Friday, January 26, 2018

Mali Hizi Tatu Tayari Unazimiliki Japo Hujui



 
Kama kuna kitu nakipenda kukifanya katika maisha ni pamoja na kujitahidi kila mara kurahisisha mambo yanayoonekana kuwa magumu kwenye jamii. Napenda kulifanya suala la kupata pesa kuwa rahisi, ndiyo maana nimeandika makala nyingi juu ya pesa, ikiwa ni pamoja na kuendesha semina za mafunzo. Lengo kuu limekuwa ni kusaidia watu wengi kufahamu na kuelewa mambo ya msingi juu ya pesa. Kitu ambacho huwa nasisitiza kila mara ninapoandika makala na kufundisha watu wengine, ni...
dhana nzima ya "mali" (assets) na "madeni" (liabilities).

Elimu na uelewa wako juu ya masuala ya kupata uhuru wa kipato na kutajirika, itategemea sana ufahamu wa dhana hizi mbili yaani “mali” na “madeni”. Kwa kujikumbusha tu ni kwamba “mali” ni kitu chochote kinachoongezeka thamani kadiri muda unavyozidi kwenda na ni kitu kinachokuwekea pesa mfukoni mwako. Kwa upande mwingine, madeni ni kitu kinachoshuka thamani kila kukicha, na kinahamisha au kutoa pesa mfukoni mwako.

Katika ulimwengu wa pesa, huwa tunaongelea “mali” na “madeni” katika muktadha wa pesa tu! Kwahiyo, “mali” ni uwekezaji ambao ukupa faida kubwa na uendelea kuongezeka thamani na mfano wake ni kama hisa na majumba ya kupangisha. Madeni kwa upande mwingine ni vitu ambavyo mara nyingi unavinunua kutumia: mfano ni kama vile; gari, radio, runinga, samani za ndani, nyumba yako ya kuishi n.k.

Licha ya kwamba suala la mali na madeni linatawala katika ulimwengu wa pesa, lazima tufahamu kuwa mali na madeni ni vitu vinavyopatikana nje ya ulimwengu wa pesa. Ni muhimu tukafahamu kuwa kuna “mali” ambazo tayari tunamiliki na zina thamani kubwa sawa na pesa ambayo huwa unaipata au kuiwekeza. 

Kutokana kutotambua thamani ya mali zilizopo tayari, watu wengi mara tu wanapopanga safari yao ya kutafuta pesa, wanataka mara moja waende kununua mali zenye kuletea pesa taslimu na kwaharaka. Lakini, muda mfupi tangu kuanza safari ya mafanikio, ujikuta kwenye matatizo makubwa na kama kawaida uanza kulalamika. “sijui jinsi ya kutafuta mali”; “niwekeze kwenye mali gani?” “Siwezi kumudu kuwekeza kwenye mali”; “ni wapi naweza kuanzia?” Ninaanzia wapi?”. Kimsingi kitu ambacho huwa hatutambui ni kwamba inabidi uwekeze katika wewe, ili uweze kuendeleza “mali” ambazo tayari unamiliki kabla ya kuanza kuwekeza pesa zako kwingine.

Kwa taarifa yako ni kwamba tayari hapo ulipo una mali tatu unazomiliki na ambazo unatakiwa kuwekeza sana katika hizo kama unavyowekeza kwenye mali au vitegauchumi vingine. Mali hizo zinaweza kuongezaka thamani na kukuletea manufaa makubwa baadae. Kinachohitajika ni utambuzi wako pamoja kuzijali kwako.

Mahusiano: Mara nyingi kuna watu ujisikia vibaya, pale unapoanza kuzungumzia mahusiano na watu kuwa ni “mali”. Kwa maneno mengine hawataki kuona mahusiano yao kama kitu muhimu ambacho wanaweza kukitumia kwaajili ya manufaa yao binafsi. Kama na wewe unayesoma makala hii upo kundi hilo, ni vizuri ukatambua kuwa hiyo siyo namna nzuri ya kufikiri. Ukweli ni kwamba, mahusiano ni “mali” yenye thamani kubwa. Dunia nzima inaendeshwa kwa kutegemea sana mahusiano. Ndiyo maana kuwa na mahusiano ambayo yanakusaidia na kukuwezesha kukua ni muhimu katika kufanikisha safari yako kuelekea kupata uhuru wa pesa au kipato.

Kumbuka kuwa tunaposema suala la kuchukulia mahusiano yako kama “mali”, haina maana kwamba uwaone watu kama chombo, au kujenga tu urafiki na watu kwa malengo ya namna gani watakusaidia. Bali ina maana kwamba unatakiwa kuchunguza mahusiano uliyonayo kwasasa, na kuona ni namna gani unaweza kuwekeza zaidi katika mahusiano hayo yaliyopo, ili kuyafanya yawe na thamani zaidi mara kwa mara. Mahusiano na familia, marafiki, makocha, washirika wako katika biashara, wakuu wako kazini, wafanyakazi wenzako; yanaweza kukupeleka sehemu nzuri ambayo hukuwahi kufikiria kufika. Chukua muda wako kuwekeza katika “mali” hii ya mahusiano na utapata malipo yasiyo na kikomo.

Utambulisho: utambulisho wako ni mali ya thamani na ni lazima kuulinda. Katika kizazi hiki kinachoitwa “dotikom” au cha kidigitari, utambulisho wako unaundwa na taarifa ambazo unazitengeneza kila siku. Inahusisha takwimu zote zinazotoka kwenye simu yako, kamera, taasisi za fedha, na taarifa za kijamii, taarifa za matibabu, usafiri, na hata za kisheria. Maisha yetu yote, huwa tunatumia kila dakika ya kila siku, kuongeza na kujenga utambulisho wetu na hilo utusaidia kuomba ajira, kununua nyumba, kufungua akaunti benki, kusafiri nje ya nchi n.k.

Kwa bahati mbaya, wengi huwa hatutambui thamani iliyopo katika utambulisho wetu kuwa ni “mali” mpaka pale utambulisho wetu unapoibiwa. Mfano; maharamia wa kwenye mtandao wakipata taarifa zako wanaweza kuziiba na kuzitumia kwa faida yao binafsi. Taarifa zako zikishaibiwa, maana yake ni kwamba, utambulisho wako au mali ambayo uliichukulia kwa mzaa, inaanza kukuzuia kuishi maisha yako. Unaweza kutaka kuchukua mkopo mahala na ukakuta tayari mtu mwingine alishachukua mkopo jina lako, wengine wanaweza kuanza kutibiwa kwa kutumia taarifa zako na ukaona deni la matibabu linazidi kupanda.

Katika maisha yetu ya kila siku, huwa tunafanya kazi kwa bidii kutengeneza utambulisho wetu ambao unakuja kuwa mali baadae. Utakuta tunajitahidi kujenga jina kwa watoa mikopo, tunalipa madeni yetu kwa wakati n.k. Kwa kufanya hivyo kwenye “mali” hii, tunaweza kuongeza thamani yetu na kusonga mbele katika safari yetu ya kuelekea kwenye "uhuru wa kipato" na "utajiri".

Bila utambulisho mzuri, kuna wakati tunazuiliwa kufanikisha vitu vingi muhimu maishani. Ndiyo, maana unatakiwa kulinda utambulisho wako kwa namna yoyote ile. Kwahiyo, lazima kuwekeza kwenye mali hii ya utambulisho ili hatimaye utambulisho wako uzidi kuongezeka thamani na kukuletea manufaa zaidi.
 
Akiri yako: Katika kitabu chake cha “Rich Dad Poor Dad”, bwana Robert Kiyosaki alipata kuandika kuwa, akiri yako ni “mali” yenye thamani kubwa sana. Kwenye kitabu chake hicho bwana Robert anaendelea kutuasa juu ya umuhimu wa kuwa waangalifu kwa kile tunacholisha akiri zetu. Ukweli ni kwamba, akiri yako ni “mali” pekee duniani ambayo haitakaa ishuke thamani.

Akiri yako ina manufaa na mapato yasiyo na kikomo, kwasababu ni rahisi kuboresha akiri yako kama ukiamua. Unaweza kujifunza kila mara na ukakua na kubadili mawazo na fikra ambalo ni jambo zuri! Ukweli ni kwamba hakuna ukomo wa ukuaji wa akiri yako. Ndiyo maana katika mtandao wa MAARIFASHOP tunachukulia suala zima la kuongeza maarifa na elimu kuwa kipaumbele cha kwanza na hatua muhimu katika kufanikisha safari yako ya kuelekea kwenye uhuru wa kipato.

Kuwekeza kwenye mali hii ya “akiri yako”; maana yake ni kwamba unaongeza elimu, unajifunza vitu vipya, kujaribu kupata uzoefu wa vitu vipya, na kutumia muda wako kukuza uelewa wako. Uzuri ni kwamba katika siku ya leo na umri huu, kuwekeza kwenye akiri yako ni mojawapo ya mali chache ambazo hazikugharimu sana. Kwa kutumia aina mbalimbali za kozi za mtandaoni, na mafunzo ya bure, unaweza kabisa kuwekeza kwenye akiri yako kila siku unayotaka na ukaweza kufaidika.

Ndugu msomaji wa MAARIFASHOP na mpenda mafanikio, lazima uanzishe utaratibu wa kuwekeza katika wewe kwanza kabla ya kuanza kuwekeza kwenye kitu chochote kile. Hili ni somo ambalo mpaka sasa ni watu wachache wameweza kulielewa ipasavyo. Watu wanapojifunza juu ya “mali” na “madeni”, wanataka kurukia kwenye biashara ya majumba au kuanza kununua hisa, mazao n.k huku wakitelekeza mali za thamani ambazo tayari wanamiliki.

Mali tatu, ambazo tayari nimeeleza hapo juu, zinajenga msingi imara kwako wewe, na utakuwezesha na kukuruhusu kufanikiwa pale utakapoanza kuwekeza kwenye mali au vitegauchumi vyenye kukuingizia kipato moja kwa moja. Chukua muda wako kuwekeza katika mali hizo tatu kwa bidii na maarifa na uone jinsi safari yako ya kwenda kwenye uhuru wa kipato itakavyokuwa rahisi sana.

Unahitaji kuchukua hatua sasa bila kusubili, maana tayari ni asubuhi. Endelea kutumia wa MAARIFA SHOP kujenga na kukuza thamani ya akiri yako, utambulisho wako na mahusiano yako. Weka e-mail yako kwa bonyeza neno “wa “NIUNGE, ili kuwa karibu na maarifa na elimu ambavyo ni kila kitu kwa mafanikio yako.

No comments: