Wednesday, March 1, 2023

UZIO WA MJI NANI ANAFUNGUA LANGO LAKE?

“Mahitaji ya lazima ni machache lakini vitu tunavyovitaka havina kikomo” ~ Cypridion Mushongi


Wengi tunafahamu nyumba nyingi zina uzio wa aina fulani na tumezoea kuona walinzi wakikaa langoni kwa lengo la kulinda usalama wa watu na mali. Anayekaa LANGONI ndiye anayeruhusu watu na vitu kuingia na kutoka.

Ukweli ni kwamba“Mji ni..sawa tu na UZIO” ambao una lango la kuingilia na kutoka nje!

Tofauti na uzio wa nyumba uliozoeleka, “uzio wa mji” hauonekani kwa macho ya kawaida isipokuwa kwa macho ya fikra au ubongo.

Kwa maana nyingine ni kitu kisichoonekana. Ndiyo maana imekuwa siyo rahisi kufahamu kuwa mji nao una walinzi mbalimbali wanaokaa LANGONI.

Walinzi katika mji ni wale watu wanaodhibiti vile vitu vinavyoingia mjini.

Mfano; wiki iliyopita nikiwa naongea na baadhi ya watu wanaochoma mahindi kwenye mitaa fulani ya jiji la Mwanza, niligundua kuwa idadi ya watu wanaoingiza mahindi mabichi mjini ni ndogo sana ikilinganishwa na idadi ya wachoma mahindi mitaani hasa nyakati za jioni.

Kwangu mimi “waingizaji wa mahindi mabichi mjini ni walinzi wa mji na wanakaa LANGONI”.

Shughuli ya kukaa LANGONI mwa mji, unajipatia mwenyewe tofauti na mlinzi wa nyumba ambapo hupewa ajira na mwenye nyumba. Kama mji ni UZIO basi yatupasa kukaa langoni (getini).

Kukaa langoni mwa mji inamaanisha kuzalisha au kusambaza kitu chochote kwa watu waishio mjini, ilimradi tu kiwe ni cha thamani. Pia, ni muhimu ukawa na uwezo wa kudhibiti upatikanaji wake.

Kwenye ulimwengu wa AJIRA, mtu anayekaa langoni ni mlinzi wa watu na mali, lakini kwenye ulimwengu wa KAZI mambo ni tofauti.  
Anayekaa langoni ndiye ana udhibiti wa uzalishaji na usambazaji wa bidhaa au huduma mojawapo ambayo inategemewa na watu wengi. Ndiyo maana ninasema watu ambao wanadhibiti uchumi wa mji wanakaa LANGONI.

Kukaa langoni ni kuwa na uwezo wa kudhibiti usambazaji wa kitu muhimu kimojawapo kati ya vile vinavyopendelewa na watu wanaoishi mjini.

Watu waliowengi walikuja mjini kwa lengo moja tu! La kutafuta maisha mazuri.  
Ndiyo maana wote wamejikusanya ndani ya mipaka ya mji na wengi wao hawatengenezi bali wanatafuta pesa ndani ya uzio wa mji.

Habari njema ni kwamba watu waliojikusanya mjini, wengi wao hawana matarajio ya kurudi kijijini na wana kiu ya mahitaji isiyokuwa na kikomo.

Kwa maneno mengine kitu chochote cha thamani utakachowaletea watakinunua tu! Kwasababu, watu hawa hawana muda tena wa kwenda kutafuta vitu hivyo vinakopatikana nje ya UZIO wa mji.

Mji ni mkusanyiko wa watu ambao wengi wao wanapenda sana unafuu, urahisi wa upatikanaji vitu, hawapendi ugumu na usumbufu kwasababu walikimbia vijiji vyao kutokana na ugumu wa maisha.

Watu wa mjini maisha yao siku zote ni kukaa ndani ya UZIO au mipaka ya mji. Pia, hawana tena uvumilivu wa shida zile zilizowasukuma kutoka maeneo yao ya awali.

Kama wewe ni miongoni mwa watu ambao wangependa kukaa LANGONI mwa mji, basi unahitaji kusoma tabia ya hawa watu wa mjini kuhusu “utumiaji na ulaji” wa vitu mbalimbali ikiwemo tabia ya utumiaji pesa!

Kumbuka kuwa tabia mojawapo kuhusu matumizi binafsi ya pesa ni ile hali ya “kupata na kutumia” siku hiyohiyo.

Kwa wanufaika wa ajira rasmi na isiyo rasmi, kitu cha kwanza kufanya pindi wapatapo AJIRA ni kujenga nyumba ya makazi, ili kuachana na adha ya kulipa kodi ya pango.

Baada ya kumiliki nyumba ya makazi, kinachofuata ni kupata na kutumia. Wanapata na kutumia kutokana na msukumo wa hisia za matukio ya kimaisha. Mfano; starehe, misiba, sherehe, ununuzi wa vitu mbalimbali vya ndani, chakula, elimu n.k.

Wale ambao tayari wanamiliki makazi yao wenyewe ni watu muhimu sana kwako wewe unayejiandaa kukaa langoni mwa mji, kwasababu hawa ni watu wa “pata-tumia”.

Ili uweze kupata fursa ya kukaa LANGONI mwa mji ni lazima huwe na KAZI badala ya AJIRA!

Kazi tofauti na ajira ndiyo itakuwezesha kukaa LANGONI kwa maana utaweza kuzalisha au kusambaza vitu mbalimbali ndani ya UZIO wa mji.

Utafutaji wa wazo la biashara ufuate mwelekeo wa kufikiri kupitia utengenezaji wa picha ya mji/jiji kama UZIO.

Picha au taswira yako ya UZIO yawezakuwa ya mamlaka ya mji mdogo, manispaa, jiji, kijiji, kata, wilaya, mkoa n.k.  
Kisha vuta picha ya wewe ukiwa unafungua mlango ili kuingiza bidhaa zako ili ziwafikie watu mbalimbali wanaoishi ndani ya UZIO au mipaka ya mji.

Ukishapata picha hiyo, nenda mbali zaidi kwa kufikiria ni bidhaa/huduma gani unaweza kuidhibiti.

Na hapa husiwaze kufanya hivyo ndani ya muda mfupi! Mchakato huu unaweza kukuchukua miaka kadhaa kabla ya kufikia kiwango kikubwa cha udhibiti.

Unahitaji kuwa na ndoto ya muda mrefu. Husijali, hata kama itakuchukua miaka 10 na Zaidi kufikia ndoto yako.

Kwahiyo, jambo la kuweza kukaa LANGONI mwa mji, halitakuwa tukio la siku moja bali itakuwa ni mchakato ambao utakulazimu kuanza kidogo kuelekea lengo lako la kuishi LANGONI mwa mji wa chaguo lako.

Kama ni mpenzi wa kukaa LANGONI mwa mji basi kila wakati tumia mtandao wa MAARIFASHOP kupata maarifa ya kukuza uchumi wako!

Ili kuweza kupata makala mpya kila zinapochapishwa, bonyeza neno; NITUMIE MAKALA kisha sajiri barua pepe yako. Na kama unapenda kupata mafunzo ya kila siku kwa njia ya whatsap bonyeza hapa: MAFUNZO.

TENGENEZA PESA USITAFUTE PESA!

No comments: