fursa na uwezo wa kubadili thamani tuliyonayo leo kuwa kubwa zaidi kesho. Pengine, inawezekana wewe unayesoma makala hii unajiuliza maswali mengi ya kwanini uongeze thamani yako?

Na mimi ninakwambia kuwa ni muhimu sana ujitahidi kadiri inavyowezekana kuongeza thamani yako kila siku, kwasababu thamani yako ikishuka kwenye jamii, na uwezo wako wa kuingiza kipato utashuka ghafla.

Endapo uwezo wako wa kuingiza kipato utazidi kushuka basi ujue umasikini tayari utakuwa umefika nyumbani kwako bila gharama yoyote. Dada yangu mmoja Kemmy Christopher ambaye ni mfanyabiashara wa kimataifa, aliwahi kuniambia kuwa “Umaskini unakuja kwako bila gharama yoyote LAKINI unaondolewa kwa gharama kubwa sana”. Kwahiyo, tunapoogelea suala la kushuka kwa thamani yako siyo jambo la mzaha wala masiala.

Ukiona watu wengine wanakuweka kwenye kundi fulani la watu wa hali duni na wewe ukaendelea kuishi maisha kama ya watu wa kundi hilo kwa miaka mingi, basi ujue moja kwa moja wewe unaishi kama “chapatti”!. Yaani wewe haubadiliki miaka nenda rudi uko vile vile.

Wakati umefika sasa wa kuchukua hatua za makusudi na za dhati juu ya kuongeza thamani yetu kila siku kwani kwa kufanya hivyo tutakuwa tunaongeza uwezo wetu wa kuingiza kipato cha juu zaidi kila siku itakayopita.

Tunahitaji kutambua kuwa thamani tuliyonayo kwa sasa tuna uwezo wa kuipandisha na tukaonekana watu imara, bora zaidi na wapya kila siku.

Kitu pekee kitakacholeta mabadiliko na kukuondoa kwenye maisha ya kuishi kama chapati ni kujifunza kila siku mambo mapya yanayohusu kazi unayoipenda kuifanya, maisha unayopenda kuishi, mafanikio unayoyataka n.k.

Lazima tuige na kujenga tabia kama ya watoto – “kujifunza kila siku”. Tukiweza kujifunza mambo mapya kila siku ni wazi kwamba tutakuwa tumeachana na maisha ya kuishi kama “chapatti” ambayo ikishatengenezwa huwa thamani yake haiongezeki hata kidogo.

Tabia ya kujifunza kila siku itaboresha kama siyo kubadili kabisa kile unachofikiri kila siku. Ukishakuwa umebadilisha kile unachofikiri basi ujue kuwa na kile unachokiona kitabadilika. Mwandishi Dk. Faustin Kamugisha anasema “Ukiweza kubadili unachokiona unabadili unachokizalisha”. Maana yake ni kwamba unapoanza kuona kitu tofauti na kile cha siku zote ni wazi kuwa utaweka jitihada za kupata hicho kitu kipya. Kupatikana kwa kitu kipya ndiko kutazaa maisha mapya ambayo ni tofauti na yale ambayo umekuwa huyapendi.

Endelea kujifunza kila siku hapa ~ http://maarifashop.blogspot.com

No comments: