Tuesday, July 23, 2024

Kuna Uzuri Gani Katika Kushindwa?



Je, wewe ni kati ya wale wanaoshangaa kuona ‘kushindwa’ ni jambo zuri? Mmmh! Unaona kama utani hivi, Hapana! Siyo utani! Ni ukweli, watu wengi tunashindwa kila..
siku angalau zaidi ya mara moja.

Katika maandalizi ya kuanza safari ya kuelekea maisha ya ndoto yako, wengi wetu huwa tunaangalia mambo mawili tu! Pale tulipo muda huo na kule tuendako.

Siyo rahisi kuona matatizo au changamoto zilizopo kwenye njia yako kwa wakati huu wa hatua ya wazo.

Katika safari yako, ni lazima utakutana na mchanganyiko wa ‘kushindwa’ na ‘kufanikiwa’. Matatizo na changamoto nyingi zinajulikana baada ya kuanza utekelezaji wa mradi wako wa biashara.

Ukisha kuanza, ndiyo unapata kufahamu ni wapi hasa kuna vikwazo vya namna gani. Vikwazo vinakufanya uchelewe kutimiza ndoto yako.

Kwa mara ya kwanza inaweza kuchukua takribani miaka 10 au zaidi kwa mtu kujenga utajiri. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, mwanzoni mtu anakabiliana na kushindwanyingi zilizojaa njiani.

Ni kawaida sana kukuta mtu anatumia takribani miaka 10 au zaidi kujenga utajiri na baadae ukaporomoka ghafla na kuisha kabisa.

Lakini mtu huyu akianza tena upya, mara hii utashangaa anatumia takribani miaka 3 hadi 4 kurudisha utajiri wake.

Kitendo cha kutumia muda mfupi kurudisha utajiri haraka kuliko mwanzo kinafafanua vyema uzuri wa kushindwa.

Kwamba unaposhindwa mara ya kwanza, na baadae ukaamua kuanza tena upya, unapata fursa ya kutambua aina ya matatizo na changamoto zilizokuwepo, lakini pia unafahamu fika ni wapi hasa ulijikwaa mara ya kwanza.

Tunapofanya kitu tukashindwa mara nyingi na pengine tukalazimika kuanza upya, unafika wakati tunajua bayana kitu gani hasa hatupashwi kukirudia kukifanya!

Unapojaribu kwa mara nyingine, tayari unajua ni vitu gani vya kuepuka, unajua njia za mkato, unajua mambo gani ya kufanya kwa garama nafuu, unajua ni aina gani ya wafanyakazi wa kwenda nao n.k.

Mara ya kwanza inachukua muda mrefu kwasababu unakuwa hujui ni wapi kuna vizingiti gani, hujui njia rahisi na kwa ujumla wake unakuwa hujui mazingira halisi yanayofaa kustawisha mradi wako wa biashara.

Somo muhimu la kujifunza ni kwamba, kumbe neno ‘kushindwa’ halimaanishi mwisho au huwezi kuanza tena! Bali linamaanisha; kuanza tena, kubuni mbinu mpya, kubadili mikakati n.k.

Mradi wa biashara unaokushinda kuufanya leo, tambua kuwa unaweza kuufanya kwa mara nyingine.

Ukishindwa, fanya mabadiliko na uanze tena! Rudia kufanya tena katika muda muhafaka.

Kuna mtu anapata wazo zuri la biashara, lakini anakaa nalo miaka mingi, kwanini? 

Eti! anaogopa ‘Kushindwa’. Wengine wanaanza halafu wanaachia njiani kwasababu wanaogopa ‘Kushindwa’.

Mwingine anakwambia ninaogopa kushindwa mara siwezi nikafanya vile. "Kwani unadhani ni nani anapenda kushindwa?" Lakini, endelea kushikilia na endapo ikitokea ukashindwa, sema niko tayari kuendelea!

Kumbuka wakati unajifunza baiskeli ulianguka! Hilo lilikuzuia kuipanda tena? 

Unaanguka unaenda ukutani unalia, maumivu yakiisha unarudi kujaribu tena! 
Leo hii tunakuona uko vizuri hadi unashiriki mashindano ya mbio za baiskeli.

Kama kila aliyejifunza kuendesha baiskeli alianguka mara ya kwanza! Kwanini tusitumie kanuni zile zile za mtu anayeanza kujifunza baiskeli?

Tunaweza, na lazima tuweze kufanya hivyo, na wewe utaweza.

Unayesoma Makala hii ni kwamba katika mchakato wa kusaka mafanikio “jiandae kushindwa” kwasababu ‘kushindwa’ ni jambo zuri na ni sehemu ya mchakato wa kufanikiwa.

Jiandae ‘kushindwa’ kwani hili halikwepeki. Kuna siku litatokea, ambapo mambo yako hayatenda kama ulivyopanga! Na huo ndiyo uhalisia katika ulimwengu wa biashara.

Na mimi hapa najaribu kuwa muwazi kwako. Nasema tena ‘Jiandae’ kwa hilo na likitokea sema ‘Bw. C. Mushongi’ aliniambia kuhusu hili jambo. 

Ha haa! Sitajali hata ukisemaa! Na wewe usijali kama likikutokea, kwani kadili utakavyokutana na ‘Kushindwa’ ndivyo utakavyozidi kusogelea ‘Kufanikiwa’. Yaani "unashindwa mara nyingi mpaka unabakiza kufanikiwa!

Wewe kama mjasiriamali, kila wakati jiambie maneno haya; "Kwangu mimi, kushindwa si chochote bali ni fursa yangu ya kujifunza na kukua”.

Unahitaji MAARIFA kuuona uzuri ndani ya ‘Kushindwa’. Kupitia kujisomea makala mbalimbali zinazopatikana katika mtandao wa MAARIFASHOP utaweza kutajipatia mbinu za uhakika wa kufanikisha maisha ya ndoto yako.

Ili kupata makala mpya kila zinapochapishwa, bofya neno MAKALA MPYA kisha sajiri barua pepe. Kwa wale wanaopenda kupata mafunzo kwa njia ya whatsap bofya kwenye neno MAFUNZO.



No comments: