Wednesday, July 3, 2024

Mjasiriamali Biashara yako Inakufa Kwasababu hizi

∞∞∞ "Ni bora kuishi na mtu aliyeshindwa kuliko mtu mwenye Mashaka ~ Cypridion Mushongi" ∞∞∞

Biashara ni mradi au mfumo unaotengenezwa na mjasiriamali kwa lengo la kuzalisha bidhaa au huduma inayokidhi mahitaji ya wanajamii (wateja) mbalimbali duniani. 

Wakati wote, biashara inapoendelea kutimiza malengo ya kuanzishwa kwake, hapo tunasema kuwa “Biashara yako ni hai na inaishi”. Tunasema biashara “imekufa” endapo..
itashindwa kutimiza malengo ya kuanzishwa kwake ambayo ni kushindwa kuzalisha bidhaa au huduma zinazokidhi mahitaji ya wateja wake.

Yako mambo mengi yanayoweza kuua biashara yako na katika ya hayo kuna yale ambayo ndiyo hasa chanzo cha kifo. Ukiuliza kinachoua biashara, mara nyingi utaambiwa vitu vile vilivyozoeleka, lakini ambavyo siyo chanzo kikuu. 

Vitu utakavyoambiwa ni kama: “hakuna mzunguko wa pesa, mtaji mdogo n.k. Lakini ukweli ni kwamba kuna vitu ambavyo havitiliwi maanani lakini kimsingi ndivyo huwa ni kisababishi kikuu kama hivi hapa:

1. Kuwa mtu mwenye mashaka: Mara nyingi “mashaka” ni jambo linaloua biashara nyingi. 

Mjasiriamali mwenye mashaka na biashara yake, siku zote anakuwa na tabia ya kutoipa kipaumbele namba moja katika kuwekeza muda, fedha, vifaa, teknolojia n.k. maana yake, mjasiriamali unakaa na mashaka muda wote. 


Inashangaza kuona mjasiriamali unajipa muda mwingi wa kutilia mashaka biashara uliyoanzisha, kuliko muda wa kutafuta ubunifu, teknolojia, fedha kwaajili ya kukuza biashara yako.

2. Kukatishwa Tamaa: Daima kukatishwa tamaa, hufanywa na watu wanaokuzunguka au watu wako wa karibu. 

Ni hivi! Unapoona rafiki yako anakwambia kuwa biashara fulani huiwezi ni ngumu, maana yake anakwambia kuwa ugumu huo, uko kwake yeye. Lakini anaongea kwa sauti kana kwamba huo ugumu ni kwako wewe. 

Unapoona mtu anaongelea kuhusu ugumu wa kufanya biashara fulani, tambua kuwa mtu huyo anajaribu kukuuzia ugumu alionao yeye juu ya biashara hiyo unayotaka kuifanya.

Kama ukimkubalia kwasababu tu! ni ndugu au rafiki, basi ujue kuwa umeamua KUNUNUA ugumu na yeye AMEUZA kwako. Kwahiyo, mwisho wake utakachokipata ni kushindwa! 

Kukatishwa tamaa mara nyingi hufanywa na watu ambao kimsingi tunawaita “watafutaji” wa pesa. Kama wewe ni mjasiriamali yaani "mtengenezaji" pesa, tambua kuwa watakaokuja kukukatisha tamaa ni watafutaji ambao siyo wenzako. 

Mtafutaji hawezi kuwa rafiki wa mjasiriamali (mtengenezaji), kwasababu mnatumia mfumo na mtindo tofauti wa maisha. 

Maswali ya kujiuliza ni je, mtafutaji ni nani? Na je, mtengenezaji ni nani? Nitawatofautishaje ili nijue nani wa kumsikiliza? Majibu ya maswali haya utayapata kwenye makala zitakazochapishwa siku za usoni hapa MAARIFASHOP.

3. Kuwa na Hofu: Mara nyingi, hofu huwa ni jambo LA kufikirika au hisia tu! siyo uhalisia wa mambo. 

Hofu hukuzuia kuanza kufanya biashara na siku zote, mtu mwenye hofu anakuwa na tabia ya kusitasita katika maamuzi ya kuchukua hatua.

4. Fikra Hasi: Kuwepo kwa fikra hasi kunatokana na ukweli wa kanuni ya sayansi inayosema kwamba "Chanya Huvuta Hasi"

Unapoanzisha bisahara, kwako wewe hilo ni jambo "Chanya"

Ndiyo maana, biashara ikianza tu! Unaanza kukumbana na mambo "Hasi" kutokana na ukweli kwamba, biashara yako (Chanya) imeanza kuvuta "Hasi"

Ukianza kukumbana na hali hiyo usilalamike badala yake jikite katika kutafuta namna ya kuondoa au kupunguza athali zake.

Unapokumbwa na jambo lolote ambalo ni "Hasi" libadilishe kwa kuweka mambo matano (5) ambayo ni "Chanya". 

Umahiri wako katika kujenga na kulinda biashara yako isife, ndio unakujengea UJASIRI WA KUTAFUTA MALI. Ukifikia hatua hii, jamii inakupa hadhi ya kuitwa MJASIRIAMALI

Kwa wajasiriamali wa zamani na wale wapya, endelea kupata MAARIFA yatakayokuwezesha kupata mafanikio. 

Ili kupata makala mpya kila zinapochapishwa, bonyeza neno MAKALA MPYA kisha sajiri e-mail yako. 

Kwa wale wanaopenda kupata mafunzo kwa njia ya whatsap bonyeza neno MAFUNZO.

KARIBU WOTE KATIKA KUSAKA MAARIFA!

No comments: