Wednesday, April 29, 2015

Ni Vigumu Sana Kufanikiwa Kama Mara Nyingi Unaituma Pesa Yako Kununua Vitu na Kubakia huko Bila Kurudi




Mara zote ukishakupata pesa (kuingia mfukoni), kinachofuata huwa ni kuzitumia hata kama ukizitunza kwanza, mwisho wake huwa ni kutumika kwaajili ya kukidhi mahitaji ya vitu na huduma mbalimbali. Watu wengine upenda kusema kwamba “pesa ni mzunguko”. Mzunguko wa pesa una vipengele viwili ambavyo ni “Kuingia na Kutoka”. Kwa lugha rahisi tunaweza kusema kuwa pesa ina milango miwili, kuna mlango wa pesa kuingia na kutoka kwako.

Kwa yeyote anayetafuta mafanikio makubwa ni lazima kuangalia milango hii miwili (kuingia na kutoka) na hapa ndipo kuna tokea makundi mawili ya watu ambao ni masikini na tajiri. Kwa upande wa maskini tayari wamejenga hofu kubwa sana na muda wote wana wasiwasi ya pesa kutoka na kupotea. Kutokana na hofu hii, maskini wengi sana wemejijengea tabia ya kuibana pesa ikisha ingia mifukoni mwao, huku wakidhani kuwa hilo ni suluhisho la wao kutoishiwa na pesa. Matokeo yake linapokuja suala la kuwekeza au kuchangamkia fursa kubwa wanakuwa waoga sana wa kuthubutu kutokana na hofu ambayo imejengeka kwa muda mrefu ndani ya fikra zao.

Wenzao ambao ni matajiri wao, mara tu pesa inapoingia, kitu cha kwanza ujiuliza ni kitu gani wanaweza kukitoa ili kuondoa kero kwenye jamii ikiwemo le iliyowazunguka. Kwahiyo, wao uweza kuiachia pesa yao kutoka lakini kwa malengo ya kuituma malighafi ambayo pengine ikiunganishwa na mambo mengine uweza kurudi na bidhaa au Huduma ambayo ni hitaji muhimu kwenye jamii. Kwa kufanya hivyo, hata wale maskini walioogopa kuiachia pesa yao mwanzoni, wakati huu uweza kuituma kwa matajiri hao na mzunguko uendelea hivyo hivyo na mwisho ni umaskini uliokithiri.

Kama tulivyoona kuwa kuna milango miwili ya pesa kuingia na kutoka. Mlango wa kwanza ni wa kuingilia (pesa inaingia mfukoni) na wa pili ni wa kutokea (pesa inatoka nje ya mfuko wako). Pesa ikishatoka nje ya mfuko wako, kuna mambo mawili ambayo yanatokea; kwanza pesa inaweza kutumwa mali ambayo iwapo itaongezewa thamani na kutoa bidhaa au huduma ambayo ikiuzwa tena inarudisha ile pesa iliyotoka mwanzoni na nyongeza juu (faida) na hii yongeza ni kwasababu ya thamani iliyoongezeka.  Pili pesa inaweza kutoka nje ili kufuata vitu ambavyo kwako wewe unakuwa ni mtumiaji wa mwisho; kiasi kwamba pesa iliyotumwa vitu vya aina hii, kamwe haiwezi kurudi hata ungefanyaje.

Watu wengi hasa waajiriwa pamoja na wakulima, huwa pesa zao zikishatoka kwa mwenyewe, mara nyingi huwa hazirudi kwasababu ya kutumwa vitu ambavyo wewe ndiye mtumiaji wa mwisho. Sababu kubwa ya waajiriwa ufanya hivyo ni kwasababu ya kutegemea mshahara mwisho wa mwezi. Hali hii humfanya mtumishi pamoja na mkulima kuishi maisha ya kawaida sana ambayo huwa hayabadiliki miaka nenda rudi. Baadhi ya vitu ambavyo pesa ikitumwa kuvifuata yenyewe hairudi ni vingi sana; mfano: Runinga Redio, Karo za wanafunzi, gari la kutembelea, n.k.

Bila kuingilia mipangilio mbalimbali ya watu walionayo, unaweza kuona kuwa pindi tu tunapoanza kazi ya kuajiriwa tunaanza vizuri lakini muda mfupi tu! tunawahi kutekwa na utamaduni wa kupeleka pesa kule ambako huwa hairudi. Na kwenye jamii tulizomo watu wanahamasishana kufanya hivyo. Na mpaka sasa watu wengi wamekuwa wakiishi kwa mazoea, kwamba unapopata ajira eti unashauriwa na wenzako kununua kiwanja na kujenga nyumba ya kuishi na vitu vingine vyenye kupeleka pesa bila kurudi.  

Watanzania, tunahitaji kubadili tabia pamoja na mtazamo wetu juu ya mapato na matumizi ya pesa; tunahitaji kujifunza ni jinsi ya kutuma pesa ikarudi pamoja na vitu. Pia, tunahitaji kuwa na mikakati na mbinu za namna ya kuifanya iwe nyingi badala ya utaratibu uliozoeleka wa kubana matumizi. Tukiweza kuyafanyia kazi yote haya hakika tutakuwa tumepiga hatua moja muhimu sana ya kutufikisha kwenye mafanikio tuyatakayo.

Mpendwa msomaji, endelea kuitumia vizuri MAARIFASHOP ili kujifunza mambo mbalimbali yatakayokuwezesha kupata mafanikio. Ili kupata makala mpya kila zinapochapishwa, bonyeza neno TUMA MAKALA MAARIFASHOP kisha sajiri barua pepe yako. Na kama unapenda kupata mafunzo ya kila siku kwa njia ya whatsap bonyeza neno MAFUNZO

No comments: