Katika maisha yetu ya kila siku, neno “kesho” linatumika sana kama njia
pekee ya kuhairisha mambo mengi, ambayo kimsingi yalitakiwa yafanyike “leo”.
Kesho ni miongoni mwa maneno yanayopendwa kutumiwa kama kinga ya kukataa
kutimiza majukumu fulani ya leo. Badala ya mtu kusema “HAPANA” kitu hiki,
anajibanza nyuma ya...
kesho, huku akidhani kuwa ataweza kufanya au kutimiza
majukumu ya leo siku ya kesho. Matokeo yake, kesho ikifika anasogeza tena mbele
kwasababu kuna kesho nyingi mbele yake. Kwa maneno mengine ni kwamba, tunahitaji
kujiadhari sana na “kesho” kwani bila kufanya hivyo, tutajikuta kwenye hali ya
umaskini wa mkubwa.
Ni ukweli usiopingika kuwa neno
baya kuliko maneno mengine na linaloongoza kwa kuharibu maisha ya binadamu ni neno
liitwalo “Kesho”. Watu wengi hasa maskini, watu ambao hawajafanikiwa, wasiokuwa
na furaha, na wale wasiokuwa na afya njema ni kundi la watu ambao upendelea sana
kutumia neno “kesho”.
Ndiyo maana watu wa namna hii,
mara nyingi upendelea kusema maneno kama “nitaanza uwekezaji kesho au “nitaanza
kutumia lishe bora kesho” au nitaanza mazoezi ya kupunguza uzito kesho! Wengine
usikika wakisema “ nitaanza kusoma vitabu au mtandao kesho.
Ukichunguza kwa undani unagundua
kuwa neno “kesho” linatumika sana
kumaanisha kuwa jambo fulani litaanza kufanyika siku ambayo siyo ya leo. Ndiyo
maana utasikia nitaanza hiki siku ya kesho, wiki, mwezi, mwaka kesho au wakati
ujao.
Kwanini
watu upendelea kusema kesho?
Sababu ni moja tu kwamba tunayo
hulka ya kupenda kufanya vitu vingi kwa mara moja na ambavyo haviko katika
mpango maalum. Tunapenda sana kufanya kazi kwa kufuata kasi ya matukio
yanayoendelea kutokea. Kwahiyo, mambo au shughuli za leo zinapozidi uwezo
unaamua kuzipeleka siku ya kesho. Kwa mfano unaweza kukuta kwamba kufika saa
sita mchana wa leo, tayari umekwisha hairisha shughuli za kutosha siku nzima ya
kesho.
Lakini uzoefu unaonyesha kuwa unapoona
kitu hujakifanya leo, basi ujue siyo muhimu. Kuhusu kitu gani muhimu ufanye
leo, hakiji hivi hivi, ni lazima shughuli zako nyingi za kila siku zifanyike
kwa kulenga ndoto yako ya maisha yaweza kuwa ni miaka mitano, kumi au na zaidi.
Bila kuwa na ndoto au maono juu
ya maisha unayotaka kuyaishi, lazima utaendelea kufanya kazi zako nyingi kwa
kufuata matukio ya siku husika. Mwisho wake kila utakapofanya tathmini ya miaka
5 au 10 iliyopita unajikuta umezidi kurudi nyuma, hapo ndipo utaanza kutafuta
wa kumlaumu. Kuchanganyikiwa kwa watu wengi ambako uambatana na msongo mkubwa
wa mawazo, mara nyingi uja kwa njia hii.
Kwahiyo, ni muhimu kwetu wote
tunaotaka maisha huru kutambua kuwa vitu vyote muhimu kwa maisha yetu ni vile vinavyofanyika
leo. Maisha yako siyo kesho, wiki, mwezi, mwaka au miaka kumi ijayo BALI maisha
halisi, ambayo una fursa ya kufanya kazi itakayo kuletea mafanikio makubwa siku
za mbeleni ni pale unapoamka kitandani asubuhi hadi muda ule unapolala usiku.
Unapofikia hatua ya kulala baada ya kuwa umefanya kazi mbalimbali mchana kutwa
basi ujue ukilala maisha yameishia hapo.
Ni muhimu tukafanya yale yote
yaliyo muhimu leo. Ukishatambua hilo, utakuwa wa kwanza kuona umuhimu wa
kuianza siku yako mapema alfajiri. Makala hii unayoisoma wakati huu, nimeanza
kuiandika leo usiku huu saa “tisa na
dakika ishirini na sita hadi kumi na moja alfajiri”. Nafanya hivi ili
kuipanua siku ya leo, ambapo kwa kufanya hivyo, ninapata uwezo wa kufanya vitu
vingi muhimu siku ya leo. Kwa maana nyingine ni kwamba ili tupate mafanikio
tuliyoyalenga na zaidi, lazima tuwe watu wa kuanza siku yetu mapema.
Kwa tulioajiriwa, bado tusiwe na
wasiwasi na muda kwasababu wengi wa waajiri wetu wanadhibiti masaa nane tu! Na
sisi tunadhibiti masaa 16 yaliyobaki.
Kwahiyo, tukijipanga vizuri tunaweza kujikuta tunayo masaa 8 ambayo
tunaweza kuyawekeza kwa faida. Haya masaa 8 yanajumuisha yale masaa kabla ya
saa moja na nusu asubuhi na baada ya saa tisa na nusu alasiri hadi saa nne
usiku kabla ya kulala.
Ukiharibu masaa yale kuazia unapoamka
asubuhi hadi unapokwenda kulala usiku, ujue kuwa umeharibu maisha yako.
Kushindwa hakuji siku moja BALI ni matokeo ya kushindwa kidogo kidogo kila
siku. Ukiona umeshindwa au unakabiliwa na umaskini usifikiri ni jambo ambalo
limetokea leo bali ni kutokana na wewe kuchezea yale masaa ya kuanzia unapoamka
hadi unapolala.
Kwa wale wasomaji wa MAARIFA
SHOP ambao ni vijana, mnaweza kusema “LEO NDIYO DILI”. Hii ikiwa na
maana kwamba tukifanya kazi sana leo tutapata ushindi au mafanikio kidogo na
kesho tukifanya kama au zaidi ya leo tutapata mafanikio kidogo.
Yale mafanikio kidogo kidogo
tunayovuna kila siku ndiyo kwa ujumla wake yatatufanya kuwa na mafanikio
makubwa miaka 5 au 10 ijayo na hapo ndipo wengi watakapoanza kukutambua kwamba
na wewe huwa upo!
Jitahidi kuipenda na kuikumbatia LEO
na uachane kuwa na mpenzi wa KESHO kwasababu, neno hili linaharibu sana maisha
ya watu wengi kuliko maneno mengine. Achana na neno“kesho” kwasababu haitatokea huione kesho. Kesho huwa haipo. Kesho
huwa ipo tu kwenye akiri za watu waota ndoto bila vitendo na wale washindwa. Nimalizie
kwa kusema kuwa sijawahi kuiona “kesho” kitu
tulichonacho pekee ni “Leo”. LEO ni neno la washindi na KESHO ni neno la washindwa.
Unahitaji
kujifunza vitu rahisi vya kufanya, ili kuifanya siku ya leo iwe na mafanikio. Fanikisha
hili kwa kubonyeza neno “MAARIFA
SHOP” kisha
weka barua pepe yako kwa mafunzo ya uhakika zaidi.
No comments:
Post a Comment