Friday, April 22, 2016

Siri ya Watu Kupenda Mikate Imefichuka



“Kama pesa ni kazi iliyoisha, wewe pesa yako kazi yake imefanywa na nani?” ~ Cypridion Mushongi
Jumapili ya tarehe 17/04/2016…nilikuwa nyumbani nasikiliza mziki wa injiri, mara tu ukapigwa wimbo wa “Mikate” ambao umeimbwa na “AIC Chang’ombe Vijana Kwaya”. Katika wimbo huu waimbaji wanasikika wakiimba kuwa “Watu Wanapenda Mikate” . Wimbo huu umebeba ujumbe mzito na unaeleza..... jinsi ambavyo watu wanatumia mikate kuhonga wengine, ili kujipatia upendeleo wa kila aina.

Katika wimbo huu, wanakwaya wametumia bidhaa ya mkate kupeleka ujumbe kwa jamii juu ya namna ambavyo watu wengi wanavyotafuta “PESA” kwakutumia njia za haramu, kiasi kwamba wengine wako tayari kuua, kusaliti n.k binadamu wenzao ilimradi tu wamepata pesa.

Kitendo cha baadhi ya watu kutafuta pesa kwa njia zisizo halali kinaonyesha kuwa watu wengi tuna mapenzi makubwa na pesa – kumbuka kupenda pesa siyo dhambi. Hoja ya msingi hapa ni kwanini watu wanapenda pesa (mikate) zaidi kuliko kitu chochote?

Mikate ni bidhaa kama bidhaa zingine na inapatikana baada ya mchakato maalum kufanyika na kukamilika. Katika mchakato wenye shughuli mbalimbali za kuzalisha mikate, utaona kuwa mikate inakuwa ni kitu cha mwisho kutokea. Baada ya mikate kuzalishwa kinachofuata cha zaidi ni kuitafuna basi, alafu ikiisha tunaanza kazi ya kutafuta mikate mingine.

Kwahiyo, inatosha kusema kuwa MIKATE ni sawa na PESA. Kama ambavyo mikate katika mchakato wa usindikaji ni kitu cha mwisho kutokea au hitimisho la kazi ya usindikaji wa ngano, basi pesa nayo ni hivyo hivyo.

Pesa yoyote tuliyonayo ni matokeo ya kazi fulani fulani na kwa maana hiyo, siyo kitu kinachoweza kupatikana kwa ghafla. Ni lazima kuwe na mchakato unaotokana na utekelezaji wa shughuli mbalimbali. Shughuli zote katika mchakato zinapokuwa zimekamilika ndipo pesa inatokea kama zao!

Mchakato wa kutafuta pesa unahitaji mambo gani?
A. Muda na Uvumilivu: Ili pesa ipatikane, inahitajika MUDA kutegemea ni pesa kiasi gani unatafuta – Ni nani yuko tayari kusubili?. Uzoefu umeonyesha kuwa pesa nyingi (ya bila kikomo) inachukua muda mrefu kabla ya kupatika na ukweli ni kwamba, mchakato wake unazo shughuli nyingi ambazo zinahitaji muda mwingi kukamilika. Kutokana na ukweli huu juu ya uhitaji wa muda katika kutafuta pesa, inatosha kusema kuwa kusubili pesa mpaka ipatikane inahitajika “Uvumilivu” wa hali ya juu - Nani yuko tayari kuvumilia hizo zinazoitwa shida?.

Katika ulimwengu wa sasa, ni watu wachache sana ambao wako tayari kuvumilia, na kwa maana hiyo hawako tayari kusubili. Kama wewe siyo mtu wa kusubili mchakato wa pesa ukamilike, basi ujue wewe utapenda kufuata njia ya mkato ambayo matokeo yake huwa siyo mazuri kabisa.

B. Kulipia Gharama Kabla: Mchakato wa kuzalisha bidhaa na huduma ambazo hatimaye uzaa pesa, unahitaji kulipa gharama, ili uweze kukamilika. Lakini, ukweli ni kwamba watu waliowengi hawako tayari kulipa gharama za kuendesha mchakato wa kuzalisha PESA. Kupata matokeo ya pesa inakulazimu kulipa gharama zote kabla ya kupata pesa hiyo unayoitafuta –“Nani yuko tayari kufanya hivyo”? Ni wachache”.

Kwahiyo, biashara ya kutafuta pesa ni sawa na ule mtindo wa “lipa kabla ya kula”. Mjasiriamali wa uhakika ni yule ambaye yuko tayari kulipa gharama kabla ya kupata, na hata kama hana uhakika wa pesa kupatikana. Tunaposema gharama, hatumaanishi gharama tu zile za pesa, bali ni zaidi ya hapo.

Michakato mingine ya kutafuta pesa nyingi inakutaka wewe kuwa tayari kulipa gharama kabla, ambazo ni kama vile; kutakiwa kuachana na baadhi ya marafiki zako wa karibu, kupunguza au kuacha kunywa pombe, kulala masaa machache, kuamka mapema kila siku, kuwa mbali na familia, kunywa uji usio na sukari n.k.

Uzoefu unaonyesha kuwa, pesa nyingi na hasa ambazo hazina kikomo, zinapatikana baada ya mhusika kufanya kazi na kulipa gharama zote zinazotakiwa mfurulizo kwa kipindi kisichopungua miaka mitatu hadi mitano; pia kuna michakato mingine ya kupata pesa ya uhakika inahitaji kuendelea kulipa gharama mpaka muda wa miaka 10 na kuendelea kutegemea na ukubwa wa ndoto ya mhusika.

Niambie wewe uko tayari kulipa gharama kama hizo kabla? hata kama huna uhakika wa kupata pesa tarajiwa? – Hakika ni watu wachache ambao wako tayari kulipa gharama kabla ya kupata pesa nyingi. Ndiyo maana wamechagua kutafuta pesa kidogo kidogo ili maisha yaende.

C. Maarifa: Mchakato wa kupata pesa nyingi una shughuli nyingi ambazo zinahitaji kutumia maarifa ili uweze kupata matokeo ya uhakika. Maarifa mapya ambayo yanakusaidia wewe kupanga na kujiongoza katika kutekeleza shughuli za mchakato wa kutafuta pesa, yanapatikana kwa gharama pia.

Hii ni kutokana na ukweli kwamba maarifa mengi tuliyonayo yanapitwa na wakati kila siku inayopita. Lazima kuwekeza muda na pesa, ili kuboresha au kupata maarifa mapya. Katika dunia ya leo, kama haujishughulishi na kutafuta maarifa mapya juu ya hicho unachopenda kufanya basi ujue kuwa baada ya muda mfupi utajikuta ulikuwa tajiri lakini ghafla unafirisika – unabakia kusema pesa ina siri kubwa!

D. Ubunifu: Kupata pesa nyingi kunahitaji ubunifu wa hali ya juu hasa katika masuala ya uwekezaji. Ubunifu si kitu cha kutazamia bali ni kitu ambacho lazima ufikiri kwanza ndipo ukipate. Hali halisi ya maisha ni kwamba, watu wengi hawapendi michakato ya pesa inayowasumbua akiri zao. Matokeo yake wanaishia kufanya michakato kama ile inayofanywa na wengine wengi. Matokeo yake nao wanapata pesa kama wenzao au pungufu ya wenzao.

Unapofikia hatua ya kupokea pesa kama pesa unakuwa umepokea “kazi iliyoisha”. Kwa maana hiyo, uhitajiki tena kufuata mchakato wa kusubili, kuvumilia, kulipa gaharama kabla n.k, kama mwanzo. Ukiona watu wanashangilia wanapopata pesa hasa ambayo hawajaifanyia kazi, basi ujue kuwa wanajisikia amani sana kwasababu, wanakuwa wameepukana na kazi kama vile kutenga muda, kulipa gharama kabla, ubunifu, kuvumilia, kusubili n.k.

Kwakuwa pesa ni matokeo ya mchakato, ni wazi kwamba kila mchakato una mwenyewe na kwa maana hiyo, kila pesa ambayo haiko mfukoni mwako ina mwenyewe. Kama wewe ni mtu wa kufuata njia za mkato kila mara, ili kupata pesa basi ujue kuwa kutajirika kwako ni muujiza. Kwasababu, wale wote wenye pesa zao watakuwa kama ukibahatika wanakupa pesa kidogo sana na kwa muda ambao wanajisikia kufanya hivyo bila kujali shida zote ulizonazo.

Kwa upande mwingine, pesa unayopata kwa kukwepa mchakato wa upatikanaji wake, ni vigumu sana kubaki nayo, kwasababu pindi unapoitumia ikaisha, huwezi tena kupata pesa nyingine mara moja. Hii ni kutokana na ukweli kwamba wewe unayepata pesa nje ya mchakato wake unakuwa huna umiliki wowote wa mchakato huo. 
 
Unapoanzisha na kumiliki mchakato wa kuzalisha pesa ni kwamba ikitumika ikaisha, basi mchakato wako unaoumiliki unazaa tena pesa nyingine. Kwahiyo, unaendelea kuvuna pesa nyingi bila kikomo – Huku ndiko kutajirika!

Tunahitaji kutambua kuwa matajiri wengi duniani walianzisha na kusimamia michakato ya kuleta pesa. Ndiyo maana wengine pamoja na kwamba walishafariki, bado ile michakato waliyoianzisha na kuijenga mpaka leo inaendelea kutoa pesa.

Sasa imefika zamu yako kuanzisha na kujenga michakato ya kudumu ya pesa. Na huu ndio wakati muhafaka wa kujitoa kwenye kundi la wapenda “pesa au mikate” ya bure. Jijengee tabia kama ya matajiri ambao upendelea zaidi michakato ya kuleta pesa kuliko pesa yenyewe.

Kama uko tayari kuanzisha na kumiliki michakato ya kuleta pesa bila kikomo, jitahidi kuwa karibu na mtandao wako wa MAARIFA SHOP kwa kubonyeza neno “KARIBU” ili kuwa kwenye kundi kubwa la watu ambao wameamua kuendelea kujifunza namna bora ya kujiletea mafanikio makubwa maishani.

No comments: