Monday, August 28, 2017

Fursa Nyingi Tuko Maskini Kwanini?


Mapema leo 28/08/2017, nilikuwa naangalia na kusikiliza video juu ya kongamano la wadau wa zao la mpunga, lililofanyika kuanzia tarehe 14-18 mwezi septemba 2015. Mkutano huo ulihusisha zaidi wanasayansi na wataalam wa kilimo cha mpunga. 

Katika mkutano huo, mmoja wa washiriki ambaye ni Profesa Nuhu Hatibu aliwasilisha mada yake iliyojulikana kama “Biashara ya kikanda kwa mazao ya chakula kama nyenzo ya kuufanya utafiti utumike katika kutengeneza utajiri” au kwa lugha ya Kingereza; “Regional Trade in Food Staples as an Instrument for Getting Research into use for Wealth Creation”. Katika video hiyo Profesa Nuhu Hatibu, alitoa nasaa za maana sana na akaeleza
mengi juu ya FURSA nyingi zilizopo, hasa katika ukanda wa nchi za Afrika Mashariki. Baada ya kusikiliza nimepata kutafakari zaidi juu ya dhana nzima ya kitu kinachoitwa “FURSA”

Ni kweli tunazungukwa na fursa nyingi, licha ya kwamba watu wengi bado wanaishi maisha duni. Neno “fursa” limekuwa maarufu sana siku hizi, hasa kwa wale wanaojiita wajasiriamali. Pia kumekuwa na mahubili mengi juu ya umuhimu wa watu kuamka na kuchangamkia “fursa”, kama njia muhafaka ya kupambana na umaskini. Lakini, pamoja na mahubili yote hayo, mwamko wa watu kuchangamkia fursa bado ni mdogo na kiasi kikubwa, umaskini unazidi kuongezeka kila siku.

Ukweli ni kwamba kuwepo kwa “fursa” ni jambo moja na kutumia au kufaidi “fursa” ni jambo jingine. Ukiangalia idadi ya watu wanaotumia fursa zilizopo ni wachache sana. Na hapa tunajifunza kwamba fursa ikiachwa bila kuchukuliwa inalala au inapotea kabisa.

Kwanini hatutambui na hatuchangamkii fursa zilizopo?
Moja ya sababu za msingi ambazo zimetufanya wengi kushindwa kuchangamkia fursa ni pamoja na uelewa mdogo juu ya neno “fursa”. Ukichunguza kwa undani unagundua kwamba, kila linapotajwa neno “fursa” wengi hawapati picha kamili ya kile kinachozungumziwa. Kwahiyo, ndani ya akiri za wengi kuna picha ya fursa ambayo ni tofauti na maana halisi ya dhana yenyewe kama ilivyo. Kwa maneno mengine ni kwamba, dhana nzima ya neno “fursa” ni kitu kigeni.

Dhana ya “fursa” imeanza kufahamika baada ya nchi yetu kuanza kuingia kwenye mfumo wa uchumi wa soko. Sheria, kanuni na desturi za uchumi wa soko, zinamuhitaji kwa kiasi kikubwa kila mmoja kutumia pesa, ili kupata mahitaji aliyonayo. Huko nyuma mfumo wetu wa uchumi ulikuwa siyo lazima kuwa na pesa ili kupata mahitaji. Ukichunguza kwa kina unagundua kuwa neno “fursa” halikuwepo kwenye misamiati ya maneno ya lugha zetu za asili (lugha za makabila).

Wale tuliokwenda shule rasimi, hasa ngazi za juu, tumekutana na msamiati wa neno “FURSA” zaidi zaidi kwenye makongamano ya biashara na uwekezaji. Kwa jinsi hali ilivyo ni kwamba, jamii kwa ujumla haijaweza kupata nafasi muhimu ya kuweza kufahamu kwa undani dhana nzima ya “fursa” na hivyo kukosa uwezekano wa kufaidi neema nyingi zilizojificha ndani ya “fursa”.

Tunahitaji weredi na umahili wa dhana ya “fursa” kama kweli tunataka kuongoza mapambano dhidi ya umaskini. Katika kuongoza mapambano dhidi ya umaskini ni sharti kila mmoja wetu ambaye anadhani anachukia umaskini, kujitahidi kuwa mbobezi na mweredi wa kutambua au kubaini fursa. Lakini kumbuka kuwa haitoshi tu kuwa mweredi wa kuzitambua fursa bali inatakiwa kuwa mjasiri, imara na mahili wa kuchangamkia fursa zinazoendelea kujitokeza.

Jambo la pili; ambalo linasababisha wengi kushindwa kuchangamkia fursa zilizopo ni watu wengi kutokuwa na ndoto ya maisha mazuri akirini mwao. Yawezekana ukanikatalia kuwa hakuna asiyekuwa na ndoto ya maisha mazuri—sawa! Lakini, anza na wewe mwenyewe kwa kujiuliza swali endapo iliwahi kutokea siku moja au masaa ukakaa bila kufanya chochote ukitafakari maisha ambayo ungepeda kuishi hapo siku za mbeleni—jibu lako ni siri yako

Haya kama siku ni muda mrefu, je? Ilishawahi angalau kutenga masaa walau mawili ukiwa sehemu tulivu peke yako kujadiliana na akiri pamoja na roho yako juu ya maisha unayoyataka? Endapo hujawahi kufanya hivyo basi jua moja kwa moja na wewe ni mmojawapo wa wale “wasiokuwa na ndoto ya maisha mazuri vichwani mwao”.

Utafiti na uzoefu unaonyesha kuwa mpaka sasa kuna hali ya watu wengi kutokuwa na ndoto ya maisha mazuri vichwani mwao na hivyo kujiona dhaifu wa kupambana na umaskini walionao. Kukosekana kwa ndoto za maisha mazuri kunawafanya watu hao kukosa shauku, ari, nguvu, fikra za kutafiti mazingira yanayowazunguka n.k. Tabia ya kutokuwa wadadisi wa mazingira yanayotuzunguka, inatusababishia giza nene kiasi cha kushindwa kutambua fursa zilizopo.

Jambo la tatu; ni kutojua cha kufanya baada ya kubaini fursa. Pengine yawezekana watu wengi hawajui chakufanya mara tu wanapokuwa wamegundua fursa. Wengi wetu fursa nyingi tunazozitambua zinaishia tu mdomoni au kwenye fikra basi! Ukweli ni kwamba kwa jinsi “fursa” ilivyo peke yake haiwezi kutusaidia chochote. 

Niseme kuwa huwezi kufaidi fursa mpaka hapo utakapoweza kuunganisha rasirimali mbalimbali. “Fursa” ni kitu ambacho hakishikiki kwa mikono na hakionekani kwa macho ya kawaida, ndiyo maana hatuwezi kufaidi fursa kama ikibakia jinsi ilivyo.

Kinachotakiwa kufanyika tukishabaini au kutambua “fursa” ni kufanya utafiti kwanza, ili kupata uwezo wa kuchangamkia fursa hiyo. Ni muhimu kuchukua tahadhari wakati wa kufanya utafiti. Kamwe “Utafiti usifanyike kwa lengo la kubaini ugumu uliopo badala yake utafiti uwe ni kwaajili ya kubainisha upenyo wa wewe kupita kuelekea kukamata fursa husika”

Wakati mwingine, matokeo ya utafiti wa “fursa” yamekuwa ni kisababishi cha watu wengi kushindwa kuchukua hatua. Hii ni kutokana na ukweli kwamba tafiti nyingi juu ya “fursa” zimepelekea kugundua orodha ndefu ya vikwazo na changamoto—Yote haya yamekuwa yakiwakatisha watu wengi tamaa kiasi cha kushindwa kuchangamkia fursa zilizopo.

Changamoto zinazozunguka “FURSA” zimekuwa zikiwakatisha tamaa sana wajasiriamali na zimezidi kuwatia woga miaka nenda rudi. Lazima utafiti utumike katika kutuletea majibu ya tuwe watu wa namna gani; tuwe na nini ili kuweza kuifaidi fursa husika basi! Na siyo kutuorodheshea changamoto na vikwazo. 

Kwahiyo, utafiti na uchambuzi utusaidie kufahamu ukomo wa fursa husika, kwani kuna fursa zingine zinadumu kwa muda mfupi, na nyingine kwa muda mrefu. Pia, utafiti utusaidie kubaini na kupanga bajeti (rasirimali, pesa, nguvukazi n.k) ya vitu vyote vinavyohitajika, ili angalau kuweza kuanza safari ya kuikamata fursa iliyopo mbele yako.

Mwisho tunajifunza kwamba fursa ni “nafasi ya kufaidi” endapo utatimiza matakwa yote yanayohitajika. Kazi ipo kwenye kipengele cha kutimiza matakwa. Wengi wanatambua na kuvutiwa na fursa zilizopo, lakini inapofikia suala la kutimiza matakwa wanajitoa, wanaona ni bora wabaki kama walivyokuwa. Kwao, kutimiza matakwa ni usumbufu. Lakini, usumbufu ndiyo gharama kubwa kuliko pesa taslimu ambayo mtu anatakiwa hailipe, ili aweze kufaidika na FURSA iliyopo. Kuanzia sasa jiweke sawa na uwe tayari kulipa gharama zote zinazozunguka fursa nawe utaikamata fursa.

Jitahidi kuendelea kuongeza maarifa kila mara. Endelea kujipatia maarifa yatakayokujengea kujiamini na kufanya maamuzi sahihi wakati ukiendelea na safari ya kuelekea kwenye ndoto yako. Ili kupata maarifa endelea kuwa karibu na MAARIFA SHOP ili kuwa mjanja wa kukwepa umaskini.

No comments: