Sunday, January 7, 2024

Heri ya Mwaka Mpya Itapatikana Ukifanya Jambo Moja

Kuipatia Dunia Kunalipa Kuliko Kuidai Dunia” ~ CYPRIDION MUSHONGI


Mwaka 2023 ulikuwa mwaka wa KUIDAI DUNIA kila kitu tulichokipenda. Hali hii imetokana na ukweli kwamba, kila binadamu anahakikisha anakuwa na maisha yenye Faraja – yaani maisha yenye kumpatia kila kitu anachohitaji.

Uhitaji wa maisha ya faraja, unaongozwa zaidi na matamanio au tamaa za kibinadamu, ambazo hazina ukomo. Tabia hii ya kupenda faraja, humfanya mtu.. kutafuta kila namna au njia yoyote, ilimradi inakidhi haja ya tamaa aliyonayo.

Msukumo mkubwa wa kutii kiu ya tamaa zetu, umefanya watu waliowengi kujikita zaidi kwenye maisha ya KUTAFUTA kuliko KUTENGENEZA. Maisha ya KUTAFUTA yalifanikiwa sana zama zile za kale ambapo, binadamu aliishi kwa kuwinda (KUTAFUTA) Wanyama na kuokota (KUTAFUTA) matunda porini au mbugani.

Kutokana na changamoto mbalimbali, wanyama na matunda vilianza kupungua na pengine kupatikana mbali sana na nyumbani. Hapo ndipo binadamu akagundua sayansi ya kulima na kufuga (KUTENGENEZA) wanyama. Hapa tunamuona binadamu akibadilisha mfumo wa maisha ya KUTAFUTA na kuingia maisha mapya – yaani ya KUTENGENEZA.

Katika nyakati hizi tulizomo inashangaza sana kuona binadamu akirudi kwenye maisha ya KUTAFUTA kwa kasi ya 4G, na ni wakati ambapo vitu vya bure vimepungua sana na vinaendelea kuadimika kila kukicha.

Nyimbo za vijana kama vile “Zingatia maokoto” na “Acha ni-enjoy maisha yenyewe ni mafupi” ni mojawapo ya viashiria tosha kwamba binadamu tayari amerudi nyuma kifikra sawa na wakati ule wa zama za kale za kuishi kwa kutegemea KUTAFUTA au KUOKOTA kila kilichotayari.

Hapa maswali ni mengi! Mfano; endapo unapenda kuokota kilichopo au kilichodondoka! Je, kisipotengenezwa kitadondoka kutoka wapi? Na kutoka kwa nani? Ni nani huyo atatengeneza kitu chake, halafu alegeze mikono kikudondokee?.

Maisha ya KUTAFUTA au “KUOKOTA” yamesababisha tabia ya watu KUDAI kila kitu wanachohitaji na hata kisicho mali yao.

Kwasasa, tuko kwenye zama ambazo kila mtu anamtaka kila mwenzake amfanyie kitu fulani (ANADAI). Kwa maneno mengine, kila mtu ANADAI kila kitu apewe na dunia au mwenzake. Tumekuwa watu wa KUDAI kila kitu…tunadai tuombewe, tupewe kazi, tuelimishwe, tulindwe, tusaidiwe, tutibiwe, tuheshimiwe, tupendwe, tulishwe, tufadhiliwe, tukopeshwe, n.k.

Orodha ya madai yetu kutoka kwenye dunia ni ndefu sana. Swali ni je, hivi vyote tunavyodai visipotengenezwa na mimi vitatoka kwa nani? jambo hili linatupeleka kwenye hali ya mahangaiko yasiyokuwa na kikomo sawa na tamaa zetu zisivyokuwa na kikomo.

Ukweli ni kwamba suala la KUTAFUTA, KUOKOTA au KUDAI kilichopo tu! Kama zile zama za kale, haliwezi tena kukuletea maendeleo ya kweli.

Suruhisho pekee ni kuirudia tena nguvu ya akili, ili ituongoze kujenga maisha ya kuwa WATENGENEZAJI wa kile tunachotamani kiwepo. Tukumbuke kuwa, vitu vyote tunavyotamani kuvipata ni lazima vitengenezwe – hivyo tunahitaji zaidi watu ambao ni WATENGENEZAJI kuliko WATAFUTAJI waliojaa duniani.

Dunia iliyojaa WATAFUTAJI ni dunia yenye watu wa KUIDAI DUNIA kila kitu. Kwamba, tunakuwa na watu wa kutumia tu! Bila wao kuzalisha (KUTENGENEZA) chochote!

Habari njema ni kwamba, vitu vingi tunavyodai kutoka duniani vitapatikana tu! endapo kila mmoja wetu atakuwa tayari kutumia muda wake kutengeneza walau kitu kimojawapo. Na hapa namaanisha mimi kuwa tayari kutengeneza chochote chenye thamani kwa maisha ya binadamu. Nikifanikiwa kufanya hivyo, basi nitakuwa NIMEIPATIA kitu dunia na sitakuwa sehemu ya WANAOIDAI dunia.

Mwaka huu wa 2024, huwe ni muda wa kuondoka kwenye kundi la watu wa KUIDAI DUNIA VITU, na kujiunga na kundi la watu maalumu wenye KUIPATIA VITU DUNIA.

Je, Nitaipatiaje Vitu Dunia?

Katika kujiunga na kundi maalumu la “KUIPATIA DUNIA VITU”; ni muhimu kubuni na kuanzisha miradi ya kiuchumi au kibiashara. Ubunifu na uanzishaji wa miradi ya namna hii uanze kwa kubaini na kuangalia matatizo, kero na/au changamoto zilizopo kwenye umma hasa ule uliotuzunguka. Baada ya kubaini matatizo yaliyopo, huku tukiongozwa na falsafa ya “kila tatizo lililopo duniani ni biashara”!

Nguvu ya akili itumike ipasavyo kupata suruhisho. Kama mradi wako wa kiuchumi utaanzishwa kwa makusudi ya kutoa thamani au kuleta suruhisho, basi ujue kuwa watu wanaoathiriwa na matatizo au kero ulizobaini, watakuwa tayari kukulipa pesa, ili kupata “suruhisho hilo uliloipatia dunia”.

Niseme kwamba “KUIPATIA DUNIA VITU kunalipa kuliko KUIDAI DUNIA”. Kwa maana vitu vya thamani (suruhisho) unavyozalisha, siyo kwamba unawapatia watu bure, bali kiu yao ya kupata suruhisho inawafanya wakulipe pesa kiasi unachotaka wewe.

Ndugu yangu hasa mtanzania unayesoma Makala hii, jitahidi mwaka huu, kuielekeze nguvu yako ya akili katika KUTENGENEZA SURUHISHO mbalimbali kwaajili ya kujibu kero na matatizo yaliyopo, ili huweze kustahili kulipwa pesa.

Kila wakati, tumia vizuri mtandao wako wa MAARIFASHOP kujipatia mwongozo wa maarifa ya jinsi ya kuishi maisha ya KUTENGENEZA na ambayo yatakuhakikishia maendeleo ya kweli.

No comments: