Wednesday, May 18, 2016

Elimu ya Pesa Yaanza Kupatikana


"Mwanzo wa kutajirika ni pale utakapojua mwelekeo wa matumizi ya pesa yako, ama ni zaidi kwa viingiza pesa au ni zaidi kwa vitoa pesa!"  ~ Cypridion Mushongi

Watu wazima tuliowengi sasa hivi tunajua kusoma na kuandika. Tumepitia kwenye njia na hatua nyingi, ikiwa ni pamoja na kutumia gharama kubwa kwaajili ya kutafuta kuelimika na kufuta ujinga tuliokuwa nao. Tunamshukuru Mungu, hicho ni kitu kimoja ambacho shule zetu zinakifanya vizuri. Lakini,...
ukweli uliodhahiri ni kwamba watu wazima wengi, bado tunakosa kabisa! elimu ya pesa na masuala yote yanayohusu fedha.

Shule zetu ziko vizuri katika kufundisha kusoma, kuandika na mahesabu ya kawaida kama vile: kujumlisha, kutoa, kugawanya, kuzidisha n.k., Lakini shue hizi hizi haziko vizuri katika kuwaandaa watu kufanya kazi na pesa. 

Karibu kila mmoja anayehitimu masomo iwe katika shule za sekondari au vyuo, anakuwa ni mbumbumbu katika masuala mengi yanayohusu pesa na fedha kwa ujumla. Kwa maana nyingine ni kwamba watu wengi bado tunao uelewa mdogo sana kuhusu kufanya kazi na pesa.

Katika kuanza safari yako ya ukubwani juu ya elimu ya fedha unahitaji kufahamu kuwa kuna mambo makuu manne ninayopenda ni kushirikishe leo ili yakusaidie katika kumudu elimu hii hadimu ya pesa na fedha.

Anza kufahamu historia ya pesa: Ili kupata pesa ni muhimu ukafahamu historia ya pesa tokea ilivyoanza hadi sasa. Kuweza kufahamu kitakachoweza kutokea mbeleni, ni lazima kuelewa na kufahamu kwanza yaliyopita juu ya pesa. Historia ni kama treni. Inasukumwa mbele kwenda uelekeo fulani na kuzidi kuongeza kasi kadili inavyoendelea. Haiwezi kugeuka nyuma bali kuzidi kwenda mbele. Kama unaweza kuona inakotokea – na jinsi ilivyo na haraka, basi ni wazi kwamba utakuwa na wazo zuri sana juu ya inakokwenda, angalau kwa muda mfupi.

Jifunze na kuelewa ripoti yako ya fedha: Moja ya ufunguo muhimu wa wewe kuweza kuwa tajiri ni kufahamu jinsi ya kusoma na kuelewa sehemu kuu tatu za ripoti yako ya fedha. Hizi ni pamoja na ripoti ya mapato na matumizi, pili ni ripoti ya ulinganifu kati ya Viingiza Pesa na “Vitoa Pesa” na tatu ni ripoti ya mtiririko wa pesa kuingia na kutoka. Watu wengi ujifunza katika madarasa ya uhasibu kuhusu namna ya kusoma ripoti ya mapato na matumizi peke yake na ripoti ya ulinganifu wa “viingiza pesa” na “vitoa pesa” peke yake.

Kinachofurahisha ni kwamba, hatahivyo, madarasa haya ya uhasibu, huwa hayafundishi kwanini ripoti moja ni muhimu kwa nyingine, kwani ripoti hizi zina mahusiano ya karibu sana au jinsi ripoti moja inavyoathiri nyenzake.

Kama unaweza kumudu jinsi ya kufahamu uhusiano uliopo kati ya taarifa ya mapato na matumizi na ile ya ulinganifu wa viingiza pesa” na “vitoa pesa”, basi utaweza kuelewa haraka iwapo uwekezaji wako ni wa vitu vinavyoleta pesa mfukoni au ni wa vile vinavyotoa pesa mfukoni. Ukifahamu na kuelewa hili, itakuruhusu wewe kutengeneza au kuwa na uwekezaji sahihi kila mara. Uwekezaji sahihi ndio utakupatia tiketi ya kufikia uhuru wa kipato haraka.

Fahamu jinsi ya kupima uimara wa viingiza pesa: Ufunguo muhimu katika elimu nzima ya fedha ni kufahamu namna ya kupima kama kiingiza pesa ni imara au la! Njia nzuri ya kuweza kulifanya hili ni kutambua na kuzingatia maeneo yote muhimu ya biashara na uwekezaji. Maeneo haya ni pamoja na kuziangalia nyenzo na vitu vyote vinavyohusu “kiingiza pesa” ulichokichagua. Hapa tunazungumzia vitu kama vile: timu ya watu unaofanya nao, uongozi, dhamira, mtiririko wa pesa kuingia na kutoka, mawasiliano na mahusiano, mfumo, sheria, kanuni na taratibu, na mwisho ni bidhaa/huduma unayoizalisha (matokeo).

Jua namna ya kufanya makosa: Haiwezekani ukajifunza kitu chochote bila kufanya makosa kadiri unavyoendelea na mchakato wa kutafuta uhuru wa kipato. Ufunguo kamili ni wewe kuweza kujifunza somo kutokana na kila kosa unalofanya, na siyo kuruhusu makosa yakuondoe kwenye mchezo au yakukatishe tamaa ya kuendelea na kile unachokianya . Angalia kushindwa kama fursa ya kujifunza.

No comments: