Monday, March 20, 2017

Utajiri au Umaskini Utokana na Nini?



 


Kila mmoja ninaamini anao uwezo wa kuwa tajiri, isipokuwa binadamu huwa na fikra tofauti juu ya mambo yale yale. Kitu kilichoko akirini mwako ndicho kinacho leta tofauti ya hali ya Maisha unayoishi kwa sasa . Maana yake ni kwamba, jinsi ulivyo wewe ni zao la yale yote unayofikiri kila siku. Watu waliofanikiwa kuwa matajiri, wana mambo kama 5 ambayo wameyafanya kuwa kama kanuni zao za kudumu na kwakuwa ni kanuni, wao huzitekeleza na kuziishi kila siku. Kanuni zenyewe ni....

Namba moja: Matajiri wana fikra vichwani mwao kwamba kila kitu duniani kipo kwa wingi. Lakini maskini wao ufikiri kwamba kila kitu duniani hakitoshi. Kwa maneno mengine ni kwamba, masikini kila wakati anafikiria uhaba, jambo ambalo umletea wasiwasi na kumnyima uwezo na moyo wa kusubili mambo makubwa yatokee kwake.

Watu wote tuko duniani hapa hapa, lakini tunatofautiana sana utajiri tulionao. Kitu kimojawapo kinachosababisha utofauti huu mkubwa ni jinsi tunavyofikiri na mtazamo tulionao juu ya ukweli wa rasilimali zilizopo hapa duniani.

Matajiri wao uamini katika ukweli kwamba fikra za binadamu ndizo uzaa vitendo na vitendo uzaa matokeo, ambayo ni pamoja na pesa. Kwa vyovyote vile ukifikiria kupata pesa kiasi fulani lazima ufikirie kitu cha kufanya ambacho ukikifanya kitakuletea pesa zaidi ya ile uliyokuwa unahitaji. Uzuri wa matajiri ni kwamba, wao ufikiria na kuiona pesa kwenye akiri yao tayari kabla ya kuishika au kuipata. Maskini wao ufikiria na kuona uhaba ndani ya akiri yao kabla ya kupata pesa.

Kwakuwa maskini wao ufikiria uhaba kwanza kabla ya kitu kingine, ndiyo maana uishia kufanya kazi ndogo ndogo na vitu vidogo vidogo, ambavyo mwisho wake umpatia pesa kidogo (haba) zinazolingana na uhaba alioufikiria mwanzoni kwenye akiri yake. Kwa maana nyingine watu maskini pesa kidogo wapatayo, uifikiria mapema kabla hata ya kuanza kazi ya kuitafuta.

Namba mbili: Matajiri wao uona fursa mbele yao, wakati maskini wao uona matatizo tu mbele yao.

Mfano mwalimu mmoja alifundisha wanafunzi darasani, lakini mwisho wake wanafunzi wengi wakashindwa vibaya sana wakalazimika kukaririri darasa. Mwalimu huyu alianza kulalamika na kusononeka. Mara akafikiria kuwa darasa hilo yawezekana lina wanafunzi ambao hawana uelewa wowote ni wabovu wa kufikiri. Mwalimu mwingine aliposikia na kujionea hali halisi ya kushindwa kwa wanafunzi hawa, akaona fursa.

Baada ya kuona fursa hiyo, akatunga kitabu cha mwongozo wa “jinsi ya kufahuru mtihani na akatoa fursa kwa wanafunzi kuweza kulipia na kupata masomo ya ziada. Kitabu pamoja na masomo ya ziada kwa wanafunzi ni vitu vilivyompatia pesa nyingi wakati mwalimu huyo mwingine aliendelea kulalamika huku akiandamwa na umaskini wake kama kawaida. Walimu hawa wawili wanawakilisha makundi mawili ya watu—maskini na tajiri ambao tofauti zao ni fikra tofauti kwa kitu kile kile.

Namba tatu: Matajiri wao ununua vitegauchumi ambavyo baadae uwatengenezea faida na faida hii wao uiwekeza tena na tena. Kitendo hiki cha kurudisha faida kwenye vitegauchumi kila mara, uwapa fursa ya kuifanya faida waliyoipata kuzaa pesa nyingine zaidi.

Namba nne: Matajiri wao ujali sana kuwa na mtandao wa watu waliofanikiwa. Maskini wao upenda kukaa peke yao, kufanya kazi peke yao n.k. Matajiri uona umuhimu sana wa kuwa na watu waliofanikiwa. Unapokuwa na mtandao wa watu waliofanikiwa unapata nafasi ya kusikiliza simulizi zao za mafanikio, na wakati mwingine wanapata kukwambia njia sahihi walizotumia kufanikiwa. Mambo yote mazuri unayojifunza kutoka kwao, ukufanya na wewe upende na kuanza kufanya kama wao.

Namba tano: Matajiri wao pesa uwafanyia kazi wakati watu maskini ufanyia kazi pesa. Maana yake ni kwamba, maskini wanafanya kazi kwa niaba ya pesa na kwa upande wa pili pesa inafanya kazi kwa niaba ya tajiri. Kinacholeta tofauti hapa ni kwamba kwakuwa tajiri pesa inamfanyia kazi, anakuwa na muda wa kufanya vitu vingine vingi ndani ya masaa 24.

Maskini yeye anafanya kila kitu mwenyewe, kwasababu anaogopa kutumia pesa isije ikaisha—muda wote anajihami pesa isiishe, ingawaje mara zote imekuwa ikiisha bila kujali ubahili wake. Tatizo la kufanya kazi mwenyewe, ni kwamba unatakiwa kufanya kazi muda wote wa Maisha yako, kwani siku ukiacha pesa nayo inakatika. Ndiyo, maana inakuwa vigumu kusafiri au kufanya kitu chochote kile nje ya hiyo kazi. Maisha ya namna hii si mazuri hata kidogo. Tunahitaji kufanya kazi ambazo mwisho wake zinatupatia mazingira ya kuwa na uhuru wa kuchagua mambo mbalimbali tunayoyapenda.

Jaribu kutafakari baada ya kusoma makala hii, vuta picha ya maisha yako binafsi na uone kati ya makundi hayo mawili—maskini na tajiri wewe uko wapi na unaelekea wapi hata kama ni miaka 10 ijayo usijari, ilimradi tu una malengo mahususi. Ukisha pata picha amua unataka kukaa katika kundi lipi. Maamuzi yoyote utakayokuwa umeamua yasimamie na usilalamike hata siku moja. Ikitokea ukaona upande uliochagua kuishi haukufuraishi tena, basi fahamu kwamba wewe unao uamuzi wa kuhamia upande ambao unakidhi matarajio yako, kwani kikubwa katika maisha ni Amani na furaha.

No comments: