Saturday, April 30, 2016

Umuhimu wa Kutafuta Pesa Bila Sababu ni Huu


“Unashindwa kupata pesa nyingi kwasababu unatafuta pesa kulingana na shida unazotegemea kupata siku zijazo” ~ Cypridion Mushongi
Siku moja nilikuwa naongea na rafiki yangu ambaye aliwahi kuniuzia kiwanja siku za nyuma. Baada ya mwaka mmoja tangu rafiki huyo aniuzie kiwanja, tulikutana mjini Bukoba na hapa aliniuliza juu ya mpango wangu wa kukiendeleza kiwanja hicho. Jibu langu kwake lilikuwa...
“kwasasa sina pesa, ngoja kwanza nijipange”.

Jibu hili la kwamba mimi sina pesa halikumridhisha sana, ndipo akaniambia maneno mazito tena kwa lugha ya kihaya! “Amahela Geija Omubyemba!” Tafsiri isiyo rasimi kwa maneno haya ni kwamba “pesa uja wakati wa matatizo na shida”.

Shida na matatizo yanayozungumziwa hapa ni kama vile kuugua au kuuguliwa, kupatwa na msiba, harusi, kesi mahakamani, kudaiwa, karo za shule, ndoa kuvunjika n.k.

Tulipoachana nililazimika kuandika maneno yale kwenye kitabu changu cha kumbukumbu za kila siku. Wakati nikiendelea kundika nilizidi kutafakari kwa kina, juu ya jambo hili la pesa kupatikana wakati wa matatizo na shida. Nilizidi kujiuliza ni kwanini pesa ipatikane tu wakati tunapopatwa na shida au matatizo?

Bilashaka, maneno ya rafiki yangu huyu, yalilenga kunikumbusha kuwa, pindi nikiamua kwa dhati kuanza ujenzi, kwa vyovyote vile pesa itapatikana tu!.

Ukichunguza kwa kina, utagundua kuwa watu wengi ambao ni maskini ndani ya fikra zao, hawana na hawafikirii kuwa na pesa nyingi. Maisha ya maskini ni kana kwamba wakati ambao hakuna shida au matatizo, haoni haja ya kutafuta pesa!

Kwahiyo, kama hakuna shida, mara nyingi watu wengi uchagua kutokuwa na pesa. Kwa maana nyingine ni kwamba, watu wa namna hii wanapopatwa na shida, ndipo uanza kuona umuhimu na ulazima wa kutafuta pesa.

Kwa watu wa namna hii hasa maskini, shida na matatizo ndivyo vinakuwa sababu kubwa na kichocheo cha mtu kutafuta pesa kwa namna yoyote hile. – Pesa upatikana kwa muda mfupi!.

Katika hili tunajifunza mambo mengi, lakini mojawapo ni kwamba “watu wengi tunashindwa kupata pesa nyingi kwasababu hatujafikia hatua ya kutafuta pesa bila sababu zinazotokana na shida. 

Ukitafuta pesa baada ya kusukumwa na mahitaji ya matatizo pamoja na shida, basi ujue fika kuwa zikishapatikana zitatumika mara moja kwaajili ya kuondoa shida ambayo ndiyo ilikutuma uzitafute.

Matatizo na shida vikiisha na pesa inaisha. Pesa ikishaisha na wewe unaedelea kuishi maisha yako ya siku zote. Maisha ambayo umezoea kupata pesa ndogondogo basi!. 

Matatizo mengine yanapoibuka ndipo unaanza upya kujituma tena kutafuta pesa ili kukabiliana na shida zilizo mbele yako.

Imaonekana bila kuwepo sababu maalum na hasa inayotokana na shida/matatizo ya wakati huo, wewe hauko tayari kutafuta pesa. Kwahiyo, ni sawa na kusema “hakuna shida hakuna haja ya pesa”. Kwa maana nyingine ni kwamba, wakati ambao siyo wa shida, kutafuta pesa ni usumbufu. "Mtindo wa maisha ya namna hii ni hatari sana kwa maisha yako".

Watu wengi wanashindwa kupata pesa nyingi kwasababu, wanatafuta pesa kulingana na shida au matatizo wanayotegemea kupata siku zijazo. “Haya ni majanga”!
Watu waliofanikiwa (matajiri) mara nyingi utafuta pesa bila sababu zitokanazo na shida. Unapotafuta pesa bila sababu ya matatizo na shida unakuwa na wakati mzuri wa kufikiria na kuendeleza miradi mikubwa na yenye tija kwa watu wengi. Hii ina maana unatulia na kutafuta pesa bila kukurupuka -Yawezekana ndiyo maana matajiri wana pesa nyingi.

Ikumbukwe kuwa, kila kitu afanyacho binadamu anakuwa na sababu. Lakini, jiulize, wewe unatafuta pesa kwasababu gani? Aina ya sababu ndiyo itakufanya ama upate pesa nyingi au upate pesa kidogo sana.

Sababu ya maskini kutafuta pesa ni kumaliza shida/dharura, majanga aliyonayo. Lakini, watu matajiri utafuta pesa ili kuzidi kupata vitu vingi na utajiri kwa ujumla. 

Kwahiyo, ndoto, malengo, sababu, dhamira n.k. ya kutafuta pesa ndizo zinatofautiana kati ya mtu na mtu. Kwa maana hiyo, wewe ndiye wa kubadilisha malengo na sababu ya kutafuta pesa.

Mpaka hapa ni kwamba, kama wewe ni mmojawapo wa watu wanaotafuta mafanikio, ni lazima uwe mtu wa kutafuta pesa bila ya kusukumwa na sababu zitokanazo na shida/matatizo. Jitahidi kujituma sana kutafuta pesa ikiwezekana jitume kuliko yule atafutaye pesa kwasababu ya shida na matatizo.

Sasa umeyajua haya! Ni lazima tuanze pamoja kutafuta pesa bila sababu zitokanazo na shida/matatizo.

Hatujachelewa hata kidogo tuanze leo.

Kwa maoni zaidi au ushauri jiunge NA mtandao huu kwa kubonyeza neno hili: MAARIFA SHOP.

No comments: