Monday, March 27, 2017

Pesa Inatakiwa Kuja Kwako Kwasababu Hii


Kila binadamu amezaliwa kama mchumi na anapaswa kuwa mchumiLakini, kwa wastani watu wengi siyo wachumi kwasababu hatujui thamani ya vitu ambavyo tayari tunavyo. Kuwa mchumi maana yake—siyo kuwa mbahili bali ni ile hali ya kuweza kupata matokeo makubwa kutokana na matumizi kidogo. Kazi ya kupata matokeo makubwa kutoka kwenye matumizi madogo si kitu cha hivi hivi bali ni..
kitu kinachotulazimu wote kujifunza “Menejimenti” ya rasirimali mbalimbali kwa lengo la kupata bidhaa au huduma.

Katika mtazamo wa Maisha ya binadamu ni kwamba neno menejimenti ni uwezo wa wewe kuweza kuongeza thamani ya kipaji chako abayo ambacho kimsingi ndiyo zawadi uliyopewa na Mungu. Zawadi au kipaji chako unatakiwa ukitoe nje katika sura ya suruhisho kwa matatizo yanayoikabili jamii na dunia kwa ujumla na hasa tukianza na wale waliotuzunguka.

Ili haya yote yaweze kufanyika ni lazima kila mmoja ajifunze kuwa na kuishi Maisha ya “meneja”. Kuwa meneja siyo lazima uwe bosi wa kampuni Fulani au msomi uliyebobea bali ni ule uwezo wa kuweza kuunganisha nguvu ya akiri na nguvu ya mwili kuzalisha bidhaa au huduma. Pia lazima kazi ya menejimenti iambatane na udhibiti katika kutumia rasilimali zilizopo ili hatimaye mambo makubwa yatokee kutoka kwenye mambo madogo.

Endapo ukiamua kuwa na kuishi kama meneja, pesa ni rahisi kuipata, na katika hali ya kawaida hakuna sababu ya pesa kutokuja kwako. Kwa maneno mengine, pesa siyo tatizo bali tatizo ni manejimenti ya pesa. Pesa inahitaji nidhamu, juhudi, maarifa bila kuchoka na udhibiti. Watu wengi tunafaulu kiasi fulani kipengele cha kutafuta pesa, lakini mbinu tunazotumia kudhibiti pesa zetu ni za kizamani sana na zimepitwa na wakati. Matokeo yake, pesa nyingi tunayoipata, hatujui inapoteaje na inaenda wapi.

Maana nyingine ya manejimenti ni ile hali ya kuwa mbunifu, mwangalizi na mdhibiti wa rasirimali ili ziweze kutumika kulingana na vipaumbele vilivyowekwa na mhusika. Katika historia ya Maisha ya binadamu, imeonekana kuwa Mungu huwa hatoi pesa kwa waumini BALI yeye utoa pesa kwa mameneja.

Kila wakati unapoomba kupata pesa Mungu anakupa WAZO. Tatizo la waumini wengi tunataka taslimu (cash), hatutaki MAWAZO. Na tukumbuke kuwa, ili mawazo yetu yaweze kubadilika kuwa pesa, lazima kitumike kitu kinachoitwa “menejimenti”. Kwa maana nyingine ni kwamba, pesa yoyote inakuja kwako endapo utatumia “menejimenti” katika kutumia vizuri rasilimali kwa malengo na makusudio ya WAZO

Usidhani wewe huna pesa, nasema pesa unayo, LAKINI unachokikosa ni menejimenti ya mawazo pamoja na jinsi ya kuyageuza kuwa pesa. Manejimenti ndiyo lengo la msingi kwa binadamu yoyote yule. Ukweli ni kwamba, kila utakaposhindwa kuwa na menejimenti ya vitu au mawazo uliyonayo lazima upoteze hata hicho kidogo ulichonacho. Menejimenti ndiyo inayovuta rasilimali zingine kuja kwako. Kama hakuna menejimenti, biashara yoyote haiwezi kukua hata kidogo.

Kutokana na sisi kushindwa kuwa mameneja wa Maisha yetu; ndiyo maana hatuwezi kulipa madeni tunayodaiwa; ndiyo maana tunawafanyia kazi watu wengine hata kama wanatutukana na kutudharirisha bado tunawafanyia kazi kwasababu moja tu! tumeshindwa kuwa mameneja wa mstakabali wetu wa Maisha.

Kutokana na kushindwa au kupuuzia umuhimu wa menejimenti; tumebaki kuwa watu wa kutegemea “miujiza”. Lakini kumbuka kwamba miujiza siku zote ni kwa wale watu wavivu. Nashangaa watu wengine wanaenda kanisani eti pesa zao ziombewe kwa Imani kwamba baada ya muda si mrefu zitaongezeka—Inahitajika nguvu ya akiri ya ziada kuweza kulitambua hili sawa sawa. 

Endelea kujifunza kila siku kwa kujiunga na mtandao wako wa https://maarifashop.blogspot.com. Ili kujiunga bonyeza neno NISAJIRI, kisha weka e-mail yako na kufuata maelekezo machache hapo itakuwa rahisi kupata Makala nzuri kila zinapochapishwa hapa

No comments: