Wednesday, May 25, 2016

Hii Ndiyo Hasara ya Kulipa Kwanza Watu Wengine


“Unapopata pesa ukatenga akiba kwanza, tunasema umejilipa kwasababu pesa hiyo imebaki kwako na ndiyo mbegu ya kuzalisha pesa nyingi zaidi” ~ Cypridion Mushongi
 
Watu wengi tunajua kuwa ukishafanya kazi ya mwajiri kinachobakia ni kulipwa mshahara au ujira, nje ya hapo hatuna habari. Ukilipwa na mwingine unafurahi sana. Furaha unayoipata ukiwa umelipwa mshahara, pengine ndiyo inakusukuma kutumia mara moja kipato chako kila unapolipwa. Hali hii ya kufurahia kulipwa pesa na wengine ndiyo imezidi kutuweka utumwani maisha yetu yote.

Kila tunapolipwa pesa, kazi yetu ya kwanza huwa ni
kujipatia mahitaji na kulipa madeni (kutumia) basi! Tunatumia pesa inaisha ndipo tunatafuta pesa nyingine. Yaani inakuwa ni kama mchezo wa “paka na panya”.

Ukweli ni kwamba, paka anapomuwinda panya na kufanikiwa kumkamata, mara moja biashara ya kutafuta panya mwingine huwa inaishia hapo hapo. Na panya aliyekamatwa akishaliwa, ndipo paka anapata wazo la kutafuta panya mwingine.

Ebu jiulize wewe binafsi ni kitu gani ambacho huwa unafanya kwanza pindi unapoingiza pesa mfukoni? Twambie unapokuwa umepokea mshahara; umefanya biashara umepata faida; umepata zawadi kutoka kwa wazazi, watoto au marafiki huwa kwanza unafanya nini?. Birashaka utaniambia matumiziya kifamilia au yako binafsi. Ukiniambia matumizi ninakuelewa, kwani hata mimi nilizoea kufanya hivyo __ kutumia!.

Imekuwa kawaida yetu wengi tunapopata pesa huwa tunaanza na kutumia (kujipatia mahitaji na kulipa madeni), kabla ya kufanya kitu kingine. Mara nyingi tunawahi kununua vitu ambavyo tunadhani ni muhimu wakati siyo muhimu. Kwasababu, hatuwezi kudhurika wala kuathirika tukivikosa __ na hakuna ulazima wa kuvipata leo leo.

Tukishapata pesa tunajikuta tuna mahitaji mengi ambayo tunataka pesa yoyote tuliyopata itumike mara moja kuyatimiza. Jiulize kabla ya kupata hiyo pesa, mbona ulikuwa huna shauku ya kupata hayo mahitaji unayoyaita ya muhimu? Ina maana wewe kwako matumizi yanaonekana kadiri unavyopata pesa? Niambie, hayo matumizi yalikuwa wapi kabla ya hapo?. Jaribu kulifanyia kazi hili, lisije likawa ndicho kizingiti cha wewe kukosa mtaji wa kufanya vitu vyenye kukuletea pesa nyingi hapo mbeleni.

Wajasiriamali pamoja na wawekezaji waliobobea wanatwambia kwamba “haijalishi unapata pesa kiasi gani, BALI ni kiasi gani unakaa nacho”. Watu wengi tunajitahidi kutafuta pesa na Mungu mara zote ameweza kutujalia tumepata, lakini shida yetu kubwa ni kushindwa kukaa na pesa.

Tunahitaji kuweza kuitunza pesa kwa muda, kabla ya kufanya maamuzi yoyote juu yake. Hii itakuwa ni hatua muhafaka sana kwa yeyote ambaye ana dhamira ya dhati ya kufikia uhuru wa kipato ambao ni endelevu au kipato bila kikomo.

Jenga utamaduni wa kuhakikisha kila unapopata pesa yoyote, itunze kwanza japo kwa muda fulani kabla hujakimbilia kufanya matumizi ya aina yoyote ile. Waweza kuiweka sehemu utakayoona ni salama kama vile benki.

Katika kipindi hicho ambacho utakuwa umeamua kutunza pesa zako, endelea na maisha yako uliyokuwa nayo kabla ya kupata hizo pesa. Jitahidi, kuendelea na maisha yako kana kwamba huna pesa uliyotunza. Yawezekana wakati ukiendelea kutunza pesa, kuna kitu cha thamani ambacho unatamani kukinunua na ukiangalia pesa uliyotunza unaona kabisa bei yake iko ndani ya uwezo wako; lakini husifanye hivyo, kwasababu pesa yako itakuwa kwenye kipindi cha kutunzwa au kuhatamiwa.

Suala la kutunza au kuhatamia pesa kwanza kila unapoipata, yawezekana lisieleweke kirahisi. Lakini nia na madhumuni ya utaratibu huu ni kutaka wewe ujenge nidhamu ya pesa, ili hatimaye uwe mtu mwenye uwezo mkubwa wa kuimiliki au kuiendesha pesa __ na sio wewe kumilikiwa au kuendeshwa na pesa.

Kuna watu ambao wakiwa na pesa utawajua tu! wanakuwa na furaha sana, wanachangamka zaidi, na pia utawaona wakitembelea sokoni na madukani, huku wakinunua hiki na kile. Watu wa namna hii, unakuta hawana muda wa kutulia mpaka pesa hizo ziishe. Kwao ni mpaka pesa ziwaishie ndipo wanapata upya akiri nzuri ya kufikiria maendeleo.

Ukweli ni kwamba, kila tunapopata pesa tunashawishika kuitumia, matatizo ndio yanajitokeza, mara tunaona vitu vizuri n.k. Hali hii ndiyo uletaa tabia ya kupendelea matumizi kwanza kabla ya kutenga Akiba.

Ni muhimu kujiwekea akiba kila upatapo pesa. Ili kujenga tabia ya kuweka akiba ni lazima ujizoeshe kwanza kukaa na pesa kwa muda, bila kufanya chochote au matumizi yoyote. Ukishakuwa umeweza hilo, hatua ya pili ni kuanza utaratibu wa kutenga asilimia fulani kama akiba. Suala hili la akiba ndilo linatakiwa kupewa kipaumbele namba moja pindi tupatapo pesa yoyote ile.

Kwa maana nyingine ni kwamba, tunatakiwa kupanga matumizi kwa pesa le tu inayobaki baada ya kutoa akiba. Utaratibu huu wa kutenga akiba kwanza ndio tunaita kujilipa kwanza kabla ya kulipa watu wengine. Hapa unatakiwa utofautishe “kujilipa mshahara” na “kujilipa kwanza”.

Unapopata pesa na ukatenga akiba kwanza, tunasema umejilipa kwasababu pesa hiyo imebaki kwako na ndiyo mbegu ya kuzalisha pesa nyingi zaidi.

Lakini, ukipata pesa ukaenda kununua mahitaji yako au kulipa madeni uliyokuwa nayo kwanza, basi ujue kuwa moja kwa moja umefanya kazi ya kulipa watu wengine kwanzakabla ya kujilipa wewe. Tabia hii ya kulipa watu wengine kwanza kila mara tunapopata pesa, ndio imetufanya tuwe maskini hadi leo. Pia, tabia hii ni mbaya na inasemekana ndiyo imechangia kwa kiasi kikubwa kuzalisha maskini wengi duniani.

Kama wewe ndio kwanza unaanza safari yako ya kuelekea kwenye utajiri, niseme hakuna namna, ni lazima ujifunze kuwa na tabia hii nzuri ya kujilipa kwanza wewe kabla ya kutumia pesa kwa mambo mengine.

Anza leo kutumia kanuni hii ya kutenga akiba kwanza na matumizi mengine ndiyo yafuate. Kwa ufupi ni hivi: pata pesa, itunze kwanza kwa muda, halafu kabla ya kuitumia tenga akiba kwanza, baada ya hapo fanya matumizi yako ya muhimu na kisha zinazobaki fanya mambo yako ya anasa. Jaribu kuishi kwa utaratibu huu mpaka pale utakapoona umewekeza vya kutosha katika miradi inayokuletea mapato makubwa yasiyokuwa na kikomo.

Kwakuwa pesa siyo hesabu ni tabia, unahimizwa kujifunza kwa hali na mali tabia hii ya “kujilipa kwanza”, halafu mambo mengine mazuri yatafuata, endapo utaanza leo.

Ili kujfunza tabia ya kutafuta, kumiliki na kendesha pesa, usiishie tu kusoma makala hii, bali ujenge utamaduni wa kujisomea masuala ya pesa na biashara hasa kupitia mtandao wako wa http://maarifashop.blogspot.com.

Hapa utakutana na makala nzuri zitakazozidi kukufungua akiri na hatimaye kuharakisha safari yako ya kwenda kwenye mafanikio makubwa.

Pia, kwaajili ya kupata makala hizi pamoja na mafunzo mbalimbali kupitia e-mail yako unaweza kujiunga na mtandao wa MAARIFA SHOP kwa kubonyeza neno NITUMIE MAKALA...

No comments: