Monday, August 7, 2017

Sababu za Wateja Kuwa Zaidi ya Bosi ni Hizi Hapa


Katika maisha yetu ya kila siku, matendo yetu sikuzote yanadhihirisha na kuthibitisha kile tunachofikiri na kuwaza. Hii ndiyo kusema kwamba, kitu cha kwanza na muhimu kuwa na maisha bora yanayoambatana na uhuru wa kifedha ni jinsi tunavyofikiri na kutenda. Watu wengi wanafikiri mpaka watakapokuwa na mali nyingi ndipo watajiita au kujiona matajiri. Suala la kuwaza wengi wetu hatulipi kipaumbele, kiasi kwamba wengine wanadhani kukaa na kufikiri ni
kupoteza muda, wanaona bora wakatende tu basi. Lakini, siku zote matendo mema na yenye manufaa yanategemea sana fikra na mawazo mazuri. Tukiwaza vibaya tujue tutatenda vibaya. Kwa maana nyingine ni kwamba, kama kweli tunataka maisha mazuri, tunataka utajiri, tunataka uhuru wa kipato au tunataka familia imara, lazima tuhakikishe tunaboresha sana fikra na mawazo yetu.

Kuwa na fikra nzuri au mawazo mazuri kunalipa sana. Kwa mfano; watu wawili wanaweza wakawa na malengo yanayofanana, LAKINI katika kuwaza mmoja anaweza kuwaza na kuamua kutafuta ajira ambapo bosi (mwajiri) wake akaamua kuwa anamlipa mshahara wa shilingi 700,000/- kwa mwezi. Kwa mshahara wa shilingi laki saba kwa mwezi, mtu huyu atakuwa na uwezo wa kufikisha shilingi millioni 21 endapo ataiweka hiyo pesa bila kuigusa kwa kipindi kisichopungua miezi 30. 

Wakati mtu huyu wa kwanza alifikiri na akaamua kutafuta ajira, mwenzake yeye akifikiri na kuamua kushawishi shirika au taasisi kama ya umoja wa mataifa na wakakubali kumpatia zabuni ya kuwajaza T-shirt, hali itakuwa tofauti kabisa na yule aliyeajiriwa. 
Mfano: Endapo taasisi itampatia zabuni ya kutengeneza T-shirt kama 5000 hivi, kwa faida ya shilingi 4,000/- @ Tisheti, maana yake ataweza kutengeneza shilingi million 20 kwa mkupuo mmoja tu! (pengine ndani ya siku moja au wiki moja). Haya ndiyo maajabu ya kuwaza—mmoja anapata milioni 21 kwa miezi 30 (miaka 2.5) wakati mwenzake anapata karibu kiasi kile kile cha millioni 21 ndani ya wiki moja. Unaweza ukadhani hizi ni ndoto na ukahisi kama haiwezekani, lakini nakuhakikishia inawezekana sana.

Mtu huyo huyo anayeamini katika ajira, anaweza kubadilisha ajira ili kulipwa pesa nyingi zaidi. Kwahiyo, badala ya ajira ya awali ambayo ilimlipa shilingi laki 7 kwa mwezi, ajira mpya ikawa inamlipa shilingi milioni moja kwa mwezi. Sasa fikiria bosi mpya anamlipa shilingi millioni moja kwa mwezi na kama kwaida akaweka pesa yote bila kuitumia. Ndani ya muda wa mwaka mmoja au miezi 12, atakuwa umefikisha kiasi cha shillingi millioni 12. 

Sasa najiulize, endapo nina ndoto ya kupata shilling BILIONI MOJA, itanichukua miaka mingapi kuipata? Kwamfano wa huyu mtu anayepata mshahara wa shilingi millioni 12 kwa mwaka, itabidi mtu huyo atumikie ajira yake kwa muda wa miaka 84. Sasa kama inahitajika miaka 84 kupata bilioni moja, wewe sasa hivi una miaka mingapi?—Jibu lako ni siri yako!

Kumbe shilingi bilioni moja inawezekana tukiamua kufikiri tofauti. Kwa mfano, Tanzania ina jumla ya watu karibia milioni 48, kama tungeweza kusambaza unga wa nafaka kwa watu milioni 5 kwa mwezi kwa faida ya shilingi 50/- kwa kilo, tunahitaji miezi minne tu kupata bilioni moja. Kwa maana nyingine ni kwamba ukiweza kufanya kazi hiyo kwa muda wa miaka 3 hadi 5 tayari wewe unauaga umaskini na tabu zake zote.

Mahesabu hayo hapo juu yanatufundisha kitu kimoja muhimu kuwa, kama kweli tunataka tutajirike, lazima tuache kuhangaika na mabosi, kwasababu tukiendelea kuhangaika na bosi haitakaa itokee tutajirike. Kwahiyo, ni muhimu sana tuamue kuhangaika na wateja badala ya mabosi. Katika mifano yote niliyotoa hapo juu, ni wazi kwamba ukiamua kuhangaika na wateja unapata pesa nyingi na kwa kipindi mfupi.

Ili kuweza kujihusisha na wateja badala ya mabosi, unahitaji kujifunza kanuni za kuuza, uongozi, upendo, mahusiano, mawasiliano bila kusahau thamani na ubora wa bidhaa au huduma unayotoa kwa wateja wako. Hakikisha bei unayomtoza mteja ikiwezekana iwe chini kuliko thamani ya bidhaa au huduma. Ikiwa utaweza hilo, basi wateja (watu) watakuwa tayari kutoa pesa yao mfukoni kwa hiari. Kama mteja wako anatoa pesa kwa hiari, maana yake wewe uliye na bidhaa au huduma unastahili kulipwa na unatakiwa kujiamini kwamba pesa hiyo hata kama ni nyingi kiasi gani umeifanyia kazi.

Siku nzuri ya kuanza kuhangaika na wateja ni leo, kila mmoja mwenye kuchukia umaskini, ajikite kwenye kutafiti matatizo, kero, changamoto zinazowakabili watu wengi ndani ya kijiji, wilaya, mkoa, taifa na nje ya nchi. Ukishabaini hitaji hasa la watu, leta suruhisho likiwa kwenye sura ya bidhaa au huduma, utashangaa jinsi watu (wateja) watakavyoanza kuleta pesa kwako kwa wingi wa ajabu. 

Kwa jinsi hali ya maisha ilivyo sasa, naona na ninaamini kuwa njia sahihi na muhafaka ya kuweza kutimiza ndoto za maisha mazuri yenye furaha na uhuru wa kipato, ni kutumia muda wako mwingi kuhangaika na WATEJA na siyo MABOSI.

Kwa mafunzo Zaidi juu ya namna nzuri ya kuboresha fikra na mawazo yako weka e-mail yako kwa kubonyeza maneno haya: MAARIFA SHOP.

No comments: