Saturday, December 30, 2017

Unaposikia Uwekezaji Katika Hisa Unapata Picha Gani?



“Mtu anayeuza hisa ni sawa na mtu anayeuza kuku wakati anapenda mayai” ~ Cypridion Mushongi
Neno "hisa" limekuwa maarufu sana miongoni mwa watanzania. Umaarufu wa neno hili umekua kutokana na kuenea kwa taasisi za VICOBA na SACCOS maeneo yote nchini yaani mijini na vijijini. Pamoja na watu wengi kuanza kushiriki zoezi la kununua na kumiliki hisa katika hatua mbalimbali, bado wengi wanakiri kuwa uelewa wao juu ya..
dhana nzima ya uwekezaji katika “hisa” bado uko chini. Siku ya tarehe 28/12/2017 niliulizwa maswali mengi juu ya “hisa” mara tu baada ya kuaga wenzangu kwenda kwenye mkutano wa nne wa mwaka kwa wanahisa wa kampuni ya Bukoba Investment Group (BIG) — http://big-ltd.com.


Katika kubadilishana mawazo, niligundua kuwa watu wengi wameanza sasa kupata shauku ya kuwekeza kwenye hisa, lakini inaonyesha wazi kwamba wanakosa fursa ya elimu na maarifa juu ya “UWEKEZAJI WA HISA”. Kwakuwa siku hiyo nilikuwa nawahi kwenda kwenye mkutano huo wa BIG, nimeona niandike makala juu ya HISA, kwa lengo la kukuza uelewa wa wale wote ambao ni wasomaji wa MAARIFA SHOP, na wale wenye nia ya kutengeneza kipato kupitia uwekezaji katika hisa.

Kwahiyo hisa ni nini hasa?



Naweza kusema kuwa hisa ni umiliki wa pamoja wa kampuni, vicoba, saccos, au biashara. Kwa maneno mengine, hisa ni uwekezaji na utaratibu wa pamoja katika kuongeza au kukuza mtaji wa kampuni au biashara. Unapo nunua hisa, maana yake umechangia katika mtaji wa kampuni husika. Ndiyo maana kampuni ikipata faida kutokana na biashara iliyofanyika, wewe mwenye hisa unapata gawio kama sehemu ya faida kulingana na hisa ulizonazo. Vilevile, kama ilivyo biashara nyingine, kampuni ikipata hasara na wewe unapata hasara na hakutakuwa na faida ya kugawana. Ukiwekeza kwenye hisa unapata fursa ya kuwa sehemu ya wamiliki wa kampuni au biashara husika.

Kwa mfano; chukulia kuwa unataka kuanzisha biashara au mradi kwa mtaji wa shilingi 1,000,000, lakini wewe unazo shilingi 200,000 tu; unaweza ukatafuta watu wanne na kila mmoja akachangia shilingi 200,000 na mwisho wake mkapata jumla ya shilingi milioni moja (1,000,000/-) kama mtaji wa kuanza kufanya biashara. Kama biashara yenu hiyo mlioianzisha itazaa faida, basi kila aliyechangia mtaji atapata sehemu ya faida hiyo. Endapo mambo hayakwenda vizuri biashara ikaleta hasara, basi hiyo inakuwa hasara kwa wote.

Ukinunua hisa kwenye kampuni, basi ujue kuwa umechangia katika mtaji kwaajili ya uendeshaji wa biashara ya kampuni hiyo. Kwahiyo, kuanzia hapo unaanza kuhesabika kuwa ni miongoni mwa wamiliki wa kampuni hiyo. Nguvu na umuhimu wako katika kampuni hiyo utatokana na kiasi cha hisa unazomiliki. Kwa mfano; kama kampuni ina mtaji wa shilingi laki sita na wewe ukanunua hisa za shilingi laki tatu, inamaana kwamba unamiliki asilimia 50% ya mtaji wa kampuni. Kwakuwa unamiliki kiasi kikubwa cha hisa, maana yake unakuwa na nguvu na vigezo vya kushiriki kwenye vikao nyeti vya maamuzi juu ya uendeshaji wa kampuni au biashara husika.

Kuna uzuri gani ukimiliki hisa?
Faida bila kikomo: Uwekezaji katika hisa ni kitu kizuri sana kwasababu, unatengeneza faida bila kikomo ambayo pia huitajiki kufanya kazi au kuwepo. Maana yake ni kwamba ukishawekeza kwenye hisa, kampuni husika inafanya kazi kwaniaba yako na wewe unakuja kupata gawiwo la faida. Kutegemeana na kampuni, faida inaweza kugawiwa kila baada ya miezi mitatu, sita au mwaka.   
Kutenganisha biashara na maisha yako binafsi: Biashara ya hisa inakupa fursa ya kutenganisha biashara na maisha yako ya kila siku. Maana yake ni kwamba unapopata matatizo kama wewe binafsi siyo rahisi kuingilia au kugusa biashara ya kampuni ambayo unamiliki hisa. Kwa mfano ikitokea mwanahisa amesafiri, anaumwa au amefariki, shughuli za kampuni haziwezi kukwama, kwasababu jukumu la kufanya kazi za kila siku lipo mikononi mwa menejimenti na watumishi wa kampuni husika na siyo wewe kama wewe.

Dhamana ya mkopo benki: Hisa zinaweza kutumika kama dhamana kwaajili ya kupata mkopo wa benki. Badala ya mtu kutumia nyumba yake au kiwanja chake kama dhamana, hisa za kampuni inayotambulika kisheria, zinaweza kutumika kama dhamana ya mkopo.

Fursa ya pesa kukufanyia kazi: Umiliki wa hisa unakupa fursa hadimu ya pesa yako kukufanyia kazi huku wewe ukipata muda wa kuendelea kufanya mambo yako mengine. Kimsingi, wengi tunaifanyia kazi pesa na wakati mwingine tunatumia muda wetu mwingi katika kuitumikia pesa badala ya pesa kututumikia.

Kupunguza kasi ya pesa kukuhama: Ununuzi wa hisa unasaidia kutuliza pesa yako na hivyo kusaidia pesa yako isikuache haraka. Watu wengi tuna changamoto ya kushindwa kuzuia pesa kuhama kutoka mifukoni kwenda kwa watu wengine, hasa pale tunapopata pesa inayozidi mahitaji yetu ya lazima. Njia inayotumiwa na wengi ni ile ya kuweka akiba benki, SACCOS, VICOBA n.k. lakini kadiri hamu na shauku ya kutaka kufanya kila kitu inavyozidi kuongezeka ndivyo tunavyo kimbilia kwenye ATM na kutoa pesa ile ambayo wiki moja iliyopita tuliitenga kama akiba. Kwahiyo, ununuzi wa hisa ni sehemu ya uhakika ya kuweka pesa ambazo huwezi kuzitoa haraka. Unapowekeza kwenye hisa, siyo rahisi kupata pesa zako kama unavyoenda kutoa kwenye ATM, kwasababu ukitaka kupata pesa yako, inabidi kwanza ujaze fomu maalum kwaajili ya kuuza hisa na inabidi usubiri mteja ajitokeze ili zinunuliwe.

Njia ya kukuza mtaji: Umiliki wa hisa unasaidia kama njia mojawapo ya kukuza mtaji. Ni rahisi kujenga na kukuza mtaji kupitia hisa kwasababu unawekeza pesa kidogokidogo kila mwezi kwa muda mrefu. Mtaji wako unaweza kukua kutokana na ongezeko la thamani ya hisa na pia kupitia gawiwo la faida inayotengenezwa na kampuni mwisho wa mwaka. Mfano; ukiangalia takwimu za bei ya hisa za benki ya NMB kwa kipindi cha miaka minne utaona kuwa tarehe moja ya mwezi Januari 2013, bei ya hisa moja, ilikuwa ni shilingi 1,120/- na kufika tarehe moja mwezi Januari 2017, bei ya hisa moja iliongezeka hadi kufikia shilingi 2,750/-. Kwahiyo, kama mtu angekuwa ametumia akiba yake kununua hisa za shilingi 500,000/- mwaka 2013 angepata hisa 446, ambazo baada ya miaka minne mtaji wake ungekua hadi kufikia shilingi 1,226,500/-

Je? Hisa zinapatikanaje?
Hisa zinapatikana kwenye soko la hisa, ambalo hapa Tanzania linajulikana kama soko la hisa la Dar-Es-Salaam au Dar-Es-Salaam Stock Exchange Market (DSE). Soko la hisa ni mfumo wa kibiashara ambapo wawekezaji na wafanyabiashara, ununua hisa za makampuni mbalimbali kama njia ya kuwekeza pesa zao kwenye mtaji kwa lengo la kupata faida hapo baadae. Hapa Tanzania yako makampuni zaidi ya 20, ambayo yameorodheshwa au kuandikishwa kwenye soko la DSE. Hisa katika soko la DSE zinauzwa kupitia kwa kwa madalali (brokers), mfano ni “orbit securities” na wengine wengi. Kwa uelewa zaidi wa jinsi ya kununua na kuuza hisa za makampuni, tembelea tovuti ya DSE; http://www.dse.co.tz

Ni kwa jinsi gani hisa utengeneza faida?
Faida kwenye hisa inapatikana kwa njia mbili, moja ni kwa njia ya kuongezeka kwa thamani ya hisa. Kwahiyo, unapowekeza kwenye hisa kwa mpango wa muda mrefu, unanufaika kutokana na ongezeko la thamani ya hisa ulizonunua. Kwa mfano; kama ulinunua hisa 100 kwa bei ya shilingi 400 kila moja na baada ya miaka miwili bei ya hisa ikawa imepanda kufikia shilingi 850, maana yake ni kwamba kadiri bei ya hisa inavyozidi kuongezeka, ndivyo pesa zako zinavyozidi kuongezeka. Na hii ndiyo uiwezesha pesa yako kuongezeka maradufu kwa muda wote ambao mtu anakuwa anamiliki idadi ya hisa husika.

Njia ya pili juu ya upatikanaji wa faida ya hisa ni pale unapopata gawio kutoka kwenye biashara ya kampuni husika. Baadhi ya makampuni huwa yanatoa gawio kila mwisho wa mwaka wa fedha wa kampuni husika na gawio hilo hugawanywa kwa kila hisa.

Kwa mfano unakuta labda kampuni inatangaza gawio la shilingi 100 kwa kila hisa. Ina maana kama una hisa 1,000/-; maana yake unapata gawio la shilingi 100,000/-. Lakini hisa zako bado zipo pale pale, kwasababu, hapa unagawiwa faida tu na hisa zako (mtaji) zinabaki. Ukiamua unaweza kutumia pesa ya gawio kununua tena hisa zingine na hivyo kuongeza idadi ya hisa unazomiliki. Kumbuka kuwa njia hii ya kupata gawio ndiyo nzuri kwasababu unalipwa faida na mtaji wako unabaki kukutengenezea faida kwa awamu nyingine.


Faida itokanayo na hisa inagawiwaje? Katika kugawa faida iliyopatikana kwa wanahisa, kampuni husika itachukua faida iliyopatikana
baada ya kulipa madeni na kodi zote zinazodaiwa na kugawanya kwa idadi ya hisa zilizopo ili kupata faida kwa kila hisa.Baada ya hapo ndipo kila mtu anapata kujua faida aliyopata kwa kumiliki hisa katika kampuni husika. Mwanahisa ataweza kujua faida aliyoipata kwa kuchukua idadi ya hisa anazomiliki na kuzidisha na kiasi cha faida kwa kila hisa, iliyotangazwa na kampuni kupitia mkutano mkuu wa wanahisa.

Biashara ya hisa ina hasara gani?
Kama ilivyo biashara nyingine, biashara ya hisa nayo ina hasara wakati mwingine na hii inatokana na ukweli kwamba, hisa siyo kitu chenye faida tu wakati wote, zipo hasara na hatari pia. Hapa nakutajia chache tu kati ya nyingi;
  • Kukosa udhibiti wa pesa yako: Ukishanunua hisa, huna tena udhibiti wa moja kwa moja wa pesa zako, kwasababu wanaoendesha na kuongoza biashara ya kampuni ni watu wengine. Kama kampuni inaendeshwa na watu wengine, maana yake wakifanya makosa yanakuathiri na kukugharimu moja kwa moja na hukuna namna ya wewe kudhibiti hilo.
  • Kampuni kufirisika: Kampuni ikifirisika na wewe unapoteza kabisa kile ulichowekeza, na pia kampuni ikipata hasara na wewe unapata hasara.
  • Hali ya uchumi wa nchi: Kushuka kwa uchumi wa nchi ikiwemo mfumuko wa bei, vinaweza kuathiri thamani ya hisa, ambapo badala ya kupanda bei zinaweza kushuka bei.
 Uzoefu umeonyesha kuwa ukiwekeza kwa muda mfupi kwa matarajio ya faida ya haraka, unapata hasara. Lakini ukiwekeza kwa muda mrefu, kuanzia miaka mitano hadi kumi na kuendelea, utaona ongezeko la thamani ya hisa zako. Kwahiyo, ili kupunguza hatari ya kupata hasara kwenye soko la hisa, unashauliwa kuwekeza kwa muda mrefu.

Mwaka 2017 unakwisha ndani ya masaa 30 yajayo. Nimekuletea makala hii ili iwe chachu na chanzo chako cha kukuza uelewa wako juu ya fursa ya uwekezaji katika hisa. Unatakiwa kutumia muda huu uliobaki kwa mwaka huu kutafakari ili hatimaye ufanye maamuzi magumu ikiwa ni pamoja na kuanza uwekezaji mara moja ifikapo Januari mwaka mpya wa 2018.

Mtandao wa MAARIFA SHOP, unakujali na utaendelea kukupa elimu na maarifa mbalimbali juu ya uwekezaji, biashara, afya, pesa, mahusiano, uongozi, maisha ya familia n.k; kwa viwango ambavyo vitakuwezesha wewe kuchukua hatua na kuwa mtu wa tofauti kimafanikio. 

Niseme nakutakia HERI YA MWAKA MPYA WA 2018 na uzidi kutumia mtandao wa http://maarifashop.blogspot.com kama kitovu na chanzo kikuu cha elimu na maarifa kwa mafanikio yako.

No comments: