Monday, May 1, 2017

Leo ni Siku ya Wafanyakazi au Siku ya Wenyekazi Duniani


Kwa miaka mingi tumekuwa na utamaduni wa kupumzika na kusherekea eti! “sikukuu ya wafanyakazi” kila ifikapo tarehe moja mwezi Mei ya kila mwaka. Lengo au ajenda kuu ya siku hii ya leo, imekuwa ni kudai uboreshwaji wa maslahi ya watumishi (waajiriwa) kutoka kwa waajiri (wenyekazi).

Kusherekewa kwa siku hii ya “Mei Mosi” kunathibitisha mambo makuu mawili, ambayo ni
ama waajiriwa wanafurahia maisha ya ajira au hawafurahishwi kabisa. Ukichunguza aina ya ujumbe ambao umekuwa ukiwasilishwa siku kama ya leo “Mei Mosi” na zilizopita, unapata kuona kuwa waajiriwa wengi mpaka sasa hawajaweza kupata furaha tarajiwa kwenye maisha ya ajira.

Kukosekana kwa furaha ndani ya Maisha ya ajira, siyo tu kunatokana na maslahi duni, bali ni kutokana na ukweli kwamba, ni vigumu mwajiri husika, kuweza kumridhisha kila mtu kwa jinsi apendavyo, bila mwajiri kuwa ameingilia maslahi yake (yeye kama mwenye kazi).

Kitendo cha waajiri wengi kushindwa kuwaridhisha waajiriwa (watumishi) wao, ndilo chimbuko la sisi waajiriwa kufikia kuamua kuungana kwa lengo la kujenga uwezo wa kupambana na waajiri katika kudai maslahi ambayo tanadhani tukiyapata tutafurahi au tutaridhika. 

Mara nyingi tumekuwa hatupati hicho tunachokidai na hivyo tumejikuta tukiwa ndani ya migogoro na waajiri wetu. Matokeo yake muda mwingi wa kutumikia ajira zetu tumejikuta tukiishi kwa misuguano mingi na mwisho wa yote tumeendelea kuishi Maisha duni na yasiyokuwa ya furaha.

Kwanini madai ya maslahi ni ya kudumu?
Suala la kudai maslahi ni la kudumu kwasababu sisi ambao tumeajiriwa ni kama vifaa vya kufanyia kazi kwa mwenyekazi (waajiri). Katika muktadha wa ajira, sisi waajiriwa ni sawa na komputa, gari, mashine n.k. 

Tofauti ni kwamba sisi ndiyo njia muhafaka ya kuwezesha vitendea kazi vingine viweze kufanya kazi. Ikiwa wewe ni mojawapo wa vitendea kazi, basi ujue kuwa yawezekana mtazamo wa mwajiri wako juu yako ni kwamba wewe ni sehemu ya matumizi au gharama za uendeshaji.

Kwahiyo, linapokuja suala la kukuboreshea maslahi wakati mwingine, inaweza kusababisha faida isipatikane au ikapatikana kidogo sana. Uzuri wa mwajiriwa ni kwamba hata akibaniwa maslahi leo hafi, ataendelea kufanya kazi japo chini ya kiwango, lakini baadae mambo yakiboreshwa ataweza kufanya kazi kwa kiwango cha juu.

Tofauti ya binadamu na nyenzo nyingine kama gari ni kwamba, gari likiishiwa mafuta, lazima pesa itafutwe kokote; nje ya hapo hakuna kitakachoendelea. Kwahiyo, mwajiriwa hasishangae sana kuona kila mwaka hapewi pesa ya likizo, lakini pesa ya kufanya ya magari na komputa hazijawahi kukosa!!

Leo, unaposherekea siku hii ya “Mei Mosi” ni vizuri ukafahamu kuwa kuna tofauti kubwa kati ya kazi na ajira. Hapa tunaona kwamba KAZI ni kitu cha kudumu, lakini AJIRA yoyote duniani ni ya muda. Kazi huwezi kufukuzwa, lakini Ajira unafukuzwa. 

Kwenye Ajira unapangiwa cha kufanya, lakini Kazi wewe ndiye unayepanga utaratibu gani utumike kuifanya. Kwa kifupi KAZI ni pale unapofanya jitihada za kuipatia dunia kitu bora na kizuri (bidhaa au huduma) na AJIRA ni pale unapoamua kuidai dunia ikupatie kitu bora unachokipenda (bidhaa na huduma).

SOMA; AJIRA SIYO KAZI NI AJIRA NA KAZI SIYO AJIRA NI KAZI

Ukitafakari pamoja na mimi juu ya suala zima la kazi na ajira, unakuja kuona kwamba, siku ya leo tunasherekea sikukuu ya wafanyakazi (Mei Mosi) tukidhani sisi (waajiriwa) ni wafanyakazi. Ukweli ni kwamba tunasherekea sikukuu ambayo siyo yetu. "Naona kana kwamba, wenye sherehe ya leo ni wenye-kazi (waajiri) na sio wenye-ajira (waajiriwa)".

Kwa jinsi hali ilivyo ni kama waajiri ndio wana kazi na sisi wengine ni kama tumewekwa kwa malengo ya kusaidia kazi zikamilike. Ndiyo maana tunaitwa waajiriwa (watumishi). Kwa maneno mengine tunaweza kusema; “waajiriwa ni watumishi wa kazi za wengine”.
Kuajiriwa ni vibaya?
Kuajiriwa ni jambo zuri na jema, isipokuwa unahitaji kujihoji juu ya suala hili zima la AJIRA. Mpaka sasa wengine tuko kwenye ajira LAKINI kwa mtazamo chanya. Kwetu sisi ajira ni awamu ya pili ya shule ya Maisha. Kwahiyo, tuko kwenye ajira kwa lengo la kusoma na kujifunza mambo muhimu yatakayotusaidia kufikia ndoto zetu kwa haraka na kwa urahisi.

Kutokana na mtazamo huo, ndio maana tumeamua kutumikia ajira kwa nguvu zetu zote, ili kujijengea tabia nzuri ya uchapa kazi na nidhamu ya kufanya yale tunayotakiwa kufanya. Tunafahamu fika kuwa pindi tutakapomaliza shule hii ya awamu ya pili—Yaani AJIRA, na kuanza kufanyia kazi ndoto zetu, vitu vikubwa viwili ambavyo tutavihitaji ni “kufanya kazi kwa bidii na kuwa na nidhamu”.

SOMA; HABARI NJEMA KWA WANAOTAFUTA AJIRA

Siku ya Mei Mosi ya leo, iwe chachu ya kutuchochea kutambua kuwa, kama tulivyosoma kwa bidii shule ya awamu ya kwanza (msingi—mpaka chou kikuu), na shule ya awamu ya pili kupitia AJIRA, tunatakiwa nayo kuisoma kwa juhudi na maarifa.

Tujitahidi na kuhakikisha tunafahuru kwa kiwango cha juu sana licha ya matatizo na changamoto tunazokutana nazo. Matarajio ni kwamba kama tukifanya vizuri kwenye AJIRA lazima na kwenye kutekeleza ndoto zetu pia tutafanya vizuri na hakika itafika siku tuanza kuishi Maisha ya ndoto zetu—hasa uhuru wa kipato.
Kwanini ni Muhimu Kuichukulia AJIRA Kama Shule? Tunasema AJIRA ni kama shule/darasa awamu ya pili kutokana na ukweli kwamba, ikiwa umeingia kwenye ajira kwa malengo hayo ni wazi unapata fursa hadimu ya kujifunza kwa vitendo na kwa undani zaidi na pia unapata uzoefu juu ya hicho unachofanyia kazi.

Wale wote watakaoamua kuichukulia AJIRA kama shule au darasa, ni muhimu wakatabua kuwa lazima ufike wakati wamalize shule (ajira). Inasemekana kuwa muda mzuri wa kusoma na kumaliza shule (ajira) awamu ya pili ni kuanzia mwaka 1—10. 

Baada ya hapo, kwa wale wanaopenda uhuru, kipato kikubwa, heshima, kuwa karibu na familia yako, kusafiri n.k. wanatakiwa au wanatarajiwa kuanza maisha ambayo unatakiwa kutengeneza kazi.

Ukianza kutengeneza kazi zako ni sawa na kufungua shule awamu ya pili kwaajili ya wengine. Kwasababu, ukishatengeneza kazi, lazima uwaajili watu wengine kwaajili ya kukusaidia kazi zako ziweze kukamilika kwa haraka zaidi. Wale wote watakaokuwa wameajiriwa na kazi yako, watahesabika kuwa ni sehemu ya gharama za kuendesha kazi yako. 

Ukifikia kuwa mtu wa kiwango cha kutengeneza kazi basi, ujue kuwa wewe hutakuwa mtu wa kulipwa mshahara tena, badala yake utaanza kuwa mtu wa kupokea kile kinachobaki baada ya kuwa umelipa gharama zote za uzalishaji na uendeshaji. 

Kwakuwa wewe ndiye unayepanga na kudhibiti kila kitu ni wazi kwamba utapata namna ambayo ni rafiki kwa wewe kuweza kuhakikisha kinachobaki ni kikubwa kulingana na nguvu na rasilimali utakazokuwa umewekeza. Ndugu msomaji wa mtandao huu: http://maarifashop.blogspot.com jitahidi sana kuitumia siku ya Mei Mosi ya leo kuwa siku muhafaka kwako kuweza kuanza kutafakari na kujihoji wewe mwenyewe juu ya mustakabali wa maisha yako.

Lazima ujiulize, hicho unachokifanya ni KAZI au AJIRA? Kama jibu lako ni kazi basi endelea kuifanya kwa viwango vya juu sana. Kama jibu lako ni AJIRA basi, tumia siku ya leo kubadilisha kwanza fikra na mtazamo wako juu ya ajira na zaidi anza kuichukulia ajira yako kama shule/darasa awamu ya pili.

Ukibadili mtazamo wako leo, hakika ndani ya muda mfupi utendaji wako kazini utaongezeka, kero zitapungua, utapata amani zaidi. Pia, kwasababu utaanza kuitumia ajira kama shule basi ni wazi kwamba utaanza kuwa mbunifu zaidi kazini—vyote hivi na mengine mengi vitakuweka kwenye nafasi nzuri ya kuweza kupata masilahi mazuri zaidi— na hivyo kukufanya uweze kumaliza shule yako ya awamu ya pili mapema iwezekanavyo.

NAWATAKIA SIKUKUU NJEMA YA MEI MOSI. Kuendelea kupata maarifa makubwa jiunge na mtandao wa MAARIFA SHOP kwaajili ya kujifunza zaidi.

No comments: