Sunday, June 28, 2015

Wewe ni Mjasiriamali Lakini Punguza Hili

“Watu wengi tunatumia kitu cha bure “usingizi” kujikosesha fursa hadimu”
“Masaa (muda) tunayotumia kufanya kazi ndiyo pesa yenyewe”
Kitu kinachoitwa “usingizi” ni kitu ambacho kipo siku zote na muda wote, na wakati huo huo ni kitu ambacho unatakiwa kuwa makini nacho hasa kama unataka mafanikio makubwa. Usingizi ni kitu ambacho huwezi ukakitumia kikaisha, kwahiyo, hata ukiukosa kwa muda fulani, bado utaukuta muda wowote ukiutaka. Usingizi” ni zawadi ambayo kila mwanadamu amepewa kiasi cha kutosha na ni kitu ambacho hakina ukomo. 

Habari njema ni kwamba, usingizi wa mtu hauwezi kuibiwa na wala mtu akilala usingizi wake, si rahisi kutumia usingizi wako. Kwa maana nyingine, tunasema kwamba usingizi ni hazina ya kwako peke yako. Usingizi haununuliwi kutoka kwa mtu mwingine, kwasababu kila mmoja ana wa kwake. Usingizi wote tulionao ni kitu ambacho tunakipata bure na itoshe kusema “Mungu aksante kwa zawadi hii ambayo tunapata bure kwa kipindi chote cha maisha yetu”.

Ajabu ni kwamba, “watu wengi tunatumia kitu cha bure “usingizi” kujikosesha fursa” hadimu ya kutafuta maisha ya ndoto yao. Tabia ya kuendekeza usingizi, imesababisha kupoteza muda mwingi, ambao tungeutumia katika uzalishaji na hatimaye kupata kipato. Mara nyingi watu ambao wanaendekeza usingizi na uvivu, ndio hao hao ambao kila kukicha wanalalamika maisha magumu na kibaya zaidi wanawatwisha mzigo wa lawama watu wengine, eti hawakuwajibika ipasavyo!.

Ikumbukwe kuwa, mwili wako usipotumia nguvu katika kazi zenye kuzalisha mali, bado nguvu uliyonayo itatumika kupiga soga, kuangalia runinga, kupiga umbea, kuangalia mpira, n.k. ukishakuwa umefanya vyote hivi, pale nguvu ikikuishia moja kwa moja mwili wako utajisikia kupumzika na hivyo kupata usingizi utakao kulazimu kulala. Hali hii inapojirudia rudia, inakujengea mazoea ya uvivu, jambo ambalo litakukosesha nguvu na uwezo wa kupambana na umaskini.

Mjasiriamali ukishaanza kushindwa kuutawala usingizi wako, basi ujue kuwa mambo mengi mazuri yataanza kukupita. Mfano: unakuta kuna watu wengi wanaofahamu kuwa, ili kulinda afya zao ni muhimu kuamka mapema na kufanya mazoezi, lakini mpaka sasa ni watu wachache wanaoweza kufanya mazoezi masaa yale ya alfajiri. Utakuta mtu anakwambia mimi ninapenda kufanya mazoezi asubuhi lakini, usingizi wa saa kumi na moja huwa ni mtamu, siwezi kuuacha. Mtu huyohuyo, ambaye anashindwa kuacha usingizi wa alfajiri anajikuta akiambulia magonjwa. Ukishakupatwa na magojwa ni wazi kwamba kuna mengine yatakusababishia maumivu makali ambayo, yatakukosesha usingizi ule uliokuzuia mwanzoni kuamka mapema na sasa kuukosa tena kwa gharama kubwa.

Usingizi pamoja kwamba ni kitu kizuri, lakini kinachukua “masaa” yetu mengi ambayo tuna uwezo wa kuyatumia vizuri katika shughuli nyeti za uzalishaji mali. Ikumbukwe pia kuwa, pesa uliyonayo inatokana na muda uliowekeza kwenye shughuli za uzalishaji mali. “Masaa (muda) tunayotumia kufanya kazi ndiyo pesa yenyewe” kwasababu uzoefu unaonyesha kuwa mtu ambaye anaamka na kuanza kazi mapema (alfajiri) kila siku amepiga hatua kubwa sana kimaendeleo kuliko anayechelewa kuamka.

Kwahiyo kama kuna kazi ya muhimu katika maisha yako, acha usingizi ukafanye hiyo kazi, kwani unapomaliza kazi hiyo, utalala usingizi wako kwasababu usingizi ni kitu ambacho kipo na hakipotei kamwe. Tukiendelea kufanya kazi kwa bidii ni wazi kwamba tutapata mafanikio makubwa ndani ya muda mfupi na hapo tutakuwa na fursa na muda wa kutosha sana kulala usingizi. Wewe ndiye mwenye maamuzi juu ya matumizi ya muda na nguvu yako. Chagua kuwekeza muda na nguvu nyingi kwenye shughuli za uzalishaji mali na ufanye maamuzi kwa kuanza leo, maana ujachelewa.  

Mpendwa msomaji, endelea kuitumia vizuri MAARIFASHOP ili kujifunza mambo mbalimbali yatakayokuwezesha kupata mafanikio. Ili kupata makala mpya kila zinapochapishwa, bonyeza neno TUMA MAKALA MAARIFASHOP kisha sajiri barua pepe yako. Na kama unapenda kupata mafunzo ya kila siku kwa njia ya whatsap bonyeza neno MAFUNZO

No comments: