Monday, March 13, 2017

Ugonjwa wa Kuchoka Unatumaliza!


“Chanzo kikuu cha ugonjwa wa kuchoka ni watu wengi kufanya kazi ambazo hawazipendi” ~ by Cypridion Mushongi.
Ugonjwa ni hali ya kutojisikia vizuri, na wakati mwingine hali hii uambatana na maumivu makali sana. Katika ulimwengu wa afya, magonjwa yamegawanyika katika makundi makuu mawili. Kundi la kwanza ni magonjwa ya kuambukiza, mfano: kipindupindu, malaria, ukimwi n.k.

Kundi la pili ni
magonjwa yasiyo ya kuambukiza, kama vile shinikizo la damu, kisukari, tezi dume n.k. Lakini mara zote tumekuwa hatuoni au tumeshindwa kutambua ugonjwa wa “kuchoka” ambao nao kimsingi upo kwenye kundi la magonjwa yale ambayo siyo ya kuambukizwa.

Tunaweza kusema kuwa ugonjwa huu wa “kuchoka” ni ugonjwa sugu na umekuwa hatari kwa maisha ya binadamu kwa muda mrefu sana. Watu wengi hasa hapa kwetu Tanzania wanaugua sana ugonjwa huu.
 

Chanzo kikuu cha ugonjwa wa kuchoka ni watu wengi kufanya kazi ambazo hawazipendi. Watu wengi wanafanya kazi za ajira siyo kwasababu wanazipenda bali ni kwasababu ndiyo njia pekee ya wao kuweza kujihakikishia usalama wa chakula basi!

Unapofanya kazi ambayo huipendi, mara nyingi unajikuta kila unapoanza kufanya kazi unakuwa na wasiwasi na mawazo mengi nje ya kazi hiyo unayoifanya. Kwahiyo, wasiwasi na mawazo hasi ni visababishi vikubwa vya “kuchoka”.

Akiri inayoshangaa itakufanya kila wakati uchoke sawa na kukimbia umbali wa kilomita 15. Akiri ya binadamu ni sawa na betri yenye moto asilimia 100%. Unapoamka asubuhi au unapoanza siku yako, betri yako inakuwa imejaa moto au “charge” kwa asilimia 100%.

Unapofika ofisini na kukaa kwenye kiti, mara unatumia nguvu kuwazia jinsi rafiki yako alivyokusema vibaya juzi kwenye kikao, hapo unatumia asilimia 20%. Mara unawazia ujaenda kijijini kwenu siku nyingi na hujapeleka watoto kuwaona bibi na babu yao, lakini hapa unagundua kuwa huna pesa kwasababu, kazini kwako huwa hawalipi pesa ya likizo japo unastahili kulipwa, hapo unatumia asilimia 30%, mara unawaza kuwa binti wa kazi anavyomshindisha njaa mtoto wako, hapa asilimia 20% zinapungua; unawazia jinsi ulivyopata hasara kwenye mradi wako wa boda boda ambayo ulinunua kimya kimya kwasababua ofisini wakijua wataanza kukuzonga hapo asilimia 15% zinakweda.

Unapokuja kushituka kuanza kazi rasimi za ofisi, betri yako inakuwa imebakiwa na moto kidogo kama asilimia 15%. Kwa maana nyingine ni kwamba unafanya kazi kwa muda wa saa moja hadi mbili, moto unaisha na baadae kuzima kabisa—kuchoka!

Unaporudi nyumbani jioni unajisikia umechoka sana, wakati kiuhalisia hujafanya chochote cha maana. Mara nyingi hata watoto wako hutaki kabisa wakusemeshe, eti kwasababu una uchovu kwasababu ya kazi za ofisi. Lakini, cha kushangaza, ukifika tu nyumbani unawasha TV kwa kisingizio cha kutuliza uchovu ulionao.

Ebu niambie kwa maisha ya namna hii FURAHA itatoka wapi? Na kama furaha haipo nguvu ya kufanya kazi ili tupate pesa za kutosha itatoka wapi?

Mafanikio ya mtu yoyote yanatokana na kukamilisha yale uliyopanga na ulipaswa kuyafanya. Hakuna furaha utakayoipata maishani kwa kukumbuka jinsi ulivyoangalia runinga (TV) mwaka mmoja uliyopita, au jinsi ulivyoshindwa kwenda likizo na familia kwasababu ya kukosa nauli. Lakini, utapata furaha na amani sana moyoni utakavyoanza kukumbuka jinsi ulivyomaliza kujenga nyumba yako mwaka jana, utakumbuka jinsi ulivyo mwezesha hadi akapata mafanikio makubwa.

Ili kupata furaha na nguvu ya kufanya kazi—hatimaye pesa, lazima tuone kuwa athari za ugonjwa wa “kuchoka” dhidi ya uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla ni kubwa sana. Kwasasa, tunaweza kusema kuwa ugonjwa wa “kuchoka” ndio kisababishi namba moja cha umaskini na ufukara kwa watanzania waliowengi.

Kwahiyo, kama ugonjwa wa “kuchoka” ni hatari namna hii, tunadhani ugonjwa huu unahitaji tiba au dawa ya haraka. Habari njema ni kwamba, tiba yake imo ndani ya mtu mwenyewe (binafsi), kwasababu “kuchoka” ni ugonjwa wa kujitengenezea mwenyewe,

Ili tiba ya kuchoka ambayo imo ndani yako, iweze kukutibu ni lazima uwe tayari kujifunza mfumo mpya wa Maisha, lakini pia uwe tayari kutekeleza yale uliyojifunza kwa vitendo. Njia muhafaka na ya uhakika kuweza kujifunza jinsi ya kutibu ugonjwa wa “kuchoka” na kupata mfumo mpya wa maisha ambao ni wa kimafanikio zaidi ni kusoma vitabu.

Nashauri, usome hasa kitabu cha MEGALIVING! 30 DAYS TO A PERFECT— “The Ultimate Action Plan for Total Mastery of Your Mind, Body & Character” By Robin S. Sharma. Kama wewe unayesoma makala hii sasa hivi unataka kutibu ugonjwa wa “KUCHOKA” na kubadilisha mfumo wa Maisha yasiyokuwa na mafanikio, bonyeza maandishi haya: NITUMIE KITABU, ili kwa kuanzia uweze kujipatia nakala ya kitabu hicho hapo juu na vingine vingi kulingana na mahitaji yako.

No comments: