"Kufungamanisha Furaha Yako na KUTOA ni Bora Kuliko Kufungamanisha na KUPATA" - Cypridion Mushongi
Watu walio wengi wakipata faida wanafurahi sana, hii ni kutokana na ukweli kwamba jamii yetu kwasasa imejenga tabia ya kwamba maisha ni..
KUPATA na siyo vinginevyo.Sasa tumefikia mahala tukajifanya kujisahaulisha kana kwamba hakuna KUTOA bali maisha ni KUPATA tu!. Kutokana na mazoea hayo watu wengi WANATOA lakini ni katika hali ya kulalamika, kunung’unika na wakati mwingine kulazimishwa.
Hoja hii ya KUTOA na KUPATA inaelezeka vizuri kwenye kisa kimoja hapa chini cha mama mmoja niliyekutana naye mwezi wa Tano 2020:
“Siku moja tulimtembelea mama mmoja ambaye anafuga sungura nyumbani
kwake Bukoba. Lengo la ziara yetu tulitaka kuona ni kwa jinsi gani ananufaika
na mradi huo wa sungura. Mama huyo alitueleza kuwa alianza ufugaji akiwa na sungura mmoja, ambaye
alimnunua kwa bei ya shilingi 1,000/- kutoka kwa mwanafunzi
aliyekuwa anatafuta pesa ya kununua daftari la shule. Mama huyo alikiri mbele
yetu kuwa sungura wanamlipa sana, ambapo alisema kuwa idadi ya sungura ambao
alikuwa tayari amewauza walikuwa wamemuingizia kipato cha karibia shilingi LAKI
TANO. Kilichotushangaza ni pale alipotwambia kuwa UFUGAJI WA SUNGURA UNA KAZI
SANA. Hapo ilibidi tummulize kulikoni? Alitujibu kuwa yeye anapata adha kubwa
ya kuwatafutia magugu mashambani. Kutokana na hali hiyo ambayo kwake yeye
ilionekana ni KERO kulisha sungura, tayari alikuwa ameanza kupunguza idadi ya
sungura hao na kuanza kujielekeza kwenye mradi mwingine wa ufugaji wa kuku”.
Kisa hiki kilinifanya nitambue kuwa mama huyu anawakilisha kundi kubwa la watu ambao maisha yao yametawaliwa zaidi na shauku ya KUPATA bila KUTOA.
Kwamba wao wanapotoa hawafurahi hata kidogo, kila wanapopata mwanya wa kukwepa KUTOA wanafanya hivyo bila kujali athari zinazoweza kujitokeza kwenye miradi wanayomiliki.
Jambo la KUTOA kwao ni usumbufu, ni gumu, ni kazi sana na ni la ukakasi n.k. Matokeo yake ni kwamba leo hii, madhara ya kutopenda KUTOA ni makubwa sana.
Mfano wa madhara ya kutopenda KUTOA ni kwenye afya zetu. Hii ikiwa ni pamoja na kuwa na afya duni sana hasa mashambulizi dhidi ya magonjwa.
Kwani ili tuwe na afya bora inatupasa KUTOA muda kwaajili ya kupumzika, kufanya mazoezi, kutoa pesa kujipatia matunda na mbogamboga kwaajili ya kuimalisha kinga ya mwili, kunywa maji n.k.
Madhara ya kushindwa KUTOA kweye biashara: Biashara nyingi zinashindwa kukua na kuendelea, siyo tu kwasababu ya kukosa pesa BALI ni kwasababu ya kushindwa KUTOA.
Watu wengi wamejenga tabia ya kulalamika na kunung’unika. Nimefuatilia karibu kila mmoja analalamikia kazi, mradi au biashara anayofanya kuwa ni ngumu.
Mwingine anaenda mabli hadi kuulalamikia mradi wenyewe kuwa umemukamua sana – “eti umetumia pesa nyingi sana kwenye mradi.
Wale walio na miradi ya ufugaji utasikia kauli kama hizi; nguruwe anakula sana, kuku wanakula sana n.k. Kauli zote hizi zinabeba ujumbe wa chuki juu ya suala zima la KUTOA.
Kwa maana nyingine ni kwamba wengi hawako tayari KUTOA kile kinachotakiwa kutoka kwao kwenda kwenye kile wanachofanya japokuwa nao wanatamani MAFANIKIO kutoka kwenye hicho wanachokifanya.
Kutopenda KUTOA kuna athari kwenye kuchagua mradi wa biashara na pia kunakupunguzia uwezo wako wa kuchangamkia fursa za kibiashara.
Nadhani umesikia mara nyingi watu wakiuliza ni biashara gani inalipa; wakimaanisha kuwa tayari wanao mtaji (PESA) ya kufanya biashara. Ukiona hivyo ujue huyo mtu anaangalia ATAPATA nini kwenye biashara na siyo yeye ATATOA nini.
Mara nyingi watu wanaokuwa na mtaji halafu wakaenda kuuliza biashra gani wafanye ni nadra sana kukuta biashara zao zinadumu. Hii ni kwasababu wanatoa mtaji tu basi na kusahau vitu vingine kama nilivyovianisha hapo juu.
Natakiwa NITOE nini
ili nistahili kufurahi NINAPOPATA?
Yawezekana watu wengine wanashindwa KUTOA kwasababu pengine hawafahamu ni vitu gani hasa wanatakiwa KUTOA ili KUPATA kikubwa.
Tunaposema KUTOA tunamaanisha zaidi ya kutoa PESA, ukiwa na kitu au mradi unaoufanya unatakiwa KUTOA vitu kama UONGOZI, UFUATILIAJI NA USIMAMIZI, NGUVU, MUDA, FIKRA, MAARIFA, UBUNIFU, UTAYARI, UVUMILIVU, IMANI NA VILE VYOTE UTAKAVYOVIKOSA KUTOKANA NA WEWE KUJIHUSISHA NA MRADI WAKO HUO.
Vyote hivi ikiwa ni muhimu sana na vina thamani sawa na pesa. Wengi wanapoanzisha miradi wanadhani kwasababu tu wameweka mitaji mikubwa, basi mambo yameisha.
Matokeo yake mradi unakosa mambo niliyoyataja hapo juu na hivyo kufanya kuwa ngumu kurudisha zile pesa ambazo zilizowekezwa kama mtaji….. Hali hii inapotokea ndipo unakutana na mtu akiwa analaani vikali jinsi ambavyo amepata hasara.
Kwahiyo, kuanzia sasa tuache kabisa kulalamikia miradi ambayo kimsingi ndiyo inakwenda kukuletea mafanikio.
Tutambue kuwa tunahitaji KUTOA hata ikibidi kuzidi kile tunachokipata, baada ya muda tutashuhudia KUPATA kwa wingi kutoka kwenye miradi tunayoianzisha na kuisimamia.
Nitoe rai kwa wajasiriamali wote kwamba tubadilike sasa kuhusu jinsi ya kufanya na kuendesha biashara.
Pamoja na kutafuta mtaji, tunatakiwa kufanya tathimini ya pande zote mbili yaani lazima kuchambua juu ya nini TUTAPATA kutoka kwenye biashara tunayotarajia kuifanya na pia tuchambue ni vitu gani hasa VITAHITAJIKA kutoka kwetu.
Mpendwa msomaji wangu wa MAARIFASHOP nakupa siri leo kuwa kuna maisha mazuri sana kwenye KUTOA. Lakini usiniulize swali la mbona mimi sina cha KUTOA? Mimi mbona ni maskini?
Na mimi nakwambia kuwa kila mwenye KUPATA kitu chochote jua ana uwezo wa KUTOA chochote. Kwahiyo, kila utakapofikiria juu ya fursa fulani, kitu cha kwanza ni wewe kufikiria kwa upande wako uko tayari KUTOA nini? ili kunufaika na hiyo fursa?
Hivyo ni muhimu sana furaha zetu zikafungamanishwa na KUTOA badala ya kuzifungamanisha na KUPATA. Tuzidi kujitahidi kufurahi pale TUNAPOTOA, kwasababu tunavyotoa ndivyo thamani yetu inavyozidi kupanda na hivyo kutimiza kusudi letu la kuwepo hapa duniani.
Endapo umejifunza chochote kwenye makala hii, na pia ungependa kupata program za mafunzo kwa siku za hivi karibuni juu ya biashara, ujasiriamali, uongozi, uwekezaji na jinsi ya kupata mafanikio, tafadhali bonyeza neno MAFUNZO ; kusajili barua pepe (e-mail) yako ambapo utatumiwa mafunzo moja kwa moja.
No comments:
Post a Comment