Wednesday, July 31, 2024

Biashara Ina Mshindani Hatari Huyu Hapa

 

Miradi ya Biashara ni Viumbe Hai” ~ Cypridion Mushongi
Mwandishi wa vitabu anayejulikana kama 'Napoleon Hill' aliandika kwenye kitabu chake cha ‘THINK & GROW RICH’ kwamba Mawazo ni vitu. Ndiyo maana tunasema, miradi mingi ya biashara..
tunayoiona leo ilianzia vichwani mwa wajasiriamali kama wazo.

Mjasiriamali anapoanzisha mradi wa biashara ni sawa na kufanya kazi ya uumbaji wa kitu kinachokwenda kuishi hadi hapo atakapoamua kife. 

Kwa mtazamo wa uumbaji wa wazo na vitu, ni wazi kwamba “Miradi ya Biashara ni Viumbe Hai”.

Ndiyo kusema kwamba biashara yoyote inazaliwa, inakua, inaishi na ikibidi inakufa. 

Ili biashara yako iweze kukua na kuishi kwa muda mrefu, inahitaji ‘mazingira’ mazuri ambayo yatasaidia kukua na kuishi kwa miaka mingi ijayo.

Dhana ya ‘mazingira’ kwa biashara, inamaanisha kila hali inayokuzunguka wewe pamoja na biashara yako.

Katika hali ya kawaida, kukua na kuishi kwa biashara yako kunataka 'mazingira rafiki' ambayo yanatengenezwa na wewe mwenyewe kama mmiliki. 

Suala la kutengeneza 'mazingira rafiki' ni lazima na siyo jambo la hiari au utashi binafsi!

Biashara inapoanzishwa, inamtaka mmiliki kuwa na tabia zinazoendana na mahitaji ya biashara yenyewe.

Tabia yako kama mmiliki ni kiungo muhimu sana katika kujenga mradi wa biashara wenye tija, kwani tabia ambayo ni kinyume cha matakwa ya mradi, inaweza kudhoofisha sana biashara yako.

Ukianzisha mradi wa biashara, usiangalie tu ile bidhaa au huduma unayokwenda kuzalisha au kuuza! Badala yake angalia pia tabia yako wewe kama mmiliki.

Wajasiriamali wengi wanazichukulia biashara zao juu juu tu! Kiasi kwamba hawatambui ni kwa kiasi gani tabia zao kama wao zinavyoweza kuathiri ustawi na ukuaji wa miradi mbalimbali ya biashara zao.

Kutokutambua athari mbalimbali zinazotokana na tabia za mmiliki, kumesababisha USHINDANI kutokea ndani – yaani mmiliki anakuwa 'mshindani' wa biashara aliyoianzisha yeye mwenyewe. Kwa maana nyingine mjasiriamali unashindwa kutii matakwa ya biashara yako ndiyo maana tunakuita 'Ushindani'. Kwa mfano;

"Biashara inataka uamke kila siku saa 10 alfajiri, lakini wewe unashindana kwa kusema usingizi wa asubuhi ni mtamu".

 "Biashara inataka utenge asilimia kumi (10%) kama akiba ya kulinda mtaji, wewe unashindana kwa kutumia pesa yote katika vitu visivyohusiana na biashara yako".

"Biashara inataka kuwa na kauli nzuri kwa wateja, wewe unashindana kwa kutoa lugha zenye kuudhi wateja"…

"Biashara yako inakutaka kuwa msafi na nadhifu wewe unashindana kwa kutojali uchafu uliopo kwenye mazingira ya biashara"….n.k.

Naweza kusema kuwa mifano kuhusu namna ambavyo tumekuwa 'Washindani' wa biashara zetu wenyewe ni mingi sana. 

Kutokana na uwepo wa aina hii ya 'Ushindani', biashara nyingi zimeporomoka na nyingine kufa kabisa.

Ni muhimu kuwa makini na aina hii ya 'Ushindani' kwasababu mara nyingi haujulikani na hauonekani kirahisi.

Kwahiyo, badala ya kuelekeza fikra na nguvu zote kwenye bidhaa inayozalishwa au kuuzwa peke yake, ni muhimu pia kuangalia upande wa tabia ya mmiliki wa biashara husika.

Ndugu mjasiriamali, unalo jukumu kubwa la kutambua tabia gani ni za muhimu kuzifanyia kazi kwa lengo zima la kukuza na kusitawisha biashara yako.

Katika kulifanyia kazi hili, jiulize swali; “Biashara yangu inataka mabadiliko ya tabia zipi na zipi?”  
Ukifahamu aina ya tabia zinazohitajika itakusaidia sana “KUEPUKA USHINDANI DHIDI YA BIASHARA YAKO.

Unahitaji MAARIFA kuuona ni jinsi gani wewe kama mmiliki unakuwa ‘Mshindani’ mkuu wa biashara yako. 
Kupitia elimu na ujuzi unaopatikana hapa MAARIFASHOP utaweza kujipatia fikra mpya na mbadala zitakazosaidia kufanikia maisha ya ndoto yako.

Unaweza kupata makala mpya kila zinapochapishwa, kwa kubofya neno MAKALA MPYA kisha sajiri E-mail yako. Kwa wale wapenzi wa kupata mafunzo kwa kupitia simu janja bofya neno MAFUNZO.




No comments: