Monday, August 14, 2017

Unajua Kwanini Kwanini Yako ni Muhimu?


"Kwanini yako" ndiye mlizi wako dhidi ya changamoto na wakatisha tamaa" ~ Cypridion Mushongi
Kwa mtazamo wa kimafanikio, kuweza kuuishi ukweli ni muhimu katika kufikia malengo yako hasa, uhuru wa kipatao/fedha. Jaribu kufikiria ulipokuwa bado mdogo, wakubwa zako walikuuliza unataka nini ukikua, pengine ulisema unataka kuwa mwanasayansi mashuhuri, mpishi, mwimbaji au daktari wa mifugo n.k. Na unaweza kukumbuka walionekanaje ulipowapa majibu hayo? Yawezekana walikukatisha tamaa kwamba haiwezekani au walikutia moyo kwa kukwambia kuwa unaweza ukawa mtu yeyote unayetaka kuwa, ilimradi
unasoma kwa bidii na kujituma sana wewe mwenyewe binafsi.

Lakini, sehemu fulani kwenye safari yako ya maisha, wengi huwa wanasahau kile walichowahi kukiwazia wakiwa wadogo. Wengine walipata taarifa kwamba ndoto zao zilikuwa haziwezekani kufikiwa. Ama walipata changamoto, walifanya makosa, au walipata ushauri mbaya na wenye kukatisha tamaa. Baadae walibadilisha gia na kwenda kwenye kitu ambacho pengine ni rahisi au ni kile kilichozoeleka zaidi kwa watu wengi. Na kutokana na mazingira ya namna hii, ndoto zao zilipotea kupitia dirishani au mlango wa nyuma.

Wakachukua kazi za kwenye meza/dawati ambazo mwanzoni walizichukia, wakijipa matumaini na ahadi kwamba itakuwa ni ya muda tu si ya kudumu. Alafu maisha yalianza kwenda. Kama yalivyo majukumu ya mtu mzima, huwa tunatekwa na majukumu mengi katika maisha yetu. Kwa mfano: mtu mzima unakuwa ni mlinzi, mtafutaji wa riziki, kiongozi wa familia, mchungaji, mpatanishi, muhudumu, mwalimu na orodha inaendelea haina mwisho. Katika mazingira ya namna hii, ni rahisi kupoteza mwelekeo kuhusu sisi ni kina nani na kushindwa kutambua ni nini hasa tunahitaji kwenye maisha yetu. Huwa tunafuata baadhi ya kanuni na njia ambazo ni rasimi na kushangaa kwanini hatufanikiwi. Kwanini kazi yangu kwa mwajiri hairidhishi? Kwanini sijafikia malengo yangu ya kipato? Kwanini bado niko kwenye hizi mbio za sakafuni?
 
Muda wa Kuwa Mkweli Juu Yako ni Sasa
Hauko peke yako. Utafiti unaonyesha kuwa karibu 60% ya watu wazima huwa wanatamani wangekuwa wamefuatilia ndoto zao za wakati wa ujana wao. Lakini, hakuna sheria wala kanuni inayosema kwamba ukishafanya uchaguzi au maamuzi kwamba ni lazima kung’a ng’ania chaguo lako—haipo! Unaweza kabisa ukayaelekeza maisha yako kwingine muda wowote kulingana na hali halisi, hulazimishwi kukaa hivyo ulivyo sasa.
 
Hatua ya kwanza: ni kuwa mkweli wa nafsi yako juu ya wewe ni nani. Hatua ya pili: ni kuheshimu na kupokea jinsi ulivyo. Lazima uishi kulingana na ukweli wa nafsi yako, vitu unavyoviamini, ndoto zako, maadili yako, kipaji chako, na kwa kila kitu kinachokufanya wewe kuwa wewe. Hatua ya tatu: lazima ueleze na ufafanue “kwanini yako”. Kama uko tayari kufanya mabadiliko, lazima yawepo kwa sababu za msingi na dhati, na kwa vitu vyote ambavyo ni vya maana na muhimu kwako. Kufikia ndoto zako, na hasa kama umepitia mzunguko mrefu kwa muongo (miaka 10) au miongo miwili (miaka 20) iliyopita, haitakuwa rahisi. Kiukweli safari yako ya mafanikio inaweza kuwa na maumivu na wakati mgumu katika kufikia malengo. Ndiyo maana “kwanini yako” lazima iwe inaeleweka fika bila chenga ndani ya akiri na fikra zako. 

Hatua ya nne: ni lazima hiyo “kwanini yako” huwe na uwezo wa kuihisi ndani ya moyo wako na rohoni mwako. Kwasababu, kitu kinachoitwa “kwanini yako” ni hisia ambazo utaziegemea na kuzitegemea wakati ule mambo yatakapokuwa magumu.

Kumbuka kuwa “kwanini yako” haiwezi kuwa tu pesa au faida, kwasababu kuna njia nyingi za kutengeneza pesa na faida, lakini ambazo siyo za furaha. “Kwanini” inatakiwa kuwa imara katika kuleta hamasa, na inatakiwa kuwa kitu fulani kinachokuhamasisha wewe kuendelea kujisukuma mbele mpaka kufikia ndoto yako.

"Kwanini yangu" uniongoza kwenda kwenye ndoto yangu
"Nilimaliza masomo yangu ya chuo kikuu cha Makerere (Uganda) mwaka 2000, nikiwa na shahada ya uchumi kilimo (agricultural economics). Katika kipindi hicho (2000) serikali ilikuwa bado imesitisha ajira mpya tangu miaka ya 90. Kwa maana nyingine nilimaliza chuo wakati ambapo kulikuwa na upungufu ajira serikalini (sekta binafsi ilikuwa ndo kwanza inazaliwa). Katika tafuta tafuta nikapata kuajiriwa kama kibarua katika Kituo cha Utafiti wa Kilimo Kanda ya Ziwa Ukiriguru (Mwanza) na baadae Maruku (Bukoba). Nikiwa kama kibarua mwenye shahada, nilikubali kulipwa mshahara wa kima cha chini. Mshahara wangu kama walivyokuwa vibarua wengine mfano walinzi, madereva, wahudumu wa ofisi n.k, ulikuwa mara nyingi unatokana na makusanyo ya ndani ya Kituo cha Utafiti (self-help fund)—chanzo ambacho hakikuwa cha uhakika sana, kwani wakati mwingine tulilazimika kusubili hadi miezi mitatu. Niliendelea na shughuli za utafiti kama kibarua kwa muda wa miaka minne. Mwaka 2004 mwishoni ndipo nilifanikiwa kupata ajira rasimi inayotambua taaluma na kiwango changu cha elimu. Hatahivyo, baada ya kupata ajira rasimi, hali ya uchumi haikubadilika sana, kiasi kwamba katika kipindi chote hicho, maisha hayakuwa rahisi".
Sasa, kama nisingekuwa na “kwanini yangu” kubwa na ambayo ni imara katika kipindi hicho cha maisha yangu hasa nikiwa kibarua, unadhani ningeweza kuhimili hali hiyo ngumu? Pengine isingewezekana. Ilikuwa inaogopesha na kutisha sana kuishiwa kila senti, lakini niliendelea kujikumbusha “kwanini yangu” tena na tena, nilipiga picha yangu juu ya kile ninachokitafuta na kujua ndani ya moyo wangu kuwa kufuatilia ndoto yangu, ili kuwa na thamani kuliko kujitoa sadaka kwa kipindi kifupi na makali, ugumu, changamoto amabazo nimekuwa nikizipitia. Nilifahamu kuwa kuishiwa pesa lilikuwa ni suala la muda tu! Lakini umaskini ilikuwa ni suala la milele. 
 
Nikiangalia safari yangu niliyoianza rasmi mwaka 2000 baada ya kutoka chuoni ninajifunza jambo moja kwamba “kuwa mkweli juu yako ni muhimu na ni lazima kama mtu unataka kutimiza ndoto zako”. Nguvu yako na shauku inayochochewa kila mara na “kwanini yako” itakupitisha salama kwenye mashimo ya changamoto, mashaka, vikwazo na vizuizi. Kuanzia leo tambua “kwanini yako” halisi, kisha ndoto yako halisi na ifanye kuwa kweli kwako—hakika utafanikiwa.

“Kwanini yako” haitaimarika hivi hivi bila kujiongezea maarifa kila mara. Endelea kujipatia maarifa yatakayokujengea kujiamini na kufanya maamuzi sahihi wakati ukiendelea na safari ya kuelekea kwenye ndoto yako. Ili kupata maarifa endelea kuwa karibu na MAARIFA SHOP inayofanya maarifa juu ya mafanikio yawe ni halali yako.

No comments: