Tuesday, May 31, 2016

Mbinu Hizi za Kupata Pesa Zinakufaa



 "Visingizio ndio misumari ya kujenga daraja la kushindwa" ~ Cypridion Mushongi

 

Kupata pesa kunahitaji vitu vingine zaidi ya pesa. Vitu vingine zaidi ya pesa ni pamoja na wewe kufahamu na kujifunza tabia na mbinu mbalimbali wanazotumia wale waliofanikiwa tayari. Kwakusoma makala hii tayari umekwisha anza safari yako ya kutengeneza pesa nyingi na hatimaye kuishi maisha ya ndoto yako.

Ni vizuri safari yako ikaanza kwa kufahamu kwanza mbinu hizi tisa ambazo ni muhimu ukazitumia katika harakati zako za kujenga utajiri kwa sasa na siku za usoni.
 Mbinu hizi ni
rahisi kuzitumia na hapa chini unapata maelezo ya mbinu moja baada ya nyingine:

Uwe tayari kuwa mtu wa tofauti: Usifanye maamuzi yako kwa kuzingatia au kuangalia kile kinachosemwa kufanywa na kila mtu. Badala ya kufuata waliowengi wewe tafuta vile vitegauchumi ambavyo havithaminiki sana halafu vibadilishe kuwa vyenye thamani ya juu. 


Watu wanapenda kufanya kile ambacho kila mmoja anakifanya, lakini ni vizuri ukajenga tabia ya kuwa juu zaidi ya waliowengi kwa kila kitu unachofanya. 

Ili uweze kupima na kuona kama uko juu ya walio wengi, jipime wewe mwenyewe kwa kutumia vigezo vyako binafsi na siyo kulinganisha na wengine.

Wekeza tena faida yako: Mara nyingi unapotengeneza faida yoyote kutoka kwenye biashara yako unaweza kushawishika kuitumia. Lakini, jitahidi kushinda vishawishi, na badala yake iwekeze tena faida hiyo. 

Kumbuka hata pesa kidogo inaweza ikazaa pesa nyingi. Maana yake ni kwamba usjijari ni faida kidogo kiasi gani, bali wewe endelea kuiwekeza na mwisho wake utaona matokeo yenye kufurahisha.

Usikae kunyonya kidole gumba: Kusanya mapema taarifa zote muhimu ambazo unahitaji katika kufanya maamuzi, na muulize rafiki yako au ndugu yako kuhakikisha kuwa unakwenda na muda uliopangwa kakamilisha. 

Ni muhimu ukafikiria kwa makini hicho unachotaka kukifanya na kisha kifanye kwa vitendo. Kama unakaa na kufikiri tu bila kutenda na wakati huo huo hauchukui hatua yoyote, basi huko ndiko kunaitwa “kunyonya kidole gumba”.

Kuwa makini na matumizi madogo madogo: Kutambua na kuwa makini kwa kila matumizi hata kama ni madogo kiasi gani, kunaweza kuzalisha faida. 

Uzoefu umeonyesha pesa nyingi tunazopata zinapotea kupitia haya yanayoitwa matumizi madogo madogo. Kutokana na udogo wake, hata unapotoa pesa haikuumi hata kidogo, matokeo yake unajikuta kama ilikuwa shillingi laki moja utashangaa nusu imeishakatika ndani ya wiki moja.

Weka kikomo cha pesa unayokopa: Kuishi kwenye madeni na mikopo ni hali ambayo siku zote inakunyima uhuru wa kufanya mambo yako. Jadiliana na mtoa mikopo ili uchukue na ulipe marejesho kwa kile unachoweza kumudu. Halafu ukishakuwa uko huru na madeni, anza kuweka akiba ambayo unatakiwa kuiwekeza ili izae pesa nyingi.

Kuwa mvumilivu: Mambo yote makubwa uchukua mchakato mrefu kuzaa matunda. Pia, lazima huwe tayari kuvumilia hali ngumu inayoweza kujitokeza huku ukizidi kufanya kazi kwa bidii bila kuchoka au kukata tamaa. Ukiweza kujenga moyo wa uvumilivu na rahisi kuweza kushinda dhidi ya mshindani mwenye nguvu kuliko wewe.

Fahamu muda gani wa kuacha: Ukiwa unapata hasara au unashindwa au unafanya makosa, jaribu kutafakari na kufikiri kwa makini kisababishi na uone kama hali hiyo inaweza kudhibitiwa. 

Utaratibu wa tathimini ya makosa makubwa yaliyojitokeza unakusaidia sana kujua muda gani muhafaka ambao unatakiwa kuwa mbali na hasara au kuacha. 

Endapo ukiona hakuna namna ambayo unaweza kurekebisha hali ya hasara unayoipata, basi jitahidi kutoruhusu mihemko ya hisia ikakudanganya ukaingia kwenye biashara ya kujaribu tena.

Tathimini hatari iliyobele yako: Kujiuliza maswali juu ya hatari iliyoko mbele yako, kunaweza kukusaidia kuona madhara na hatari zinazoweza kujitokeza pale utakapokuwa ukijaribu kufanya maamuzi. Pia, inaweza kukuongoza kufanya chaguo sahihi.

Fahamu nini maana ya mafanikio: Pamoja na kuwa na pesa nyingi, kamwe usipime mafanikio yako kwa kuangalia kiasi cha pesa ulichokuwa nacho. 

Ukifikia miaka ya uzeeni utagundua kwamba mafanikio yako katika maisha yanapimwa kwa kuangalia idadi ya watu ambao umewasaidia. Na hicho ndicho kipimo hasa juu ya namna gani umeweza kuishi maisha yako.

Jitahidi kutumia mbinu nyingi zikiwemo hizo hapo juu. Anza kuchukua hatua moja baada ya nyingine kwa kuanza taratibu kujifunza kanuni na mbinu madhubuti za kutafuta utajiri. 

Kumbuka kuwa maisha mazuri yanayoambatana na uhuru wa kipato, vyote vinawezekana endapo utaamua kwa dhati kuanza mara moja safari yako ya kutengeneza pesa. 

Jitahidi kusoma vitabu na makala mbalimbali hasa zinazopatikana hapa MAARIFA SHOP. Waweza pia kuwa karibu na blog hii kwa kubonyeza “NAJIUNGA” ili kujipatia makala nzuri moja kwa moja kupitia barua pepe, kila mara zinapotoka.

No comments: