- Unapoamua kuwekeza nguvu kazi yako kwenye shughuli za uzalishaji ndipo unapata bidhaa.
- Unapokuwa na bidhaa/huduma ndipo watu wengine sasa huamua kutoa na kutuma pesa zao kwako, ili kujipatia bidhaa/huduma husika.
Leo hii watu wengi tunahangaika,
tunanungunika na tunalalamikiana juu ya kukosekana kwa pesa. Kila mtu
anamtuhumu mwenzie juu ya hali duni ya maisha. Maisha duni yametokana na kukosekana
kwa mahitaji. Ili binadamu apate mahitaji, kwa sehemu kubwa anahitaji pesa na
hii mara nyingi inatokana na bidhaa au huduma ambazo umezalisha mwenyewe.
Uzalishaji wa bidhaa au huduma zilizonyingi unategemea zaidi matumizi ya nguvukazi,
ambayo chimbuko lake ni afya bora.
Mtu mwenye afya bora, kwa vyovyote vile ni mtu mwenye kuwa na nguvu yakutosha
kufanya shughuli mbalimbali na hasa za kiuchumi. Nguvukazi hatupewi na mtu
yeyote, bali unakuwanayo kwa kuzaliwa ilimradi, uwe na utaratibu wa kujali afya
yako basi!.
Kwakuwa kila mmoja wetu anamiliki na
kuitawala nguvukazi yake mwenyewe, maamuzi ya kutumia nguvukazi yako kwa mtu
mwenyewe. Kuna kundi la watu wanaotumia nguvukazi yao zaidi kwenye “Uzalishaji Pesa” na kuna wengine wanaitumia
zaidi kwenye shughuli ambazo siyo za uzalishaji wa pesa (Non Income Generating Activities ~ NIGA). Hapa Tanzania, bado watu
wengi wanawekeza nguvukazi kubwa zaidi kwenye shughuli zisizo za uzalishaji pesa.
Shughuli nyingi ambazo siyo za uzalishaji pesa, zinatumia sana pesa, hali
inayopelekea watu wengi kutumia kuliko wanavyozalisha pesa. Kama nguvu-kazi
yetu nyingi inawekezwa zaidi kwenye shughuli ambazo siyo za uzalishaji, basi
tujue kabisa kuwa tutapata bidhaa/huduma kidogo, na hatimaye tunaishia kupata pesa
kidogo.
Watu wengi tunataka na tunatamani sana “maisha bora”; maisha ambayo tutakuwa na
uwezo endelevu katika kupata chochote tunachohitaji kama lilivyo kusudio la
Mungu kutuweka hapa duniani. Kwakuwa, maisha bora ndiyo kusudio la watu wengi,
basi inatupasa tubuni mchakato wa maisha bora badala ya hali ya sasa ambayo
tumejikita kwenye shughuli za kutafuta pesa ambazo hazina mpangilio. Kwa sasa ukichunguza
harakati nyingi za kutafuta pesa, unagundua kuwa kila shuguli inajitegemea
kiasi kwamba kukamilika kwa shughuli moja hakuna uhusiano wowote na shughuli
nyingine. Jambo hili la kufanya shughuli ambazo hazina mpangilio maalumu unaolenga
kupata maisha bora, ndiyo linatufanya tukose mwelekeo na hatimaye kushindwa
kuyafikia maisha ya ndoto yetu. Kwahiyo, zoezi la kutafuta pesa na hatimaye
maisha bora ni lazima kulifanya kuwa la ki-mchakato
zaidi kuliko ki-shughuli zaidi. Kupitia
fikra, utafiti, vitabu na hitoria za watu waliofanikiwa; nimejifunza kuwa, ili uweze
kuyafikia maisha ya ndoto yako (maisha
bora) ni muhimu upitie mchakato maalum. Mfano ni kama huu hapa chini:
AFYA BORA NGUVUKAZI BIDHAA
PESA MAHITAJI MAISHA BORA
Ukichunguza mchakato wa kupata pesa hapo
juu unaona moja kwa moja kuwa pesa siyo matokeo ya mwisho ambayo binadamu
anayatafuta bali pesa ni sehemu tu ya mchakato wa maisha bora. Katika mchakato
wa kupata maisha bora, pesa ipo katika nafasi ya nne kati ya vitu sita muhimu
ambavyo vinahitajika kupewa kipaumbele kama unataka kufanikiwa. Mafanikio
makubwa yameshindikana kufikiwa na watu wengi, kwasababu ya kutilia mkazo zaidi
kitu kimoja tu! ambacho ni PESA. Michakato yetu mingi ya kutafuta pesa,
haitilii mkazo vitu vingine kama “afya,
nguvukazi na bidhaa”. Kwa maana nyingine tunaweza kusema kuwa hatupati pesa
kwasababu mara nyingi mchakato wa kutafuta pesa na hatimaye maisha bora “tunauanzia katikati”.
Unapopanga mkakati au mchakato wa
kutafuta pesa na wakati huo huo ukaacha kuzingatia na kujali afya yako, basi
ujue kuwa uwezekano wa wewe kupata maisha bora ni mdogo sana. Kumbuka afya bora ndio chimbuko la nguvu
ulizonazo ambazo ndio hukupatia rasilimali “nguvukazi”. Unapoamua kuwekeza
nguvu kazi yako kwenye shughuli za uzalishaji ndipo unapata bidhaa au huduma ambazo
hugeuka kuwa pesa. Unapokuwa na bidhaa/huduma ndipo watu wengine sasa huamua kutoa
na kutuma pesa zao kwako, ili kujipatia bidhaa/huduma husika. Kwahiyo, iwapo
utakuwa umezalisha bidhaa nyingi utapata pesa nyingi na ni pesa hiyohiyo ambayo
na wewe utaitoa na kuituma kwa watu wengine ili kupata bidhaa/huduma na
hatimaye kukidhi mahitaji yako mbalimbali. Unapofikia hatua ya endelevu wa kupata
kile unachohitaji kwa muda muhafaka, ni wazi kwamba unakuwa tayari umefikia
maisha bora ambayo ni ya ndoto yako na hapa ndipo unaanza kupata vitu vile ulivyokuwa
ukivipenda lakini ulilazimika kuviacha kwa muda ili kuruhusu mchakato wako wa
maisha bora ukamilike.
Kwahiyo, tunapojiandaa kuanza safari ya
kutafuta mafanikio ni lazima tujitahidi kuanza mchakato wa kutafuta maisha
bora, kwa kuanza na ujenzi wa afya bora,
ili itupatie nguvukazi itakayo tuwezesha
kuzalisha bidhaa za kuleta pesa nyingi kukidhi mahitaji kwa kiwango endelevu na
hatimaye kufikia maisha bora ambayo
ndiyo ndoto yetu.
Mpendwa msomaji, endelea kuitumia vizuri MAARIFASHOP ili kujifunza mambo mbalimbali yatakayokuwezesha kupata mafanikio. Ili kupata makala mpya kila zinapochapishwa, bonyeza neno TUMA MAKALA MAARIFASHOP kisha sajiri barua pepe yako. Na kama unapenda kupata mafunzo ya kila siku kwa njia ya whatsap bonyeza neno MAFUNZO.
No comments:
Post a Comment