“Bei ni kile unacholipa. Thamani ni kile unachopata” ~ Warren Buffet
Wimbo ulioenea kote nchini sasa hivi ni “kushuka thamani ya pesa au shilingi ya Tanzania”. Watu wengi tunashusha lawama kwa watu waliopewa madaraka hasa ya kuongoza taasisi za kifedha.
Lakini nimetafakari sana jambo hili. Fikra na imani yangu vinanituma kuamini kuwa....
kama kila mtu akishughulika na kazi ya kupandisha thamani yake kila siku, haiwezekani thamani ya pesa yetu ikashuka.
Kwenye makala zangu zilizopita nimewahi kuandika juu ya uhusiano uliopo kati ya pesa na thamani. Thamani ya kitu chochote ndiyo pesa ambayo mtu huwa tayari kulipa endapo anahitaji kitu hicho. Kwahiyo, ni sahihi tukasema kuwa “thamani ni pesa”.
SOMA; Mafanikio Yako Yamejificha Ndani ya Thamani
Kwenye makala zangu zilizopita nimewahi kuandika juu ya uhusiano uliopo kati ya pesa na thamani. Thamani ya kitu chochote ndiyo pesa ambayo mtu huwa tayari kulipa endapo anahitaji kitu hicho. Kwahiyo, ni sahihi tukasema kuwa “thamani ni pesa”.
SOMA; Mafanikio Yako Yamejificha Ndani ya Thamani
Katika ulimwengu wa biashara, watu wengi utumia pesa kama chombo cha kubadilishana thamani zilizopo ndani ya bidhaa na huduma. Ikitokea kwamba bidhaa na huduma nyingi mnazobadilishana kila siku ni za nje ya nchi, kwa vyovyote vile lazima mtakuwa mnafanya kazi ya kushusha thamani ya pesa yenu wenyewe.
Kwa kawaida ni kwamba thamani kama thamani siku zote, huwa imefungiwa ndani ya bidhaa au huduma. Kimsingi kinachonunuliwa na watu siyo bidhaa kama bidhaa au huduma BALI watu ununua “Thamani”. Kwa mfano: mtu anaponunua nguo siyo tu nguo bali ni thamani ya nguo ambayo yaweza kuwa ni kujistili, kujikinga na baridi, kupendeza, kuonekana mpya n.k. Ndiyo kusema kwamba nguo fulani itakuwa ya thamani kubwa kwa mtu, endapo itakuwa na uwezo wa kukidhi lengo au hitaji la muhusika.
Thamani za bidhaa na huduma zetu, haziwezi kuwa kubwa kama sisi wazalishaji wake hatuna mkakati wa kujiongeza thamani mara kwa mara. Ili tuweze kutengeneza thamani kubwa lazima sisi tuwe wa thamani kubwa kwanza. Kama hatufanyi jitihada zozote za kuongeza thamani tuliyokwisha kuwa nayo, ni wazi kwamba thamani yetu itabaki ile ile miaka yote au itazidi kushuka kadiri miaka itakavyozidi kwenda mbele - Shilingi ya Tanzania nayo itashuka!.
Thamani yako kwenye jamii inaongezeka au kupanda kwa kujifunza mambo mapya kila siku. Unapokuwa mtu wa kujifunza, unapata nafasi hadimu ya kukuza ubunifu wako. Ubunifu hasa wa kuweza kutatua changamoto zilizopo kwenye jamii, ndiyo unakuwezesha kutengeneza na kuzalisha thamani ambayo wewe na watu wengine wataitumia kutatua changamoto zao kwa wepesi na haraka zaidi.
Kujifunza kila siku ndio kunakuza na kuendeleza mawazo ya kiubunifu. Wazo lolote la kiubunifu linapofanyiwa kazi huwa linazaa “suruhisho” za changamoto mbalimbali zinazo ikabili jamii au dunia kwa ujumla.
Ili mawazo mapya na mazuri yaweze kutoka vichwani mwetu lazima kuhakikisha tunafanya kila linalowezekana kuilisha akiri yetu kwa kufanya jitihada za kujifunza kila siku. Endapo tutafanya hivyo, basi tutazaliwa upya na kuwa watu wenye fikra mpya. Hizi zitakuwa ni fikra zenye uwezo wa kujibu au kukabiliana na changamoto mpya - Umaskini wa kipato!!!.
Wananchi kutoka nje ya nchi (Ulaya, Marekani, Asia) na nchi chache kutoka Africa (Africa Kusini, Ghana, Ethiopia, Kenya na Botswana n.k), wanajitahidi sana katika kujiongeza thamani kupitia matokeo ya tafiti mbalimbali – wanasoma sana; wamejenga utamaduni wa kujihoji kila wakati, wanajitathimini mara kwa mara.
Matokeo ya tathimini ndiyo wanayatumia kupandisha thamani kwa kufanya mambo yaliyo bora kuliko siku za nyuma. Tathimini na kujifunza vinawawezesha kufanya vizuri leo kuliko jana – Thamani yao inapanda kila siku….!
Ebu fanya tathimini ya haraka haraka: Mwaka 2015 umepita, je? umefanya jambo gani jipya na ni watu wangapi walinufaika na jambo hilo?.... Kama hakuna jipya ulilofanya, basi ujue moja kwa moja kuwa thamani yako imeshuka.
Wananchi waliowengi (nje ya nchi) wamejijengea uwezo mkubwa wa ubunifu. Kuwepo kwa ubunifu mwingi ngazi ya mtu binafsi, ndiko kumesaidia sana katika kuziambukiza taasisi zao “Ubunifu” na hivyo kuzifanya ziweze kuzalisha bidhaa na huduma bora zaidi – Za thamani kubwa!.
Kutokana na kujikita kwa ubunifu ndani ya akiri za watu katika nchi hizo za nje, kumekuwepo na hali ya upatikanaji wa SURUHISHO za changamoto kwa haraka. Kwa maana nyingine ni kwamba, watu hawaandamwi na changamoto kwa muda mrefu – Wanawahi kupata suruhisho!.
Kwakuwa na sisi hapa Tanzania tunakabiliwa na changamoto nyingine kama zao, basi inatubidi tuziache pesa zetu kwa kununua pesa zao, ili angalau zituwezeshe kununua suruhisho mbalimbali kutoka nje ya nchi, ili zitusaidie kutatua changamoto tulizonazo – Shilingi ya Tanzania inashuka thamani wakati pesa yao inapanda thamani.
Kwa maana nyingine ni kwamba changamoto ndizo zinatengeneza mahitaji. Kwahiyo yeyote anayewahi kuleta suruhisho, ndiye huyo atakayeweza kujipatia pesa kutoka pande zote za dunia.
Kadili watu au nchi itakavyokua inawahi kutoa SURUHISHO za changamoto mpya ndivyo itauza thamani (suruhisho) kwa watu wengi zaidi. Tukiwahi kutengeneza thamani mpya, watu wengine wakija kuiga kutengeneza thamani kama zetu, sisi tutakuwa tunafikiria kutengeneza vitu vingine vipya.
Ebu jiulize kama tungefikiria mapema na tukawa wa kwanza kupata na kulifanyia kazi wazo la kutengeneza njiti za kuondoa mabaki ya vyakula kwenye meno (tooth picks), tungekuwa tumetengeneza thamani kiasi gani kwenye jamii?.
Jiulize hata kama tungeamua kuuza kwenye nchi za Afrika Mashariki peke yake tungekuwa tumeuza pesa ngapi hadi sasa. Jaribu kupata picha ya thamni ya njiti za meno, kwa maana ya jinsi zinavyohitajika na kutumiwa kila siku na mamilioni ya watu. Kama hivyo ndivyo, ni kwanini shilingi ya Tanzania isipande thamani?.
Watanzania lazima tukuze ubunifu, kwani huu ndio utakuwa chimbuko la suruhisho za changamoto zinazowakabili watu wengi. Unapofanikiwa kubuni suruhisho mbalimbali za kero na changamoto zilizopo kwako binafsi au kwa watu wengine ndiyo thamani yako inapanda na kuwa kubwa. Ukweli ni kwamba, ili kitu fulani kiwe cha thamani kubwa ni lazima kiwe kinagusa maisha ya watu wengi wakiwamo watu wa nje ya nchi yetu.
Ikiwa watu walioko nje ya nchi yetu watavutiwa na kuoyesha mahitaji yao makubwa ya thamani za bidhaa na huduma tunazozalisha hapa Tanzania; basi wahitaji wa thamani kutoka Tanzania wataanza kutafuta shilingi ya Tanzania kwa lengo la kutaka kupata pesa yetu, ili iwasaidie katika kujipatia bidhaa na huduma zenye thamani inayokidhi mahitaji yao. Mazingira haya ndiyo yatafanya wageni wengi kuacha pesa nyingi za kigeni hapa nchini kwa lengo la kujipatia thamani (bidhaa na huduma) zinazopatikana hapa hapa Tanzania. Kadili mchakato huu utakavyozidi kuimarika, ndivyo tutakavyozidi kushuhudia shilingi ya Tanzania ikipanda kwa kasi ya ajabu.
Kwahiyo, ifike mahala tutambue kwa pamoja kuwa suala la kupandisha thamani ya pesa halitokei hivi hivi. Kupanda kwa thamani ya pesa ya nchi ni mchakato unaojumuisha jitihada za kuongeza thamani zinazofanywa na mtu mmoja mmoja.
Kiukweli ni kwamba thamani ndani ya bidhaa na huduma tunazotumia kila siku zinatokana na fikra au akiri za watu binafsi na si vinginevyo. Na sasa ninasema : “Katika ulimwengu wa biashara, shilingi ya Tanzania haiwezi kupanda zaidi ya thamani yetu sisi".
Watanzania wote tulio na umri wa kutafuta riziki, tutambue kuwa suala la kupandisha thamani ya shilingi ya Tanzania ni letu. Kila mmoja ajikite katika kujiongeza thamani binafsi, shilingi itapanda yenyewe. Suala la kupandisha thamani ya pesa halianzi na jumuia wala taasisi, linaanza na wewe.
Hakuna binadamu atakayekuzuia kupanda thamani, isipokuwa wewe mwenyewe. Thamani ya shilingi haiwezi kushuka bila sisi kuwa tumeshuka thamani wenyewe. Kwahiyo, badala ya wewe kuongelea kushuka kwa thamani ya shilingi, jiangalie na jipime wewe leo unaonaje thamani yako miaka miwili iliyopita ikoje, ukilinganisha na sasa hivi?
Kila mmoja wetu afikirie zaidi kujiongezea thamani kuliko kufikiria waziri kuongeza thamani ya shilingi. Kama thamani yetu wenyewe itaongezeka, ni lazima thamani ya pesa itaongezeka tu….!
Leo saa imefika, kila mmoja wetu aongeze thamani yake popote alipo na kwa umoja wetu tutapandisha thamani ya shilingi ya Tanzania.
Jitahidi kuwa karibu na mtandao wa MAARIFA SHOP Kwa kubonyeza neno “KARIBU”, Kama njia muhafaka ya kuendelea kujifunza mbinu madhubuti za kuongeza “thamani” katika maisha yako.
No comments:
Post a Comment