Monday, April 24, 2017

Kuchukia Makosa ni Kuchukia Masomo ni Kweli?



Siku zote watu wengi wanapojihisi kuwa wamefanya makosa, mara nyingi usikitika sana, ujawa na woga, wengine ukata tamaa ya kuendelea kufanya kile walichokuwa wakifanya. Lakini, ukweli ni kwamba
ukubwa au udogo wa makosa ni suala la mtazamo wa muhusika pamoja na wale wanaoguswa na jambo lililotokea.

Kimsingi, hakuna makosa duniani, isipokuwa kuna masomo ambayo yanakusaidia wewe kuweza kukua na kuwa mtu wa hali na hadhi ya juu katika Maisha. 

Ebu jaribu kukaa chini na utafakari yale unayofikiria ni makosa, alafu uondoe woga na kuanza kufikiria ni masomo gani unaweza kujifunza kutokana na makosa hayo. 

Na ujiulize ni kwanini yamekuwa yakikusononesha kila kukicha na hivyo kukufanya usiwe mwenye furaha. Wakati mwingine yameweza kukuharibia siku yako ya leo, ambayo ndiyo inayotengeneza kesho kuwa nzuri.

Kitu kinachoitwa makosa zaidi zaidi kinachochewa na ubinafsi—hali ya watu wengi kujipendelea zaidi kuliko watu wengine. Kutokana na ubinafsi huo, watu wengi wanaamini kwa dhati kwamba watu wanaoweza kufanya makosa ni wengine. Hapa unaona kwamba kila linapotokea tatizo au kosa watu wengi na hasa viongozi wanatafuta kila namna ilimradi makosa yaonekane yamefanywa na watu wengine.

Kwangu mimi naona kwamba, makosa ni ile tu hali ya kushindwa kufikia matarajio uliyokuwa nayo kabla ya kuchukua hatua. Katika kujaribu kufikia malengo na matarajio kuna vitu vingi sana ambavyo havipo katika udhibiti wetu na hivyo vyote usababisha lolote kuweza kutokea na hivyo kuwa kinyume na matarajio ya awali.

Ni kwa jinsi gani makosa utokea?
Unapopata wazo la kuwa au kupata kitu fulani, ni wazi kwamba unapata kuwa na matarajio ya kiwango fulani cha matokeo ndani ya fikra zako. 

Kwa maneno mengine, unakuwa na picha ya hali halisi itakavyokuwa machoni mwako na kwa watu wengine baada ya kuwa umekamilisha kazi ya kutengeneza hicho ulicholenga kupata.

Kwahiyo, tofauti kati ya matarajio yako na hali halisi baada ya kazi kukamilika ndiyo uzaa neno “Makosa” au “Mafanikio”. 

Pale matokeo ya kile ulichokifanya yanapokuwa kinyume na matarajio yako, ndiyo wengi ujiona wamekosea na mwisho jamii husika uyaita “makosa”. Kama matarajio yanalingana na matokeo au matokeo yanazidi matarajio, mara nyingi tunasema “umefanikiwa”.

Kwahiyo, ikitokea ukufikia malengo au hukupata matokeo uliyoyatarajia, kinachotakiwa siyo kusononeka wala kutafuta wa kumlaumu, bali ni kukaa chini na kujihoji mwenyewe juu sababu zilizopelekea wewe kushindwa kufikia matokeo tarajiwa.

Ukitumia utaratibu wa kujihoji kila mara unaposhindwa kitu chochote, ndipo unagundua kuwa hakuna kitu kinaitwa makosa, bali kuna masomo (ulichojifunza baada ya kushindwa). 

Nakuhakikishia, ukifuata njia hii, kamwe hutakaa uchukie makosa hata siku moja na, huwezi tena kushindwa kuwa na moyo wa kukubali makosa yaliyotokea chini ya uangalizi wako.

Kuna faida kubwa katika kukubali makosa. Faida ya kwanza ni kwamba unafungua akiri yako kupokea somo jipya lililotokana visababishi vya wewe kushindwa kupata motokeo tarajiwa. Pia, unapata fursa ya kujua ni njia ipi inaleta mafanikio na ni ipi ikifuatwa haileti mafanikio.

Kimsingi tunaweza kusema kuwa neno “makosa” ni la kawaida sana kama yalivyo mengine mfano: “mafanikio, juhudi, maarifa n.k. Tendo la makosa linaonekana la tofauti kutokana na mazingira tuliyolelewa. 

Tangu tukiwa wadogo tunafundishwa na kuhimizwa kutofanya makosa. Wazazi, walezi, walimu, viongozi n.k. wote wanatutaka kuepuka makosa— “matokeo yake uthubutu wetu katika kuchukua hatua mbalimbali umefifia kabisa hasa kadiri umri unavyoongezeka”.

Mara nyingi kila ulipofanya makosa ulipewa adhabu, faini kali iliyoambatana na viboko. Ukiwa shuleni, kitu kikubwa unachofundishwa ni kuogopa kufanya makosa—Ni marufuku kufanya makosa shuleni.

Kutokana na kukulia katika mazingira kama hayo, leo hii wewe unajiona ni mtu mzima lakini unaweza kukuta unao utu uzima wa kiwiliwili tu! Zaidi ya hapo umejaa woga wa kuchukua hatua mbalimbali za kuboresha maisha, kisa unaogopa kufanya makosa.

Anza leo kuyaona makosa kama masomo ya kujifunza, ili yakusaidie kupambana na changamoto zitakazojitokeza ukiwa kwenye safari yako ya kuelekea kwenye maisha ya ndoto yako na hasa kuwa na uhuru wa kipato.

No comments: