Mara nyingi watu wengi tunapozeeka udhania kwamba tumekua kumbe ndio kwanza tunazidi kuwa watoto wachanga. Mafanikio makubwa yanapatikana kwa urahisi kwa wale tu waliokua na si waliozeeka. Ukikua ndipo unapata-
mafanikio, watu wengi hatujafanikiwa kwasababu hatujakua hata kidogo, japo kuwa tunakwenda kuzeeka.
Inabidi “kukua”. Watu uzeeka, lakini wawe wamekua na siyo kuzeeka peke yake. Watu wengi uishi kwa kutunzwa na kukingwa na wazazi, wakitoka kwenye kinga ya wazazi bado wanakwenda kwenye kinga ya kampuni binafsi, shirika au serikali.
Kwa maneno mengine watu wengi tunategemea zaidi mtu mwingine kutulinda/kutujali au mtu mwingine abebe majukumu yetu kutokana na sisi kukosa busara na akiri ya msingi nay a kawaida. Ndiyo maana tunatafuta kwa nguvu zetu zote usalama wa ajira au kupata hifadhi ya mwajiri.
Watu wengi sana utumia muda wao mwingi kutafuta dhamana ya maisha na katika maisha yao yote ujitahidi sana kukwepa hatari (risks), ambazo wanazohisi zinaweza kuwapata endapo wakithubutu kufanya chochote kujikwamua kiuchumi. Pia, wengi wetu tumekuwa tukikwepa kukua na mara zote kutafuta wazazi wa kurithishwa, ili watutunze na kutujali.”
Mimi na wewe tunafahamu watu wengi ambao hawana uwezo wa kufurukuta bila mafao ya uzeeni (pension). Tunafahamu, watu ambao hawajazeeka au kufikia umri wa kuchukua mafao yao kutoka kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii, lakini ukiongea nao sasa hivi tayari wameanza kuhesabu kwamba pension yao na bima za afya vitakuwepo kuwatunza uzeeni na au siku za mbeleni.
Ukweli ni kwamba kinga au aina hizi za hifadhi ya jamii zilitengenezwa na kuwekwa wakati wa zama zile za mapinduzi ya viwanda huko Ulaya na Marekani. Mifuko ya hifadhi ya jamii wakati huo iliwekwa kwaajili ya kutoa kinga kwa wale vibarua maskini wa viwandani, ambao walikuwa ni wahitaji kwelikweli. Bahati mbaya leo hii kuna watu wengi, hasa wale waliosoma na wanalipwa mishahara mikubwa bado wangali wakihesabu au wakitegemea waajiri wao wawatunze na kuwajali.
Kwasasa tuko katika kizazi cha taarifa kinachoambatana na teknolojia ya habari na mawasiliano, na ni muda ambao tunaanza kukua na kuwa watu wazima kifedha na kimapato. Kwa maana nyingine, huu ndio muda muhafaka wa kuondoka kwenye kinga ya mwajiri na programu za hifadhi za kijamii, ili kuwaachia wale ambao kimsingi wanahitaji kwa dhati kabisa.
Nilipomaliza kidato cha sita, nilifikiri nimekua na kwamba nilikuwa tayari ninajua majibu yote ya maswali mengi katika maisha. Mara nyingi siku hizi huwa nasema “ningekuwa ninajua wakati huo, hiki ninachokijua leo”. Kuna vitu vingi nilifanya siku za nyuma ambavyo hatahivyo ninajivunia kuvifanya, lakini siwezi kuvifanya leo.
Kukua maana yake ni kufanya vitu kwa njia tofauti na ilivyokuwa zamani kadiri umri wetu unavyoongezeka. Kuendelea kufanya yale yale ya zamani kila siku ya maisha yetu, kwa kiwango kikubwa ni kwamba maendeleo ya akiri na hisia zetu zote zitakuwa zimekamatwa na kutekwa. Dunia inabadilika, na inakua ya viwango vya juu vya maisha, kwahiyo na sisi lazima twende na kasi ile ile.
Kukua ni kuwa na utayari au utashi wa kuzidi kuongeza uwezo wa kwajibika kujitunza wewe binafsi na familia yako bila kumtegemea mama, baba wala mwajiri. Kukua pia, ni pamoja na kuwa tayari kuwajibika kwa vitendo, elimu yako, na utu uzima wako kwa ujumla.
Kama unataka kuwa na maisha ya uhakika wa kipato siku za mbeleni, ni lazima sasa kufahamu kuwa uchumi wa soko huwa ni kupanda na kushuka na hakuna mtu yoyote ambaye yuko hapo kwaajili ya kukulinda au kukupa kinga dhidi ya mtikisiko wowote wa kimaisha unaoweza kutokea. Kadili tutakavyokua kwa haraka na kuukabili ukweli, ndivyo itakavyokuwa rahisi kukabiliana na hali ya maisha ya baadae kwa umakini na uwezo mkubwa.
Katika zama hizi taarifa na mawasiliano, wengi wetu tunahitaji kukua na kuachana na mawazo yaliyokuwepo karne ya 18 zama zile za mapinduzi ya viwanda huko Ulaya, ya kutegemea mtu mwingine kuwajibika kwaajili yako ili kukuhakikishia usalama wa ajira na usalama au uhakika wa kipato.
Kukua ni kuendelea kupunguza utegemezi kwa mtu mwingine, katika kuendesha maisha yako. Na zaidi hapo kuzidi wewe kujitunza, kujipatia mahitaji yako na mahitaji ya wengine. Kwangu mimi naona “kukua ni mchakato mrefu wa maisha”, mchakato ambao watu wengi wanajitahidi kuukwepa kwa kuendelea kutafuta usalama wa ajira na usalama wa kifedha unaotolewa na mtu mwingine tofauti na wao wenyewe.
Kuendelea kukua ni tabia moja muhimu sana. “Kama unataka kuishi maisha utakayo na siyo maisha uwezayo”, basi inatupasa kukua haraka zaidi kuliko watu wengi ambao wanapendelea kukua kama kinyonga.
Leo ni siku yangu ya kuzaliwa kwa mara ya 45. Hii ina maana kwamba siku ya jana (08/09/2016) ndiyo siku ambayo nimetimiza 44 ya kuzaliwa na wakati huo huo, mtoto wangu wa kwanza KEEN MUJWAHUZI amemaliza mtihani wake wa kumaliza elimu ya msingi (darasa la saba).
Katika mwaka huu wa 45 ambao nimeuanza rasimi leo, nitajitahidi sana kukua bila kuzeeka na ninaomba sana Mungu anisaidie nikue kwa viwango vya juu sana.
Katika kutimiza malengo na majukumu haya, ninaomba ushirikiano wa kila mmoja wenu na hasa wale wapenzi wa mtandao maarufu wa MAARIFA SHOP.
Kama uko tayari kushirikana na mimi ili KUKUA pamoja mwaka huu, bonyeza neno “USHIRIKIANO” , ili hatimaye tuweze kuwasiliana mara kwa mara kupitia barua pepe na njia nyingine za mawasiliano.
KARIBU TWENDE KAZI PAMOJA
No comments:
Post a Comment