Saturday, June 6, 2015

Elimu ya Ajira Haiwezi Kukupa Kazi

http://maarifashop.blogspot.com
  • Zaidi ya Asilimia 90% ya Watu Wenye Utajiri Mkubwa Walitafuta Pesa Nje ya Mfumo wa Ajira....Maana Walitengeneza Kazi!.


Katika makala ya “Ajira Siyo Kazi ni Ajira na Kazi Siyo Ajira ni Kazi.... niliandika kuhusu tofauti iliyopo kati ya kazi na ajira, ambapo tuliona kuwa kazi” ni majumuisho ya majukumu mbalimbali uliyojipa wewe mwenyewe kazi, unajisimamia na kujiwajibisha mwenyewe kutimiza majukumu uliyojipa mwenyewe bila kutegemea kulipwa chochote mpaka matunda ya kazi hiyo yapatikane, hata kama ni muda mrefu (mwaka na zaidi). Na tuliona kuwa “Ajira” ni kufanya kazi ambayo siyo ya kwako, waweza kuwa unaipenda au huipendi. Kwa maana nyingine katika ajira unapangiwa majukumu maalum ya kufanya na mwenye kazi, ukiyakamilisha basi umemaliza kazi, zaidi ya hapo yanayobaki hayakuhusu.

Ukifuatilia kwa undani zaidi juu ya mfumo wa elimu duniani, utagundua kuwa mfumo huu umetujenga katika mtazamo wa kutafuta na kupata “AJIRA” badala ya “KAZI”. Kama hivi ndivyo, basi tujue kuwa tumepata elimu ya yale tu! ambayo wenye kazi wanayataka na lengo lake likiwa ni moja tu “kupata watu watakaomudu majukumu ambayo watapangiwa na wenye kazi. Haijalishi  kama elimu hii inazingatia maslahi na matakwa yako, ukishindwa unatupwa nje na kubatizwa jina la “huna akiri na wewe uliyepatwa na mkasa huu ukilikubali tu jina hili, umekwisha!.

Ukifahuru usijisifu sana na wala ukishindwa usijilaumu wala kuumia sana, kwani unapofahuru ni sawa na kusema “umekuwa mahili katika kujua yale tu kwa kiasi kikubwa wanayoyataka wengine”. Lakini tukumbuke kuwa yale wanayoyataka ni mambo machache sana ukilinganisha na yale yote unayoyahitaji ili kupata maisha ya ndoto yako. Unapokuwa umeshindwa tunasema husiumie sana kwasababu yawezekana yale uliyoyajua na kuyapenda kuyasoma hayakuwa mengi na hayakufundishwa kwasababu tu hayakuwa katika orodha ya yale wanayotaka wenye kazi. Kwahiyo, unaposhindwa mtihani usivunjike moyo bali huendelee kujiona kuwa wewe ni mwenye akiri nyingi na unaweza vitu vingi, isipokuwa vitu hivyo abavyo unaviweza, bado vingi haviko kwenye mitahala ya elimu rasimi ambayo umeshidwa. Habari njema ni kwamba, vitu hivyo unavyovijua vizuri, ukivitumia unaweza kutengeneza kazi kubwa yenye kukuletea matunda mengi sana, ambayo watu watakuletea pesa nyingi ili ujipatia matunda hayo.

Ukiwa wewe ni msomi, utakubaliana na mimi kuwa iwapo ukiamua kwenda nje ya mfumo wa ajira utagundua kuwa mambo mengi yaliyoko nje ya ajira ni tofauti kabisa na yale tuliyonayo vichwani mwetu na hasa sisi wenye shahada kutoka vyuo vikuu. Kumbe yale mambo ya nje ya ajira nayo yanahitaji kujifunza upya bila kujali kuwa wewe una cheti au shahada. Lakini, masomo ya nje ya ajira yenyewe hatuingii darasani bali tunajifunza kwa kuanza kufanya kile unachotaka kujifunza. Masomo ya mfumo wa nje ya ajira unanikumbusha maneno aliyowahi kuyasema mtaalamu wa zamani katika fani za hisabati na fizikia bwana Albert Einstein kuwa “ELIMU ni kile kinachobaki baada ya kuwa umesahau yale uliyofundishwa shuleni”. Hapa kwetu Tanzania, hali ni mbaya kwa maana yale tuliyofundishwa shuleni na vyuoni mengi hayatumiki nje ya mfumo wa ajira. Matokeo yake tunajikuta tunasahau mambo mengi, huku tukibakiza elimu kidogo sana, kitu ambacho kinafanya wasomi wengi kuishi maisha duni ambayo siyo maisha ya ndoto zetu.

Ukizingatia maneno ya Bwana Albert Einstein ni dhahiri kwamba, elimu iliyobaki vichwani mwetu ni kidogo, kiasi kwamba haiwezi kututoshereza kukabiliana na changamoto nyingi ambazo ziko nje ya mfumo wa ajira. Kwahiyo, wakati ni sasa ambapo tunatakiwa kuwekeza nguvu nyingi kwenye kujifunza haraka mambo mapya ambayo mengi hatukuweza kuyapata shuleni na kwenye ajira. Aina ya mambo ya kujifunza yatategemea mtu mweneywe pamoja na kazi anayopanga kuitengeneza. Jitahidi kujifunza kwa wale wote ambao wamefanikiwa katika kile unachopanga kukifanya kama wapo. Ili uweze ujifunza kutoka kwa wazoefu unahitaji kujifunza mbinu mbalimbali za kujenga mahusiano na urafiki kwa watu wanaokuzidi au wanaishi maisha yale unayoyataka. Tunahitaji kujifunza kwa kuanza na usomaji wa vitabu na makala mbalimbali, vyote hivi vitakuhamasisha na kukujenga kifikra. Fikra sahihi ndizo zitafungua uwezo wa akiri yako kuona na kuchangamkia fursa mbalimbali za kiuchumi, ambazo zitakuwezesha kupata utajiri au maisha yale unayoyatamani siku zote.

Mwisho! Kumbuka kuwa, karibia asilimia 90% ya watu walio na utajiri mkubwa ni wale waliotafuta pesa nje ya mfumo wa ajira ...... maana walitengeneza kazi!.

Mpendwa msomaji, endelea kuitumia vizuri MAARIFASHOP ili kujifunza mambo mbalimbali yatakayokuwezesha kupata mafanikio. Ili kupata makala mpya kila zinapochapishwa, bonyeza neno TUMA MAKALA MAARIFASHOP kisha sajiri barua pepe yako. Na kama unapenda kupata mafunzo ya kila siku kwa njia ya whatsap bonyeza neno MAFUNZO


No comments: