Tuesday, January 31, 2023

Elimu Rasmi Inatosheleza AJIRA Siyo KAZI ni Kweli?

“Kujiajiri na kuajiriwa yote ni AJIRA siyo KAZI”~ Cypridion Mushongi.


Kuna jitihada nyingi za kukuza elimu rasimi zinazowekwa na serikali pamoja na wadau wa maendeleo. 

Malengo hasa ni kuona watu wengi katika taifa wakipata elimu rasmi kwa matarajio ya.. kwamba watajikomboa kiuchumi na kijamii.

Kwa bahati mbaya pamoja na jitihada zote hizi na richa ya kwamba bado waliopata elimu rasmi ni wachache ukilinganisha na idadi ya watu kwenye nchi.

Kuna changamoto kubwa ya ukosefu wa AJIRA. 
Mwonzoni ilidhaniwa kwamba watu wakisoma wataweza kujiajiri lakini inaonekana hili nalo ni gumu kulingana mifano tunayoiona.

Kinachoonekana dhahili ni kwamba, mfumo wa elimu rasmi unaandaa watu kwaajili ya kutumikia AJIRA siyo KAZI.

KAZI ni muunganiko wa shughuli mbalimbali katika mpangilio maalum kwa lengo la kupata matokeo au suruhisho fulani. Suruhisho laweza kuwa ni bidhaa au huduma zenye kukidhi mahitaji ya binadamu.

Kimahesabu, tunaweza kusema KAZI ni sawa sawa na shughuli 1+ shughuli 2 + shughuli 3 + Shughuli 4…...n.k. na mwisho tunapata matokeo tarajiwa.

Matokeo ya KAZI ni “bidhaa au huduma” na hizi ndilo hitaji na lengo hasa la “Mwenye-Kazi”, na pia ndiyo suruhisho ya changamoto au kero zilizopo kwenye jamii.

SOMA; AJIRA siyo KAZI ni AJIRA na KAZI siyo AJIRA ni KAZI

AJIRA ni kwamba mwajiriwa unapangiwa shughuli za kufanya na “Mwenye-Kazi” na wengine wanapangiwa shughuli nyingine za kufanya, ili kuleta matokeo tarajiwa.

Ndiyo maana tunasema kwamba elimu rasmi imelenga kutumika Zaidi kwenye AJIRA na siyo kwenye KAZI.

Elimu rasmi ambayo ni ya AJIRA, haimpi muhusika nafasi ya kufikiri na kutenda kimfumo au kimchakato badala yake inamfanya mtu kufikiri na kutenda kishughuli au kimatukio.

Utendaji wa kishughuli au kimatukio unatokana na ukweli kwamba elimu rasmi inamfanya mtu kubobea katika eneo moja dogo na maalumu.

Ndiyo maana kila inapopatikana KAZI wanahitajika wafanyakazi au wafanya-shughuli wengi wenye ujuzi na taaluma mbalimbali.

Wafanya-shughuli hawa kwa ujumla wao wanaweza kukamilisha shughuli zote zinazotakiwa na hivyo kuleta matokeo yanayotarajiwa na “Mwenye-Kazi”.

Kwahiyo, kuna ulazima mkubwa wa watu hasa wanaoitwa “wasomi” kutambua kuwa AJIRA na KAZI ni vitu viwili tofauti.

Haitoshi kusema watu wasome ili kujiajiri, kwasababu, kujiajiri siyo suruhisho la ajira hatakidogo. Ndiyo maana huko siku za nyuma niliwahi kusema kuwa “Kujiajiri na kuajiriwa yote ni AJIRA siyo KAZI”.

KAZI ndiyo huzalisha AJIRA kwa wingi, lakini pia ikumbukwe kuwa AJIRA haiwezi kuzalisha KAZI.

Elimu rasmi imejikita katika “mfumo wa maelekezo”. Mfumo huu hautoi nafasi kwa muhusika kuweza kuhoji kile anachofundishwa. 

Ndiyo maana wote tuliopata elimu rasmi, mara zote tumeaminishwa kuwa kuna jibu moja katika maisha.

Lakini ukweli ni kwamba changamoto zitokanazo na michakato ya kiuchumi na kijamii haziwezi kutatuliwa kwa njia au mbinu moja wakati wote.

Uhalisia ni kwamba changamoto nyingi zinajibiwa na KAZI ambayo kimsingi inahitaji wasomi wenye kuleta jibu Zaidi ya moja.

Yanahitajika majibu mengi tofauti hatakama ni kwa changamoto na matatizo yanayofanana.

KAZI tofauti na AJIRA inahitaji wasomi wenye majibu tofauti kwa swali lile lile moja! Hawa tulionao, wengi wana jibu moja tu! Linalofanana..

Wasomi wengi walioajiriwa na ambao wamepata elimu rasmi yenye mlengo wa AJIRA hawawezi kutumia elimu hiyohiyo kutupatia watu wenye uwezo wa kutengeneza KAZI ambazo hatimaye huzaa AJIRA nyingi zaidi.

Nchi nyingi za Afrika ikiwemo kwetu Tanzania, zina upungufu mkubwa wa watu walio na uwezo wa kutengeneza “KAZI” lakini pia kuna upungufu wa wasomi au wataalamu wa kuhudumia “WATENGENEZA KAZI”.

Hapa tunahitajika kuwa “Wajanja” ili kuweza kutumia elimu hii ya “AJIRA” kupata elimu na ujuzi kwaajili ya kukidhi mahitaji ya kundi muhimu la “WATENGENEZA KAZI”.

Kuongezeka kwa watu ambao ni “WATENGENEZA KAZI” ndiko kutakuwa suruhisho la kuaminika katika kutatua changamoto kubwa ya ukosefu wa ajira hasa kwa vijana.

Endelea kutumia mtandao wa MAARIFASHOP kukuza ujanja na huwezo wa kutengeneza KAZI!

Kupata makala mpya kila zinapochapishwa, bonyeza neno; NITUMIE MAKALA kisha sajiri barua pepe yako. Na kama unapenda kupata mafunzo ya kila siku kwa njia ya whatsap bonyeza hapa: MAFUNZO.

No comments: