- Afya Bora Ndiyo Machimbo ya Kudumu ya “Pesa” tuliyonayo!
- Watu Wengi Bado Wanaamini Kuwa Kitu Kinachoitwa “Afya” Kitajileta Chenyewe!
Katika
maisha ya siku hizi inashangaza sana kuona kuwa pesa tunazotafuta zimekuwa zimekuwa
adui yetu mkubwa wa miili na afya yetu kwa ujumla. Ndiyo maana leo hii, watu
wengi “wanakula dawa kama chakula badala
ya kula chakula kama dawa”. Maana yake ni kwamba, watu wengi wanayo pesa
lakini, Asilimia kubwa inatumika kununua dawa ili waweze kusogeza maisha yao
mbele. Mwanaharakati mmoja kutoka bara la Asia aliyejulikana kwa jina la “Dalai Lama”, alipoulizwa kitu ambacho
kiliwahi kumshangaza zaidi kuhusu ubinadamu, alijibu kuwa ni Binadamu:
“Kwasababu,
binadamu anatoa afya yake sadaka, ili kutafuta pesa. Alafu anatoa pesa yake
sadaka, ili kurudisha afya yake. Na sasa anaanza kuhofia juu ya mstakabari wa
maisha yake ya baadae (future), kiasi kwamba anashindwa kufurahia maisha
yaliyopo wakati huu; Matokeo yake ni kwamba mtu huyu hawezi kuishi wakati huu
(uliopo) au ujao; anaishi kama vile hatakaa aje kufa na alafu anakufa kama vile
hakuwahi kuishi”
Maono
ya mwanaharakati huyu yanatuonyesha kwamba, muda mwingi wa maisha yetu
hatufanyi kitu chochote kinachohusu afya zetu isipokuwa tunaelekeza nguvu,
ujuzi, maarifa na rasilimali nyingine kwenye mambo tu ya kutafuta pesa peke yake.
Fikra za waliowengi ni kwamba bado wanaamini kuwa kitu kinachoitwa “afya”
kitajileta chenyewe, ilimradi uwe na pesa, na wengine wasiojua wanaamini katika
“Pesa Kwanza na Afya Baadae”.
Kwa
sasa hali ya afya kwa waliowengi siyo nzuri, na hii ni kutokana na kutokuwa na
malengo na mipango inayohusu afya. Mipango mingi inalenga zaidi kujiendeleza kiuchumi,
kielimu, kujenga nyumba nzuri, kuongeza uzalishaji, kununua magari n.k. Ni watu
wachache wenye kuwa na malengo na mikakati ya kujenga na kuimalisha afya zao. Mara
nyingi, watu wanakumbuka kujali afya zao pale wanapougua au kuanza kusikia
maumivu. Wataalam na wadau wengine wa masuala ya afya, wanatwambia kwamba, pale
unapoanza kujisikia maumivu ndani ya mwili au kuumwa kabisa, basi ujue kuwa umechelewa
kula chakula kama dawa.
Mara
nyingi, imekuwa ni kawaida kuletewa chakula bora pale tunapokuwa tayali tunaumwa
na kulazwa hospitalini, ndiyo maana ukitembelea wagonjwa, unapishana na watu
wakipeleka machupa makubwa ya jwisi na matunda ya kila aina. Vyakula hivi ambavyo
tunaletewa tukiwa wagonjwa, hakuna mtu anayeweza kukuletea tena nyumbani kwako
ukiwa mzima, kwasababu, ni matarajio yetu kuwa, ukisharudia hali yako nzuri
kiafya, utachukua jukumu la kuendelea kujali afya yako wenyewe. Lakini, cha
ajabu, hatufanyi hivyo mpaka tunapoletewa vyakula kwa mara nyingine, pindi tunapougua
tena!. Ukweli ni kwamba, jambo la kuimalisha na kulinda afya zetu
tumelichukulia la mzaa sana. Kwahiyo, ni muhimu sana tukatambua kuwa mafanikio
makubwa tunayotafuta kwasasa yataweza kufikiwa kwa haraka iwapo tutazipa afya
zetu kipaumbele namba moja, nje ya hapo maisha bora yatabaki kuwa ndoto ya
milele.
Ukitafakari
kwa kina sana, utagundua kuwa afya bora ndiyo machimbo ya kudumu ya “Pesa” tuliyonayo. Afya bora ndio
utupatia rasilimali “nguvukazi”na
pindi nguvu kazi yetu tunapoiwekeza kwa ufanisi hasa katika shughuli za
uzalishaji ndipo tunapata bidhaa au huduma ambazo watu wengine utoa na kuleta pesa
kwetu, ili kujipatia bidhaa/huduma husika. Pesa ndiyo utuwezesha kupata mahitaji
yaliyo mengi kwa muda tunaoutaka na hatimaye kufikia maisha bora ambayo ndiyo
ndoto yetu ya muda mrefu.
Kwakuwa,
pesa tuipatayo, chimbuko lake ni afya bora, ni muhimu kwa kila shilingi ya pesa
tunayoipata, mgao wa kwanza uelekezwe kwenye kuimalisha na kulinda afya.
Tunasema suala la matumizi ya pesa kwenye afya, liwe ndio kipaumbele namba moja
kwasababu afya ndiyo kisima chetu cha pesa. Unapoamua kutenga pesa kwaajili ya
afya yako, maana yake ni kwamba unazifanya pesa zako kuwa rafiki mkubwa wa
mwili wako. Pesa zinakuwa rafiki yako pale unapozitumia kujenga, kuimalisha na
kulinda afya yako kwa ujumla. Pesa haziwezi kuwa rafiki wa mwili wako, kama
hazijatumika kulisha chembe hai za mwili kupitia ulaji wa vyakula na
virutubisho muhimu. Nje ya hapo, chembe hai za mwili wako hazina uhusiano na na
pesa yako iliyoko mfukoni, benki au kwenye miradi yako ya biashara.
Wito
kama unataka mafanikio makubwa anza sasa kuweka malengo ya kupata afya njema na
kipato. Ni muhimu vitu hivi viwili viende pamoja kwasababu katika maisha ya Ujasiriamali,
vinategemeana sana na vinapoungana ndiyo tunapata furaha ya kweli. Kwahiyo,
jitahidi sana kujali afya wakati wote wa safari yako ya kusaka mafanikio ili
ukifika maisha ya ndoto yako uwe una afya njema na hapo utafurahia zaidi kuliko
anayeumwa kwasababu aliunyima sana mwili wake wakati wa safari ya kusaka
mafanikio.
Mpendwa msomaji, endelea kuitumia vizuri MAARIFASHOP ili kujifunza mambo mbalimbali yatakayokuwezesha kupata mafanikio. Ili kupata makala mpya kila zinapochapishwa, bonyeza neno TUMA MAKALA MAARIFASHOP kisha sajiri barua pepe yako. Na kama unapenda kupata mafunzo ya kila siku kwa njia ya whatsap bonyeza neno MAFUNZO.
No comments:
Post a Comment