Friday, February 23, 2018

Thamani ya Maisha Kabla ya Kifungua kinywa ni Ipi?


“Fikra ni viumbe hai” ~ Swami Sivananda
Siku zote, maisha ni kile ufanyacho kuanzia pale unapoamka kitandani asubuhi hadi pale unapokwenda kulala au unapomaliza siku yako. Kwa maneno mengine ni kwamba, kila unapoamka mapema asubuhi, maana yake umeanza maisha upya. Wengi wetu hatujaweza kutambua thamani kubwa iliyopo katika masaa haya ya kuanzia tunapoamka kitandani hadi pale tunapopata kifunguakinywa. Ukweli ni kwamba, masaa ya kabla ya kifunguakinywa ni
maisha ya thamani sana, ambayo tukijenga nidhamu ya kuyatumia kikamilifu, kwa hakika tutaweza kupiga hatua kubwa sana kimaendeleo.

Maisha kabla ya kifunguakinywa ni maisha ya kuanzia saa kumi alfajiri hadi saa moja asubuhi—ni kama masaa matatu hivi. Kimsingi masaa haya ya asubuhi yakitumiwa vizuri kila siku, yanatosha kuleta mabadiliko makubwa kimaisha. Ninaposema wewe kuishi maisha kabla ya kifunguakinywa namaanisha kwamba, kila ikifika saa kumi au kumi na moja alfajiri, tayari umeamka—yaani tayari umeanza kuishi. Maisha haya ya kabla ya kifunguakinywa yanasaidia sana katika kuiaza siku yako kwa hamasa kubwa.

Ukiwa na hamasa kubwa maana yake utafanya kazi kwa bidii na utakuwa mwenye furaha siku nzima. Matokeo ya kufanya kazi kwa hamasa na furaha ni pamoja na kuongezeka kwa uzalishaji wa kile unachokifanya kila siku. Kwahiyo, yawezekana usiweze kuamka mapema, lakini lengo la maisha kabla ya kifunguakinywa ni pamoja na kuweza kupata nafasi na fursa ya kuiandaa siku yako kimwili, kifikra na kiroho; vyote hivi, lazima viwekwe sawa kila siku kabla hujaanza kazi rasimi za siku yako.

Utafiti uliofanyika unaonyesha kuwa wengi wetu tumekosa fursa ya kufaidi maisha kabla ya kifunguakinywa kwasababu ya kukosa uelewa juu ya uwepo wa maisha hayo. Matokeo yake ni kwamba, wengi tumejikuta tukiyapoteza. Hali hii ya kupoteza masaa haya adimu, imekuwa ikisababisha kushuka kwa utendaji kazi wa siku nzima. Kwa kiasi kikubwa wengi tunatumia masaa ya kabla ya kifunguakinywa kuchapa usingizi. Ndiyo maana ni kawaida kusikia watu wengi wakisifia kuwa usingizi wa asubuhi ni mtamu sana, ingawaje thamani ya masaa hayo yakitumika vizuri ni kubwa sana kuliko utamu wa usingizi huo wa asubuhi.

Uzuri wa maisha ya kabla ya kifunguakinywa ni kwamba ni maisha ambayo unayadhibiti kwa asilimia karibu 90%. Kwa waajiriwa haya ni masaa ambayo hayajauzwa kwa mtu yeyote, hata bosi wako. Ni masaa ambayo unapata fursa ya kufikiri na kutenda kutokea ndani yako wewe kama wewe na hivyo kukuwezesha kufanyakazi kwa uhalisia zaidi. Maisha kabla ya kifunguakinywa ni tofauti na baada ya…kwasababu, baada ya kifunguakinywa walio wengi ufikiri na kutenda kwa kufuata ushawishi wa kutoka nje ya nafsi yake.

 
Nifanye nini ili kuishi na kufaidi maisha kabla ya kifunguakinywa?
Ili kuweza kufaidi maisha kabla ya kifunguakinywa ni muhimu sana ukafanya vitu vikuu vitatu muhimu: 

Kitu cha Kwanza: Muda wa utulivu wa akili na upya wa nafsi
Hiki ni kitu cha kwanza unachotakiwa kukifanya kabla ya kufanya kitu chochote, mara tu unapoamka kitandani. Usiamke tu na kuanza kufanya kazi, hilo ni kosa kubwa kiakili na kimwili. Mwili na akili, ni sawa na gari. Siku zote tunaambiwa kwamba tukiwasha gari tusianze kuondoka hapo hapo, badala yake tuliache lingurume kwa muda Fulani walau kwa dakika tano—wanasema kwakufanya hivyo tunaruhusu oil iweze kupanda kwenye injini ya gari, ili pale linapoanza mwendo tayari kilainishi kama oil inakuwa imeishaingia sehemu zote nyeti ndani ya mfumo mzima wa injini.

Kama ilivyo gari, na sisi tuko hivyo wakati huo tunapoamka asubuhi. Unapoamka kitandani, mfumo mzima wa akili na mwili wako unakuwa bado umejifunga kutokana na mapumziko uliyokuwanayo usiku mzima. Mfano; kuanzia mapafu hadi mishipa ya damu vyote vinakuwa vimesinyaa. Hewa ya oksijeni inakuwa ni kidogo kutokana na kufunga madirisha muda wote wa usiku. Kwahiyo, ukikurupuka kitandani na kuanza kufanya kile unachofanya ujue unalazimisha mwili wako na akili kufanyakazi katika mazingira magumu, ingawaje hutaona madhara yake hapo hapo badala yake utaanza kuona ukichoka mapema kabla ya siku kuisha.

Matokeo yake utakuwa unashangaa kuwa ukiingia ofisini asubuhi saa moja na nusu, ikifika kuanzia saa tatu hadi nne asubuhi, unaanza kujisikia kutokuwa na hamasa tena ya kufanyakazi, unakosa kiu ya kufanya chochote kile unachofanya. Ikitokea hali hiyo, utasingizia kuwa labda hujanywa chai, utakwenda kunywa chai utarudi saa tano, ukifika ofisini utaanza kuongea na kuchati na wenzako huku muda ukizidi kuyoyoma. Mara utashitukia ni muda wa kupata chakula cha mchana, utakwenda halafu unarudi saa nane na nusu. Ukirudi huko hoi unasubilia saa tisa na nusu saa ya kurudi nyumbani. Maajabu ni kwamba, mtu wa namna hiyo akifika nyumbani anakuwa amechoka sana, matokeo yake anakuwa ni mtu wa kufika na kujipumzisha kwenye sofa, huku akiangalia runinga. Mwisho wake siku inaisha hivihivi bila kufanya chochote cha maana.

Kwahiyo, tunatakiwa mara tu baada ya kuamka kitandani tutenge muda wa walau dakika kumi bila kuanza kufanya chochote (utulivu wa akili). Kwakufanya hivyo, tunatoa mwanya kwa mfumo wetu wa akili pamoja na mfumo wa mzunguko wa damu kujiandaa na kuwa katika kasi inayotosha kuhimili mikiki mikiki ya siku husika. Utulivu wa akili ni muhimu sana kwasababu kukosekana kwake, taratibu taratibu mwili uanza kuzorota na kupoteza uimara wake. Endpo utaamua kuwa unatenga muda mfupi mara baada ya kuamka kitandani, basi huo utakuwa ni uamuzi bora ambao uliwahi kuufanya na utakupeleka kwenye ufanisi katika maeneo au nyanja zote muhimu za maisha yako.

Najua utaniambia uko bize, lakini kusema kwamba huna muda kila siku kwaajili ya kupumzika na kutafakari muda ule wa alfajiri ni sawa na kusema huna muda wa kuweka mafuta kwenye gari lako, kwasababu eti una kazi kubwa ya kuendesha gari, lakini baadae likiishiwa mafuta utasimama tu utake usitake, ambapo muda huo utakuwa umekwisha haribu gari lako.

Watu maarufu na wenye bidii kama Michael Jordan, Obama, Robin Shama na wengine wengi wanatambua thamani kubwa inayopatikana kutokana na utulivu, nidhamu na kupumzika kwa akili. Nchi kama China na India, kipindi cha ukimya na utulivu kila siku ni kitu cha kawaida kama ilivyo kula chakula—kila mmoja ufanya hivyo kuanzia umri mdogo. Kwahiyo, na wewe kama ni mpenda maisha bora ni muhimu sana ukafanya hivyo, ili kurutubisha maisha yako. Utulivu na ukimya wa akili kwa muda fulani pale unapoamka ni muhimu sana katika kutengeneza picha bora kwa maisha yako. Bwana “Swami Sivananda” ambaye alikuwa mwalimu wa dini ya kihindu na mtetezi mkubwa wa mazoezi ya kimwili, kiakili na kiroho yaani “Yoga”; aliwahi kusema kuwa “fikra ni viumbe hai”. Na kwa maana hiyo akasema kwa moja ya funguo muhimu katika maisha yako ni kubadili picha uliyonayo juu ya maisha yako. Picha ya maisha uliyonayo kwenye fikra, inajengwa zaidi na picha uliyonayo juu ya maisha yako. Kimsingi akili zetu zinafanyakazi kupitia picha zilizopo tayari akilini mwetu na zinaweza kubadilika endapo tutabadili kile tunachokitaka katika maisha yetu. Hali hii uleta kujiamini na imani juu uwezo wako na nguvu uongezeka haraka na hivyo kukuwezesha kufikia malengo yako kwa urahisi na haraka.

Kitu cha Pili: Mazoezi ya Kimwili
Unatakiwa kutumia walau dakika 30 kila siku katika kupalilia afya kamilifu ambayo imelala ndani ya hekaru la mwili wako. Mazoezi ya kila siku kama ambavyo umekuwa ukisikia mara nyingi, ni mojawapo ya njia muhafaka ya kufikia hali ya ubora binafsi. Kama mtu angekwambia kwamba, atakupa siri ya maisha marefu na ya utulivu, pengine ungeweza kufanya chochote kile, ili kupata siri hiyo. Lakini kwasasa siri ni yako sasa: Fanya mazoezi kila siku na utaona nguvu ya ajabu na hamasa ya kazi ikiingia katika maisha yako, ambapo kwa hakika itabadili maisha yako kwa kasi.

Mazoezi kidogo kila siku, yatakufanya kuwa mtu mtulivu asiyekuwa na papara zitokanazo na msongo wa mawazo. Mazoezi yataboresha umakini wako, tija na uzalishaji, ubunifu na pia yanasaidia kuboresha dunia yako ya ndani. Kuwa na nguvu tele zitokanazo na programu ya mazoezi, kutakuwezesha wewe kuchukua hatua chanya kuelekea kwenye ndoto zako. Tembea, endesha baiskeli, ogelea, kimbia, palilia bustani, pata hewa safi, lakini achana na tabia ya kuamka na kukaa kwenye sofa kutazama TV! Utajisikiaje pale marafiki zako watakapoanza kukwambia “unaonekana vizuri na unaonekana kijana” Utajisikaje pale utakapojisikia kuwa na nguvu za kufanyakazi siku nzima?

Wengi tunadhani mazoezi wanapaswa kufanywa na watu wanene tu! Dhumuni la mazoezi siyo kupunguza unene tu! bali kuna manufaa mengine hasa ya kiakili na kifikra unayapata kutokana na kufanya mazoezi. Unapata utulivu wa akili na hivyo kujipa nafasi ya kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.

Kitu cha Tatu: Maendeleo Binafsi
Maendeleo binafsi kimsingi ni shughuli yoyote ambayo inakupa elimu na uelewa juu ya nyanja zote za maisha yako. Maendeleo binafsi ni pamoja na upya wa akili na kupunguza msongo wa mawazo. Muda wako wa kila siku kwaajili ya maendeleo binafsi unaweza kuutumia kwa kusoma kitabu cha hamasa kama “Megaliving”. Unaweza kusikiliza vidio za hamasa, au kutafakari juu ya kitabu fulani ya lishe, pesa, mafanikio, afya n.k au ukawa unaangalia jinsi jua linavyochomoza. Jambo la msingi hapa ni kwamba unaanza kuchukua taarifa muhimu na za maana ambazo zipo kwaajili ya kuboresha maisha yako

Inafurahisha kujifunza mikakati na mbinu zilizopo ambazo zinaweza kuleta maajabu kwa maisha ya watu kama wangelizijua. Tunachohitaji pekee ni wazo moja la nguvu kubadili kwa lengo la kuwa na maisha bora.

Kitu ambacho utofautisha mafanikio na kushindwa ni kwamba, mafanikio yanahitaji mtu mwenye kiu ya mawazo mapya, elimu mpya na ujuzi mpya. Watu waliofanikiwa wana njaa ya kila kitu ambacho kinaweza kuwapa makali ya kuboresha maisha yao. Jibu la maisha ya ukamilifu na furaha lipo hapo nje tu na ni tele kama hewa tuvutayo. Funguka, ili vyote hivyo vipate kuingia na kwa muda wote endelea kuwa macho muda wote, ili pale inapojitokeza unavyo.

Ukweli ni kwamba mafanikio hayawezi kutokea kirahisi kama hautajumuisha suala la “maendeleo binafsi” katika mkakati wako wa maisha. Mafanikio katika kazi bila kukua kifikra hayawezi kuleta furaha maishani. Kwahiyo, ni lazima ukubali kuwa unahitaji kubadilika na kuanza kuishi zaidi “maisha kabla ya kifunguakinywa”. Lakini unahitaji kuwa jasiri, ili kuweza kuishi maisha hayo. Kama wewe siyo mtu wa asubuhi unatakiwa kubadili mawazo inawezekana ikawa changamoto wanzoni lakini utakapoanza kupata manufaa kutokana na kutimiza mila na desturi za maisha kabla ya kifunguakinywa (alfajiri), hakika utaanza kuyathamini masaa haya na mafanikio makubwa yataanza kupatikana.

Endelea kujifunza mengi kupitia mtandao wako wa MAARIFA SHOP, ili kuweza kupata makala mpya kila zinapotoka weka e-mail yako kwa kubonyeza neno hili: MAKALA.

Kupata mafunzo kila siku kwa njia ya whasap bonyeza neno MAFUNZO

No comments: